Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali imejiandaa kumjibu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kwa ushahidi; na sasa inachofanya ni kumsubiri arejee nchini.

Amesema serikali inatambua kuwa Lissu anatibiwa, na kwa maana hiyo si jambo la busara kujibizana na mgonjwa.

Waziri Mkuu ametoa msimamo huo katika mahojiano maalumu na JAMHURI yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dodoma muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa 14 wa Bunge mwishoni mwa wiki.

“Sisi tuna taarifa kwamba Tundu Lissu anaumwa na hatuwezi tukajibishana na mtu ambaye ni mwenzetu, amepata tatizo. Hii ni Tanzania, watu wanasema – ana uhuru wake wa kusema, lakini sisi tuna nafasi nzuri ya kufafanua.

“Yeye amezungumza kwenye chombo cha Deutsche Welle (DW) [Shirika la Utangazaji la Ujerumani], sisi hatuwezi kusafiri mpaka Deutsche Welle kwenda kujibu. Tunazo taratibu zetu za kujibu, na hayo anayoyasema Watanzania wanayajua,” amesema.

Ameulizwa kama kauli za Lissu haziiathiri Tanzania – ndani na nje ya nchi, naye amejibu: “Sisi hatuna shida na kauli zake kwa sababu Watanzania wanajua. Watanzania wanajua jitihada zinazofanywa na serikali hii ikiongozwa na rais wetu. Watanzania wanamsikiliza, lakini wametulia kwa sababu wanajua ndani ya nchi hatuna hilo, na mtu yeyote anayetaka kujua hilo aje nchini, aje ashuhudie kama hapa sijui kuna uminywaji wa demokrasia atakuja kuona.

“Aje aone kama nchi hii watu wanauliwa sana, kama serikali inaua atakuja kuona, kama watu wanauawa hapa nchini kungekuwa na crises [sintofahamu] ndani ya nchi, lakini iko salama, inaendelea vizuri, na sisi bado tunakaribisha wageni kutoka pote duniani waje – Tanzania ni nchi salama.”

Amesema athari zilizopo ni “kumwona Mtanzania mwezetu akikosa uzalendo anapowaambia na kuwaaminisha huko nje kwamba yeye anasema hivyo.

“Sisi tunaamini kule kuna balozi, kwa hiyo balozi zinaweza zikajibu. Serikali hatuwezi kwenda front [mbele]. Tunajua ni mwenzetu aliyepata madhara makubwa ambayo hata sisi hatukufurahia, na bado yuko hospitalini kwa hiyo ngoja arudi.

“Tukishajua ametibiwa atakaposema atajibiwa kwa forum [jukwaa] analotumia yeye. Akienda TBC na sisi tutaenda huko, lakini kwa sasa hatuwezi kumjibu. Anatumia DW sawa, balozi ziko kule zitafanya kazi hiyo kama ambavyo mmeona Balozi wa Ujerumani ameamua kumjibu. Sisi tunamsubiri akirudi hapa, akisema TBC, tutakwenda TBC tutamjibu, tukijua kwamba sasa amerudi na yuko salama, lakini kwa sasa tunajua ana tatizo la kiafya.

“Sisi tunamwombea arejee katika hali ya kawaida, aje nyumbani tushirikiane naye kwenye maendeleo pale ambako atahitaji kushauri serikali, atushauri. Lakini kama atazungumza jambo ambalo halina tija kwa Watanzania tutamjibu kwa ushahidi.”

Waziri Mkuu ameonekana kutotaka kuingia kwenye undani wa suala la Lissu akisema Watanzania wanahitaji zaidi kuona kero zao zikipata majibu kuliko malumbano ya kisiasa kwa jambo ambalo halikutendwa na serikali.

Anapinga madai kwamba serikali haikuonyesha ‘huruma’ pindi alipoumizwa.

“Nisingependa sana kuzungumza mambo ya Tundu Lissu, lakini Mheshimiwa Rais alimtuma Mheshimiwa Makamu wa Rais kwenda kumsalimia kule Nairobi, Kenya. Rais ndiye kiongozi wa nchi, alimtuma Makamu wa Rais. Rais aliandika kueleza masikitiko yake kwa tukio la Lissu kushambuliwa. Sote tulihuzunishwa mno kuona hali ile ya kushambuliwa kwake.

“Kwa hiyo serikali tulishamsalimia. Haina maana sasa leo aende rais, kesho aende waziri mkuu…muhimu zaidi serikali imeshiriki kuonyesha masikitiko kwa tukio lile. Suala la fedha za matibabu ni jambo jingine. Yeye [Lissu] ni mtumishi wa Bunge, kuna taratibu zake za kifedha. Serikali haiwezi kutoa fedha kwa yeye kwa sababu taratibu za kiserikali za kiutumishi ziko tofauti,” amesema.

 

Msimamo wa Serikali kwenye elimu

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze utekelezaji wa sera ya elimu bure ya msingi, umekuwapo uhaba mkubwa wa vifaa na walimu. Waziri Mkuu anasema: “Elimu bure imekuwa na mwitikio mkubwa. Yako maelekezo ambayo tumeyatoa kwenye Serikali za Mitaa ambako shule za msingi na sekondari ndiko ziliko, na mamlaka hizi ndizo zenye dhamana na shule hizi.

“Yako mahitaji makubwa sana ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, walimu, vitabu lakini haya tumeyagawa. Kwa kuwa shule hizi za msingi na sekondari asili yake ni za wananchi, kwa maana ya mamlaka ya Serikali za Mitaa – vijiji, kata na wilaya – pale ambako kunakuwa na upungufu halmashauri inawajibika kuboresha. Tunatambua idadi kubwa ya shule zenyewe lakini pia wanafunzi. Tunapotaka kuendeleza shule hizi miundombinu, vifaa, walimu tunashirikiana na Serikali Kuu.

“Mheshimiwa Rais aliposema wakati ule wananchi wenyewe wakiwa ndio wanasimamia maendeleo ya shule, tulianza kuona michango holela. Kesho unasikia wameagizwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa darasa, kesho wameagizwa…wakati ule kulikuwa na michango isiyokuwa na tija. Tulipositisha, kwanza tulijua shule zinahitaji fedha kujiendesha. Tukatenga shilingi zaidi ya bilioni 23 kwa ajili ya sekondari na shule za msingi – ziende kwenye utawala waweze kununua vifaa vidogo vidogo. Walimu wakuu wanapewa fedha kila mwezi.

“Tunafanya hilo kwa sababu tusingependa kuona Watanzania wanachangishwa fedha. Wakati mwingine tunajua Watanzania hawa hawana fedha, wengine walikuwa wanafanya watoto kubaki nyumbani.

“Pili, tukiwa tunajua kwamba shule hizi ni za wananchi, wanawajibika kuweka miundombinu -tumegundua uwezo huo si mkubwa sana kwao kwa hiyo Serikali Kuu inawaunga mkono. Tunao mradi unaitwa Progress for Results. Mradi huu tumetenga fedha zinazosaidia ujenzi wa miundombinu – nyumba za walimu, madarasa, maabara, matundu ya vyoo – hizi tunazipeleka kwa awamu. Juzi tu tumepeleka mgawo wa vyumba vya madarasa katika halmashauri, si chini ya Sh bilioni 5 katika halmashauri zote nchini.

Michango shuleni

“Hatujazuia michango, lakini tumezuia michango ya ovyo. Lakini pia tumeweka utaratibu wa michango. Kama shule ‘A’ au ‘B’ inahitaji kujenga darasa na inahitaji sapoti kutoka kwa wadau, kazi hiyo itafanywa na mkurugenzi wa halmashauri.

“Tumefanya hivyo ili kudhibiti njia ya upokeaji wa fedha za michango kutoka kwa wananchi kwa lengo la kutaka zitumike kama ilivyokusudiwa. Kwa hiyo sasa mkurugenzi kwa sababu ndiye mwenye shule pale ambako bodi ya shule kwa sekondari na kamati ya shule kwa shule za msingi inaona kuna umuhimu wa kuchangisha fedha kutoka kwa wazazi ili zifanye kazi fulani; kazi hiyo itafanywa na mkurugenzi na yeye ndiye atakayetangaza mchango, ataelekeza mchango ukusanywe na nani.

“Mkurugenzi ataenda kutangaza michango itakayokusanywa na ataratibu namna ya kujenga majengo hayo yaliyokusudiwa, au matumizi ya michango hiyo. Kama kuna mtu anataka kuchangia haturuhusu mtu yeyote kupokea hiyo michango kwa sababu tunaondoa mwanya wa kila mmoja kufanya chochote anachokiona – kuanzisha michango anayoiona yeye. Nchi yetu ni kubwa, monitoring inahitajika na close control. Kwa utaratibu huu tumeondoa mamlaka za watu kufanya mambo wanayoyataka – hii ni kwa uzoefu – na sasa michango haijazuiliwa, lakini mkurugenzi atapewa taarifa na ata-act mara moja kuja kwenye kikao cha kuhamasisha watu, itatamkwa na yeye na atatoa utaratibu wa kuchangia na ni yeye anayepokea ili pia aje kuwajibika kutoa taarifa za jambo lililokusudiwa kwa kuwashirikisha wao pia hata kwenye ujenzi, matumizi na kadhalika,” amesema.

Jiji la Dodoma

Waziri Mkuu amesema uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi jijini Dodoma ni sahihi na tayari umeshaanza kuonyesha matunda makubwa.

“Kwanza niwahakikishie wananchi kwamba uamuzi wetu ni sahihi na kwamba makao makuu ya nchi ni Dodoma, na kwamba shughuli zote za serikali sasa zitafanyika Dodoma.

“Tumeshaleta watumishi karibu asilimia 96; asilimia 4 ni wale ambao wana shughuli na mji mkuu wa zamani (Dar es Salaam). Kwa hiyo tutakapojiridhisha shughuli zao zote zimekamilika ndipo watakuja, kwa sababu kuna wizara ambazo zinahitaji baadhi ya watumishi wachache wawe Dar es Salaam. Hao tumewaachia kwa muda, wapo kama asilimia 4 tu.

Kwa sasa huduma mbalimbali zinatolewa Dodoma kwa ile hadhi ya makao makuu. Ofisi za serikali zimeshajengwa na deadline ilikuwa tarehe 31 (Januari, 2019), nasubiri tu kwenda kukabidhiwa funguo za kila ofisi. Tunakwenda kupokea ofisi ili mawaziri wahamie. Kilichobaki sasa ni kutangaza tarehe ya mawaziri wote kupatikana kule [kwenye ofisi mpya].

Mbona STK, STL zinashindana barabarani?

Waziri Mkuu amesema unapohama mji hauwezi kuhama kwa asilimia 100 kwa wakati mmoja na kuwa Dar es Salaam ni kituo cha kibiashara na ziko wizara zinapaswa kukutana na watu kwenye kituo cha Dar es Salaam; na wengine Dodoma.

“Bado mawaziri watakwenda, lakini wapo watumishi wengine wanafanya kazi mikoa ya kusini kwa hiyo bado watapita Dar es Salaam, kwa hiyo Dar es Salaam bado itakuwa njia ya kupita. Kuwepo kwa shughuli kadhaa Dar es Salaam, na kwa kuwa wageni wetu wengi wanaamini shughuli bado ziko Dar es Salaam, kwa hiyo tunajitahidi kuwavutia na kuwafikisha Dar es Salaam hasa kwa kuwa miundombinu mikubwa bado iko Dar es Salaam, wapo wengine wanahitaji hadhi ya mambo fulani fulani Dar es Salaam.

“Kwa hiyo bado wategemee kutakuwa na safari kadhaa za kwenda Dar es Salaam, si kwa sababu ya kupishana tu njiani kama maonyesho, bali kwa sababu baadhi ya huduma ziko huko. Hadi hapa tulipofika tumejitahidi sana kwa sababu mambo kama nilivyosema asilimia 96 yako Dodoma,” amesema.

Mwito kwa sekta binafsi

Waziri Mkuu anahamasisha sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizoko Dodoma, akisema wanaochelewa wanaweza kujutia baadaye kwa kuzikosa.

“Kuna fursa kubwa sana kwa sekta binafsi kwa Dodoma kwa sababu kunahitajika huduma mbalimbali. Tunahitaji shule, tunahitaji maeneo ya kupata huduma za afya, tunahitaji miundombinu, tunahitaji masoko, tunahitaji mahoteli, nyumba za kulala wageni…zote hizo zinategemea sekta binafsi, si serikali.

“Kwa hiyo sekta binafsi bado ina fursa ya kuwekeza na kufanya biashara nzuri hapa Dodoma. Ni kiasi tu cha kujua kwa idadi hii kubwa watu wanahitaji kuwa na shule tofauti tofauti, anayehitaji aje atengeneze shule yake hapa, aje ajenge hospitali yake, aje kujenga masoko yake, tunahitaji shopping malls [maduka makubwa], tunahitaji vyombo vya usafiri.

Fursa ziko nyingi. Kwa hiyo sisi ambao tunafanya kazi na sekta binafsi tunategemea sana na tunaamini improvement ya makao makuu mapya itaboreshwa pia na sekta binafsi. Kwa hiyo mwito wangu kwa sekta binafsi ni kutumia fursa iliyopo kuja kupata tija kwa kuwekeza kwenye sekta yoyote ambayo mwekezaji anadhani kibiashara itamletea tija,” amesema waziri mkuu.

Please follow and like us:
Pin Share