Pengo lililoachwa na mshambuliaji mahiri wa kikosi cha Simba, Emmanuel Okwi, limewanyong’onyesha mashabiki kiasi cha kupungukia matumaini ya kuona timu hiyo ikifanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania Bara, msimu huu.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo ulioanza Jumamosi iliyopita ni hatua ya mwisho ya kumpata bingwa wa ligi hiyo ambayo hadi sasa inaongozwa na kikosi cha Yanga, lakini linaweza kutokea lolote hasa kwa vile hadi sasa kila timu imebakiza mechi 12 ambazo zinatosha kubadili matokeo ya sasa.


Simba imemuuza Okwi hivi karibuni kwenda klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa kitita cha dola 300,000 [sawa na Sh milioni 480].


“Ikumbukwe kwamba Okwi alinunuliwa na Simba kwa tahamni ya dola 20,000 [Sh milioni 32] miaka mine iliyopita.


Kumuuza kwa dola 300,000 maana yake ni kwamba Simba imepata faida mara 15 ya gharama ilizotumia kumnunulia,” ameeleza Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga.


Mashabiki wa Simba wanaamini kwamba Okwi alikuwa na nafasi kubwa ya kusaidiana na wengine kuipaisha timu hiyo katika mzunguko wa mwisho wa ligi hiyo.


Mbali na ujuzi wa kuzifumania nyavu za timu pinzani dimbani, Okwi alikuwa akiwezesha wenzake wakiwamo Felix Sunzu, Amri Kiemba na wengineo kupachika mabao baada ya kupasua ngome za mabeki na kugawa pasi za mwisho.


Hata hivyo, Kamwaga anawatoa wasiwasi wanaodhani timu yao hiyo itayumba akisema hivi sasa ina kocha mtaalamu, Patrick Liewig, hivyo wote wategemee kupata mafanikio katika ligi hiyo.

inaelezwa kuwa Liewig ana utaalamu wa kutosha wa kufundisha kandanda na kuwajenga wachezaji wengine watakaofanana na Okwi, hasa wenye umri mdogo na kuingia kikosi cha kwanza.

1027 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!