Nyuma ya pazia

 

Nyuma ya makala za nina ndoto kuna makala nyingi zilizowahi kuandikwa na hazijawahi kusomwa na mtu yeyote isipokuwa mimi mwandishi.

Nyuma ya nyimbo wanazoimba wasanii wengi na tunazisikia zikichezwa redioni na nyingine tumepakua na kuweka katika simu zetu, kuna nyimbo nyingi ambazo ziliimbwa miaka ya nyuma na hatujawahi kuzisikia.

Nyuma ya video nyingi za kuchekesha za Joti, Kelvin Hart, Eric Omondi, Profesa Harmo, Kansiime Anne na Deogratius wa Cheka tu, kuna video nyingi za kuvunja mbavu ambazo hatujawahi kuziona.

Nyuma ya magoli bora tunayoona wakifunga kina Christian Ronaldo, Lionel Messi na Mbwana Samatta kuna magoli mengi yaliwahi kufungwa mazuri zaidi ya hayo lakini hatujawahi kuyaona.

Mbele ya kila kitu kuna nyuma ya pazia. Huko kuna mambo mengi ambayo huwa hatuyaoni. Sisi tunaona na kufurahia matokeo tu.

Historia ya Yusufu, ambaye ni komandoo wa ‘Nina Ndoto’, kama tungeamua nina ndoto iwe filamu, ina mengi ya kutufunza. Maisha ya Yusufu yana nyuma ya pazia inayokatisha tamaa.

Yusufu hatimaye anakuja kuwa waziri mkuu katika nchi ya ugenini, Misri; historia ya maisha yake inasikitisha. Hakupendwa na ndugu zake, ndugu zake walitaka kumuua baadaye wakabadilisha umauzi na kumuuza kwa Waishmaeli kama mtumwa, alipofika Misri wakamuuza kwa Potifa, akida wa Farao, mkuu wa majeshi ili awe kijakazi wake.

Nyuma ya pazia ya maisha yake haikuishia hapo, maisha yake yalikuwa ni shida baada ya shida, kila kukicha afadhali ya jana. Alipokuwa nyumbani mwa Potifa, mke wa Potifa akataka kumbaka, Yusufu akakataa. Mke wa Potifa akamsingizia kuwa alitaka kumbaka, akapiga kelele Yusufu akakimbia na kuacha vazi lake. Maskini wa Mungu, Yusufu hana pa kujitetea, wahenga walisema: “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.” Kwa Yusufu hekima hiyo ya wahenga haikufaa kitu.

Potifa aliposikia habari hizo akaamuru Yusufu atiwe gerezani. Pamoja na magumu yote aliyopitia alitoka gerezani na kuwa waziri mkuu baada ya kusota kwa miaka miwili.

Inawezekana unapitia mengi sasa ambayo yanakatisha tamaa, ngoja nikwambie kitu rafiki yangu, “Upo nyuma ya pazia.” Kuna siku utatoka na kuona nuru. Inawezekana unaona giza tu, kumbuka giza linapokuwa nene, asubuhi huwa inakaribia. Wakorea wana msemo usemao: “Usiogopeshwe na kivuli, kinaonyesha kwamba jua linakaribia.”

Haijalishi upo katika handaki refu namna gani, lenye giza nene, kuna mahali linafika mwishoni, kuna mwanga na utaona nuru tena.

Thomas Edson, mvumbuzi wa balbu ya umeme alishindwa zaidi ya mara 1,000 kutengeneza balbu ya umeme inayowaka, zoezi la 1,001 lilifaulu. Anashauri akisema: “Kitu kikubwa kinachotukwamisha ni kwamba tunakata tamaa haraka. Njia sahihi ya kufanikiwa ni kujaribu mara nyingine tena.” Ukiwa nyuma ya pazia jaribu tena na tena na tena.

Rafiki yangu, Godius Rweyongeza, alipotafakari juu ya maisha ya nyuma ya pazia aliamua kuandika kitabu chenye jina, ‘Nyuma ya ushindi kuna kushindwa, kushindwa, kushindwa.’

Unapokuwa nyuma ya pazia kumbuka pia kumuomba Mungu akujalie na kukuongoza kila siku. “Muombe Mungu huku ukiwa umeweka juhudi zako,” ni methali ya Kihaya.

Mwanateolojia wa Marekani, Reinhold Neilbur, aliomba akisema: “Mungu nijalie utulivu wa mambo ambayo siwezi kuyabadilisha, ujasiri wa kubadili mambo ninayoweza kubadilisha, hekima ya kujua utofauti.”

Wachezaji kabla ya siku ya mechi hufanya mazoezi makali na baadaye wanakwenda uwanjani kucheza mechi. Nyuma ya pazia ni muda wa kufanya mazoezi, huwa hauna mashabiki.

Mwanamuziki kabla ya kupanda jukwaani kuburudisha huwa anafanya maandalizi nyuma ya pazia na matokeo yake hufanya mambo makubwa. “Watu wengi wamezoea kuona matokeo ya kazi. Hawawezi kuona upande wa kazi uliopitia ili kutoa matokeo,” anasema Michael Jackson, mwanamuziki maarufu na ‘Mfalme wa Pop.’

Unapokuwa nyuma ya pazia jipe moyo kila siku na sema: “Ipo siku pazia hili litafunguka na nitaonekana. Ipo siku kazi zangu zitaonekana. Ipo siku watu watanikubali. Ipo siku nitatimiza ndoto yangu.”

Mwandishi wa Kifaransa, George Sand, anasema: “Roho ambayo haijawahi kuumia haiwezi kupata furaha.” Baada ya dhiki faraja. Faraja hiyo wanaipata wale tu wanaoona na kukubali kuwa muda wa nyuma ya pazia upo na utapita tu.

By Jamhuri