Yusufu alikuwa mtoto wa Yakobo. Akiwa na miaka 17 baba yake alitokea kumpenda sana maana alikuwa ni mwana wa uzee wake, akamtengenezea kanzu ndefu.

Ndugu zake walipoona anapendwa zaidi wakaanza kumchukia. Siku moja Yusufu akaota ndoto na kuwaambia ndugu zake, “Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga maganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.”

Ndugu zake wakamwambia, “Je, ni kweli utatumiliki sisi?” Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake na kwa maneno yake.

Siku nyingine akaota  ndoto ambayo ilimwogopesha hata baba yake maana aliota akiwa kiongozi mkubwa. Ndugu zake wakazidi kumchukia wakapanga njama iliwamuue.

Kwenye jamii zetu na mazingira yetu ya kila siku kuna akina Yusufu wengi. Kuna watu wengi walikuwa na ndoto kubwa, lakini ndoto zao zimezimwa kama mshumaa.

Kuna watu walikuwa na uwezo mkubwa wa kubadili picha inayoonekana sasa na kuleta picha mpya, lakini wameshindwa kwa sababu wameambiwa ndoto zao si za kweli.

Ni mara ngapi umeambiwa maneno kama haya? Kazi uliyochagua si sahihi. Masomo unayosomea hayana ajira. Kipaji ulichonacho hakiwezi kukufikisha popote. Huna akili. Wewe ni kilaza. Huwezi kufika popote. Wewe ni mtoto mkorofi, hauna mbele wala nyuma.

Kuna nyakati zinafika unahitaji kuwa kama Yusufu. Watu wanaofanana na Yusufu ni wale walioambiwa mambo fulani hayawezekani, lakini wao wakaziba masikio na kuendelea kupiga hatua katika hatua ya ziada na kufika mbali maana walijua hakuna msongamano kwenye hatua ya ziada.

Martin Luther King Jr. aliwahi kusema, “Nina ndoto.” Yusufu alikuwa na ndoto. “Haijalishi unatokea wapi. Ndoto zako ni za kweli,” ni maneno ya Lupita Nyong’o.

Wanasema ndoto siyo unachokiota wakati umelala. Ndoto ni kile kitu kinachokufanya ukose usingizi. Kwa msingi huo ukiendelea kulala siyo rahisi kutimiza ndoto zako, bali ukiamka unaweza kuzifanya ndoto zako kuwa kweli.

John Paul DeJoria akiwa katika shule ya upili (kidato cha tano na sita) mwalimu wake alimwambia hawezi kufika popote kimaisha. John Paul pamoja na kuhangaika katika kutafuta maisha kuna siku alikumbwa na ukata wa hali ya juu, mke wake akamkimbia na kumwachia mtoto wa miaka miwili.

Alianza kuokota chupa tupu zilizotumika na kuziuza ili amtunze mwanae. Siku zote alimwambia mwanae, “Tutatoka kimaisha pamoja.” Alifanya pia biashara ya kuuza magazeti mlango hadi mlango.

Ilifika hatua akaamua kuanzisha kampuni watu wakamwambia hana elimu yoyote ya biashara na hana pesa za kutosha za kuendesha biashara. John Paul akaendelea kukomaa.

Mwaka 2015, gazeti la Forbes lilimtaja kama tajiri namba 234 kati ya matajiri 400 kutoka Marekani akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.8 za Marekani. Yeye pia ni mwanzilishi wa bidhaa za nywele zinazojulikana kama Paul Mitchel.

John Paul DeJoria ni Yusufu wa leo. Kuna haja ya wewe kuamini katika ndoto zako na hakuna mtu atakayekuja kufanya ndoto zako kuwa za kweli isipokuwa wewe mwenyewe. “Wakati ujao unamilikiwa na wale wanaoamini katika uzuri wa ndoto zao,”

alisema Eleanor Roosevelt.   Je, upo tayari kuishikilia ndoto yako hata kama hakuna anayeona uwezo ulionao?

Je, upo tayari kuhakikisha ndoto yako inakamilika hata kama wazazi wako, ndugu zako na hata marafiki zako wa karibu wanasema huwezi kufika popote?

Tatizo kubwa linalosababisha watu wengi kuachana na ndoto zao ni kusikiliza sauti za wengine kuliko sauti zao za ndani. Familia ya Yusufu haikuamini katika ndoto zake, lakini yeye alijiamini.

“Kila ndoto huanza na yule anayeiota. Kila mara kumbuka kuna nguvu ndani yako, uvumilivu na kiu ya nyota za kuibadili dunia.” (Harriet Tubman).

Usikubali hata siku moja ndoto yako izimwe ghafla kama mshumaa.

“Kinachonihamasisha ni wale watu wanaoniambia huwezi kufanya kitu fulani. Tafadhali niambieni siwezi kufanya kitu fulani,” (Darren Hardy). Yusufu alihamasishwa na maneno ya ndugu zake. Maneno ya wanaokukatisha tamaa yakupe hasira ya kutimiza ndoto zako na wala si kurudi nyuma.

By Jamhuri