Mada hii inazidi kunoga. Inanoga kwa maana kwamba kila ninapojiandaa kuandika sehemu inayofuata linajitokeza jambo linalonisukuma kuanza nalo. Wiki hii si jingine bali ni jinsi Bunge lilivyojidhihirisha kuwa na nguvu ya pekee.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, wakati amesimama bungeni na kusema zinahitajika saini 70 tu kumwajibisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda wapo walioona anajifurahisha.

Kwa mshituko wa chama tawala CCM, saini 70 zilipatikana ndani ya saa tano tu na kati yake walikuwamo wabunge wa CCM waliosaini haraka. Hii ilimaanisha nini? Hii ilimaanisha utayari wa wabunge hawa kumwondoa Waziri Mkuu madarakani, na kwa hiyo kuilazimu Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete kuvunja tena Baraza la Mawaziri.

Wapo waliosema hili lisingewezekana, hawa walikuwa wanajidanganya. Hili lilikuwa takwa la kisheria na kikatiba. Baada ya saini hizo kupatikana katika Bunge lijalo la Juni, Spika angepewa taarifa ndani ya siku 14 na mjadala ungeendeshwa ndani ya Bunge, na si hilo tu, bali zingepigwa kura za siri.

Hapa zilihitajika kura 176 tu, kumwondoa Waziri Mkuu na hatimaye Baraza lote liondoke. Kumbuka kasheshe yote imeanzishwa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hili Rais Kikwete ameliona. Amejua kuwa ndani ya wabunge hao hao wa CCM wapo wanaotamani uwaziri. Hawa wangeweza kufanya kampeni usiku kucha na hivyo wangewezesha upatikanaji wa idadi hiyo ya kura. Wapo wenye makundi yao ya urais mwaka 2015 wangeweza kuendesha kampeni na ikafanikiwa.

Ni kwa mantiki hiyo kulikuwa hakuna jinsi isipokuwa akina Mustafa Mkulo kuondoka. Hili sasa limeniibulia hoja niliyokuwa nikiifikiria na kutaka iingizwe katika Katiba mpya.

Kwamba mawaziri wasiwe wabunge. Hawa wateuliwe kwa taaluma zao, kisha wakathibitishwe bungeni, na hivyo ikitokea kwamba kuna waziri aliyebofoa, basi Bunge litampigia yeye tu kura ya kutokuwa na imani na ataondoka ili apatikane mwingine badala ya hatari ya kuvunja Serikali yote.

Hii itawafanya mawaziri kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anatenda kwa mujibu wa ahadi zake kwa Watanzania kupitia bungeni. Niliwahi kuliandika hili kwamba Bunge letu linatumia mfumo wa uwakilishi. Kama ingewezekana tulipaswa leo Watanzania wote kwenda bungeni kutoa mawazo yetu. Wananchi ndiyo mabosi wa Rais kupitia kura zetu.

Ndiyo mantiki inayokuja kuwa kwa vile tunakabidhi mamlaka yetu kwa njia ya uwakilishi kwa wabunge, basi Serikali yote inawajibika kwetu wananchi kupitia bungeni. Hii ndiyo inayowapa wabunge nguvu ya kuishauri na kuisimamia Serikali. Zitto kwa mara nyingine amethibitisha nguvu ya Bunge kuisimamia Serikali baada ya Buzwagi. Mawaziri sita sasa out.

Wiki iliyopita katika sehemu ya tatu, nilisema kwenye makala haya yanayotaka kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika, kuwa wapo wanaojiuliza mapato ya kitaifa yatakuwaje. Leo napenda kulijibu swali hili na pia nilihusishe na ujenzi wa miundombinu. Moja tutaandaa na kuandika kanuni inayohusu ukusanyaji na mgawanyo wa mapato kitaifa.

Bila kujali ukubwa au udogo wa jimbo husika kati ya Serikali za majimbo niliyopendekeza chini ya Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar, itakuwa ni shuruti kwa kila Jimbo kuchangia asilimia 25 ya mapato pake kwenye mfuko mkuu wa Hazina ya Tanzania (Consolidated Fund).

Ile asilimia 75 inayobaki itumike katika shughuli za maendeleo na matumizi ya kawaida ya Jimbo. Misaada ya kimataifa nayo igawanywe kwenye majimbo kwa kufuata misingi ya ukubwa wa Jimbo na idadi ya watu.

Kwa kuwa Serikali ya Tanzania itakuwa ndogo na ina mawaziri na watendaji wachache, hiyo asilimia 25 itakayotoka kwenye kila Jimbo, italifanya taifa kuwa na uwezo mkubwa kifedha. Madeni yaliyokopwa kabla nayo yapigiwe hesabu na kurejeshwa kwa kiwango cha asilimia kutoka kila Jimbo bila kubaguana, ila kwa miradi mipya majimbo yakikopa yalipe yenyewe bila kuwabebesha mzigo wengine.

Iwe sheria kuwa kila Jimbo litawajibika kutunza na kuhifadhi barabara kuu zinazopita katika jimbo husika kwa kiwango cha lami, Jimbo litahudumia miundombinu ya kitaifa kama maji, umeme na mingine inayokatiza katika jimbo husika kutoka mwanzo wake hadi mpaka wa Jimbo.

Nafahamu hapa zitaibuka hoja dhaifu kuwa kuna mikoa au majimbo yasiyo na rasilimali za asili hivyo kwayo itayawia vigumu kujiendesha. Hapa ndipo ulipolala uongo wa kuchongwa.

Kwa nchi kama Afrika Kusini, Jimbo la Gauteng makao yake makuu ni Johannesburg. Hili ndilo Jimbo ambalo awali lilikuwa na utajiri mkubwa, lakini baadaye majimbo kama Kwa Zulu-Natal yakaamua kuwekeza katika uvuvi na wakapata utajiri mkubwa.

Ni kwa mantiki hiyo, hoja kwamba Jimbo la Kanda ya Ziwa lina madini, Kanda ya Kaskazini lina utalii ikiwamo Mlima Kilimanjaro au Kanda ya Nyanda za Juu Kusini lina chakula kingi hivyo majimbo mengine yatakufa njaa, ni hoja dhaifu. Kwa kulifahamu hilo, kudai kuwa Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida watakufa njaa kwa vile wanategemea ruzuku ya Serikali, hapo ndipo tunapopaswa kunoa bongo zetu.

Kwanza imebainika sasa kuwa mikoa kama Dodoma na Singida kilimo cha alizeti na karanga kinakubali kwa kiasi kikubwa. Kama nchi ya Malaysia wanaishi kwa kuuza mafuta ya mawese, itakuwaje wakubwa hawa wa Singida wakiamua kulima alizeti katika maeneo yote zinakostawi!

Hapa watauza mafuta hadi Rwanda, Budundi, DRC, Uganda, Kenya, Asia, Ulaya na Marekani na hasa ikitiliwa maanani kuwa mafuta ya alizeti yanavyosifiwa kwa ubora, watapata fedha hadi watoe misaada kwa Marekani. Hapa tutakuta tunakuza ajira ghafla.

Kila jimbo litakuwa linafanya kazi na kutimiza msemo wa ‘asiyefanya kazi na asile’. Uzalishaji utakuwapo na ajira zitakuwa nyingi hivyo shida tutazitupa mkono. Kwa yale majimbo yatakayochechemea katika kipindi cha mpito, yatapata fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina. Ruzuku itatoka moja kwa moja Serikali Kuu na kwenda kwenye majimbo haya.

Njia kuu za uchumi zitakuwa mikononi mwa wananchi, kitakachobaki ni kuboresha miundombinu na kusimamia kwa karibu miradi ya maendeleo kisha kwa kuwa wakuu wa majimbo watakuwa viongozi wa kuchaguliwa na wana hofu kuwa wasipotenda sawa na ahadi zao watang’olewa madarakani, sioni kwa nini wananchi hawa wasifanikiwe kwa kiasi kikubwa. Kiongozi atakayeshindwa anaondolewa bila aibu.

Hili nilirudie. Ukubwa wa nchi yetu nacho ni kikwazo cha maendeleo ya haraka. Nchi inajiendesha bila usimamizi wa karibu. Maendeleo hayaji au kazi hazitendeki pasipo usimamizi wa karibu.

Makala iliyopita nilitoa mfano wa nchi kama Rwanda kuwa Rais Paul Kagame anaweza kuitembelea Rwanda yote asubuhi hadi jioni, tena kwa kutumia gari akarejea na kulala nyumbani kwake. Ni rahisi mno kusimamia vyema eneo la kiutawala likiwa dogo.

Najua litakuja swali la umoja wa kitaifa, utaifa wetu na mshikamano. Hili nalo lisikupe hofu. Nitalijibu katika makala yajayo na baada ya hapo nitaanza kuizungumzia Katiba yenyewe itakayorejesha Serikali ya Tanganyika ikaenda sambamba na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nitajadili Katiba iwe ya aina gani kuepusha utaratibu wa sasa ambao bila kujua tunamwingiza mfalme madarakani (si Rais) kupitia sanduku la kura.

Katiba ya sasa inampa Rais nguvu kubwa ajabu. Rais ni kila kitu. Rais ni mwanzo na mwisho. Kwa Katiba tuliyonayo anaweza akaamuru mtu afungwe na akapelekwa gerezani bila kupitia mahakamani. Je, tutafikaje huko? Usikose toleo la wiki ijayo.

1220 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!