Na MWANDISHI WETU

Paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Kristu Mfalme- Tabata, Padre Peter Shayo na mfuasi wake Denis Emidi, wapo hatarini kufungwa miaka miwili jela kwa kosa la kung’oa mawe ya upimaji uliofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, DDar es Salaam.

Taarifa hizi zimelifikia JAMHURI zinaonyesha kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wameanza mchakato wa kisheria dhidi ya Kanisa Katoliki kupitia Parokia ya Kristu Mfalme kutokana na wawili hao kushirikiana kung’oa alama za upimaji katika kiwanja kilichopo jirani na linapojengwa Kanisani Katoliki Kimanga, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Sheria ya ardhi inasema mtu anayeng’oa jiwe lililipandwa na Idara ya Ardhi, anapaswa kulipa faini isiyopungua Sh 720,000 au kifungo cha miaka isiyozidi miwili, au vyote kwa pamoja.

Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu ameliambia JAMHURI kwamba kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 11 (l) vya sheria ya Upimaji Ardhi Sura ya 324 “Mtu yeyote atakayezuia au kukwaza kazi ya upimaji ardhi ikiwa ni pamoja na kung’oa alama za upimaji atakuwa ametenda kosa la jinai.”

Sahaibu anasema sheria inaelekeza kwamba mbali na adhabu hiyo, mtu huyo anaweza pia kuamriwa na mahakama kulipia gharama za kurudishia alama na gharama nyingine za upimaji na kurejesha alama hizo.

Padre Shayo anatuhumiwa kutoa agizo la kung’olewa kwa mawe yenye namba DOY 3, DOY4 na DOY 5 kwa madai kwamba alama hizo zimewekwa kwenye kiwanja ambacho bado kina mgogoro kati ya Kanisa na Familia ya Amina Shaban.

Hata hivyo, Amina ameliambia JAMHURI kwamba kiwanja hicho amabacho ni mali ya urithi kutoka kwa marehemu baba yake, Shaban Kibwana hakina mgogoro.

Mgogoro ulimalizika baada ya taratibu rasmi kufanywa na Manispaa ya Ilala kufufua mipaka kwa kiwanja cha Kanisa na matokeo kuonesha ukomo wa mipaka (ya Kanisa), ambapo matokeo rasmi yalitolewa kwa familia na Kanisa pande zote mbili.

Anasema baada ya utambuzi huo familia ilichukua uamuzi wa kupima eneo kupata umiliki rasmi, lakini Desemba 8, 2017 wakati watendaji wa Manispaa wanapanda mawe ya mipaka, Padre Shayo alifika na askari na kumpeleka Amina na kijana wake katika kituo cha polisi Tabata.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa akifuatilia vikao mbalimbali kati ya pande zote kujadili mchakato wa fidia, alifika kituoni hapo ambapo baada ya maelezo Polisi kutolewa na pande zote ilielekeza kesi hiyo kupelekwa kwa Mamlaka husika, kuanzia Baraza la Kata la Ardhi na kuamuru mawe yaliyopandwa yasiguswe mpaka suluhisho litakapopatikana.

Amina anasema baada ya siku kadhaa alifika kiwanjani hapo na kukuta mawe yameng’olewa. Alienda Serikali za Mitaa kwa lengo la kutoa taarifa na kuyakuta mawe hayo na taarifa ya maandishi kwenye daftari kuwa aliyeyapeleka pale (Denis Emidi).

Taarifa hiyo iliyopokelewa tarehe 12/12/2017 ilisomeka hivi “Mr Denis Emidi kutoka Kimanga Parish ameleta mawe ya mipaka matatu yaliyokua yanawekwa kwenye kiwanja chenye migogoro eneo ya kanisa, tunasubiri maelekezo mengine, 0754589692/0715549692.”

Amina alipeleka malalamiko ofisi ya Kata ambapo Denis aliitwa na kukiri kung’oa mawe kwa agizo la Padre Shayo na kueleza kwamba hukua na taarifa ya zuio la polis.

“Mimi ni miongoni mwa wasimamizi wa ujenzi wa kanisa hili la  Kimanga ambalo linasimamiwa na Parokia ya Kristu Mfalme. Ni kweli  niling’oa mawe baada ya kuelekezwa hivyo na Baba Paroko, ” alisema Denis.

Katika toleo namba 340 la April 03-09 mwaka huu katika gazeti la JAMHURI, ilielezwa kwamba Padre Shayo amekua akiipiga danadana familia ya Amina licha ya kukaa vikao mbalimbali kujadili kiwango cha fidia kwa agizo la Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa.

Taarifa zilizolifikia JAMHURI zinaonyesha kuwa baada ya gazeti hili kuchapisha taarifa hii ya uchunguzi, Paroko Shayo na wapambe wake wamekimbilia kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala wakidai kuwa wanahujumiwa. Mkurugenzi amewapangia wakutane na Mkuu wa Idara ya Ardhi ndani ya wiki hii.

1727 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!