Olduvai: Bustani ya ‘Eden’

Julai 17, 1959 Mary Leakey aligundua fuvu katika eneo linaloitwa FLK-zinj katika Bonde la Olduvai, Ngorongoro mkoani Arusha. Lilikuwa fuvu la zamadamu wa jamii ngeni, hivyo yeye na mume wake Louis Leakey waliita Zinjanthropus boisei.

Hapa ndipo mahali kunakotambulika duniani kote kuwa ndiko kwenye asili ya binadamu. Kutoka hapa binadamu walisambaa katika sayari yote ya dunia. Mamia kwa mamia ya wanasayansi watafiti wa mambo kale humiminika Olduvai kila mwaka kufanya utafiti na ugunduzi wa masalia ya binadamu na wanyama wa kale – miaka milioni kadhaa iliyopita.

Mwaka huu Tanzania na ulimwengu wa wataalamu wa mambo kale wanaadhimisha miaka 60 tangu kuvumbuliwa kwa fuvu la binadamu wa kale zaidi duniani, yaani Zinj. Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na wadau mbalimbali wameanza maandalizi ya kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika baadaye mwaka huu. MWANDISHI WETU anaeleza historia ya Zinj. Endelea…

Mwaka 1911 mtaalamu wa Kijerumani aitwaye Wilhelm Kattwinkel alifika katika Bonde la Olduvai akiwa katika safari ya utafiti kuhusu mbung’o na ugonjwa wa malale.

Aliokota visukuku vichache na kwenda navyo Ujerumani na kumuonyesha mtaalamu wa jiolojia, Hans Reck, naye akafanya safari ya kitafiti katika bonde hilo mwaka 1913.

Visukuku (fossils) zaidi ya 1,700 vilikusanywa mwaka huo pamoja na kunyambulishwa kwa matabaka ya miamba yanayofanya bonde hili. Baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, Tanganyika ilikoma kuwa koloni la Mjerumani na kuwa chini ya uangalizi/usimamizi wa Uingereza. Mwaka 1931, Louis Leakey ambaye ni mtaalamu wa malikale wa Kiingereza alimsindikiza Hans Reck katika safari yake ya kwanza ya kitafiti Olduvai baada ya kumtembelea Reck mwaka 1928 huko Ujerumani na kuona baadhi ya visukuku vilivyotoka Olduvai.

Louis Leakey alirudi Olduvai mwaka 1932 akiwa na mtaalamu wa miamba, E. Wayland. Mwaka 1934 Leakey alibainisha awamu ya kwanza ya muhula wa mawe na kuuita Oldowan ukachapishwa mwaka 1936.

Mwaka 1935 Leakey aliokota kipande cha fuvu dogo la zamadamu katika eneo la MNK na kuliita eneo hilo Mary Nikol Korongo, mwanamke aliyefuatana naye katika utafiti huo.

Mwaka uliofuata alimwoa mwanamke huyo, ndiye Mary Leakey. Wawili hao waliendesha safari kadhaa za kitafiti katika Bonde la Olduvai, mwaka 1941, 1953, 1955 na 1957. Miaka kati ya 1940 na 1960 ilikuwa ya kitafiti katika bonde hili wakikagua bonde lote na kubainisha idadi kubwa ya maeneo ya akiolojia na paleontolojia. Awali, mwaka 1935 waligundua eneo la BK na kulifanya eneo lenyewe onyesho la nje kutokana na wingi wa masalia yaliyokuwapo. Kati ya mwaka 1951 na 1957 walichimba eneo la BK na SHK ambalo ni tabaka la pili.

Mwaka 1959 familia ya Leakey walielekeza nguvu katika tabaka la kwanza baada ya kugundua meno matatu ya zamadamu katika eneo la MK. Baada ya kuchimba mita zaidi ya 8 ya jivu la volkano waliamua kumsubiri mpiga picha, Des Barlett, ndicho kipindi Mary Leakey alipoona katika eneo la FLK karibu na kambi, masalia ya Zinjanthropus (OH5) ajulikanae sasa kama Paranthropus boisei.

Ugunduzi huu ulibadilisha kwa kiasi kikubwa mwenendo wa utafiti katika Bonde la Olduvai. Ufadhili kutoka taasisi mbalimbali uliwezesha tafiti za muda mrefu na uchimbuzi mkubwa ambao kwa miaka 10 uligundua maeneo ya akiolojia muhimu zaidi ulimwenguni.

Maeneo kama FLK Zinj, FLK North North na DK yalichimbuliwa kwa kiwango kikubwa ambacho hakijaweza kufikiwa kwa sasa. Madirisha haya ya kuchungulia nyakati za awali yaliwezesha kueleza namna tofauti za tabia za binadamu wa kale.

Baada ya Mary Leakey hakuna tafiti nyingine zilizoendelea katika maeneo haya ya kale. Mwaka 1989, mradi wa OLAP chini ya Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani waliendesha utafiti wa miaka 20 katika ukanda wa chini wa tabaka la pili.

Mwaka 2006 mradi wa TOPPP uliendeleza utafiti katika tabaka la kwanza na la pili kwa kuchimba eneo la FLK Zinj, FLK North na FLK North North.

Mradi wa TOPPP ulichimba pia maeneo ya BK na SHK na kukusanya maelfu ya visukuku vya zana za mawe, vikiwa ni ushahidi wa kale zaidi wa uwindaji wa wanyama wakubwa wa hadi kilogramu 1,000 [tani moja].

Hivi karibuni maeneo mapya mawili yaligunduliwa katika tabaka la kwanza na kupewa majina ya Philip Tobias Korongo (PTK) na Amin Mturi Korongo (AMK) kwa heshima ya wataalamu hao wa malikale. Maeneo haya yametoa masalia kadhaa ya zamadamu na PTK imetoa msongamano mkubwa wa visukuku katika tabala la kwanza. Bado utafiti unaendelea.

 

Hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu

Takriban miaka milioni 2.6 iliyopita, zana za kale zaidi za mawe zinaanza kuonekana katika kumbukumbu za mabadiliko ya binadamu. Zilianza kuonekana huko Gona, Ethiopia.

Ubunifu huu katika historia ya chimbuko la binadamu uliambatana na utengenezaji wa nafasi maalumu katika mandhari mahali walipofanyia shughuli muhimu zaidi kama vile kutengeneza zana na kuchinja wanyama. Huu bado ni ushahidi wa kale zaidi wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu.

Kiwango cha akili iliyohitajika kutengeneza zana na kuzitumia kwa namna zamadamu hawa walivyofanya ilihitaji ubongo uliopanuka kuzidi waliotangulia ambao ubongo wao ulikuwa karibu sawa na wa sokwe.

Kipindi kifupi baadaye mabaki ya mwanzo kabisa ya zamadamu wenye ubongo mkubwa na meno madogo yalianza kuonekana. Uchache wa kumbukumbu za masalia ya kipindi cha kati ya miaka milioni 2.5 hadi milioni 2 haujawezesha kunyambulisha hatua muhimu za mabadiliko katika kipindi hiki muhimu cha mabadiliko ya binadamu.

Baada ya miaka milioni 2 iliyopita, tunapata ushahidi ulio wazi wa zamadamu hawa wanaopewa kipaumbele zaidi unaoonyesha sura za mabadiliko haya kama vile kuongezeka kwa umbo, kupungua kwa tofauti za ukubwa kijinsia, ubongo mkubwa kuliko ule wa zamadamu waliotangulia miaka milioni 4 zilizopita na kuchelewa kwa dalili za kukomaa. Hawa viumbe jamii ya Homo ndio mababu wa moja kwa moja wa binadamu wa sasa.

Maeneo ya malikale ya wakati huu yana utajiri mkubwa wa habari zinazowezesha wanaakiolojia kujenga mtiririko wa tabia za zamadamu wa mwanzo wa jamii yetu.

Tunachoona sasa kupitia madirisha haya ya kuangalia zamani ni viumbe wenye uwezo wa akili ya kushangaza, mwanzo wa binadamu. Huu ni wakati ambao zamadamu walibuni tabia tulizonazo. Utafiti katika maeneo ya tabaka la kwanza/la chini katika Bonde la Olduvai yameonyesha mwanga muhimu katika kuelewa hatua hii na kuiunganisha na ulaji wa nyama, kugawana chakula na ushirikiano wa vikundi. Kinachosisimua hapa ni hadithi ya jinsi tulivyoanza kuwa binadamu.

 

Mandhari ya Olduvai wakati wa tabaka la kwanza

Hali ya mazingira katika tabaka la kwanza la Bonde la Olduvai yanaashiria misitu iliyozunguka ziwa. Kufikia miaka milioni 1.85 iliyopita nyakati za katikati ya tabaka la kwanza, mandhari ilibadilika na kuwa mwingiliano wa misitu na uwanda wa nyasi unaolizunguka ziwa.

FLK Zinj ilikuwa kwenye mwinuko wa ukingo wa kusini mwa ziwa lililopokea maji ya mvua. Uwepo wa mwendelezo wa nyika karibu na ziwa unaashiriwa na uwepo wa wanyama wakubwa na wadogo pamoja na viashiria vya aina mbalimbali za miti.

Tathmini ya masalia ya mifupa ya miguu ya jamii za wanyama zaonyesha wengi wa aina ya swala, dalili za mandhari mchanganyiko nyakati za kati za tabaka la kwanza kama ilivyo hivi sasa, kuliko uwanda wa nyasi.

Tafiti za mabaki ya vichwa vya aina hii ya wanyama pia vilionyesha ulaji wa mchanganyiko wa nyasi na majani laini ya nyika. Wanyama jamii ya ‘tohe’ wa tabaka la kwanza la Olduvai ambao ndio wanaoongoza kwa idadi katika eneo hili la FLK Zinj, waonyesha kuwa na umbile la miguu tofauti na jamii ya sasa. Wanaonyesha kuwa sehemu ya chini ya miguu yao ni mirefu kuliko ya juu, dalili za kuzoea kuishi mazingira tambarare yenye majimaji na kingo za nyika. Dalili hizi pia zinathibitishwa na uwepo wa aina ya majani laini, miti na vichaka kama inavyoonyeshwa na masalia na viashiria vyake katika mabaki ya udongo wa wakati huo.

Utafiti wa karibuni waonyesha kuwa FLK Zinj ilikuwa mita chache (mita 200) kutoka chanzo cha kudumu cha maji kilichowezesha uwepo wa uwanda wa miti na vichaka kuzunguka eneo hilo.

Ukanda wa juu wa tabaka la kwanza unanukuu mazingira yasiyo na mvua za kutosha, mandhari ikibadilika kuwa uwanda wa wazi ambao ni dalili za kipindi kirefu cha ukame kilichotawaliwa na mandhari ya nyasi fupi zinazotawala nyakati za tabaka la pili. Hiki pia ndicho kipindi cha zamadamu jamii ya Homo erectus waliotokana na kina Homo habilis wanaopatikana katika tabaka la kwanza.

Usikose kusoma maelezo ya magwiji wa mambo kale – Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla; Profesa Charles Musiba kutoka Chuo Kikuu cha Colorado, Marekani; Dk. Noel Lwoga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Dk. Agness Gidna kutoka Makumbusho ya Taifa na Mhandisi Joshua Mwankunda kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).