*Ajivunia maendeleo aliyowezesha

Mbunge wa Tarime mkoani Mara, Nyambari Nyangwine (CCM), ameibuka na kukanusha tuhuma za kutelekeza jimbo hilo kwa zaidi ya miezi sita mfululizo.

“Sijatekeleza jimbo, sijakaa miezi sita bila kwenda Tarime, Agosti mwaka huu nilifanya ziara katika vijiji vya Murito, Gibaso, Kegonga Kitawasi na Masanga. Wanaodai nimetelekeza jimbo langu ni wanasiasa mcharuko.


“Nilipochaguliwa kuwa mbunge (mwaka 2010) nilikuta jimbo (la Tarime) linapumlia mashine (lina matatizo mengi) lakini nimejitahidi kupigania maendeleo yake,” anasema Nyangwine katika mahojiano maalumu na JAMHURI mjini Dodoma, wiki iliyopita.


Anasema hakuna mbunge anayeweza kusukuma gurudumu la maendeleo ya wapigakura wake kwa kukaa jimboni na kujikita katika siasa ‘kavu’ siku zote bila kujizatiti kutafuta misaada ya ziada nje ya jimbo.


“Mimi kama mbunge siko tayari kukalia siasa tupu jimboni, lazima nitoke kusaka misaada katika wizara mbalimbali na kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya maendeleo ya wapigakura wangu,” anasisitiza Nyangwine.


Mbunge huyo kijana anasema utamaduni wake wa kutoka jimboni mara kwa mara umemwezesha kupata misaada ya kimaendeleo kutoka serikalini na kwa wafadhili mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hilo.


“Kwa mfano, bidii yangu ya kufuatilia na kubisha hodi mara kwa mara katika ofisi za Wizara ya Nishati na Madini imewezesha upatikanaji wa mradi mkubwa wa umeme katika vijiji kadhaa jimboni,” anasema.


Kwa mujibu wa Nyangwine, huduma hiyo itatekelezwa kupitia Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) ndani ya mwaka wa fedha 2012/2013 katika vijiji vya Kubiterere, Remagwe, Nyabisaga, Borega, Ganyange, Nyantira, Kibasuka na Nyakunguru.


Vijiji vingine ni Manga, Mangucha/Getena, Masanga na Nyarwana, Wegita, Nkerege, Magoto, Sulubu, Bisarwi, Mtana, Kembwi, Kesangura na mji wa Nyamongo. Anasema lengo ni kuhakikisha vijiji vingi zaidi jimboni vinafikiwa na huduma ya umeme kufikia mwaka 2015.


Kuhusu elimu, anasema msukumo wake kwa kushirikiana na viongozi wengine umewezesha ujenzi wa shule za sekondari zaidi ya 10 katika Jimbo la Tarime.


“Shule za sekondari zaidi ya kumi zimejengwa katika kipindi cha miaka miwili ya ubunge wangu. Shule hizo ni pamoja na Itiryo, Bomani, Gibaso, Kenyamanyori, Muriba na Nyamwigura. Fedha zilizogharimia ujenzi huo zimetoka Mfuko wa Jimbo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime,” anasema mbunge huyo.


Ujenzi wa shule hizo unakwenda sambamba na mpango wa kuongeza idadi ya walimu na vifaa mbalimbali vinavyohitajika shuleni.


“Wakati nachaguliwa kuwa mbunge kila shule ilikuwa na wastani wa walimu watatu lakini kwa sasa kila shule ina wastani wa walimu tisa, haya siyo maendeleo ya kubeza katika kipindi cha miaka miwili pekee,” anasema na kudokeza kuwa amepata mfadhili aliyekubali kutoa msaada wa umeme wa sola katika shule za sekondari 31 zisizo na umeme jimboni.


Mbali ya uwezeshwaji kutoka serikalini na kwa wahisani mbalimbali, Nyangwine anaahidi kuendelea na utamaduni wake aliouanza mwaka 2000 wa kugawa msaada wa vitabu vyenye thamani ya Sh milioni 10 katika kila shule ya sekondari jimboni kila mwaka kuinua taaluma na kuwapunguzia wazazi na walezi mzigo wa gharama za masomo ya watoto wao.


Akizungumzia uamuzi wake wa kuzuia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara (NMGM) kuendelea kulipa ada za wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo mbalimbali, mbunge huyo anasema hatua hiyo inalenga kudhibiti ufisadi na kuwezesha wakazi wa jimbo hilo kunufaika na fedha hizo kwa usawa.


“Nimefuta mpango huo baada ya kuchunguza na kubaini fedha nyingi zilizokuwa zinatolewa na mgodi huo zilikuwa zinaishia kuwalipia ada watoto wa matajiri na kuwaacha wanaotoka familia maskini wakikosa elimu.


“Kwa mfano, niliambiwa wanafunzi wanaolipiwa ada kila mwaka ni 6,000 lakini nilipochunguza nilibaini kuwa wanaolipiwa ada ni 2,000.

Kumbe sehemu kubwa ya fedha zilizotolewa na mgodi huo ziliishia mifukoni mwa wajanja wachache.


“Badala yake niliomba fedha zote zinazotengwa na mgodi huo kila mwaka kwa ajili ya kulipa ada za wanafunzi zipelekwe katika mfuko wa halmashauri ya wilaya isimamie kuzigawa katika kila kijiji kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo ya wananchi ukiwamo mradi wa elimu,” anasema Nyangwine.


Anasema suala la elimu linapewa kipaumbele cha juu katika jimbo la Tarime kwa vile wananchi wengi wakielimika watajiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbalui, hivyo kuondokana na dhana ya utegemezi kwa kila kitu.


Kuhusu afya, Nyangwine anakiri kuwa bado sekta hiyo haijaboreshwa jimboni humo kutokana na vikwazo mbalimbali vikiwamo vitendo vya rushwa, ufinyu ya fungu la fedha kutoka serikalini, ukosefu wa wataalamu na vitendea kazi vya kutosha.


“Lakini kwa sasa ninashirikiana na viongozi wengine kuelekeza nguvu kubwa ya kushughulikia wafanyakazi wa idara ya afya wanaoendeleza vitendo vya rushwa na kudhoofisha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa,” anaahidi mbunge huyo.


Akizungumzia huduma ya maji, mbunge huyo anasema bado sekta hiyo nayo haijafanikiwa ipasavyo lakini kuna mkakati unaandaliwa kwa ushirikiano wa serikali na wahisani kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji safi na salama jimboni humo.


“Kwa upande wa barabara tumefanya vizuri, mwaka jana tulipata Sh bilioni 1.4 ambazo zilitumika kugharimia ujenzi wa barabara mpya na ukarabati wa barabara na mitaro katika maeneo ya mjini na vijijini. Lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya kujenga madaraja kadhaa,” anasema.


“Tumeanza kuelekeza nguvu kubwa pia katika suala la ulinzi wa amani ikiwa ni pamoja na kushughulikia majambazi na wachochezi wa mapigano ya kikoo. Amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya wananchi,” anasema.


Wiki hii mbunge huyo ataanza ziara nyingine ya siku saba ya kuhamasisha shughuli za maendeleo, kukagua miradi na kusikiliza kero za wananchi katika vijiji mbalimbali jimboni humo.


Anatoa wito kwa wakazi wa Jimbo la Tarime kuacha kulalamika, kujihusisha na siasa zisizo na tija, badala yake wajenge dhana ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

“Bado ninaendelea kuahidi kwamba nitajitahidi kuwatumikia wakazi wa Tarime kwa kiwango cha kuridhisha, hiyo ndiyo dhamira yangu,” anasema Nyangwine.

By Jamhuri