Na Mwandishi Wetu
 
Februari 6, mwaka 2018 ilitimia miaka 19 tangu Prof. Hubert Kairuki alipofariki dunia. Katika kipindi kama hicho, wapo maprofesa wengi waliofariki hapa nchini na nje ya nchi siku hiyo. Ni kwa bahati mbaya kuwa siku walipofariki maprofesa hawa, hata majina yao yakafa.
Hili halikutokea kwa Prof. Kairuki. Prof. Kairuki bado anaishi hadi leo. Jina la Prof. Kairuki linaishi hadi leo. Naamini kwa siku linatajwa na watu wasiopungua 2,000 katika vinywa vyao. Hawa wanaweza kuwa wagonjwa waliopata tiba katika hospitali aliyoianzisha, wanafunzi katika chuo chake, manesi waliosomea kwenye taasisi yake, wafanyakazi au ndugu na jamaa wa wahusika hao.
Tanzania inaposisitiza uzalendo wa kweli, hakika nashawishika kusema Mzee Kairuki alikuwa Mzalendo wa kweli na kwa vitendo. Laiti tungekuwa na Maprofesa 10 tu wenye uthubutu wa kufanya mambo kama aliyofanya Prof. Kairuki, tungekuwa mbali katika sekta ya afya nchini.
Matokeo chanya (with positive impact) ya kazi zake imeendelea kuwanufaisha Watanzania miaka 19 baada ya kuondoka duniani. Katika wakati ambao nchi yetu ina wastani wa Daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 50,000; kila mwaka Chuo kikuu alichoanzisha Prof. Kairuki kinatoa mchango wa madaktari 200 wanaokwenda kuhudumia wananchi sehemu mbalimbali nchini. Madaktari hao wapo kwenye hospitali za wilaya, mikoa na taifa (bara na visiwani).
 
Hospitali ya Mikocheni aiyoiacha Prof. Kairuki inatoa huduma kwa Watanzania wasiopungua 500 kila siku. Maana yake ni kwamba kama tungekuwa na maprofesa 10 tu waliofanya mambo aliyofanya Kairuki- maana yake Watanzania 5000 wangekuwa na mahala pa uhakika pa kupata tiba kila siku.
Kama Kairuki asingefanya aliyofanya maana yake wale watu 500 wanaotibiwa pale Kairuki wangeongeza msongamano wa wagonjwa Mwananyamala au Muhimbili ambako tayari kuna wagonjwa lukuki wenye kuhitaji huduma.
Jambo jingine la kudhihirisha uzalendo wa Prof. Kairuki; wakati BIMA ya Taifa ya Afya NHIF ilipoanza kutoa huduma kwa wanachama wake; hospitali zote za binafsi zilikataa kutoa huduma kwa wanachama hao sababu ya bei ndogo walizokuwa wanalipa kwa matibabu; lakini hospitali ya Kairuki ndio ilikuwa hospitali pekee ya binafsi iliyokubali kuwatibu wananchi kwa bei hizo za NHIF. Baada ya wao kuanza na wengine wakafuata… hadi leo Agakhan haikubali NHIF isiyo Green Card ambayo ni ya viongozi tu. 
Kwa ujumla tulizoea kwamba mtu akianzisha jambo na baadaye akafariki basi jambo lake nalo linakufa. Ipo mifano ya hospitali maarufu za zamani za akina Dr Andrew na biashara nyingine za wazawa zilizokufa baada ya waasisi wake kuondoka. Profesa Kairuki amefanikiwa kuepuka mkondo huo. Na siri yake ni kwamba hospitali hiyo alihakikisha wafanyakazi wake wote wanakuwa na feeling ya ownership ya hospitali- ndio ndio maana hata alipoondoka waliendelea kufanya kazi kama kwamba mwenyewe bado yupo.
Prof. Kairuki alikuwa akimshirikisha mke wake katika kila jambo alilofanya- na hivyo haikuwa shida kwa Mama Kairuki kuendelea na kazi aliyoiacha mumewe. Si hilo tu, bali pia aliwaandaa watoto wake kuendeleza kazi yake— kati ya watoto watano aliowazaa; watatu ni madaktari bingwa. Wa kwanza ni daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama kama alivyokuwa Profesa mwenyewe;
Wa pili ni daktari bingwa wa upasuaji (surgeon) na wa tatu ni daktari bingwa wa internal medicine. Madaktari hawa ni nguzo kuu ya kuendesha hospitali ya Kairuki. Vilevile mtoto mwingine ambaye sio daktari ni Mwanasheria na wakili (advocate) ambaye anasimamia masuala ya kisheria ya taasisi zote za Kairuki. Wa-tano ameingia kwenye utumishi wa umma na ni Balozi wa Tanzania nchini China.
Haya ni mambo ya kujifunza kwetu sote hasa tunaofanya shughuli za kujitegemea- kuwaandaa watoto wetu kubeba majukumu yetu baada ya sisi kuondoka.
Miaka 19 tangu kuondoka Prof. Kairuki, kazi za mikono yake zinazidi kushamiri. Tumeshuhudia katika maadhimisho ya mwaka huu mipango mikubwa ya kuanzisha mambo ya kuhudumia wananchi. Miongoni mwa mambo hayo limewekwa jiwe la msingi la kujenga kituo cha kisasa cha tiba ya uzazi Kairuki IVF Centre.
Kituo hicho kinasimamiwa na mmoja wa watoto wa Prof. Kairuki, ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya akina Mama aliyekwenda Scotland mwaka jana kupata mafunzo ya ziada na kupta Master of science in Human Clinical Embryology and Assisted Conception. Kituo hiki kitakaponza kutoa huduma kitakuwa msaada kwa maelfu ya wanaume na wanawake wenye kukabiliwa na changamoto za kupata watoto.
Aidha, tumeshuhudia mipango ya kupanua chuo kikuu cha Kairuki kwa kujenga majengo ya kisasa huko Bunju.
Pia taasisi ya Kairuki ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda. Kwa hakika, laiti tungekuwa na Profesa kairuki 10 tu…. tungekuwa mbali. Hatujachelewa – inawezekana kabisa.
 
Prof. Kairuki ameonyesha uzalendo; anastahili kujumuishwa kwenye orodha ya mashujaa wa Tanzania… mtu ambaye tangu aondoke duniani miaka 19 iliyopita bado kazi yake inaendelea kutoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 521 na indirect employment kwa zaidi ya watu 2,000 kutokana na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa hospitali hiyo.
Bahati mbaya nchini kwetu utaratibu wa kuwatambua mashujaa wa aina hii haupo… tunawathamini zaidi wanasiasa na wasanii ambao impact yao mara nyingi sio rahisi kupimika na kuwaacha watu walioacha mchango unaoonekana (tangible contribution) kwa taifa.
 
1573 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!