MSUYAWaziri Mkuu mstaafu, Cleopa David Msuya, amesema ajenda kuu ya sasa kwa Mtanzania ni kupata elimu bora, lakini anasikitika kuona Rais Jakaya Kikwete akidanganywa, naye anakubali kudanganyika. Pia amesema hajutii kauli yake aliyoitoa akiwa Waziri wa Fedha kuwa “Kila mtu atabeba msalaba wake.”
Katika mwendelezo wa mahojiano na kiongozi huyo yaliyoanza kuchapishwa wiki iliyopita, Msuya ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, anahoji: “Ni nani anayemshauri Rais Jakaya Kikwete.”


Kilichomshtua Msuya ni taarifa za Rais Kikwete kutangaza hadharani sera mpya ya elimu Mei mwaka huu, akisema Serikali yake itatoa bure elimu kuanzia ngazi ya chekechekea hadi kidato cha nne.
“Hili jambo haliwezekani. Ni uongo. Sasa mimi sijui nani anamdanganya Rais? Sijui nani ni mshauri wa Rais katika jambo zito ambalo ni ajenda kuu tangu nchi kupata Uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita?” anahoji Msuya.
Msuya ambaye ana rekodi ya kuwa Waziri Mkuu pekee aliyehudumu kwa marais wawili; Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Ali Hassan Mwinyi, anasema anachokifahamu yeye, “hamna kitu kama bure.”
Akizungumza kwa kuchangua maneno, kwa utaratibu katika mahojiano hayo yaliyochukua takribani saa tatu, Msuya anasema elimu ina gharama zake na ni kubwa.


“Elimu inataka ujenge majengo, miundombinu, sakafu, madawati, vifaa kama maabara, vitabu na walimu walio wazuri. Sasa ukisema bure kwanza unadanganya nchi…
“Hamna kitu bure, labda useme gharama zitalipwa na serikali. Sasa kama Serikali itafidia si Serikali hii hii tuliyonayo! Kodi si hizihizi tunazochanga hapa, sasa kama kuna watoto wanakaa chini, hakuna sakafu. Hakuna vyoo. Jamani hebu tuwe wakweli! Elimu bure kwa kodi gani? Wanatoa wapi hizo fedha?” anahoji Msuya.
Anasema angeelewa somo la elimu bure kama Serikali ingesema itagharamia wanafunzi wasiojiweza huku gharama ya ziada zikiachwa kwa wanaojiweza, lakini si kusema, “elimu bure.”
Msuya anasema ingekuwa vema kwa sasa wakatafutwa washauri wa kumshauri vema washauri wa Rais Kikwete.


“Ndiyo maana nilisema kila mtu atauchukua msalaba wake, kauli ambayo siijutii na nitaitetea kwa sababu ni njia ya kuwaambia watu ukweli katika maisha. Haiwezekani kusema bure. Bure maanake nini?” anahoji.
Anasema dhana ya uongozi kwa watendaji na washauri wa Rais Kikwete imefika mpaka hata kwenye miundombinu kwani inapotokea mitaro ya maji machafu kufurika hususani wakati wa mvua, “Rais atadanganywa tu.”
“Uongo ni kitu kibaya sana, kwa mfano hata Dar inapofurika maji, akinamama wanatoka ofisini na wageni wamebeba viatu vyao na sketi zao wamepandisha juu. Rais atadanganywa na waandishi…
“Lakini hapa si suala la udanganyifu ni makosa yetu ya utendaji, we should engage (tuwahusishe) waandishi ambao watakuja na ukweli wa mambo kurekebisha mambo kuliko kudanganyadanganya,” anasema.


Msuya akarudi tena kwenye mstari wa elimu akisema, “If you don’t have money (kama huna hela), huna tu. Bure maana yake nini. Kuna matatizo baadhi ya sisi au viongozi wetu kuwa na tatizo la uchambuzi wa mambo, au fikra. Huu ni udanganyifu kati ya serikali na wananchi. Wataje nani anabeba gharama. Serikali ni hii hii, au inazaliwa nyingine?” anahoji.
Msuya, anasema anachofahamu ni kwamba hata akiingia Rais mpya Novemba, mwaka huu mchakato wa kukusanya kodi ni uleule.
“Sidhani kama kuna utajiri utakaoanguka kama mana kutoka mbinguni. Kama kuna wafadhali watakaosaidia sera hiyo, pia naweza kuelewa, lakini si bure, kwa Rais ajaye naye atakuwa tegemeo letu si kusema elimu bure” anasema Msuya.
Anasema suala la elimu nchini linafanyiwa mchezo na sumu yake imefika hadi katika elimu ya juu kwa taasisi zinazotoa ujuzi wa fani mbalimbali.


Anasema mikopo kwa wanafunzi wote wanaosoma chuo kikuu, “Ni ngumu kupata na inafikia hatua inashindikana kwa baadhi ya wanafunzi. Kuna wanaopendelewa.”
Anasema ni kwenda kinyume cha sera kwa baadhi ya wanafunzi hasa watoto wa vigogo na matajiri kupata mikopo hiyo kwani inawanyima fursa ambao hawana uwezo.
“Mikopo ya elimu ya juu iwe kwa vijana ambao hawana uwezo. Tuseme tutasaidia wale wasio na uwezo au wale mnaowashawishi waingie fani muhimu kama ualimu, unesi na udaktari. Lakini hata mikopo hiyo ukisema wapate wote. Hii haiwezekani.”
Kiongozi huyo anasema amejifunza kusema ukweli na ndiyo maana hata siku moja, hajutii kutoa kauli yake ya kwamba ‘kila mtu atabeba msalaba wake.”
Kauli hiyo ya Msuya, aliitoa wakati huo akiwa Waziri wa Fedha, awamu ya kwanza ya Rais awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.


 Wakati huo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa ameng’atuka na uchumi ukiwa mgumu na Msuya anasema, kauli ile iliungwa mkono na watu wa chini waliomwelewa.
Kwa nafasi yake ya Waziri wa Fedha, Msuya aliwasilisha mapendekezo bungeni kwa niaba ya Serikali, katika ukumbi wa Karimjee jijiji Dar es Salaam. Mapendekezo yalilenga  juu ya Serikali kutoza bia, vitenge na khanga.
“Sasa katika debate pale ndani. Kulikuwa na baadhi ya wabunge wa Pwani na Zanzibar. Wakaanza kupinga kodi ya khanga na vitenge wakisema kwamba ooh sisi wengine tuna wake watatu sasa hii mmepandisha kodi, vitenge vitakuwa ghali.
“Katika kujibu nikasema uamuzi wa kuoa wake wawili au watatu ni wa kwako. Huwezi kujenga hoja kwamba Serikali ikusadie kubeba mzigo eti kwa sababu una wake wengi.
“Tunachoweza kuzungumza hapa ni kwamba je, hizi kodi tunazotoza wananchi wanaweza kumudu kwa ajili ya kusaidia taifa lao? Nikalisema hilo la kila mtu atabeba mzigo wake.


“Nikashambuliwa pale ndani na viongozi wale wenye siasa za kijamaa, lakini bahati ya ajabu ni kwamba kumbe Mzee Mwinyi alipata taarifa za watu huko nje wanasemaje.
“Unajua katika taratibu za Serikali kuna kitu kinaitwa security report (taarifa ya usalama) ambayo Rais aliipata kwamba huko nje wameipokeaje ile hoja ya ‘Kila Mtu atabeba msalaba wake.’
“Basi ripoti iliyokuja ni kwamba kwenye mabasi ya daladala la UDA huko watu wakawa wanapongeza kwamba nimefanya kitu kizuri. Watu walinukuliwa wakisema, ‘kwamba Ooh leo mmeambiwa ukweli. Waziri amesema hivi.’


“Watu wakasema huyu si mawaziri wenu wanaowaambia uongo. Huyo ndiye amesema ukweli. Kwamba hali ni ngumu na kila mtu abebe msalaba wake. Sasa Rais Mwinyi akacheka akasema, ‘ndivyo watu wanavyosema, basi safi sana’.”
Anasema kwamba shida ya viongozi wa sasa ni kutaka kuwaaminisha wananchi mambo mengine yanayokuwa ovyo. Sasa watu wa kawaida wanajua hapa tunaambiwa ukweli au tunadanganywa.
“Ingawa wanasiasa wakomunisti na ujamaa walinishambulia. Lakini watu wa kawaida walinielewa. Kwamba kwenye baa wanasema hivyo na kwenye mabasi, basi nashukuru nilieleweka na hivyo sijutii kauli hiyo kwa sababu wananchi walitoa hukumu nzuri kwa kauli ile,” anasisitiza.
Anasema ataendelea kuitetea kauli hiyo kwa sababu viongozi wa sasa wanakabili changamoto zilizoko usoni kwa ahadi zisizotekelezeka.


Anasema Watanzania wameaminishwa kwamba wanaweza kutatuliwa matatizo yao na chama kilichokisha dola, Serikali au Rais, mbunge au diwani anayeongoza kwa kipindi chake.
“Tunafikiri huko [ndiko] kwenye majawabu. Nilishanga juzi kuona kampuni moja ya simu inatoa madawati Shinyanga. Ninavyoijua Shinyanya ni miongoni mwa mikoa yenye utajiri mkubwa, ina madini na misitu.
“Hivi kweli Wasukuma wangekuwa na proper leadership (uongozi sahihi) wangeshindwa kutengeneza dawati? Kule Mwanga kwetu si matajiri kama Shinyanga, ukilinganisha. Lakini tumeweka utaratibu wa kuhakikisha tunabanana kwamba tujitegemee.


“Tunachangishana na usipochanga wenzako wanakuadhibu. Imejengwa na ni sehemu ya utamaduni wetu. Kwa hiyo ni hii dhana ya kila mtu abebe msalaba wake inalenga tuwe na msingi wa kujitegemea. Tukiwa na nia ya kutatua matatizo yetu badala ya kutazama huko nje kwamba kuna mtu atakufadhili hivi hivi, [tutaweza],” anasema.
Anasema mbali ya akili ya mtu mmoja mmoja kujitegemea, pia ni vema hata mikoa na kanda ingepewa nafasi ya kushughulikia matatizo yao wenyewe badala ya kila kitu kutegemea Serikali Kuu.
“Rais sasa imefikia hatua anatembezwa mpaka Boko na Mbagala kuona athari za mafuriko na kutoa amri kwa viongozi kwamba watoe maji. Walioko pale wanafanya nini?


“Kwa hiyo wa Kagera na wa Mtwara nao wamsubiri Rais? Tuwe na vyombo vyenye kuwakilisha watu kwenye mikoa…wakitoza kodi mambo yangekwenda haraka. Hapo ndipo tutaona maendeleo.
“Mikoa na wilaya iwe na mabunge na watoze kodi wataona mambo. Haya niliyapeleka hadi kwenye Tume ya maoni kwa Warioba. Na nchi nyingi zinafanya hivyo kama vile ukienda Italia, Marekani, India wana state (majimbo) na parliament (bunge),” anasema.
Anasema tatizo la Watanzania wengi ni woga “Wanasema ooh ukifanya hivyo nchi itavunjika na watu watataka kujitawala wenyewe. Power (mamlaka) zile zinatoka juu na zinatetemeshwa tu,” anasema.
Anasema hakutakuwa na mtu wa kuhujumu Taifa kwani Tume ya Warioba ilimwambia, “Wakasema ooh mzee huoni kama italeta possibility (uwezekano) ya kumeguka. Hakuna kumeguka. Nigeria walizuia hivyo hivyo ndiyo maana unaona mikoa mingine imeendelea.
“Sasa tunataka kufika mbali, hili lazima walikubali. Inawezekana. Watachonga akili, watachanganya. Haya ni mapinduzi hatua ya pili ya maendeleo tukisema tunangojea kutoka Serikali Kuu… tutaendelea kubaki nyuma. Wakae huko wapasue akili ya maendeleo.”
Kuhusu kujiongeza kipato au kujitegemea, Msuya ameponda mtazamo wa vijana wengi wasomi kuanzisha asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) wakidhani kwamba watapata fedha.


“Jamani, maisha hayaendi hivyo. Nashukuru kauli ya Rais Kikwete hivi karibuni akiwaambia wafadhali kwamba mkitupelekesha tunagomea misaada yao. Na tufanye wenyewe. Na mimi naamini tunaweza kufanya wenyewe,” anasema.
Anatoa mfano kuwa alipokuwa Waziri wa Fedha, alipata kuona moja ya kazi ya Idara ya Misaada kutoka nje.
“Nikaita staff (watumishi) wa idara. Sasa Wajerumani walikuwa wanatoa misaada na kuna kitu wanaita VIP latrine. Nikauliza kitu gani. Wakasema ni vyoo vya kumwaga maji inabidi vijengwe Buguruni kwa ajili ya kudhibiti nzi badala ya vyoo vya shimo.
“Nikauliza kwa hiyo tunaomba msaada kwa Wajerumani kutujengea hivi vyoo? Yaani shimo kuchimbwa mbali, halafu bomba refu kuunganiswa? Nikauliza aina hii ya vyoo navyo mnaomba msaada?
Anasema alichoshangazwa ni kuona watu wanaandika miradi ya ajabu kuomba ufadhili na kuhoji. “Yaani Mjerumani anakuja kujenga choo halafu arudi kwao akaandike ripoti kwama ametoa msaada wa vyoo?”
Anasema kwamba baada ya kuona msaada huo wa choo si jambo la kuliandikia, akaamua kufuta msaada huo na kuagiza fedha hizo ziingine kwenye shughuli nyingine za maendeleo.


Alisifu juhudi za Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Nehemia Mchechu akisema amebuni na kujenga nyumba zinazouzwa kwa bei nafuu.
“Yule kijana anakusanya vijana anafyatulisha matofali sehemu mbalimbali, ambao ni kama wamejiajiri. Safi sana. Sasa mambo kama yale yanahitaji Mjerumani kweli?,” anahoji.
Anapendekeza kwenye kila wilaya kuweka mfumo wa kujenga nyumba za kisasa kwa kutumia ubunifu wa bosi wa NHC ambaye anatumia ‘teknolojia rahisi, akili na nguvu zetu wenyewe.’
“Sasa leo bado tunalia uhaba wa madawati, halafu unasema elimu bure. Bila shaka dhana yangu ya kila mtu atabeba msalaba wake haijaeleweka. Lazima kujitegemea ili kupunguza.”


Anasema kushindwa kujitegema na kujiingiza kwenye kununua vitu vya nje kwa dola, ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa dola ya Marekani.
“Na hili litatugharimu kweli. Mafuta yapanda bei.  Na mtu wa kawaida ambaye kipato chake hakiongezeki atapata shida kweli,” anasema Msuya na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba Taifa letu tumejilegeza. Kila kitu kinaagizwa nje. Mpaka vibiriti, mifuko ya plastiki, ndala, viatu vya mitumba, nguo za mitumba zinatoka nje. Tunafika mahala kila kitu kinatoka nje. Hata chakula kinatoka nje, kuku na matunda? Nasikia yanatoka Kenya na Afrika Kusini wakati tuna matunda kutoka Lushoto na Njombe,” anasema kwa masikitiko.
Msuya anasema kwa sasa Tanzania imekuwa kama taifa la soko la bibi kwa kila mwekezaji kuja kuuza hapa na mbaya zaidi Watanzania hawapendi vya kwao. “Ndiyo maana hata hivyo vya nje, bei inapanda.”
Anasema asasi husika hazina budi kusimamia uchumi, wakabana mianya inayofanya biashara za nje kupenya nchini kwa urahisi wakati bidhaa hizo zinaweza kupatikana nchini.


Anachofahamu ni kwamba baadhi ya maduka ya kubadili fedha yanahujumu uchumi wa nchi hii kwa kufanya biashara hiyo kwa ulaghai.
“Wanathubutu kusema kwamba ukibadili kwa risiti bei inakuwa kubwa na usipodai risiti unakatwa kidogo. Zenye risiti anaripoti BoT, zile ambazo hazina risiti zina namna yake. Kuna watu wana shilingi nyingi wanazitaka hizo dola kwa kuzihamishia nchini,” anasema.
Anasema Serikali haina budi kupinga ununuzi wa bidhaa kwa dola ikiwa ni pamoja na kupanga nyumba. Anapendekeza malipo kufanyika kwa shilingi.
Pia anasema Serikali ingeshusha kodi kwa magari mapya kwa sababu ya sasa yametengenezwa muda mrefu na ni sehemu ya chanzo cha ajali.
“Tupunguze kununua maua ya plastiki na kwa wale wasafiri wa kwenda nje wakate tiketi kwa shilingi badala ya dola. Natoa angalizo mwaka 2020 yanaweza kutukuta ya Uganda ilivyoporomosha shilingi yao,” anaonya.


Ili kuipaisha Tanzania haina budi kuanzisha viwanda vingi kuzalisha vitu vingi na kuuza nje badala ya kutegemea kila kitu kununua kutoka nje.
“Hatuna vitu vya matumizi ya watu wetu na hatujazuia vitu kutoka nje. Kwa mfano, zamani tulikuwa na sabuni za kuogea kutoka Mwanza, lakini sasa hakuna. Mapanga na visu eti vinaagizwa nje. Uongozi unaokuja uzinduke,” anasema.
Anasema kwamba haiwezekani sukari ikatoka nje sambamba na saruji  akionya kwamba uingizwaji huo utaua viwanda vilivyopo sasa kikiwamo cha bilionea wa Nigeria, Dangote.
 
Je, Msuya amemzungumziaje Warioba? Usikose mwendelezo wa makala hii wiki ijayo.

 
3084 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!