Makomredi Khamis Kagasheki na Lazaro Nyalandu; Salaam. Mlipoteuliwa kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii wapo waliowapongeza. Mimi nilisita kuwapongeza.

Nilisita kwa sababu nilidhani kwa ugumu wa wizara mliyokabidhiwa msingeukubali uteuzi huo, lakini mmeukubali. Kwa sababu hiyo, nawapongeza. Nawapongeza si kwa kuteuliwa bali kwa kuukubali uteuzi huu wenye changamoto nyingi.

Nawapongeza kwa sababu mmekubali kuingia kwenye ‘mashindano’ ya kumpata waziri na naibu waziri anayeweza kudumu kwa muda mrefu kwenye wizara hiyo katika Awamu hii ya Nne.

Tangu mwaka 2005 tumekuwa na Anthony Diallo, Profesa Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga na Ezekiel Maige. Sasa Komredi Kagasheki ni wa tano ndani ya miaka saba. Kadhalika, kumekuwapo naibu mawaziri wawili. Makatibu wakuu ndani ya kipindi hicho ni Saleh Pamba, Blandina Nyoni, Dk. Ladislaus Komba na sasa yupo Maimuna Tarishi.

Idara ya Wanyamapori yenye ukwasi mkubwa, imekuwa na wakurugenzi watatu ndani ya kipindi cha miaka sita. Wakurugenzi hao ni Emmanuel Severe, Erasmus Tarimo na Obeid Mbangwa aliyesimamishwa kazi.

Ndugu zangu, kuwapo kwa mabadiliko haya makubwa ya viongozi ndani ya kipindi kifupi namna hii, kunathibitisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ina siri nzito. Si ngumu kuiongoza bali ina vishawishi vingi sana vinavyowafanya wanaoiongoza – hasa kwenye Idara ya Wanyamapori – wakose uzalendo, wakose uvumilivu na kujikuta wakiingia kwenye mtego wa ubadhirifu.

Ndugu zangu Kagasheki na Nyalandu, kwa karibu muongo mmoja nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mno habari zilizofichika ndani ya wizara hii. Nimeibua mambo mengi. Nimeshiriki kwenye mapambano kuhakikisha bei za nyara zinapanda kwa sababu hapo awali Tanzania ndiyo tuliokuwa tukilipwa fedha chache sana kwa biashara ya tembo, simba na wanyamapori wengine.

Nimeshiriki mapambano ya kuhakikisha bei za vitalu zinapanda, na tena vitalu vinawekwa kwenye madaraja. Badala ya Serikali kuambulia ada ya dola 5,000, kiasi hicho hatimaye kimepanda hadi dola 60,000 za Kimarekani kwa mwaka. Hii ni hatua kubwa.

Kwa kushirikiana na wadau wengine, tumeongoza mapambano ya kuwa na sheria na kanuni mpya za wanyamapori. Kwa juhudi hizo, tumeweza kupata Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2010. Sheria hiyo imewatambua Watanzania kuwa ndiyo wenye rasilimali hii, na kwa sababu hiyo lazima wawe wa kwanza kuifaidi kwa kiwango kinachostahili.

Ndugu zangu mawaziri, kwa miaka mingi tasnia ya uwindaji wa kitalii imehodhiwa na wageni. Haikushangaza kumuona mgeni mmoja, Gerald Pasanisi pamoja na familia yake, wakimiliki vitalu ambavyo kwa pamoja ukubwa wake ni sawa na nchi ya Djibouti! Pamoja na sheria mpya, ameendeleza mbinu hizo na kufanikiwa kujitwalia vitalu vinono karibu 20.

Yeye na wenzake kwa kutambua kuwa sheria mpya itawabana, wakaamua kuanzisha kampuni nyingine mpya kwa msaada mkubwa wa mawakala wao Watanzania.

Kwa miaka yote nimeshiriki mapambano haya kwa kusukumwa na uzalendo kwa taifa langu na wananchi wenzangu ambao ni masikini ndani ya bahari kubwa ya utajiri. Uzalendo huu umenifanya wakati mwingine nikabiliane na mazingira magumu yakiwamo hata ya kuhatarisha maisha yangu.

Kwa sasa nimo mbioni kukamilisha kitabu kinachoeleza safari yangu ya muongo mmoja wa mapambano ya kuifanya rasilimali ya wanyamapori iwanufaishe Watanzania.

Tasnia ya uwindaji wa kitalii ina utajiri mkubwa sana. Wakati sisi tukiendelea na kelele za wizi wa fedha za EPA, au kuhangaika na wakwepa ushuru magengeni, Wazungu kwa kushirikiana na mawakala wao Watanzania wanaitafuna nchi hii kupitia tasnia ya uwindaji wa kitalii.

Wanaifaidi kweli kweli kupitia utalii wa picha ambao sasa wanauendesha kwenye maeneo ambayo hakuna mtumishi wa serikali anayekusanya maduhuli. Mfano mzuri ni wa kule Kreins Camp!

Ndugu zangu mawaziri, mapambano bado yanaendelea. Hayatakoma. Msidhani kuwa baada ya kuondoka kwa Maige, mambo yamemalizika. Mambo bado. Tena basi, kwa kuanzia anzeni na hili la ugawaji maeneo ya uwindaji katika WMA. Taarifa za uhakika ni kwamba tayari kampuni kadhaa zimeshapewa maeneo hata kabla ya matangazo kutolewa magazetini! Anzeni na hilo.

Ndugu zangu, kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii kama nilivyosema hapo awali, si jambo gumu la kuhitaji muujiza. Wizara hii pamoja na kuwapo majungu mengi, ina vishawishi vya utajiri vilivyovuka mipaka. Kuna wahongaji wazuri sana, tena walio radhi kuwafungulia akaunti ughaibuni. Wapo watakaowafuata ili mkakutane Marekani, Uhispania, Ufaransa na kwingineko.

Huko mtakabidhiwa fedha nyingi, na kama itaonekana kuzibeba haiwezekani, mtafunguliwa akaunti huko huko. Hili nawaambieni mapema mkae mkijua.

Ndugu zangu mawaziri, tayari mawakala wa Wazungu wameshakaa mkao kama wa tai anayevizia mawindo ya simba! Mlipotangazwa tu kushika nafasi hizo, wapo waliofanya sherehe. Wapo waliorukaruka wakiamini kuwa sasa mambo yao yatanyooka. Na kweli, tayari kati yenu yupo aliyekwishakutana na magwiji wa ushawishi kwa faragha! Amekutana nao kama njia ya kupokea pongezi, lakini ukweli ni kwamba kinachoendelea ni kuandaa ulimbo ili mnaswe kwenye mtego.

Mapambano ya vitalu hayajakoma. Sasa kuna mkakati mkubwa wa kuhakikisha ugawaji vitalu unarejewa. Yote haya yanafanywa ili wale waliokosa waweze kuvipata. Kibaya zaidi, wanaoendesha mpango huu ni Watanzania wanaojifanya wazalendo kweli kweli, kumbe ni mawakala wa wageni.

Kuna vitalu katika eneo la Maswa ambavyo mawakala wako tayari kuwahonga hata dola milioni moja ili wapate eneo hilo nono. Nadhani mmeshapata vuguvugu hilo, na kama bado, basi subirini mtasikia na mtaona mafungu ya fedha na ahadi zisizo kifani.

Ndugu zangu mawaziri, salamu hizi nawapa mapema ili hapo baadaye tusije tukaonana wabaya. Tupo tuliodhamiria kuona kuwa Tanzania inabaki kuwa ya Watanzania.

Ndani ya wizara yenu kuna wazalendo wa kweli ambao daima tumeshirikiana katika kupeana habari na kisha kuzifikisha kwenye hadhira; na ndiyo maana hapajawahi kuwapo habari yoyote ya vitalu ikaandikwa kisha ikakanushwa! Wazalendo wanaoipenda Tanzania wapo nje ya wizara pia. Hawa tumekuwa nao bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa utajiri wa Tanzania unawanufaisha Watanzania.

Mkiongoza wizara hii kwa uwazi na kwa kuzingatia haki, mtaona mambo yakienda barabara. Mkianza kuwa wasiri, warasimu, wabezaji na msiokuwa tayari kupokea ushauri kutoka kwa wadau walio ndani au tulio nje ya wizara, haitashangaza kuona kuwa safari yenu ya kuiongoza wizara hii inakuwa ya misukosuko mikubwa. Jaribuni kuonyesha mfano wa uongozi unaozingatia uadilifu na masilahi ya Watanzania.

Utajiri wa wizara hii pekee unatosha kabisa kuyabadili maisha ya Watanzania kuwa bora kuliko ilivyo sasa. Kinachotakiwa ni dhamira na uongozi makini.

Mwisho, nirejee tena kuwapongeza kwa kuukubali mzigo huu wa kuiongoza wizara yenye changamoto nyingi. Ninachowaahidi kutoka kwangu ni ushirikiano wa dhati.

Lakini mtambue kuwa mpaka wa urafiki wetu unalindwa na masilahi ya Watanzania. Mtakapopuuza masilahi hayo ni wazi kuwa tutaonana wabaya. Karibuni. Mkiyumba tu mjue wanahabari hawatanyamaza.

Mungu awabariki sana.

1367 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!