Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), umefanya mabadiliko makubwa kwa kuwaondoa katika vituo vya kazi, baadhi ya watumishi waliofanya kazi kituo kimoja kwa miaka mingi, JAMHURI imetibitishiwa. Katika mabadiliko hayo yaliyotarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia jana, wafanyakazi 191 wamekumbwa na “hamisha hamisha” hiyo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kazi hiyo itafanywa kwa mikoa yote nchini.

Mmoja wa maofisa waandamizi wa Tanesco, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, amesema pamoja na “hamisha hamisha” hiyo, watumishi wengine watafukuzwa kulingana na ripoti za utendaji kazi wao.

 

Tayari baadhi ya watumishi wa Shirika hilo katika Mkoa wa Dar es Salaam, wameanza kupewa barua za kubadilishwa vituo vya kazi na wengine kusimamishwa.

 

“Tulianza na watumishi wenye tuhuma za rushwa, kazi hiyo haijamalizika, lengo letu ni kubadili utendaji kazi wa Shirika kwa kufanya marekebisho ya msingi. Unajua ilifika mahali image (tashwira) ya Tanesco kwa Watanzania ikawa mbaya, linaonekana ni shirika la walaji, warasimu, watu wenye kiburi na ambao hawapo kuwatumikia wananchi.


“Tumenuia kwa dhati kabisa kuhakikisha image ya shirika inakuwa nzuri na wafanyakazi wanawajibika kwa wananchi. Si wao wajione kuwa ni muhimu au bora sana kuliko wananchi wanaotaka huduma,” amesema ofisa huyo.


Ameongeza, “Hatua ya pili baada ya ile ya kupambana na wala rushwa, ni kupangua watumishi katika nchi nzima. Tumewalenga kwanza waliokaa kwenye kituo kimoja kwa miaka mingi. Kuna athari kubwa kwa watumishi kukaa katika kituo kimoja, wanageuka na kuwa miungu watu, huduma zinapoteza radha.

 

“Tumeanza na masupervisor na mafomeni. Dar es Salaam pekee tumewagusa wafanyakazi 191. Hawa wamekaa kwenye kituo kimoja kwa miaka mingi na kujisahau. Tunawapeleka mikoani, na wengine wa mikoani tunawaleta Dar es Salaam.


“Nia ni kuvunja mtandao wa mazoea maana kumekuwa na culture (umataduni) wa kutoa huduma mbaya kwa sababu ya mtu kuzoea mahali kwa miaka mingi.


“Pia wengine tunawaondoa kwa sababu hawakidhi viwango vya kuwa katika nafasi fulani fulani. Lengo ni kuongeza efficiency (ufanisi)…kuboresha huduma na kuwafanya wafanyakazi wawajibike kwa wateja.


“Tunataka wajue wao ni wafanyakazi wa Watanzania, hatutaki wajione kuwa wao ni wao; na wateja si muhimu. Tunataka kila mtumishi wa Tanesco afike mahali ajue hakuna mkubwa kuliko Tanesco, hakuna mkubwa kuliko mwananchi anayehitaji huduma bora za shirika,” amesema ofisa huyo.

1031 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!