Nyerere: Wazee wa Dar waliniamini wakaniombea dua

“Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.

“Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.

 

“Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.

“Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam). Akasema: Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.”

 

Nyerere: Tusiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu

“Katika nchi kama yetu, ambamo Waafrika ni masikini na wageni ni matajari, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi yake katika miaka themanini au mia moja ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni na wenyeji watakuwa watwana. Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri na wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.”

 

Nyerere: Watu wenye kasoro wameingia CCM

“Kutokana na umri wake mkubwa, watu wengi wenye kasoro wamejiingiza kwenye chama hiki. Sasa kimekuwa kama kokoro ambalo wakati mwingine hubeba viumbe visivyokubalika. Tunao watu wa ajabu ndani ya CCM ambao hawafanani na CCM.”

3199 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!