Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, ameitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwafahamisha kuwapo kwa mtandao mkubwa unaojihusisha na uporaji na mauaji ya watu.

Kamanda Athuman amewaeleza wanahabari hao kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha linawakamata wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu, ili kuwawezesha wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuishi kwa amani bila hofu ya kutendewa uhalifu. Hata hivyo, tukiangalia historia ya miaka ya nyuma ni wazi kuwa Mkoa wa Mbeya ulijijengea historia ya matukio ya uhalifu kama ujambazi, ushirikina na upigaji nondo, hivyo kuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi.

 

Lakini matukio ya aina hiyo yameanza kupungua kwa kasi, mara baada ya uongozi wa jeshi hilo kubadilishwa na kujikita zaidi katika kuurudisha mkoa huo kwenye hali ya usalama ili uwe kivutio kwa wenyeji na wageni wanaoutembelea.


Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linastahili pongezi kwa kufichua mtandao wa ujambazi uliokuwa ukiwakosesha usalama na amani wakazi wa mkoa huu na mikoa jirani, kutokana na wananchi kuuawa ovyo na kuporwa mali.

 

Binafsi ninapongeza kazi nzuri iliyofanywa na jeshi hilo, kiasi cha kuwapa wananchi matumaini ya kuishi bila hofu ya kukumbwa na vitendo vya uhalifu.

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeshawatia mbaroni watu 13 wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha.

 

Kamanda Athuman amesema watuhumiwa hao wamegawanywa katika makundi mawili – la kwanza ni la watuhumiwa tisa wanaoshukiwa kuhusika na tukio la kuwaua kikatili, kisha kuwazika – dereva na utingo wake.

 

Kundi la pili ni la watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya dereva wa polisi, yaliyotokea wilayani Chunya mkoani hapa, baada ya kufanyika uporaji wa Sh milioni 2.2 katika kituo cha mafuta eneo la Matundasi wilayani humo.

 

Akifafanua zaidi, Kamanda Athuman amesema jambo la kwanza lililotokea Februari 2, mwaka huu katika eneo la Mafinga, mkoani hapa, ni la watuhumiwa waliowateka dereva na utingo wake, Festo Kyando (45) na Jafari, wakawaua, kisha kuwazika porini.

 

Dereva huyo alikuwa ametoka jijini Dar es Salaam kubeba mzigo wa wafanyabiashara kuleta mkoani Mbeya, lakini walipofika mkoani Iringa walitekwa na kuuawa.

 

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza msako mkali na hatimaye watu tisa wakiwamo askari wawili (wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Watanzania-JWTZ na Jeshi la Polisi) wakatiwa mbarani na polisi, uchunguzi umebaini kuwa wamekuwa wakitoa silaha na sare za majeshi hayo.

 

Kamanda Athuman amewataja watuhumiwa hao kuwa ni MT.85393 Samwel Charles Balumwina (31), mwajiriwa wa JWTZ kikosi 844 Itende Mbeya, na G.1901PC Samwel Kigunye (27), mwajiriwa wa Jeshi la Polisi Jijini Mbeya.

 

Watuhumiwa wengine ni mfanyabiashara maarufu wa eneo la Mwanjelwa, Gath Mbilinyi (32); Rajabu Mbilinyi (25), Gregory Mtega (25), Francis Sanga (30) na ndugu watatu wafanyabiashara maarufu katika mji wa Makambako, Njombe, ambao ni Japhet Ng’ang’ana (24), Claud Ng’ang’ana (36) na Hillary Ng’ang’ana(30).

Jeshi la Polisi pia lilifanikiwa kukamata bidhaa mbalimbali katika eneo la Tunduma. Mali zilizookolewa ni nondo 397 na mabando 18 ya mifuko ya sandarusi (sulphate).


Tukio la pili lilihusisha vifo vya watu wawili wilayani Chunya – dereva wa gari la polisi na dereva wa gari la watuhumiwa – baada ya kurushiana risasi.

 

Amesema jambo hilo lilitokea Februari 6, mwaka huu, baada ya watuhumiwa wanne kufanya uporaji wa Sh milioni 2.2 katika kituo cha Matundasi. Madereva waliouawa katika tukio hilo ni Jafari wa Jeshi la Polisi na wa watuhumiwa, aliyetajwa kwa jina la Shaban John.

 

Kamanda wa polisi amewataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo kuwa ni Manase Kibona (37), Emmanuel Mndendemi, Masai Hongole, Mashaka George, John Mahenge na Narasco Mabiki.

 

Aidha, Kamanda Athuman ametaja baadhi ya silaha zilizokamatwa kuwa ni bunduki moja aina ya shotgun, gobore moja, bastola tatu zilizotengenezwa kienyeji zinazotumia risasi za shotgun.


Nyingine ni risasi 130 zinazotumika kwenye bunduki aina za SMG na SAR, sare za JWTZ zikiwamo suruali nne, mashati manne, kofia tatu na viatu jozi mbili, risasi 25 za bastola na magari yenye namba za usajili T 464BLX Toyota Corolla, T 381 BDR VITZ, T 251 AKU Toyota Pick Up, T 193 BDY Toyota Premio na T 214 ASV Toyota Mark II.


Kamanda Athuman amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Mbeya waliojitokeza kutoa ushirikiano wa kuwasaka watuhumiwa husika, na kuendelea kutoa wito kwa watu wenye taarifa za watuhumiwa wengine wajitokeze kuziripoti polisi ili hatua zichukuliwe.  Kwa mujibu wa Kamanda Athuman, upelelezi wa awali umekamilika na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.


Ingawa ni wajibu wa Jeshi la Polisi kutimiza kazi yao ya kulinda amani ya nchi na wananchi kwa ujumla, lakini yapo maeneo mengi ambapo limejikuta likilaumiwa na wananchi kutokana na utendaji kazi mbovu wa baadhi ya watendaji wanaoshirikiana na magenge ya uhalifu.

 

1666 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!