Baba Mtakatifu, Papa Francis, katika hali isiyotarajiwa amebusu miguu ya Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, akimsihi pamoja na wenzake kuhakikisha nchi hiyo hairudi kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Papa Francis amemwomba Rais Kiir na makamu wake wa awali, Riek Machar, ambaye ameasi kwa sasa, pamoja na makamu wengine wa rais waliofika Vatican kuheshimu makubaliano waliyotia saini ya kusitisha mivutano kati yao, ikiwa ni pamoja na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

“Nakuomba ukiwa kama ndugu kubaki katika amani. Nawaomba kwa moyo wangu, tusonge mbele. Kutakuwa na matatizo mengi lakini hayawezi kutuzidi nguvu. Tatueni matatizo yenu,” amesema Papa Francis.

Viongozi hao wamejikuta wakiduwaa, baada ya Papa mwenye umri wa miaka 82, ambaye anasumbuliwa na maumivu ya miguu akisaidiwa na wasaidizi wake wakati akipiga magoti kwa taabu kubusu viatu vya viongozi hao wawili wa upinzani.

Hatua ya Papa imekuwa ya aina yake katika wakati ambao taharuki imetanda Sudan Kusini, baada ya kutokea mapinduzi nchi jirani ya Sudan.

Vatican imewakutanisha viongozi wa Sudan Kusini kwa ajili ya sala ya saa 24 na mahubiri katika makazi ya Papa Francis kwa lengo la kuondoa makovu ya vurugu za wenyewe kwa wenyewe kuelekea kuunda serikali ya mseto.

“Kutakuwa na tofauti, hali ya kutokukubaliana kati yenu, ndani ya ofisi,” amesema Papa Francis kwa lugha ya Kiitaliano iliyokuwa ikitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza.

Akaongeza: “Lakini mbele ya wananchi, shikaneni mikono kuashiria umoja.”

Sudan, ambayo kimsingi ni taifa la Kiislamu, wamekuwa na uhasama na wenzao wa kusini ambao ni Wakristo kabla ya kujitenga na kuunda taifa huru la Sudan Kusini mwaka 2011.

Sudan Kusini hata hivyo ilitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe miaka miwili baadaye, baada ya Kiir kutoka kabila la Dinka kumfukuza kazi Machar kutoka kabila la Nuer, ambaye alikuwa makamu wake wa rais.

Takriban watu 400,000 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya theluthi moja ya watu milioni 12 wa taifa hilo walikimbia makazi yao, ikiwa ni idadi kubwa ya wakimbizi tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.

Pande mbili katika mvutano huo nchini humo zilitia saini makubaliano ya amani mwezi Septemba mwaka jana. Kati ya makubaliano hayo, licha ya kuunda serikali ya kitaifa mwezi ujao, wapiganaji wa upinzani waingizwe jeshini na hatimaye kujenga jeshi la kitaifa.

Katika hotuba yake ya awali, Papa Francis amesema wananchi wa Sudan Kusini wamechoshwa na vita, hivyo viongozi wa taifa hilo wanawajibika kujenga taifa hilo kwa ajili ya mustakabali mwema wa taifa hilo.

Papa alieleza nia yake ya kuitembelea nchi hiyo sambamba na viongozi wengine wa dini ili kudumisha amani.

Wengine walioshiriki sala kati ya Papa na viongozi hao wa Sudan Kusini ni pamoja na Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby, ambaye ni kiongozi wa kiroho wa Kanisa la Anglikana duniani, wanachama wa Baraza la Makanisa Sudan Kusini, na viongozi wengine kadhaa kutoka Kanisa Katoliki na makanisa mengine kutoka Afrika.

Please follow and like us:
Pin Share