Katika toleo hili tumechapisha makala ikimnukuu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Wilbroad Mutafungwa, akizungumzia masuala ya ajali.

Kwa mujibu wa Kamishina huyo wa Jeshi la Polisi, takwimu zilizopo ndani ya miaka 10 kuanzia mwaka 2011 zinaonyesha kupungua kwa matukio ya ajali za barabarani; zile mbaya na za kuogopesha watu.

Mathalani, taarifa za ajali zilizoripotiwa na kurekodiwa na Kikosi cha Usalama Barabarani mwaka 2011 ni 23,986 zilizosababisha vifo 3,981 na majeruhi 20,802; wakati kwa mwaka 2000 ni ajali 1,714, vifo 1,270 na majeruhi 2,126.

Pamoja na kulipongeza Jeshi la Polisi hususan Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kufanikiwa kudhibiti ajali hasa zile zinazotokana na uzembe, tunadhani bado kazi kubwa ipo mbele yetu na tunapaswa kuifanya kwa pamoja kama taifa, tukiongozwa na askari wataalamu wa usalama barabarani.

Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa takwimu za Kamishina Mutafungwa, pamoja na kuonyesha kupungua kwa matukio ya ajali hizo, ukweli ni kuwa vifo vinavyotokana na ajali hizo vimeongezeka kwa kiwango kikubwa sana.

Ongezeko hilo linajionyesha katika wastani wa watu waliopoteza maisha kutokana na ajali kwa mwaka 2011 (asilimia 10 tu ya ajali zaidi ya 23,000) likilinganishwa na wengine waliopoteza maisha mwaka 2000 (asilimia 74 katika ajali zaidi ya 1,700).

Kwa maana hiyo, uchache wa ajali zilizotokea haujapunguza idadi ya vifo vya Watanzania kwa asilimia katika kiwango kilichotarajiwa, na hapo ndipo ambapo askari wa usalama barabarani na wadau wengine wanapaswa kupatazama kwa makini zaidi.

Hasara zinazotokana na ajali hizi ni kubwa sana kwani mbali na kupoteza uhai wa maelfu ya watu ambao wengi wao ni nguvu kazi ya taifa na familia husika, pia husababisha fedha za kigeni ambazo zingeweza kufanya mambo mengine ya kijamii kuelekezwa katika kununua vipuri kwa ajili ya matengenezo ya magari hayo.

Lakini athari kubwa na za muda mrefu hubaki kwa familia inayompoteza ndugu yao katika ajali na wakati mwingine kulazimika kutumia kipato cha familia kumuuguza kwa muda mrefu ndugu aliyejeruhiwa kutokana na ajali.

Kuna familia zimeendelea kuubeba mzigo wa kuwatunza ndugu zao ambao kwa sasa hawajiwezi kutokana na majeraha waliyoyapata katika ajali za barabarani; na ndiyo maana tunatoa wito kwa wenzetu wa usalama barabarani kutobweteka na takwimu walizonazo, bali wawashirikishe wadau wote kuhakikisha hata kama ajali zinatokea, ziwe ni za bahati mbaya na kupunguza madhara yake; vifo na majeruhi, ikiwezekana hadi asilimia sifuri.

By Jamhuri