Hii ni hotuba iliyotolewa na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kwa wananchi waliompokea Mei 3, 2012 katika eneo la Kibara kwa ajili ya kumpongeza kwa ushujaa wake wa kuwashupalia mafisadi.

Ndugu zangu waheshimiwa sana waajiri wangu, wakati naelekea kusema machache juu ya risala yenu ya Jimbo la Mwibara, naomba kwanza mniruhusu niwashukuru kwa uamuzi wenu wa kuamua kuandaa mapokezi makubwa kama haya ambayo kwangu ni ya kihistoria.

Kikubwa zaidi, nimefarijika na uamuzi wenu na sasa nimeamini na kushuhudia kwamba mmenipokea kishujaa. Ushujaa huu ni kwa niaba yenu na hivyo mjue wana-Mwibara mmeibuka mashujaa machoni mwa Watanzania wenzenu juu ya vita ya kudumu dhidi ya ufisadi na mafisadi.

Aidha, nawashukuru kwa risala yenu nzuri na yenye kutaka maelezo juu ya nini kilijiri katika Mkutano wa Saba wa Bunge la Kumi, hususani kuibua vitendo vya kifisadi, wizi, matumizi mabaya ya fedha, ubadhirifu wa fedha na mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka, vilivyofanywa na baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi wa mashirika ya umma na halmashauri ndani ya TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).

Mimi nikiwa mwakilishi wenu, na ninyi kama waajiri wangu, mnayo sababu na haki kunitaka nitoe maelezo kwa mujibu wa risala yenu. Kwa kifupi sana na bila kumung’unya maneno ni kwamba kama baadhi yenu mlivyonitazama kwenye runinga, mlivyonisikiliza kupitia redio, na ama mlivyonisoma kwenye magazeti, au mtandao wa intaneti; nilifanya kile mlichonituma nifanye kile cha kutowaangusha, kutowatelekeza na kutowasaliti.

Aidha, nilihakikisha wakati wote wa mjadala juu ya ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na taarifa za mwaka za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma, naibua na kufichua ufisadi unaozuia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 kama tulivyoahidi kwa Watanzania.

Niliishauri Serikali yangu ya CCM iwawajibishe mawaziri wote walioguswa na ufisadi, na pia nilitia saini katika harakati za kuunga mkono hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo atakataa kumshauri Rais kuwawajibisha hao mawaziri.

Inatokana bahati mbaya ya Bunge kutokuwa na uwezo wala mamlaka kikatiba au kikanuni wa kuwawajibisha mawaziri, lakini njia pekee kwa Bunge kufanya hivyo ni kumwajibisha Waziri Mkuu ambapo pia, njia ni moja tu ya kikatiba ya kupiga kura ya kutokuwa na imani naye hata kama Bunge lina imani naye ili Waziri Mkuu aamue, ama abaki yeye kwenye madaraka au amshauri Rais kuwawajibisha mawaziri.

Ikumbukwe kwamba mawaziri, kwa mujibu wa Katiba, huteuliwa na Rais kwa kushauriwa na Waziri Mkuu. Na pia kura ya kutokuwa na imani na Rais si kuiangusha Serikali iliyoko madarakani, bali ni kumtaka Rais avunje na aunde Baraza jipya la Mawaziri. Na watu wasiojua Katiba kitendo hiki wanadai ni kuiangusha Serikali. La hasha!

Wakati nafanya yote haya niliongozwa na dhamira safi ya chama changu kinachohubiri na kusimamia misingi ya utawala bora, haki, usawa na utawala wa sheria katika kuwezesha na kujenga ustawi wa Taifa letu na maisha bora kwa Watanzania.

Lakini leo nizidi kuwakumbusha kuwa wakati wa kampeni niliwaombeni mnichague kwa sifa ya ujasiri, upendo, huruma, uchungu wa rasilimali za umma; na kwamba nitahakikisha kuwa fedha zinazotengwa kwenye bajeti kwa ajili ya maendeleo yenu zinawafikia bila kuchakachuliwa.

Inawezekana wapo waliodhani natania au nadanganya; la hasha! Leo mmenipokea kishujaa kama ishara ya kukiri kwamba maneno yangu nimeyasimamia bungeni na hakika sitarudi nyuma na ninyi pia endeleeni kuniunga mkono.

Aidha, namshukuru Rais wetu kwa kufanya matukio mawili ambayo yanathibitisha kwamba yuko pamoja na sisi wabunge, kwa yale tuliyoyafanya au kuyasema bungeni na kwamba tulikuwa sahihi.

Tukio la kwanza ni kuitisha Kamati Kuu ya CCM na kuwaeleza Watanzania juu ya namna alivyofurahishwa na michango ya wabunge juu ya taarifa za CAG na taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge, hususani suala la ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka.

Lakini hotuba yake ilikwenda mbali zaidi ya hapo na kuahidi kwamba atachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha wale wote walioguswa na taarifa za CAG na michango ya wabunge.

Aidha, tukio la pili ni katika hotuba yake aliyoitoa Mei Mosi, 2012 mjini Tanga na kuwaeleza Watanzania kuwa amefurahishwa na michango ya wabunge juu ya kuibua ufisadi ndani ya wizara, idara za Serikali, TAMISEMI na katika mashirika ya umma na kwamba siku si nyingi atachukua hatua ya kuwawajibisha wahusika.

Naomba nimalizie kwa kusema kwamba michango ya wabunge na hasa ya wabunge wa CCM na hata kutia kwangu saini kwa ajili ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, vililenga kuimarisha chama changu na serikali yake katika dhana nzima ya uwajibikaji.

Na pia nilisukumwa zaidi na kushuhudia kwamba jimboni kwangu wanafunzi wengi wanasoma wakiwa wamekaa chini, walimu hawatoshi, madarasa hayatoshi, nyumba za walimu hazitoshi na sekondari zote hazina maabara.

Pia nimeshuhudia shule zote za msingi na sekondari zikiwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia, vijiji vingi havina zahanati na pale palipo na zahanati kuna upungufu mkubwa wa dawa, waganga pamoja na wauguzi, miundombinu ya barabara ni mibovu sana, umasikini kwa ujumla umekithiri, wananchi wamekata tamaa katika kilimo na uvuvi vimekufa, na kadhalika.

Wakati haya yakiwasumbua wananchi, fedha za umma zinatafunwa na kikundi cha watu wachache (chumia tumbo).

Natoa wito kwa Mheshimiwa Rais asiishie kuwawajibisha tu wahusika, ni lazima pia wafikishwe mahakamani ikiwa ni pamoja na kufilisiwa mali zao walizozipata kwa njia ya kifisadi.

Na kwamba endapo atasita kufanya hivyo atasababisha idadi ya watu inayotafsiri kifupi cha CCM kuwa ni ‘Chama Cha Mafisadi’ izidi kuongezeka siku hadi siku.

Mimi kama kada mbunge wa CCM sipendi kama chama tuendelee kubezwa, kutaniwa na kudhihakiwa na watu kwa kupotosha ukweli wa tafsiri sahihi ya jina la chama chetu kwa sababu tu ya kuwakumbatia watu wachache wanaofanya ufisadi ambao si sera ya CCM na wala si malengo wala madhumuni kwa mujibu wa Katiba ya chama chetu.

Ndugu wana-Mwibara wenzangu, asanteni sana kwa kunipokea kishujaa na kwaherini nyote.

1217 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!