IMG-20150429-WA0071Wakati Mbita anaanza kazi katika Kamati ile ya Ukombozi, dunia iligawanyika katika pande mbili ki-mawazo na mitazamo. Hii kisiasa tuliita enzi za vita baridi kati ya mataifa ya Ulaya (upande wa Magharibi na upande wa Mashariki).
Hili nalo lilileta changamoto ya aina yake miongoni mwa wapigania ukombozi katika Bara la Afrika. Vilikuwapo vishawishi vikubwa tu. Hapo kiongozi asiyekuwa mwadilifu angeweza kutumia vibaya madaraka yake kwa nafasi kama ile na akajitajirisha sana. Vyama vya wapigania Uhuru vilikuwa kadhaa katika nchi moja. Kila chama kilijiona ndicho cha wazalendo. Hapakuwa na umoja.


Mathalan, kule Zimbabwe, walikuwa na ZANU (ya Washona) na ZAPU (ya Matebele). Kule Angola kulikuwa na MPLA (ya Agustino Neto), FNLA (ya Holden Roberto) na UNITA (ya Jonas Savimbi). Huko Msumbiji kulikuwa na FRELIMO (ya Samora Machel) na RENAMO ya Alberto). Afrika Kusini kulikuwa na ANC ya Oliver Tambo na Nelson Mandela) na PAC ya John Nyati Pokela. Namibia kulikuwa na SWAPO ya Sam Nujoma na vyama vinginevyo.


Lakini Mbita alitumia mbinu zake zote za kijeshi, za kisiasa na karama yake ya usikivu akaweza kuwalainisha na kuwaweka katika mstari ilimradi wote waelekee kwenye umoja na hatimaye wakomboe nchi zao! Hapo si ndipo lile jina la “catalyst” lilimfaa? Aliwachochea wapigania Uhuru na kuwaharakisha kufikia lengo lao kuu la kupata UHURU kwa nchi zao. Ushupavu namna hii baada ya kustaafu ATUZWA NINI Mnyamwezi wa watu? Mimi sijui, ninachojua ni kuwa mzigo mzito abebeshwa Mnyamwezi, basi ataubeba! Ndivyo alivyofanya mtani wangu Hashim Mbita.
Je, baada ya kufa kwake amezikwaje shujaa huyu? Hapo sasa wengi wetu pale Lugalo viwanja vya Hospitali Kuu ya Jeshi, walikuja kufumbuka macho na wakazibuka masikio yao walipoona na kusikia sifa alizomwagiwa toka mataifa ya nje. Wale wote waliokuwa wakiishi katika kambi za wapigania Uhuru kama Nachingwea, Mazimbu, Mgagao, Kongwa walikuwa na neno la shukrani kwa “catalyst” huyu- Brigedia Jenerali Hashim Mbita.      


Wengi wetu tulioshuhudia kuagwa (last respect) kwa mwili wa shujaa huyu pale katika ukumbi wa Hospitali Kuu ya JWTZ Lugalo, ninaamini tulifumbuka macho, tukazibuka masikio yetu na tukajua kumbe Hashim Mbita alikuwa jabali kweli kweli katika harakati za ukombozi barani Afrika. Wale wote waliofaidika kwa ushauri wake, usimamizi na miongozo waliyopata kutoka kwa Brigedia Jenerali Mbita yule mimi nikimtania kwa kumwita “The Catalyst”. Walidiriki kutamka yaliyokidhi mioyoni mwao kutamka Serikali zao zilivyowatuma.
Wawakilishi kutoka nchi 16 walihudhuria mazishi yake. Wale waliobahatika kutoa salaam zao za rambirambi pale Lugalo hawakumung’unya maneno katika kumwelezea Brigedia Jenerali Mbita, na walitumia maneno tofauti namna hii.


Hapa nyumbani nchini mwake, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa msemaji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ilisema haya: “Ni msiba mkubwa kwa Bara la Afrika”. Ni vigumu kumwelezea Brigedia Jenerali Mbita kwa lugha ya kawaida, ukapata jibu, kwani alichokifanya kitakumbukwa milele katika ukanda huu wa Kusini mwa Afrika. Kazi za Mbita zitaendelea kukumbukwa kutokana na uhodari wake wa kutunza kwa maandishi kazi zote alizozifanya za kupigania Uhuru wa nchi za Afrika kupitia mradi wa ‘Mbita Project’.
Kwa nchi za nje alianza mwakilishi wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini. Mama huyu alisema wazi wazi hivi: “Leader and commander Hashim Mbita was a hero of our liberation. He dedicated his life during difficult times”.


Aliendelea: “Mbita alishirikiana vizuri na kiongozi wa ANC Bwana Oliver Tambo kuhakikisha nchi yetu- Afrika Kusini inakuwa huru. Jambo hili lilisaidia sisi kuondoka kwenye mikono ya ubaguzi wa rangi na kuwa huru. Mbita alitusaidia kutuunganisha. Haya ya kuwafukuza wageni Waafrika wenzetu mlivyosikia hivi karibuni yametufedhehesha sana. Rais Zuma ameyapinga vikali. Ulikuwa ni ubaguzi miongoni mwa Waafrika. Kwa heshima na kumuenzi Mbita Afrika Kusini inaahidi hapa tumekomesha ubaguzi ule na hautarejea tena. Rais Zuma ameomba msamaha kwa yale yaliyotokea na kuahidi kuendeleza amani na mshikamano wetu Waafrika wote”.
Mwakilishi wa Namibia alikuwa na haya ya kusema: “Tanzaia haina budi kujivunia kuwa na mtu wa aina ya Brigedia Jenerali Mbita. Kwetu sisi, Mbita alikuwa baba, rafiki na komandoo. Alikuwa mhimili wa mapinduzi yetu Kusini mwa Afrika. Basi, Brigedia Jenerali Mbita kwetu atabaki kuwa mfano wa uzalendo wa Kiafrika nchini na Afrika nzima. Ndoto yake likuwa kuona mataifa ya Kusini mwa Afrika yanakuwa huru. Tanzania imetoa kiongozi shupavu barani Afrika.”


Zimbabwe walikuja na sifa za kipekee. Mwakilishi yule alisema: “Hakuna mtu atakayeweza kuzungumzia mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika bila kulitaja jina la Brigedia Jenerali Mbita. Huyu alikuwa ‘KITOVU’ cha ukombozi kwa nchi zote leo hii zilizo huru huko Kusini mwetu. Zimbabwe yeye ndiye alikuwa ‘UBONGO’ wetu. Tumemtumia kwa mambo mengi na hakika hakutuangusha. Mapambano siyo pikiniki, yanahitaji mtu jasiri na makini. Brigedia Jenerali Mbita aliimudu vema nafasi ile. Mbita was one of Africa’s greatest sons.” Alimalizia.


Alipokuja mwakilishi wa Chama cha FRELIMO kutoka Msumbiji akamwelezea Brigedia Jenerali Mbita kuwa ni mtu aliyepigania ukombozi barani Afrika. Alitumia nguvu zake kukomboa Msumbiji. Alikuwa nyota kwa raia wa Msumbiji. Brigedia Jenerali Mbita alijenga Uhuru wa Afrika kwa kusimamia miundombinu, huduma za kijeshi na afya katika maeneo mbalimbali ya Kusini mwa Afrika. Mwakilishi wa Msumbiji alisikitika sana kwa kifo hiki maana kimewanyang’anya mtu waliyenuia kuwa naye wakati wa sherehe za kutimiza miaka 40 ya Uhuru wao Juni 25, 2015.
Mwakilishi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa niaba ya Katibu Mkuu wa SADC alisema kuwa Mbita anaendelea kuishi katika mioyo ya Waafrika ambao alipigania nchi zao zikapata Uhuru. Kwa kuthamini na kwa kutambua mchango mkubwa aliotoa Brigedia Jenerali Mbita kwa mataifa ya SADC, waliamua kumuenzi kwa kuzindua maandiko yake juu ya harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika katika kikao chao kule nchini Zimbabwe Agosti, mwaka jana katika mji wa Victoria Falls.

>>ITAENDELEA>>

 

By Jamhuri