*Aona Pinda hana msaada, awatafuta TAHOA

*Alalama wenzake serikalini wanamhujumu

Na Mwandishi Maalumu

Katika hali inayoonesha kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, bado hajakata tamaa, sasa anahaha ili kuhakikisha kuwa wapambe wake waliohamishwa na Ikulu wanarudi kwenye Idara ya Wanyamapori.

Amekimbilia ubalozi wa Marekani nchini na kwa baadhi ya wamiliki wa kampuni za uwindaji wa kitalii ili wamsaidie kufanikisha azma hiyo.

Habari za uhakika zinasema Nyalandu amemuomba Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, aishinikize Serikali ya Tanzania ili watu wake warejee idarani.

Aidha, Nyalandu amekuwa, ama akikutana, au akizungumza kwa simu na baadhi ya matajiri wakubwa wenye kampuni za uwindaji wa kitalii na kuwasihi wamsaidie katika vita hii ambayo mshindi anaonekana ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi.

Matajiri hao ni pamoja na mfanyabiashara ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Mkoa wa Kigoma. Wakati wa Bunge la Bajeti mwaka 2012/2013 Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Peter Msigwa, alimtuhumu mfanyabiashara huyo kuwa anajihusisha na ujangili.

Pamoja nao, kuna habari zisizotiliwa shaka kuwa Nyalandu anaomba msaada kutoka kwa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA) ili waibane Serikali iwarejeshe wateule wa Nyalandu wizarani. TAHOA kwa asilimia kubwa inaendeshwa na wamiliki wa vitalu ambao ni raia wa kigeni na wazawa wanaokubaliana na matakwao yao. Kwa miaka mingi ndiyo waliokuwa na sauti katika masuala ya uwindaji wa kitalii.

Aidha, wakati wa mkutano wa CITES uliofanyika Bangkok, Thailand Machi 2013, shirika moja lisilo la kiserikali lilimtuhumu tajiri huyu kuwa ni miongoni mwa majangili wanaojihusisha na biashara ya pembe za ndovu.

Agosti 24, mwaka huu, Paul Sarakikya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori; na Julius Njau Kibebe aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi (Uzuiaji Ujangili); walipewa barua za uhamisho kwenda Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ambako wangepangiwa kazi nyingine.

Walitakiwa kuripoti ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia tarehe waliyokabidhiwa barua za uhamisho, lakini Nyalandu akawazuia; jambo ambalo ni kinyume cha sheria za utumishi wa umma. Waziri hana mamlaka ya uhamisho wa watumishi.

Hata hivyo, Nyalandu alipinga vikali mabadiliko hayo huku akimkebehi Katibu Mkuu (Utumishi) kuwa anaendekeza majungu. Kupitia dokezo alilomwandikia Tarishi, na kuwapa nakala wahusika, Nyalandu aliagiza kuwa wateule wake waendelee na majukumu yao kama kawaida na kudai kuwa hatambui mabadiliko hayo ya Ikulu kwa kuwa hakushirikishwa.

Maagizo haya ya Nyalandu yaliwapa kiburi wateule wake ambao waliendelea kubakia wizarani kwa zaidi ya mwezi mmoja huku wakishikilia ofisi na magari ya umma. Hata hivyo, wateule hawa waliomba na kulipwa pesa ya posho ya wiki moja na nauli ya ndege na teksi kwa ajili ya kwenda kuripoti kwenye vituo walivyopangiwa.

Vyanzo vyetu vya uhakika kutoka wizarani hapo, vinaeleza kuwa Sarakikya na Kibebe walitakiwa kukabidhi ofisi na magari, lakini wakakaidi.

Hata hivyo, Oktoba 8, mwaka huu walinyang’anywa magari hayo na kufungiwa ofisi pamoja na kukabidhiwa barua zilizowataka wajieleze kwanini wasifukuzwe kazi kutokana na kukaidi amri halali ya uhamisho.

“Ni baada ya hatua hizo, ndio mabwana hawa wakaripoti kwenye vituo vyao vipya vya kazi;” kimesema chanzo chetu kutoka wizarani hapo.

Baada ya uhamisho wa Sarakikya na Kibebe, Nyalandu alifanya jitihada kuhakikisha kuwa uamuzi huo wa Ikulu unatenguliwa. Ingawa Ikulu ndiyo iliyohusika na mpango huo, inasemekana kuwa alitafuta msaada wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda; jambo lililozua maswali kwamba iweje Ikulu iamue Waziri Mkuu ndio atakiwe kutengua.

Hii ni mara ya pili, Nyalandu anamtumia Waziri Mkuu kutengua uamuzi wa Ikulu unaohusiana na masuala ya watumishi waandamizi ndani ya Idara ya Wanyamapori.

Februari 24, mwaka huu, Nyalandu aliwaondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa, na aliyekuwa Mkurugenzi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Profesa Jafari Kidegesho kwenye nyadhifa zao kwa kile alichodai kuwa ni kutokuridhishwa na utendaji katika vita dhidi ya ujangili. Aidha, alidai kuwa amefanya hivyo kutekeleza Azimio la Bunge lililotaka waliohusika na kadhia ya Operesheni Tokomeza wawajibishwe.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Nyalandu alimteua Sarakikya, aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi (Uzuiaji Ujangili) kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori na Kibebe, aliyekuwa Mkuu wa Pori la Akiba Rungwa (lililoshamiri ujangili), kushika nafasi iliyoachwa wazi na Sarakikya. Inaaminika kuwa Sarakikya alikuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kabisa kumudu majukumu yake, jambo lililoilazimisha Serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza.

Aidha, Pori alilokuwa Kibebe ndilo lililokuwa limekithiri kwa ujangili wa ndovu. Katika Operesheni Tokomeza Sarakikya alikuwa mmoja wa viongozi waandamizi ‘field’, jambo linalozua maswali kwamba iweje mtu ambaye hahusiani na dhima ya uzuiaji ujangili afukuzwe kazi kwa kuzembea na kumpandisha cheo aliyekuwa kiini cha tatizo.

Baada ya kujiridhisha kuwa Nyalandu alikiuka kwa makusudi sheria na taratibu za utumishi wa umma, ambako hana mamlaka ya uteuzi wala nidhamu, na kwamba aliowatimua hawakuwa na makosa, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue aliingilia kati na kuwarejesha kazini Profesa Songorwa na mwenzake Profesa Kidegesho mwishoni mwa Aprili, mwaka huu.

Hata hivyo, Nyalandu alikuja juu huku ikiripotiwa kuwa alikula njama na baadhi ya wabunge ili wakwamishe bajeti yake kushinikiza Katibu Mkuu wa Wizara na Wakurugenzi waliorejeshwa waondolewe.

Baada ya mkakati wa kuwatumia wabunge kukwama, Nyalandu aliwasiliana na Waziri Mkuu ambaye alimshinikiza Katibu Mkuu Kiongozi kutengua uamuzi wake huku ikijengwa hofu hewa kwamba bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii isingepita endapo wakurugenzi hao wangebaki wizarani.

Baada ya Katibu Mkuu Kiongozi kutengua uamuzi wake kwa shingo upande, ilishauriwa kuwa suala la uteuzi lirudishwe kwa mamlaka stahiki ambayo ni Katibu Mkuu. Nyalandu alikuja juu na kung’ang’ania kuwa wateule wake ndio waendelee kushikilia ofisi, jambo ambalo lilivumiliwa ili kuleta utulivu ndani ya Wizara. Hata hivyo, hatua hii imeonekana kuivuruga zaidi Wizara badala ya kuisaidia.

Nyalandu, kwa kushirikiana na Sarakikya wamekuwa wakifanya makosa ya wazi ambayo ni kinyume cha Sheria na Kanuni za Wanyamapori. Moja ya kashfa ya kutisha ni ile ya matumizi mabaya ya Leseni za Rais nane zilizotolewa na Sarakikya kwa familia moja ya Kimarekani inayodaiwa kuwa na urafiki na Waziri Nyalandu. Leseni hizo ziliruhusu familia hiyo kuua wanyama 704 bila kulipa chochote serikalini.

Wanyama hawa ni pamoja na wale walio hatarini kutoweka wakiwemo tembo wanane, simba wanane, chui wanane, nyati 24 na kudu 40.  Familia hiyo, inayomiliki kampuni za uwindaji za Wengert Windrose Safaris (WWS) na Tanzania Game Trackers and Safaris (TGTS) ilikuwa haikidhi vigezo vya kupata Leseni ya Rais. Sarakikya, alinukuliwa na JAMHURI akidai kuwa ametoa leseni hiyo kwa ridhaa ya Waziri Nyalandu kwa kuwa ‘Waziri ana haki ya kuamua lolote kuhusu masuala ya wanyamapori.’

Kauli hiyo ya Sarakikya ilitafsiriwa kama upotoshaji mkubwa, na kwamba ilikuwa inadhihirisha udhaifu mkubwa kiuongozi na ukosefu wa weledi  kwa nafasi yake kwa kuwa kimsingi, Sarakikya ndiye aliyetakiwa kuhakikisha kuwa sheria na kanuni za wanyamapori nchini zinafuatwa vilivyo na mtu yeyote yule bila kujali nafasi yake na utaifa wake.

Masharti juu ya matumizi ya Leseni ya Rais yanajulikana na hakuna kifungu chochote kinachompa mamlaka waziri kuzitoa pale anapojisikia, bali inasisitizwa kuwa maslahi ya taifa lazima yazingatiwe na kwamba leseni hizi zisitumiwe kwa malengo binafsi na ya kibiashara.

Leseni hiyo iliruhusu uwindaji ufanyike katika vitalu vinne zaidi ambayo havijamilikishwa kwa TGTS kisheria. Hakuna maelezo yoyote kwa nini Waziri aliamua kuwamilikisha TGTS vitalu vinane pamoja na eneo la wazi na hivyo kukiuka Kifungu cha 38(7) cha Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009. Aidha, haijulikani kwa nini waziri aliruhusu Wamarekani hao kufanya uwindaji wa kitalii sehemu ambayo haijatengwa kama kitalu, achilia mbali ukweli kwamba eneo la Makao aliloruhusu uwindaji kufanyika halikidhi vigezo vya kisheria.

Kisheria, kitalu chochote kinapobaki wazi sharti kitangazwe kwanza na waombaji washindanishwe katika mfumo na utaratibu ulio wa haki na uwazi [Kanuni ya uwindaji wa kitalii 18(1)].

Aidha, Leseni za Rais zilitolewa kwa watoto wadogo chini ya miaka 18 kuwinda kinyume na kifungu cha 43(3) cha Sheria ya wanyamapori. Ni Sarakikya huyu huyu, chini ya kipindi cha miezi miwili, aliyeshauri Waziri Nyalandu aifutie Kampuni ya Green Mile Safaris vitalu vyote kwa kukiuka sheria za uwindaji, kosa moja likiwa la kuwindisha watoto chini ya miaka 18. Moja ya Kitalu cha Green Miles kilitolewa kinyemela kwa Kampuni ya TGTS yenye uswahiba na Nyalandu.

1732 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!