Wasanii wa muziki wa kizazi kipya wametakiwa kutumia nguvu kubwa kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kuhamasisha mambo mema katika jamii na kuacha kuimba mapenzi, kwani kufanya hivyo itawasaidia nyimbo zao kudumu kwa muda mrefu sokoni.

JAMHURI imefanya mahojiano maalamu na Mbunge wa Jimbo la Mikumi (Chadema), Joseph Haule, maarufu kwa jina la Profesa Jay (pichani), ambaye pia ni mwanamuziki mkogwe wa miondoko ya Hip hop na Bongo fleva. 

Katika mahojiano hayo, Profesa Jay anasema msanii ana nguvu kubwa katika kubadilisha jamii ili kufanya vitu ambavyo ni rafiki kwa Watanzania, jambo ambalo limewalazimu viongozi mbalimbali kuwatumia kufikishia ujumbe hasa katika shughuli mbalimbali za kiserikali.

“Baadhi ya wasanii wanaoimba nyimbo za mapenzi wanakuwa na malengo ya leo na si kesho, ndiyo maana wasanii wengi nilioanza nao muziki kipindi cha nyumba waliokuwa wanaimba mapenzi walishindwa kuendelea katika soko la muziki,” anasema Professor Jay.

JAMHURI:  Umekuwa mwanamuziki wa muda mrefu, unazungumziaje haki za wasanii?

Profesa Jay:  Sasa ni mbunge, nitahakikisha tunaondoa sheria zote ambazo si rafiki kwa wasanii na kila msanii kuwa na hatimiliki ya kazi yake ili kuepuka wizi ambao umekithiri. Pia nipo katika utaratibu wa kuandaa albamu yangu ya tano ambayo ndani yake kutakuwa na nyimbo kadhaa ikiwamo ‘kazi kazi’.

JAMHURI: Unawezaje kuendelea na kazi ya muziki huku ukiwa na jukumu kubwa la kuwatumikia wapiga kura? Huoni kama unaweza ukashindwa kutekeleza majukumu yako kwa wakati?

Profesa Jay: Mimi siwezi kuacha muziki kwa sababu muziki ndiyo ulionifanya nifahamike katika jamii yangu, muziki umenisaidia kuweza kuingia bungeni. Nitaendelea na muziki kwa muda wake lakini pia nitaendelea kutimiza ahadi zangu kwa ndugu zangu wa Jimbo la Mikumi. Ubunge si kazi ngumu sana iwapo utakuwa na malengo chanya kwa wapiga kura, wapiga kura ni binadamu, ni waelewa nimekuwa nakaa nao na kupanga maendeleo ya jimbo letu, ndiyo maana inakuwa rahisi kuongoza jimbo.

JAMHURI:  Unao mpango wa kuwa na meneja katika kazi zako za muziki?

Profesa Jay: Wapo wengi ambao ningependa wasimamie kazi zangu na wengine nipo katika mazungumzo nao, lakini bado sijafanikiwa kumpata, hii inatokana na utayari wa mhusika katika kufanya kazi. Ni vigumu kumuomba mtu kufanya kazi hiyo  ila kwa yeyote anayeitaji milango ipo wazi. Kumbuka mimi sijawahi kuwa na meneja tangu nianze muziki lakini kwa sasa nahitaji kutokana na majukumu yanayonikabili.

JAMHURI:  Kazi ya muziki imekusaidia nini kimaisha?

Profesa Jay: Siweze kusema nimejenga nyumba ngapi au namiliki magari mangapi, kwani kipindi cha nyuma nilikuwa na magari lakini yote yameharibika. Kikubwa ninachojivunia nimekuwa nembo ya Taifa na Afrika kwani hata nikifa leo watu watasema kulikuwa na mwanamuziki ambaye nyimbo zake zilikuwa zinaonya na kuelimisha. Pia nimeaminika ndiyo maana sanaa yangu imenifikisha hapa nilipo.

JAMHURI: Nini siri ya mafanikio yako?

Profesa Jay: Kujiamini kwa kile ninachokifanya na kujituma, pia nilikuwa najiona mimi kiongozi ambapo nilikuwa nawapa nguvu watu waliokata tamaa katika jamii, wakiwamo wale wanaotumia dawa za kulevya pamoja na maskini kupitia mashairi.

JAMHURI:  Unauonaje mwenendo wa maadili ya wasanii?

Profesa Jay: Kwa kipindi hiki maadili yameshuka sana tofauti na kipindi nyuma kwa sababu wasanii wa sasa wanatoa video ambazo huwezi kukaa na mtoto kuangalia, wanatakiwa kujua siyo lazima uvae nusu uchi ndiyo video yako iwe kali.

JAMHURI: Wasanii wa leo wamekuwa wakiimba mapenzi kwa asilimia kubwa, hii inatokana na nini?

Profesa Jay: Kila msanii anaimba kutokana na malengo yake, wapo wanaoimba kwa ajili ya kupata wanawake, gari zuri la kutembelea au kupata umaarufu, lakini msanii mwenye malengo mapana hawezi kuimba mapenzi kwani nyimbo za aina hiyo zinawahi kuchuja.

JAMHURI: Kitu gani ambacho huwezi kukisahau katika safari yako ya muziki?

Profesa Jay: Yapo mengi ambayo ni vigumu kuyataja sababu nikisema lazima yatawakwaza baadhi ya watu na sipendi itokee hivyo.

JAMHURI: Malengo yako yametimia?

Profesa Jay: Bado sijafikia kwani kuna mambo natarajia kuyafanya kupitia sanaa ikiwamo kuinua vipaji wa wananchi wa Morogoro kupitia studio yangu ambayo tayari nimeihamisha kutoka Dar es Salaam kuipeleka jimboni, mkoani Morogoro.

JAMHURI:  Ni msanii yupi ambaye unaona anafanya vizuri katika sanaa hapa nchini?

Professor Jay: Wapo wengi ila nitakutajia wachache kwa mfano; Diamond, Ali Kiba, Mwana FA, AY, Joh Makini na wengine wengi ambao wanaendelea kufanya vizuri. 

JAMHURI: Umeoa, na una watoto wangapi?

Profesa Jay : Nina mtoto mmoja, pia nina mchumba wangu yule yule Grace Haule ambaye natarajia kufunga naye ndoa hivi  karibuni. 

1291 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!