Wanawake zaidi ya 720 wanafariki dunia kila mwezi nchini, kutokana na matatizo ya uzazi, na kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na idadi kubwa ya vifo hivyo.  

Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonesha kuwa kila siku wanawake 24 hufariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi. Kwa mwaka mmoja wanawake zaidi ya 8,600 wanafariki, jambo ambalo linakwamisha malengo ya milenia. 

Hata hivyo, sababu zinazochangia vifo hivyo ni pamoja na kina mama wajawazito kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, kuchelewa kuanza kliniki pamoja na kujifungulia katika vituo vya afya visivyo na huduma za kutosha za uzazi.  

Mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 ujulikanao kama One Plan, ulipanga kuweka vifaa tiba vya kufanyia upasuaji wa dharura kwenye vituo vingi vya afya nchini, jambo ambalo limeshindikana hadi sasa. 

Akizindua fao jipya la uzazi la Wote Scheme na Bodi mpya ya Wadhamini wa Mfuko wa Pensheni  (PPF), Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, anasema mafao hayo mapya yamelenga kuwasaidia wananchi wa kada mbalimbali wakiwamo wanawake ambao wengi wao wanapoteza maisha kutokana na kushindwa kumudu gharama za afya.

Anasema fao la uzazi limependekezwa na Bodi ya Wadhamini ya PPF tangu Julai mosi mwaka huu, ikiwa ni ubunifu wenye umakini mkubwa  unaoonesha  kuwajali wanachama na kuhakikisha afya zao na familia zao zinakuwa bora.

“Kama mwanamke, nimefurahishwa sana na fao hili kwani najua litawasaidia sana akina mama wanapojifungua kwa mahitaji yao wenyewe na watoto wao,” anasema Mkuya.

Pamoja na hayo, amewaomba wanawake kuchangamkia fursa hiyo ya kujiunga na fao hilo jipya na watoto wao ili kuwa na uhakika wa kusoma kupitia fao la elimu linalotolewa na Mfuko huo.

Anasema kutokana na utendaji wa PPF, imethibitisha kuwa taasisi za umma zinaweza kufanya kazi nzuri kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa, kinyume cha dhana potofu iliyojengeka katika jamii kwamba serikalini na taasisi za umma kumejaa ubabaishaji.

Akielezea kasi ya kukua kwa thamani ya mfuko huo hadi kufikia zaidi ya Sh. trilioni 2 na kupata tuzo ya hesabu bora kutoka Bodi ya Taifa ya Ukaguzi na Uhasibu (NBAA) kati ya taasisi 40 za Serikali na mashirika ya umma, anasema imetokana na utendaji uliojaa uadilifu wa bodi na menejimenti ya Mfuko na hivyo kuwapa matumaini makubwa wanachama.

“Hongera pia kwa kupata hati inayoonesha utendaji wenu unaozingatia kanuni za kimataifa za utoaji wa huduma, jambo hili ni jema sana kwani kilio kikubwa cha wananchi ni kwa Serikali ni taasisi nyingi za umma kushindwa kutoa huduma zinazoridhisha,” anasema Waziri huyo wa Fedha ambaye amejiunga rasmi na mfuko huo wiki iliyopita baada ya kuzindua mafao hayo na Bodi mpya ya Wadhamini ya Mfuko wa Pensheni.

Licha ya kupata cheti cha utoaji huduma bora kwa viwango vya kimataifa (Quality Management Standard) yenye namba ISO 9001: 2008, Mfuko huo umeongeza wigo wa fao la elimu kwa kuwasomesha watoto wa wanachama ambao wamefariki wakiwa kazini kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, ukiwa ni mfuko pekee wa hifadhi ya jamii nchini kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko huo, Ramadhani Khijjah, anasema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja kuongezeka kwa thamani ya mfuko kwa zaidi ya Sh. trilioni moja ndani ya kipindi cha miaka mitatu kutoka Sh. bilioni 859.5 mwezi Septemba 2011 hadi kufikia Sh. trilioni 2.1 Juni mwaka huu.

Khijjah anasema kupata mapato yatokanayo na uwekezaji wa Sh. bilioni 318 mwaka 2013 na bilioni 496.5 kwa kipindi cha mwaka 2014 na 2015 ni sawa na asilimia 22 na 26 za “return on investments”ambao ni uwekezaji wenye tija kwa kuzingatia mfumuko wa bei kwa kipindi hicho uliokuwa na wastani wa asilimia 7.9 na 5.7.

Kuhusu kupata tuzo ya hesabu bora (best presented financial statements) ya mwaka 2013 iliyotolewa na NBAA, na tuzo tatu kutoka Shirikisho la Hifadhi ya Jamii Duniani (ISSA), zikiwamo tuzo mbili mwaka 2011 na moja mwaka 2014, kunadhihirisha jitihada zinazofanywa na watumishi wote wa Mfuko huo kwa kulenga kuwanufaisha zaidi wanachama wote. 

Katika kuongezeka kwa fao la elimu, mwaka huu Mfuko huo unawasomesha watoto 1,328 na umekwisha lipa Sh 958,388,802.13 ikiwa ni gharama za masomo yao na kwamba ni mfuko wa hifadhi ya jamii uliopiga hatua kubwa kwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na kurahisisha utendaji kazi, kati ya makao makuu na ofisi zake zote nchini.

“Kwa kuwatumia wa wataalamu wa ndani wa teknolojia ya mawasiliano, kila mwanachama wetu anapata taarifa zake zote kuhusu michango yake na taarifa nyingine za Mfuko pale alipo – iwe mjini au vijijini – bila kupoteza muda kuja makao makuu ama ofisi zetu za kanda,” anasema mwenyekiti huyo.

Anasema tuzo ya mfuko wa hifadhi ya jamii uliopiga hatua zaidi katika matumizi ya Tehama kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) mwaka 2013 iliwatia moyo na kuchochea kasi ya ubunifu wa mbinu mbalimbali za kurahisisha utendaji kazi wa Mfuko huo ambako kwa asilimia 80 wafanyakazi wa ndani ya PPF wametengeneza mifumo hiyo.

Kutokana na ubunifu huo anasema mawasiliano kati ya wanachama na Mfuko kwa kutumia PPF Taarifa kupitia ujumbe mfupi wa simu za kiganjani na kompyuta na kuanzishwa kwa huduma ya PPF Mobile App, mwanachama anaweza kupata taarifa zake za michango, madai, malipo ya pensheni na nyingine kupitia katika simu yake na kuwasiliana na Mfuko kwa njia ya simu bila malipo na kujibiwa hapo hapo.

Pia anasema kuanzishwa kwa mawasiliano kwa njia “video teleconferencing”  kati ya makao makuu ya Mfuko huo na ofisi za kanda ambako mikutano na mafunzo yanaweza kufanyika bila ya wahusika kulazimika kusafiri, kumepunguza gharama kubwa za matumizi ya fedha kwa washiriki mikutano ambao wangelazimika kuwa na safari za mara kwa mara, gharama za karatasi na muda wa kuwahudumia wanachama.

 

Changamoto za Mfuko

Pamoja na jitihada za PPF kuhakikisha wanachama wake wananufaika kutokana na michango yao, Khijjah anasema suala la fao la kujitoa limekuwa likiharibu taratibu za wanachama ambao baada ya kustaafu kwao wanakosa pensheni zao na kukabiliwa na ugumu wa maisha.

Kutokana na hali hiyo ameiomba Serikali kuangalia kwa makini suala hilo ili wanachama wanapostaafu wawe na uwezo wa kuendesha maisha yao mapya baada ya utumishi wao badala ya kukabiliwa na ugumu wa maisha kwa kukosa pensheni.

Anasema matatizo mengine ni waajiri kuchelewesha michango ya wafanyakazi wao ambayo imekuwa ikikatwa bila kuwasilishwa PPF.

Kwa upande mwingine mwenyekiti huyo wa bodi ameeleza kwamba wapangaji wa majengo ya Mfuko wa Pensheni zikiwamo taasisi za Serikali, mashirika ya umma na taasisi binafsi kwa pamoja zinadhoofisha maendeleo ya Mfuko huo kwa kushindwa kulipa kodi za pango kwa wakati.

Waziri Mkuya amekiri kwamba Serikali imekopa fedha nyingi kutoka katika mifuko ya hifadhi za jamii ikiwamo PPF na mingine kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwamo ujenzi wa shule, vyuo lakini bado haijakamilisha kulipa madeni hayo.

By Jamhuri