*Asema kauli yake inabagua wazee CCM

*Aahidi kumuunga mkono mzee Wasira

Kauli iliyotolewa na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, kwamba mtu yeyote aliyezaliwa mwaka 1961 hapaswi kuwa Rais wa Tanzania, imemkera Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine.

Hii ni mara ya kwanza kwa wabunge hao vijana, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuonesha hadharani tofauti zao za misimamo kuhusu umri wa kugombea urais nchini.


Hivi karibuni, akizungumza katika kongamano la wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, alisema wazee hawapaswi kuukodolea macho uongozi wa taifa hili kipindi hiki cha changamoto na mazingira mapya.


Nyangwine amejitokeza kumkosoa Makamba akisema kauli hiyo inajenga ubaguzi wa wazi kwa wanachama wa CCM kuhusu haki ya kugombea uongozi, jambo ambalo ni kinyume cha katiba ya chama hicho tawala.


“Kauli ya Makamba ni ya ubaguzi, inabagua wazee na kupendelea vijana, lakini pia inachochea vijana kuwachukia wazee ndani ya CCM kinyume cha katiba ya chama chetu,” anasema Nyangwine katika mahojiano na JAMHURI Dar es Salaam, wiki iliyopita.


Nyangwine anatajwa kuwa ndiye mbunge wa kwanza kujitokeza mapema kumpigia kampeni za chini kwa chini za urais Mbunge wa Bunda na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira.


Wasira ni miongoni mwa wanachama wa CCM wazee waliozaliwa kabla ya mwaka 1961, ambao kwa mujibu wa Makamba, hawastahili kukabidhiwa dhamana ya kuiongoza nchi hii.


Licha ya Wasira, wana CCM wengine wanaotajwa kuwania urais wa Tanzania kupitia Uchaguzi Mkuu ujao, ingawa kauli ya Makamba inawaweka kando, ni pamoja na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda.


Nyangwine anawatetea wazee akisema hawapaswi kubaguliwa katika kinyang’anyiro cha urais kwani ndio watu waliokomaa kisiasa na wanaoijua historia ya Tanzania kwa mapana na marefu.


“Watanzania tumwogope kama ukoma mtu anayejenga matabaka ndani ya chama. Hao wazee wanaobaguliwa na January Makamba ndiyo wanaoijua vizuri historia ya nchi hii, hivyo kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kugombea uongozi wa urais ni ubaguzi na uonevu wa waziwazi.


“Mimi binafsi ninaamini kuwa vijana wanaokimbilia Ikulu bila kujua ukubwa wa kazi ya Ikulu ni watu wasio na uvumilivu wa kisiasa, lakini pia wasiojiamini katika utendaji wao ili waweze kuwashawishi Watanzania kuwapatia madaraka,” anasema Nyangwine.


Anasema CCM anayoifahamu haina ubaguzi wa umri linapokuja suala la kugombea uongozi, bali inatoa nafasi kwa mwanachama yeyote kujipima katika kinyang’anyiro cha uongozi.


“CCM tuna utaratibu wa kuangalia mchango wa mtu na uadilifu wake ndani ya chama na nchi. Hatuna utaratibu wa kuangalia umri na hodari wa kuzungumza ndiye tumkabidhi madaraka, hatuna utaratibu huo,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa Nyangwine, kitendo cha Makamba kuchaguliwa kuwa mbunge na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri hakipaswi kuwa chanzo cha kudharau na kubagua wazee nchini.

“Nchi hii ni ya Watanzania wote, hakuna mtu mwenye hatimiliki ya nchi hii. Watanzania ndiyo wenye mamlaka ya kuona nani mwenye uwezo na kuamua awe rais wao, wala hawaangalii umri wa mtu katika kufanya uamuzi huo,” anaongeza.


Msimamo huo wa Nyangwine unaelekea kufanana na wa wanasiasa wengi akiwamo Mkurugenzi wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, aliyeeleza kushangazwa na watu wanaopoteza muda kujadili urais badala ya kuwaachia wananchi waone anayefaa kushika madaraka hayo.


“Mtu afanye kazi watu waone unafaa kupewa cheo cha urais. Acheni propaganda ya kutafuta vyeo, kuna watu wengi, hasa vijana, badala ya kufanya kazi wanapiga porojo tu za kutafuta urais,” amesema Butiku na kuongeza:


“Sasa hivi Wakristo na Waislamu wanagombania kugawana madaraka. Rais ni mmoja acheni porojo za kutaka urais, rais ni mmoja tu.”


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro, amepinga msimamo wa Makamba na kuwataka Watanzania kutokubali kudanganywa kuhusu mtu anayefaa kuwa rais.


“Watanzania hawawezi kukubali kudanganywa kirahisi. Taifa letu linahitaji rais anayefahamu elimu ina matatizo, uchumi una matatizo na rasilimali tunazo ila watu wake ni maskini. Hatuhitaji rais kijana, mzee, Mnyakyusa. Tunahitaji rais anayeenda kupigania taifa letu kwa uzalendo,” amesisitiza Mtatiro.


Kwa upande wake, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amewataka wananchi kuondokana na dhana kwamba Tanzania ni mali ya CCM, bali wafahamu kuwa nchi hii ni mali ya Watanzania wote.

“Kuna watendaji wa Serikali wamevaa miwani ya mbao, hawasikii, hawaelewi na wanawaangusha Watanzania,” amesema Filikunjombe bila kufafanua kauli yake hiyo.

Nyangwine ataja sifa za rais

Nyangwine anataja sifa za mtu anayefaa kukabidhiwa wadhifa wa urais kuwa ni mwenye uwezo mkubwa wa kuhimili ushindani wa kisiasa nchini na anayeyajua matatizo ya Watanzania tangu nchi ipate Uhuru hadi sasa.


Sifa nyingine za urais, kwa mujibu wa Nyangwine, ni mtu mvumilivu, jasiri wa kukemea maovu, asiye na kashfa za rushwa wala kujilimbikizia mali na aina yoyote ya ufisadi.


“Mtu anayestahili kuwa rais lazima pia awe na upeo mkubwa katika masuala ya uongozi na kujua mahitaji ya makundi ya wazee, wanawake, vijana, watoto na walemavu,” anasema Nyangwine na kuongeza:


“La msingi zaidi mtu anayefaa kuwa rais lazima awe mzalendo wa kweli, mwadilifu, mnyenyekevu, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi mgumu pale inapobidi kwa manufaa ya taifa.


“Pia mtu anayepaswa kuwa rais wa nchi lazima awe na sifa ya kutanguliza maslahi ya umma kama alivyofanya Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere.”


Aapa kumuunga mkono Wasira

“Kwa kusema kweli mimi ninamuunga mkono mzee Wasira kwa sababu ninajua uwezo na uadilifu wake. Siku akitangaza kugombea urais nitamuunga mkono kwa hali na mali,” anasema Nyangwine na kuendelea:


“Ninaridhika na utendaji kazi wa Wasira katika utumishi wa umma na ndio maana nilijitahidi kumuunga mkono kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe wa NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM) hadi akashinda.


“Wasira ana sifa zote za kuwa rais wa Tanzania, hana tamaa ya mali, ni mtu jasiri, ni mkweli, anajua historia ya nchi hii, ni mzalendo, si fisadi na hana kashfa yoyote.”


Hata hivyo, Nyangwinge anatoa wito maalumu kwa Watanzania kuhakikisha wanakuwa makini na kutokubali kurubuniwa na propaganda za wanasiasa wanaopanda mbegu mbaya ya ubaguzi katika suala la uongozi wa nchi.


“Tunataka vijana wajiulize wataifanyia nini Tanzania badala ya kuuliza Tanzania itawafanyia nini, lakini pia watuambie wanakimbilia kwenda Ikulu kufanya nini?

“Namshauri mbunge kijana mwenzangu, January Makamba, kuwa makini katika kauli zake, hasa zinazogusa mustakabali wa taifa letu,” anasisitiza Nyangwine.

By Jamhuri