Nini maana na umuhimu wa jina la biashara

Jina unalotumia kwenye biashara yako, yaani lile uliloandika dukani kwako, kwenye gari lako na kwingineko kwa mfano MASAI SHOP, KARAMA BEAUTY, BARAKA TRADERS, K TRANSPORTERS, KITWE BUS SERVICES na kadhalika, ndilo jina la biashara. 

Lakini si jina halali la biashara kama halijasajiliwa. Na si tu kuwa si halali, bali pia si lako, kwa kuwa yeyote anaweza kujitokeza akalisajili na akakuzuia kulitumia, hata kama wewe ndiye ulianza kulitumia muda mrefu uliopita.            

Niseme kwa tafsiri, twaweza kusema jina la biashara ni jina linalotumiwa na mtu kama jina la utambulisho wa biashara yake inayofanywa katika mfumo ambao si kampuni. 

Kampuni  zina majina, lakini majina hayo hayawezi kuitwa majina ya biashara, bali ni majina ya kampuni.

Jina la biashara ni kwa yule ambaye biashara yake imesajiliwa, lakini si kampuni.    

Aidha, mwenye biashara ambayo haijasajiliwa lakini analo jina fulani analotumia kisheria, huyo hana jina la biashara kisheria. Hilo jina si lake na mtu mwingine akilisajili anaweza kumlazimisha kuacha kulitumia. Unakuwa na haki ya jina la biashara pale tu unapolisajili kisheria.

2. Wapi waweza kusajili jina la biashara?     

Jina la biashara husajiliwa kwa Msajili wa Biashara na Makampuni (BRELA). Ukifika BRELA kama unataka kusajili jina la biashara utapewa fomu maalumu na utatakiwa kuijaza.  

Lakini kabla ya hapo utatakiwa utume maombi maalumu hapohapo BRELA ukitaka kujua iwapo jina ulilochagua kuwa la biashara limekwisha kusajiliwa na mtu mwingine au la.

Hii ni kwa sababu jina linalopaswa kusajiliwa ni moja kwa nchi nzima.  Hakuwezi kuwa na majina mawili au zaidi yanayofanana huku yote yakiwa yamesajiliwa.

Ada ya usajili ni kiasi gani?

Ada ya usajili wa jina si kubwa sana.  Mara ya mwisho mwaka 2019 ilikuwa Sh 25,000. Hiki ni kiwango ambacho wengi wanaofanya biashara na wanataka kusajili jina la biashara wanaweza kukimudu.

Kupata namba ya mlipa kodi

Kabla ya kurasimisha biashara, mtu anatakiwa kupata namba ya mlipa kodi (TIN).  Na hii inafanyika baada ya kuwa umepata cheti cha usajili wa biashara zako.

Namba hizi za mlipa kodi zinatolewa katika ofisi zote za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nchini kote. TRA wameweka utaratibu kwa anayehitaji kupata namba hiyo, ikiwa ni pamoja na  kupeleka  barua kutoka serikali za mitaa. Kwa hiyo ni lazima pia upate namba hii.

5. Kupata leseni ya biashara

Ukiwa tayari umesajili jina la biashara na umepata namba ya mlipa kodi, hatua inayofuata ni kutafuta leseni ya biashara.  Leseni hizi hupatikana ktika ofisi za manispaa.  Kila manispaa ina utaratibu wa kutoa leseni. Viambatanisho utakavyotakiwa kuwa navyo ni pamoja na ushahidi kuwa unayo namba ya mlipa kodi.

6. Faida za kurasimisha biashara

Moja ni kuwa unaweza kukopesheka katika taasisi za fedha. Lakini pia hata zile fedha zinazotolewa na serikali kwenye halmashauri kwa ajili ya wajasiriamali unaweza kuomba na ukapewa. Si rahisi kupata fedha hizi kama haujarasimisha biashara yako kisheria.

Pili, ni kinga ya biashara zako, kwa kuwa unaweza kupata bima ya majanga kama moto, na kadhalika pale tu unapokuwa umeirasimisha. Si rahisi kupata bima ya biashara ikiwa haujairasimisha.

Tatu, unaondoka katika kufanya biashara kienyeji na kuanza kufanya biashara kisasa na katika mfumo rasmi bila kujali udogo wa biashara zako. 

Hizi ni baadhi tu, lakini zipo faida nyingine nyingi.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.