Watu wa kale walitumia zana za mawe kuchinja mawindo yao. Katika kutekeleza hayo, huacha alama za chale kwenye mifupa. Hizi chale huweza kutambuliwa kutokana na umbo lake. Nyingi huwa na umbo la ‘V’ pamoja na mikwaruzo miembamba upande wa ndani isababishwayo na chembechembe ndogondogo za mawe yaliyotengenezea zana hizo.

Chale hizi husongamana maeneo maalumu ya mifupa na kwa mpangilio fulani. Mipangilio hii ya chale inahusiana na vitendo vya kuondoa nyama kwenye mifupa. Kwa kupambanua maeneo zinapoonekana chale hizi mtaalamu huweza  kuelezea namna kiwiliwili cha mnyama kilivyochinjwa na kugawanyishwa, na namna nyama zilivyokuwa kabla ya kuchinjwa. Tabia mbalimbali za uchinjaji kama kuchuna ngozi, kuondoa viungo vya ndani, kutenganisha viungo na kuchanachana huweza kutambuliwa.

Baada ya kutenganisha viungo, mifupa huvunjwa kwa kutumia nyundo. Hii iliacha bonde/mbonyeo kwenye mfupa ukiwa na michirizi midogo midogo iliyosongamana. Mfupa uliovunjwa kwa kugongwa namna hii huonyesha mpasuko wenye ukingo mkali tofauti na mfupa uliovunjwa ukiwa mkavu. Mtaalamu huweza pia kutofautisha mfupa uliovunjika kwa kugonga na ule uliosababishwa na kung’atwa kwa mgandamizo wa meno.

Vitendo vya asili kama mifupa kukanyagwa na wanyama wanapopita maeneo yenye mifupa hii, huweza kuacha alama kama chale, lakini mtaalamu huweza kuitofautisha baada ya kuiangalia kwa darubini. Alama za namna hii mara nyingi huwa pana na za kina kifupi kulinganisha na chale, na huwa na michirizi isiyokuwa na mpangilio maalumu. Huambatana pia na michubuko ambayo haipatikani katika alama zinazosababishwa na zama za mawe wakati wa uchinjaji. Alama za meno hutambulika kwa urahisi zaidi kutokana na umbo lake la ‘U’ na kutokuwa na michirizi.

Alama zisababishwazo na mizizi ya mimea na wadudu wanaoshambulia mifupa huweza kutambulika pia. Hivyo basi, mwonekano wa mifupa kutoa kumbukumbu nzuri ya vitendo vyote vilivyoathiri mifupa hiyo tangu kifo cha mnyama husika. Wataalamu wa kisasa wa mabadiliko haya hutumia utaalamu wao kutofautisha aina moja ya alama hadi nyingine na hutumia mbinu za hali ya juu kutafsiri kumbukumbu hizi.

Ulimwengu wa Homo erectus

Baada ya miaka milioni 1.5 iliyopita, unaanza ulimwengu wa Homo erectus, wakati mwingine akiitwa Homo ergaster kutofautisha na Homo erectus waliokuwa Bara la Asia. Japo kuna mabaki ya jamii ya Homo erectus ya tangu miaka milioni 1.8 iliyopita, masalia mengi yasiyo na utata ni yale ya baada ya miaka milioni 1.5. Homo erectus ni zamadamu wa kwanza kufanana zaidi na binadamu wa sasa.

Miili yao ilikuwa mikubwa kuzidi wote waliotangulia. Japo kulikuwa na kundi la Homo erectus wenye maumbo madogo, baadhi yao walifikia kimo cha kuzidi sentimeta 180 urefu.

Mabaki ya miaka milioni 1.6 iliyopita ya Homo erectus maarufu kama Turkana boy ambayo ni ya mtoto wa miaka 9 au 10, alishafikia urefu wa sentimeta 160 alipofia karibu na Ziwa Turkana nchini Kenya.

Fuvu la jamii ya Homo erectus, lilishakuwa kubwa kuzidi zamadamu wote waliotangulia. Wakiwa na ubongo unaozidi mililita 800-900, zamadamu hawa walishafikia wastani wa ubongo wa jamii yetu ya Homo sapiens wenye wastani wa mililita 1,399 (kwa mfano wa aliyewahi kutunukiwa zawadi ya Nobeli, Anatole France, ulikuwa na mililita 900 tu).

Miili ya Homo erectus ilikuwa pia ya kisasa zaidi. Uwiano wa urefu wa mikono na miguu ulikuwa sawa na wa kwetu; miguu ilikuwa mirefu kuzidi mikono. Kiwiliwili kilikuwa na kifua chenye umbo la pipa, ikielezea kuwa sehemu ya tumbo ilishapungua kutokana na kuanza kula vyakula vyenye lishe bora zaidi, nyama ikichangia kwa kiasi kikubwa. Hali hii inathibitishwa pia na udogo wa meno yao.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mabadiliko ya binadamu, wanawake walikuwa na maumbo madogo kiasi kuliko wanaume, tofauti na jamii zilizotangulia ambazo tofauti ya umbo kijinsia ilikuwa kubwa.

Uhusiano wa kijinsia katika jamii hii kwa hali hii ulifanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko na jamii za Australopithecus.

Meno ya Homo erectus yaonyesha kuwa kiwango cha ukuaji wake ni cha wastani wa kile cha sokwe na cha binadamu wa sasa. Kwa hiyo kuchelewa kukomaa ambako ni hali ya kawaida kwa binadamu wa sasa kulishaanza wakati wa Homo erectus.

Kitu kingine tunachojifunza katika maumbo ya kina Homo erectus ni kwamba waliimarika kwa mbio. Umbile la miguu yao, mifupa ya nyonga na kisogo vyaonyesha kuwa misuli iliimarika kuwezesha kukimbia.

Imekuwa ikijadiliwa kwa kirefu kuwa kuimarika kwa mbio ni mikakati ya kimaumbile ya kuwa mwindaji hodari. Hata hivyo, tafsiri hii bado ina mjadala mrefu.

Homo erectus waliendelea kutumia mtindo wa zama za mawe wa Oldowan kama waasisi wao, lakini wakaanzisha mtindo wao mpya wa zana uitwao Acheulian kuanzia miaka milioni 1.7 iliyopita.

Mtindo huu wa Acheulian ilikuwa wa zana kubwa kubwa zikiwemo aina ya mashoka (yasiyo na mpini) yaliyotengenezwa kwa wingi. Mashoka haya hayakufaa sana kwa kazi za kuchinja, hivyo yalitumika kwa kazi tofauti tofauti. Shughuli za kuchinja ziliendelea kutumia zana aina ya Oldowan. Maeneo kadhaa ya kipindi cha Acheulian yalikuwa makubwa kuzidi yale yaliyokuwa na Oldowan, ikiashiria kuwa zamadamu walitumia maeneo haya kwa shughuli tofauti tofauti na labda wakiwa makundi makubwa zaidi.

Tabia za Homo erectus

Kuishi sehemu moja iliyokuwa kama makazi yao ambako walishirikiana katika utafutaji na utumiaji wa vyakula. Hii iliwezesha hii jamii kuzoea aina tofauti ya mazingira ya ukanda wa Savanna ya Afrika. Ni maeneo machache sana ya akiolojia yaliyokwisha kupatikana yenye kuonyesha hatua za mwanzo za jamii hii katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na hata Kaskazini mwa Afrika.

Uwezo wake wa kumudu mazingira ya aina mbalimbali ulimwezesha kutoka katika Bara la Afrika na kuvamia mabara ya Ulaya na Asia; hatua iliyoanza mara baada ya miaka milioni 1.8 iliyopita.

Salomon (mwaka 1930) na Hay (mwaka 1976) walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuandika kuwa Homo erectus walitumia kwa pamoja zana aina ya Oldowan na Acheulian katika mazingira maalumu.

Kuhusu Olduvai, Hay aliandika kuwa maeneo mengi yenye zana aina ya Oldowan yalikuwa karibu na ukingo wa ziwa wakati Ashulian zilipatikana katika mazingira tambarare. Mazingira kama haya yaliripotiwa pia huko Peninj ambako maeneo yenye zana aina ya Acheulian yanapatikana mbali na makazi karibu na ziwa kuliko aina ya Oldowan.

Hali hii ilizua mjadala juu ya tafsiri ya Hay kuhusu sehemu zinakopatikana zana aina ya Oldowan na Acheulian kuashiria tabia za watumiaji zilizoongozwa na hali ya mazingira.

Maeneo mengi yenye zana aina ya Oldowan yasemekana yalisababishwa na tabia ya kukusanya wanyama waliofia kando kando ya ziwa. Tofauti na hali hii, katika Bonde la Olduvai na huko Peninj maeneo yenye Oldowan yameonekana mbali na ziwa, na wala zana hizi hazikutumika kukatia wanyama. Katika maeneo yenye Acheulian, hakuna ushahidi uliopatikana unaoonyesha kuwa zana hizi zimetumika kuwachinja wanyama. Peninj imetoa ushahidi wa kale zaidi wa matumizi ya miti katika kutengeneza zana. Zana hizi aina ya mashoka zilitumika kukata au kuchonga miti aina ya migunga.

Hii inaonyesha kuwa Homo erectus walikuwa na utaalamu wa kutumia zana za miti, vifaa ambavyo havijapatikana bado. Inaashiria kuwa mbinu zao za uwindaji zilishaendelea kiasi cha kutumia zana za miti kama mikuki.

Yadhihirisha pia kuwa mazingira ya kando kando ya ziwa walikopendelea kuishi hawa Homo erectus yalikuwa ya vipindi vifupi, labda kwa msimu muafaka kama tunavyoweza kufahamu kupitia eneo la Peninj. Ukanda wa Homo erectus ulikuwa mpana sana kwa jinsi inavyodhihirishwa na maeneo yalikopatikana mawe ya kutengenezea zana kubwa za Acheulian ambako upatikanaji wake ni katika maeneo machache na pia kwa kukutwa zana zilizotengenezwa kwa mawe ambayo asili yake siyo mahali yalipokutwa.

Alama za majeraha katika mifupa ya vidole vya wanyama kwa kukatwa na aina ya zana za mawe kama ilivyoonekana eneo la BK hapa Olduvai yanaashiria kuwa walichuna ngozi za wanyama labda kwa ajili ya kutengeneza mifuko ya kubebea vitu au kutumika kama nguo.

Please follow and like us:
Pin Share