Kadri muda unavyozidi kusonga mbele naona joto la kuwania urais linapanda. Joto hili linapanda kwa wanasiasa, wapambe wao na hata viongozi walioko madarakani wanaanza kuangaliangalia nani watamsaidia kushika dola kisha aendelee ‘kuwaenzi’.
Nasema kuwaenzi kwa maana ya utamaduni wa ovyo uliojengeka Afrika, ambapo kiongozi anatenda mambo mengi asiyoamini kwa dhati ya moyo wake, mwisho wa siku anabaki na hofu. Anaanza kuogopa kivuli chake. Ukimwambia upinzani utashinda, anaona kama unataka afungwe.
Marais wengi waliopo madarakani, waliokuwa washindani wake ndani ya chama, wenye kumwambia asiyotaka kuyasikia, basi nao huwaona kama vyama vya upinzani na hudiriki kutumia nguvu kubwa kuwanadi watu wasio na sifa, almradi kuhakikisha wanajenga ngao ya kukinga hofu yao.
Sitanii, nilishangaa sana hivi karibuni niliposikia Rais Jakaya Kikwete anasema vijana wajitokeze katika urais. Nikajiuliza wamemkosea nini akina Stephen Wassira, Edward Lowassa, Bernard Membe, Asha-Rose Migiro, Anna Tibaijuka, Mizengo Pinda na wengine wenye umri unaoendana nao?
Kwa ufupi hapa nilichokiona ni kuwa inawezekana Kikwete ameanza kuwaogopa hawa. Anadhani katika harakati za uongozi kuna mahala amewajeruhi kwa njia moja au nyingine, na sasa anatafuta kijana wa kumtunukia urais. Anajua kijana atakayepewa urais kwenye sahani ambaye haitakuwa vigumu kupokea na maelekezo yake baada ya kuingia Ikulu.
Kikwete nimwache kwa upande huo, ila nisema asianze kutumia rungu lake la urais. Awaache Watanzania wamchague rais wamtakaye, wanayedhani anaweza kuliongoza taifa hili kutoka katika lindi la umaskini, ambao Kikwete yeye aliishakiri kuwa hajui kwa nini Tanzania ni nchi maskini.
Kwa hakika kama Kikwete hajui kwa nini taifa letu ni maskini, hakika hawezi kumfahamu rais bora, mwenye uwezo wa kutuondoa kwenye umaskini. Anaweza kutuletea mwanafunzi wake. Ikiwa yeye Mwalimu hajui jibu, itakuwa miujiza mwanafunzi wake kutengua kitendawili.
Sitanii, wakati nikimpa Kikwete onyo hilo, nirejee kwa huyu Mtoto wa Mkulima tajiri, Mizengo Pinda. Pinda anasema anatangaza kimyakimpya kugombea urais, mimi nasema Pinda hatufai. Anisamehe kwa kusema hivyo na sababu ninazo. Nimewahi kuliandika hili na leo nalirudia.
Pinda alitamka kuwa Zanzibar siyo nchi. Alibanwa kidogo tu, akaufyata. Machozi yakamlenga. Leo, ukimuuliza tena Pinda swali hili kama Zanzibar ni nchi au si nchi? Sijui kama anaweza kulijibu hadharani. Natumia fursa hii kumuuliza Pinda swali hili, Mzee Pinda; hivi Zanzibar ni nchi au si nchi?
Kwa kila hali nilimshangaa Pinda kuruhusu hata mjadala huo kuendelea. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaitambua Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haiitambui Zanzibar kama nchi. Achana na uchakachuaji uliojitokeza mwaka 2010 katika mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.
Ni kutokana na kukosa msimamo kwamba nchi imeyumbishwa. Amani Karume aliposhirikiana na Maalim Seif Shariff Hamad, kufanya uaini kwa kumega madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano mwaka 2010 kupitia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar hawa walipaswa kukamatwa.
Pinda angeweza kutumia kesi ya Machano Khamis Ali kujenga hoja yake, kuwa Mahakama ilikwishatamka kuwa Zanzibar si nchi. Ni katika mazingira hayo kuwa Pinda ametikiswa kidogo tu, akalia, sasa akijitokeza Iddi Amin akafufuka wakati Pinda ni Amir Jeshi mkuu, nchi hii itakuwa salama kweli?
Wapo watu tunaweza kuangalia historia yao ya kusimamia masilahi ya nchi na tukaiona. Mtu kama Bernard Membe anaweza akasema akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ameshiriki kikamilifu kumfurusha Kanali Bakari, kule Anjouan.
Ukimzungumza Lowassa unaweza kusema aliwafukuza City Water na akavunja uzio wa tajiri Baghadad pale viwanja vya Mnazi Mmoja akaokoa rasilimali za taifa hili. Sasa Pinda anaogopa hata kutangaza kuwa anagombea urais, anasema anatangaza kimyakimya, ananitia shaka.
Sitanii, nimelazimika kugusa mada hii leo kutokana na rasilimali za taifa letu. Nasema inawezekana Kikwete amefungua chupa yenye jini ndani yake. Ni wazi kwa kiwango cha gesi iliyopatikana, Tanzania ina kila dalili ya kupata mafuta. Nchi nyingi ambazo amani yake imetetereka rasimali mafuta imechangia kwa kiasi kikubwa.
Uguduzi wa gesi wa tcf karibu 51 thamani ya gesi hii pekee ni kama dola bilioni 700. Uchumi wa taifa letu kwa sasa thamani yake ni dola bilioni 28. Ukiangalia tofauti hiyo pekee na ugunduzi unaoendelea kufanyika, unabaini kuwa Tanzania uchumi wake utafumka si muda mrefu.
Ni katika msingi huo nasema tunahitaji Rais mwenye maono. Tunahitaji Rais anayeweza kuweka mpango kazi, akasema leo tunaanza na afya, barabara, maji, elimu na huko huko zikazalishwa ajira. Tukiwa na Rais anayeona aibu kutangaza malengo yake, asiye na msimamo, basi tujue wewekezaji wataendesha hii nchi.
Wawekezaji watateuliwa kuwa mawaziri, makatibu wakuu, mabalozi na wakurugenzi wa idara mbalimbali, kisha fedha za mishahara ya watumishi wa umma zitaanza kutoka mifukoni mwa wawekezaji na si Hazina. Taifa letu tumewahi kufika hapo. Sitaki kutaja lakini na wewe unajua.
Si unakumbuka kipindi ambacho Serikali ilisita kukusanya kodi? Si unakumbuka watu walivyofikia hatua fedha wakawa wanazisunda kwenye soksi mabunda kwa mabunda? Si unakumbuka jinsi watu walivyokuwa wanakunywa bia kwa kupima urefu wa makreti huko Nyarugusu? Kodi ilikuwa hazilipwi.
Tukipata Rais asiye msemaji, Rais asiye na msimamo, Rais anayeyumba kama mwanzi, Rais anayetaka kufurahisha kila mwananchi, Rais ambaye mtoto wake anaweza kuwa na sauti kuliko Waziri Mkuu, Rais ambaye ujumbe mfupi wa simu (sms) unamtosha kuvunja Baraza la Mawaziri, tutajuta.
Sitanii, nazisikia kauli za wanasiasa walio wengi. Nia ya msingi ya wanaoutaka urais, si kulitumikia taifa hili, bali ni kuvuna. Yanayotokea leo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, yanayotokea leo Darfur na Sudan Kusini, Tanzania hatujavaa ngao ya chuma kuzuia yasitufike. Kinga yetu ni mfumo alioujenga Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Mifumo aliyoijenga Mwalimu Nyerere inavunjwa kwa kasi kubwa. Kidogo Kikwete ndiye karejesha angalau Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na hivyo kuanza kurejesha moyo wa uzalenda na utaifa. Ingawa wengi haturidhiki na miezi mitatu, lakini angalau inawakutanisha vijana pamoja.
Kizazi cha facebook ambacho hata wakati wa vita kinataka kutuma meseji na kupiga picha risasi zikirindima, kinapaswa kwenda jeshini kufundwa. Nimeangalia baadhi ya picha wanazosema vijana wa JKT wanateswa nikasikitika sana. Enzi zetu JKT ilikuwa ukifika mpaka miezi sita ya ukuruta inaisha ni ‘mwendo wa mbwa’.
Bigula la kula likipigwa ilikuwa tunakwenda kwa mwendo wa kunyakua. Filimbi ikipigwa hakuna cha Mhindi, Mnyakyusa, Mchaga, Mhaya au Mzanzibar (Mshiiri) sote ilikuwa tunanyakua kwa kuruka juu kima cha ndama. Kama ni shamba sote tulilima, mitamba tulichunga na kuni tulipasua.
Mazoezi tuliyokuwa tukiyapenda sana ya kichura kukomaza mwili na kukwepa ndege, leo wakifanyishwa vijana walioko JKT wanasema wanateswa. Huwezi kuwa na taifa kakamavu, kwa kuwa na mafunzo legelege. Bora kutoka jasho jingi wakati wa mafunzo na kuishia kumwaga damu kidogo wakati wa vita halisi.
Sitanii, makala yangu leo inazunguzia wagombea urais. Nasema nchi yetu ilikofikia inahitaji mgombea urais wa kipindi kimoja. Ukisimamia haki ni lazima uwe tayari kudhihakiwa, kuchekwa, kunyimwa baadhi ya haki na hata kufukuzwa kwenye vikao kwa kuambiwa “kama msimamo wako ni huo, basi wewe hutufai.”
Mwanadamu anapaswa kujitanabaisha. Anapaswa kuchagua kuwa wa moto au wa baridi. Unafiki, umafia, uzembe, undumilakuwili hauna nafasi katika maendeleo ya kweli. Ukiulizwa kuwa unataka nini kati ya embe na mkate, usitabasamu bali chagua moja na mambo yaishe.
Wakati nahitimisha makala hii, nasema ni lazima Rais Kikwete asituingize mkenge kwa kutuchagulia Rais. Yeyote anayejitokeza kugombea urais, iwe ni kwa upizani au chama tawala, lazima atueleze tukimchangua atalifanyia nini taifa letu na si kuja na nyimbo za ‘Ilani ya Chama inasema.’
Sitanii, narudia tukifanya kosa kwa kuchagua mgombea urais kwa sababu ya urafiki, vijisenti vya kulipa ada za watoto au kodi ya nyumba, miaka 10 baada ya 2015 itakuwa ya majuto makuu na kitakuwa kilio cha kusaga meno. Mungu ibariki Tanzania, Mungu tuangazie tumpate Rais mchapakazi.

1447 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!