Habari iliyochukua uzito wa juu kwenye gazeti hili toleo la leo inahusu vitendo vya utapeli kwenye biashara ya madini.

Jambo la kusikitisha ni kusikia kuwa kwenye genge la matapeli hao wamo watumishi wa Serikali, hasa kutoka Jeshi la Polisi.

Hizi ni habari za kusikitisha – zenye kulenga kuchafua sifa ya Tanzania katika ulimwengu huu wa utandawazi. Katika zama hizi za njia rahisi za mawasiliano, ni jambo la hatari kuendesha vitendo vya utapeli kwa sababu hakuna atakayekubali kutapeliwa halafu akakaa kimya bila kusambaza taarifa hizo sehemu mbalimbali duniani.

Jeshi la Polisi; chombo kinachotazamwa na kutarajiwa kuwa mstari wa mbele kuwalinda raia na wageni ili usalama wao na mali zao usiwe shakani, linapojiingiza kwenye matukio ya aina hii, linakuwa jambo la kusikitisha mno.

Kwa muda mrefu kumekuwapo malalamiko ya utapeli yakihusisha baadhi ya askari/watumishi katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Makao Mkuu ya Jeshi hilo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) na Mahakama.

Kesi nyingi zilizofunguliwa, ama zilivurugwa na watumishi kwenye maeneo hayo, au walalamikaji hawakupewa ushirikiano mwishowe wakakata tamaa.

Jambo baya zaidi, wahusika kwenye utapeli huu wanajulikana, lakini kwa miaka yote wameachwa watambe kana kwamba wameiweka Serikali mfukoni.

Tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano iliyodhamiria kusimamia haki bila kujali uraia wa mtu, italichukulia jambo hili kama tatizo kubwa linaloichafua nchi yetu kipindi hiki ambacho tunavutia wafanyabiashara wengi waje nchini mwetu.

Tunaamini matapeli hawa hawana nguvu wala ubavu wa kuvishinda vyombo vya dola, hivyo ni matarajio ya Watanzania wapenda nchi yao kuona hatua stahiki zikichukuliwa ili kukomesha matukio haya.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, ofisi za DCI na DPP na vyombo vingine vya ulinzi na uslama vihakikishe wahusika kwenye matukio haya wanakamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Orodha ya watu waliotapeliwa ipo. Polisi waliobobea kwenye utapeli huu wanajulikana. Mtandao mzima wa uhalifu huu uko wazi. Kinachokosekana ni utashi na dhamira ya kukomesha utapeli huu. Tunaamini Serikali italishughulikia tatizo hili kama inavyoshughulikia matatizo mengine.

By Jamhuri