Watu ni mtaji

 

Siku, wiki, miezi, miaka vinapita mbele yangu mimi kwanini nisimshukuru Mungu kwa kunilinda vyema? Nasema asante Mungu kwa zawadi ya Maisha.

Naandika makala hii nikiwa na furaha sana kwa kufikisha mwaka mwingine. Ni furaha iliyoje. Asante Mungu kwa mara nyingine. Wanasema kushukuru ni kuomba tena.

Tangu zamani ndoto yangu ilikuwa ni kuandika vitabu na kuwahamasisha watu. Nilitamani niandike makala kwenye gazeti. Haya yote leo yamewezekana.

Nipende kukutia moyo mpendwa msomaji ya kwamba ndoto yako inaweza kuwa kweli. Jambo kubwa ni uvumilivu, kufanya kazi kwa bidii na kumtanguliza Mungu daima.

Ipo sababu kwanini unaendelea kuishi na bado unapumua. Kila mmoja wetu ana sababu ya kuwepo humu duniani. Kila mmoja wetu ameumbwa kwa sababu maalumu.

Ndoto yangu ni kuwafikia watu wengi kupitia maandishi na kugusamaisha yao. Natamani siku moja watu wengi waseme, “Kwa sababu yako sikukata tamaa.” Najua sio kazi rahisi, lakini inawezekana.

Inawezekana umekata tamaa na unafikiri kwamba maisha yako hayana thamani tena.

Nikukumbushe pia kwamba “Mungu hawezi kukuacha njiani, safari yako aliianzisha mwenyewe, asingetaka angekuacha mwanzoni, unakokwenda yeye anajua,” kama alivyoimba Paul Clement katika wimbo wake uitwao Mwaminifu.

Baada ya kusema hayo, tuendelee sasa na nina ndoto. Kama kuna kitu ambacho unahitaji kukijenga kwa nguvu zako zote ni uhusiano mzuri na watu. Watu ni mtaji.

Mara nyingi utasikia watu wakilalamika kuwa hawana mtaji kwa maana ya pesa, lakini wamesahau mtaji sio pesa tu. Kama umekuwa ukinifuatilia vizuri huko nyuma niliwahi kusemakwamba kipaji ni mtaji.

Nataka nikuoneshe vile vitu ambavyo unavipuuzia, lakini vina thamani kubwa kwenye maisha yako. Usifikirie tu mtaji wa fedha, fikiria zaidi ya hapo, watu ni mtaji rafiki yangu.

Inawezekana unakosa pesa za kutimiza ndoto zako, lakini kuna mtu anazo na anaweza kukusaidia, lakini kwa kukosa uhusiano mzuri na watu utakosa pesa hizo.

Inawezekana kuna mtu ana fursa ya kuweza kukufikisha mbali lakini kwa sababu wewe si mtu unayezingatia uhusiano mzuri na watu utajikuta unakosa fursa hiyo.

Jaribu kufikiria kama kuna kitu unaweza kukifanya bila watu. Jibu lipo wazi – hakuna kitu kama hicho. Kumbe basi unahitaji watu kufanikisha ndoto zako. Jenga uhusiano mzuri na watu.

Ukivuruga kwenye uhusiano utakwama. Inawezekana una kitu kikubwa ndani yako lakini kwa sababu uhusiano wako  na jamii inayokuzunguka si mzuri watu wa jamii yako hawawezi kupokea kitu ulichonacho.

Binafsi niweke wazi kuwa nimefanikisha mambo yangu mengi kwa kuwa na uhusiano mzuri na watu.

Uhusiano mzuri aliojenga Yusufu akiwa gerezani ndiyo ulimfanya atoke gerezani na kuwa waziri mkuu.

Wasaidie wengine katika mambo yao nao watakusaidia katika mambo yako. Hiki ndicho alichokifanya Yusufu. Aliwasaidia wafungwa wenzake kutafsiri ndoto zao.

Wakati akimtafsiria mmoja wao wakiwa wamefungwa gerezani alimwambia, “Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba ukanitaje kwa Farao na kunitoa katika nyumba hii.” (Mwanzo 40:14).

Yusufu akiwa gerezani alikuwa mtu wa watu na anayeonekana kuwa kiongozi, pamoja na kuwa mfungwa, mkuu wa askari alimfanya awe kiongozi wa wafungwa, ukiwa katika taasisi za kiaskari tunaweza kusema Yusufu alikula kitengo. Nakumbuka nikiwa katika mafunzo ya JKT pale Msange-Tabora tuliambiwa, “Jeshini sifa kitengo.”

Kama huamini katika uhusiano mzuri tazama gari lililopata pancha au gari lililochomoka tairi likiwa katika mwendo kasi. Ajali inayoweza kutokea hapo si ya kufikirika au kama ajali haitatokea, basi gari hilo haliwezi kuendelea na safari.

Maisha hayategemei ni kitu gani unakijua. Maisha yanategemea unawajua watu wangapi na ni wangapi wanakujua. Kama watu hawakujui utatumia nguvu nyingi kufanikiwa. Siri ni moja ukitaka watu wakujue tengeneza uhusiano mzuri na watu.

Unapokutana na watu kuwa mkarimu kwao. Unayekutana naye leo hii huwezijua kesho na keshokutwa mtakutana wapi. Wasaidie watu kutatua changamoto zao nao watakuwa tayari kuwa karibu na wewe.

Watu watasahau uliyowaambia, uliyoyafanya, lakini hawawezi kamwe kusahau ulivyowafanya wajisikie. Kuwa mkarimu, wachangamkie watu, watu ni fursa, watu ni mtaji. Jiweke karibu nao.

By Jamhuri