Na Deodatus Balile, Dodoma

Kwanza ninaomba kuwashukuru wasomaji wangu kwa mrejesho mkubwa mno kutokana na safu hii ya SITANII kwa makala niliyoiandika wiki iliyopita. 

Katika makala ya wiki iliyopita nilimwomba DPP kutumia mamlaka yake ya kisheria kuiondoa mahakamani kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anayeshitakiwa kwa kufadhili ugaidi kwa Sh 600,000. Nilisema kesi hii inaonekana kama utani mbele ya macho ya jamii yetu na ya kimataifa.

Nilieleza pia katika makala hiyo kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI) na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) waliepushe taifa letu na balaa kubwa kwa kutotumia neno ugaidi katika kesi au wanapokamata watuhumiwa. Nilisema neno ugaidi ni zito na nchi nyingi duniani zinalikwepa kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi zao. Mnapomfungulia mtu kesi ya ugaidi au mkamtangaza mtuhumiwa kuwa ni gaidi, inakuwa fursa ya kuiambia dunia kuwa Tanzania kuna ugaidi. Hili si sawa, tuliepuke kabisa.

Lakini pia nilisema Rais Samia Suluhu Hassan anapambana kulitangaza taifa letu kitaifa na kimataifa na hadi ameamua kushiriki filamu ya kutangaza utalii. 

Tunapokuwa na kesi za ugaidi na kuwatangaza watuhumiwa kuwa ni magaidi, inakuwa sawa na kuhujumu juhudi za Rais Samia, kwani watalii anaowatafuta, kamwe hawataki kwenda nchi zenye ugaidi. Narudia, Tanzania hakuna ugaidi na yeyote anayesema upo tunapaswa kumkemea kama pepo.

Sitanii, baada ya kuandika makala hii nilipata mrejesho mkubwa hadi mimi nikashangaa. Miongoni mwa yote, nilipata mirejesho miwili ambayo nitawashirikisha ninyi wasomaji muone tunavyopaswa kuendesha kesi za watuhumiwa hapa nchini. 

Kubwa, mrejesho ninaotaka kuwashirikisha unaakisi kilio cha muda mrefu cha Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, kuwa tusikamate watuhumiwa bila kukamilisha upelelezi kwanza.

Taarifa nilizonazo kwa sasa asilimia 60 ya magereza yote nchini yamejaa mahabusu. Hawa ni watu wenye kesi mbalimbali zikiwamo za kubambikiwa kama alivyosema Rais Samia. 

Tunapaswa kuliepuka hili. Wapo watu wenye mawazo ya hovyo wanasema tuanzishe mpango wa kupanua magereza ili tuwe na nafasi ya kutosha kuwaweka wahalifu. Nasema haya ni mawazo ya hovyo. Tunapaswa kuwaza kuwa na jamii isiyo na uhalifu, hivyo tufunge magereza karibu yote.

Sitanii, mrejesho niliosema nitakushirikisha uko hivi; baada ya kuandika makala hii wasomaji wawili wiki iliyopita walinipigia simu na kunikumbusha kisa nilichokwisha kisikia na hapa ninatumia simulizi ya mmoja wa askari hao walionipigia simu: “Balile, hii makala yako iko sahihi kabisa. Mimi ni askari mstaafu, ulipogusa tukio la kushambuliwa kwa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya, Agosti 7, 1998 umenigusa kweli.

“Baada ya Ubalozi kulipuliwa sisi polisi tulifanya kazi moja tu. Hatukufanya uchunguzi, ila hatua ya kwanza ilikuwa ni kukamata kila aliyekuwa jirani na Ubalozi, aliyepita au tuliyemwona anapepesa macho. Baada ya siku tatu mahabusu za Central Polisi, Oysterbay na Salender zote zilijaa watuhumiwa. Ilikuwa hawana hata mahala pa kukanyaga, maana tulikuwa tunakamata kila tuliyemshuku.

“Baadaye walikuja askari wa FBI kutoka Marekani. Wakasema mbona mmekamata watu wengi hivi? Tukawaambia tunawashuku. Wakasema hapana. Haki za binadamu haziendi hivyo. Hapaswi kukamatwa mtu kwa kumshuku, bali mtu anakamatwa baada ya kufanya uchunguzi na kupata ushahidi usiotiliwa shaka. Tukawauliza sasa tufanyeje?

“Wale FBI walisema leteni meza hapa nje. Tukapeleka meza. Wakasema waiteni wote wanaotuhumiwa mliowakamata kisha apite mmoja mmoja tutawaambia nani ni gaidi au ameshiriki kulipua ubalozi. Tukaweka meza, tukawaita watuhumiwa wakapita mmoja baada ya mwingine. Walikuwa wengi kweli. FBI baada ya zoezi lile wakasema waachieni wote hawa hakuna mtuhumiwa hata mmoja. Tukawauliza, tukiwaachia tutaanzia wapi upelelezi? Wakatwambia waachieni tu, tutazungumza. Tukawaachia.

“Tulipoingia kwenye kikao, wakasema wale wote mliowakamata hawajui lolote katika tukio la kulipua Ubalozi. Wakatuuliza tunaweza kupata askari anayelifahamu vizuri Jiji la Dar es Salaam? Tukawaambia ndiyo. Wakasema mleteni. Akaletwa (jina linahifadhiwa) kutoka makao makuu. Wakamuuliza unafahamu eneo linaloitwa Kimara? Akasema ndiyo. Wakasema tupeleke.

“Aliwapeleka hadi Kimara. Wakamuuliza unaifahamu gereji ya (jina linahifadhiwa), akasema ndiyo. Wakamwambia tuonyeshe. Aakawapeleka hadi gereji. Pale gereji wakasema fundi anayeitwa (jina linahifadhiwa) yuko wapi? Akaitwa huyo fundi akaja. Wakajitambulisha kwake na kumweleza kuwa wao ni FBI kutoka Marekani na wanafuatilia ulipuaji wa Ubalozi wa Marekani. Wakamsihi asiwe na wasiwasi hawatamkamata, bali awape ushirikiano na taarifa watakazomwomba, ikiwa anazo.

“Wakamuuliza. Wiki mbili zilizopita ulitengeneza boksi la chuma hapa gereji? Akasema ndiyo. Wakamuuliza huyo mteja mlikuwa mnafahamiana? Akasema hapana, ila alikuja hapa alikuwa na kanzu nyeupe na ndefu nyingi, akanielekeza nimtengenezee boksi la aina hiyo. 

Wakamuliza kama anajua anapoishi huyo mtu, akasema hajui. Wakamwambia alipigiwa simu na huyo mtu siku… baada ya hapo huyo fundi gereji waliongozana naye kwenda maeneo ya Ilala na kwingine ambapo walikamatwa watu wawili waliosaidia Ahmed Khalfan Ghailani kukamatwa nchini Pakistan na akawataja wenzake. Watu 14 dunia nzima walikamatwa na kuwekwa katika Gereza la Guantanamo Bay, Marekani.

“Sasa sisi hapa kwetu kuna kesi nyingi mno ambazo hazikustahili kuwa mahakamani. Hii ya Mbowe nayo sina uhakika kama ilistahili kuwa mahakamani. Tunatumia vibaya nafasi ya uchunguzi na kuipaka matope nchi yetu. Wakati umefika sasa kabla ya kukamata mtu, ni lazima tufahamu fika kosa lake halisi, ushiriki wake, tuwe na vielelezo na mashahidi wa uhakika bila kutegemea polisi ambao mara kadhaa wakibanwa na mawakili wanababaika.”

Sitanii, sasa kwa ushuhuda huu mimi niongeze nini? Ninachoweza kusema hapa ni kuwa Tanzania ni nchi yetu sote. Tunajenga nyumba moja, hatuna sababu ya kugombea fito. Tuelekeze nguvu katika vita ya kiuchumi. Wazee wetu wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere walikwisha kutukomboa kisiasa, hizi harakati zinazoendelea tuzungumze kama taifa, tupambane na maadui watatu; ujinga, maradhi na umaskini. Haina tija sisi Watanzania kupambana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu za kisiasa kumbe tunachafua jina la nchi yetu. Mungu Ibariki Tanzania.

By Jamhuri