Polisi aiba bandarini

*CCTV Camera alizofunga Injinia Kakoko zamuumbua
*Tukio lake lazua tafrani kubwa, IGP Sirro alishuhudia
*Bandari sasa kama Ulaya, imefungwa kamera 486
*Polisi wafanya mbinu kumtetea mwenzao, wagonga mwamba

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

Mfumo mpya wa ulinzi aliouanzisha katika Bandari ya Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Deusdedith Kakoko, umemnasa askari Polisi aliyekabidhiwa jukumu la kulinda mali za bandari na wateja wake akiiba, JAMHURI limebaini.
Miaka ya nyuma kulikuwapo wizi wa kutisha katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na hujuma zilizokuwa zinafanywa na baadhi ya watendaji wa bandari kuhakikisha Kamera za Usalama (CCTV) hazifanyi kazi.
Katika miaka ya 2013, 2014, 2015 na 2016, Gazeti la JAMHURI limeandika habari nyingi za bandari kueleza ubovu wa mfumo wa kamera jinsi nyaya zilivyokuwa zinakatwa na kuifanya bandari ulinzi ufanyike kwa macho ya binadamu, suala lililotoa mwanya kwa watu wasio waaminifu kuiba mizigo ya wateja.

Kati ya mapendekezo yaliyotolewa na Gazeti hili la JAMHURI ni kuhakikisha bandari inafunga mfumo wa CCTV Camera maeneo yote ndani na nje ya ofisi zilizopo bandarini na inakoshushwa, kupakiwa na kuhifadhiwa mizigo.
Askari PC Stephen Shawa, bila kujua kuwa kuna mfumo wa kamera unaonasa picha na sauti bandarini, aliiba kofia ya pikipiki ya mteja. “Unajua siku za nyuma ilikuwa kawaida kwa askari wanaofanya kazi bandarini kuiba mizigo ya wateja. Walifahamu kuwa wanaaminiwa, ndio waliokabidhiwa jukumu la ulinzi, hivyo hata wakiiba kitu hakuna mtu wa kuwafanya chochote na wanafichiana siri,” amesema mtoa habari wetu.
Siku ya Jumanne, Agosti 8, mwaka 2018, saa 05:40:28 asubuhi ilikuwa siku ya aibu kubwa kwa PC Stephen. Uchunguzi unaonyesha kuwa aliingia sehemu ya wazi zinakoegeshwa pikipiki, akidhani yuko peke yake, akaenda hadi mwisho wa jengo kujiridhisha kuwa hakuna anayemwangalia pale bandarini kisha akachukua kofia ngumu ya mteja na kuondoka nayo.

Ukimwangalia anavyotembea, anaonekana anatembea kwa tahadhari huku akijihami, kwani anaangaza macho kuhakikisha ameona kila sehemu kuwa ni yeye tu aliyeko eneo la tukio na haonwi na mtu mwingine yeyote.
“Mteja alipotoka nje akakuta kofia yake haipo. Akalalamika mara moja kuwa imekuwaje kofia yake ipotee wakati ameiacha kwenye pikipiki.  Kwa kweli ilileta tafrani kubwa. DG Kakoko aliingilia kati. IGP [Simon] Sirro alijulishwa akaja hapa, ilikuwa ni mtiti kweli kweli.

“Kwa kweli huyu askari hakujua kuwa mambo yamebadilika bandarini siku hizi. Hakufahamu kuwa CCTV za sasa zipo hadi ofisini kwa DG na kwamba hata sindano ikidondoka inaonekana. Alifikiri mambo bado yako kama zamani. Kimsingi alikamatwa na kuswekwa ndani, baadaye wenzake wakaanza juhudi za kumtetea na mpaka leo hatujui hii kesi imeishia wapi,” kilisema chanzo chetu.
JAMHURI limemtafuta Mhandisi Kakoko, aliyekiri tukio hilo kuwapo: “Ni kweli huyu askari aliiba kofia ya pikipiki, lakini kwa mfumo wa CCTV tulizonazo zinazosikia hadi sauti, tukamnasa vizuri tu. Nikamkabidhi kwa IGP Sirro. Naamini wanaendelea naye ingawa sijasikia amefikishwa mahakamani.

“Kwa sasa bandari zetu zimebadilika. Usalama ni wa hali ya juu. Iwe ni gari au kitu chochote bandarini, kila mtu alipo mfumo (system) unamwona. Udokozi ndani ya bandari umekwisha kwa asilimia 100. Mizigo ya wateja inalindwa na teknolojia kwa sasa. Kamera zinaifanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa.”
Katika kuboresha ulinzi bandarini, uongozi wa TPA umeweka mfumo maalumu na wa kisasa wa ulinzi unaoitwa Integrated Security System (ISS). Mamlaka ya Bandari imefunga mfumo wa kamera maalumu 486 (CCTV Camera) zilizowekwa kila sehemu bandarini, vifaa maalumu vya kusoma vibao vya namba za magari ambavyo vimewekwa kwenye mageti ya bandari, mashine za ukaguzi wa mizigo midogo midogo (X-rays), mashine za ukaguzi wa watu wanaoingia na kutoka bandarini (walk through metal detectors), turn styles kwa ajili ya kudhibiti upitaji wa watu getini, bollards na barriers kwa ajili ya kudhibiti upitaji wa magari getini, vifaa maalumu vya kubaini urukaji ukuta au uzio bandarini (perimeter intruder detection system) na taa maalumu ili kuongeza mwanga usiku ndani ya bandari.

Pia katika kuimarisha ukaguzi wa makasha yote yanayopita bandarini, TPA ina mashine maalumu (scanners) za kukagulia makasha yote yanayoingia au kutoka bandarini. Pia TPA imeshakamilisha uwekaji wa mashine mpya mbili na nyingine moja ipo katika hatua za mwisho za kumalizia uwekaji, ambayo itatumika kukagulia makasha yanayoingia au kutoka kwa treni. Lengo ni kuhakikisha mizigo yote inayopita bandarini ni salama na halali.
Kutokana na kuimarishwa ulinzi katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita hakuna wizi wowote wa mizigo ya wateja uliotokea. Jitihada hizi pia zimechangiwa na ulinzi shirikishi wa wafanyakazi wote ambapo licha ya kuwepo kwa askari wenye jukumu la ulinzi lakini kila mfanyakazi ni mlinzi.

JAMHURI limehojiana na Kamanda wa Kikosi cha Bandari Tanzania, SACP Robert Mayala, amesema kwamba askari huyo hakuiba kofia hiyo kama inavyosemwa.
Kamanda Mayala amesema PC Stephen aliombwa na askari mwenzake amsaidie kumpeleka Kariakoo kutokana na yeye kumiliki pikipiki, lakini kutokana na askari huyo kutokuwa na kofia ngumu kwa ajili ya abiria ambaye angempakia kwenye pikipiki, alichukua kofia iliyokuwa imewekwa kwenye pikipiki iliyokuwa imeegeshwa jirani na pikipiki yake.

“Unajua hapa kwetu kuna eneo ambalo polisi huwa wanaegesha pikipiki zao, sasa yeye alichukua ile ‘helmet’, akachukua akijua anakwenda mara moja na kurudi. Alidhani pikipiki na kofia ile ni ya polisi mwenzake kumbe ilikuwa siyo,” amesema Kamanda Mayala.
Kamanda Mayala amesema PC Stephen alichukua kofia hiyo kwa dhumuni la kuirudisha muda mfupi (alijiazima) aende Kariakoo na kurudi bila kukamatwa na askari wa usalama barabarani.
Hata hivyo, Kamanda huyo wa Polisi hakueleza bayana kwa nini alikuwa na kofia moja ngumu badala ya kuwa nazo mbili kama utaratibu unavyotaka. Pia PC Stephen alikamatwa kwa kutumia ushahidi wa CCTV Camera na kuwekwa ndani, na si kweli kwamba aliirejesha mwenyewe.

Alipoulizwa ni hatua zipi zimechukuliwa dhidi ya PC Stephen baada ya kuwepo taarifa za wizi wa kofia hiyo, amesema kwamba tukio hilo lilijenga taswira ya wizi na kuilazimu ofisi yake kufungua jalada la uchunguzi wa tukio zima na baada ya kujiridhisha kuwa Stephen hakuwa na nia mbaya lilifungwa.
Alipoulizwa taarifa za askari huyo kutokuwepo bandarini pamoja na polisi kumwona kuwa hakuwa na kosa lolote alilofanya, amesema kwamba kutokana na tukio hilo kutokuwa na taswira nzuri kwa askari huyo amehamishwa kituo cha kazi.
Alipoulizwa ni wapi alipohamishiwa, amesema kwamba alirudishwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lakini hakuwa tayari kueleza wilaya na kituo alichopelekwa.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa PC Stephen Shawa baada ya sakata hilo alipewa uhamisho kwenda mkoani Shinyanga ambapo ndipo alipo mpaka sasa.
Mtoa taarifa amesema polisi huyo alihamishwa kutokana na maaagizo kutoka juu kusafisha upepo uliokuwa umechafuka wakati huo.
“Unajua huu uhamisho ilikuwa ni amri kutoka juu, hivyo ni kweli amepelekwa huko, lakini si unajua wakubwa wanaweza kukueleza zaidi,” amesema.