Rais Magufuli. Mtetezi wa Wanyonge na Wajane. Tunakushukuru. Tunakupongeza. Tunakuombea. Uzi uwe ule ule.”

 

Wanawake hatuna budi kumshukuru na kumpongeza Rais John Magufuli, kwa kututetea sisi wajane tunaonyanyaswa na mifumo dume na kuporwa haki zetu na watoto wetu. Jana (Februari 2, 2017) Rais alitenda makuu kuagiza kwamba yule mama aliyekuwa ameonewa na kuhangaishwa kwa muda mrefu; sio tu kesi yake isikilizwe, lakini pia apewe ulinzi wa polisi.

Kwa kumbukumbu zangu hii haijawahi kutokea kwa mnyonge aliyekata kamba za ulinzi mkali unaomzunguka Rais badala ya kwenda rumande kupewa ulinzi wa polisi yeye mwenyewe. Hili linathibitisha kauli ya mara kwa mara ya Rais kwamba “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu”.

Kwa kuwa Rais kajitanabaisha na kudhihirishia umma kuwa yeye anachotaka ni ukweli na uwazi, huyu mama mwenzetu alikuwa na nguvu na imani kwamba akimfikia Mheshimiwa Rais Magufuli matatizo yake yatakwisha. Atapata kusikilizwa na haki yake ambayo vyombo vya utawala na Mahakama vimeshindwa kumpatia kwa muda mrefu, itapatikana. Vyombo hivi hushindwa kwa sababu baadhi ya wahusika wanakuwa na maslahi binafsi katika migogoro kama hiyo. Wanaichukulia migogoro hiyo kuwa fursa na mtaji wasiopenda uishe. Kwa hiyo anayedai haki yake anawekewa vikwazo na wale waliotarajiwa kumsaidia. Kilio cha yule mama na maelezo yake yalikuwa wazi – kahangaishwa kwa muda mrefu. Alikuwa tayari kujilipua. Ninampongeza mama kwa kutokata tamaa. Na ninampongeza kwa ujasiri kuja mbele ya Rais pamoja na ugumu wa hatua hiyo. Aidha, ninamwombea mafanikio kwa hatua zinazofuata. Mungu hujibu uonevu kwa wanaomtumainia.

Katika kujadili suala hili nami sina budi kurejea tukio kama hili mapema Januari 2, mwaka huu Kyamyorwa, Mkoa wa Kagera. Akiwa katika ziara ya tetemeko mkoani kwetu, Rais Magufuli alinitetea na kuniokoa mikononi mwa watesi wangu wa muda mrefu jimboni kwangu Muleba Kusini. Kwa sababu za kisiasa walikuwa wananikashifu kwa kudai nimepora ardhi ya wananchi wakati wao ndio walikuwa wakiwadanganya wananchi wahamiaji kutoka mikoa jirani na kuwalipisha fedha kwa kuwadanganya watawagawia shamba langu la urithi kutoka kwa marehemu mume wangu aliyemilikishwa shamba hilo kihalali miaka mingi ya nyuma eneo likiwa pori tupu.

Watu hao wanajificha nyuma ya pazia la siasa za upinzani na huwa wanawarubuni hata maafisa wa Serikali wasio waaminifu na wenye tamaa ya ardhi hiyo wao wenyewe kunisumbua.

Rais Magufuli alifika hapo na kuwakuta vijana wa kukodishwa- tayari wana mabango ya kunikashifu nimepora ardhi. Walikuwa wanaongozwa na Diwani Khalid Swalehe (CHADEMA) wa Kata ya Kasharunga ambaye mtaji wake wa kisiasa ni kunikashifu na shamba akishirikiana na wabaya wengine ngazi za juu.

Awali, genge hilo kama kawaida yao walishaandaa vijana wa kunizomea Rais aliposimama Muleba Mjini. Waliamini mara baada ya kushuhudia zomea zomea Rais akifika Kyamyorwa kwenye shamba langu na kukutana na mabango na kelele dhidi yangu ataninyang’anya shamba ili kuwafurahisha wananchi hao. Wengine wala hawakuwa wenyeji, bali walikuwa wamesombwa kutoka mbali.

 Videdea vya pikipiki kutoka Kyamyorwa kuelekea Muleba mjini vilikuwa tayari. Mgeni rasmi kupokea maandamano hayo (jina nalihifadhiwa) tayari alikuwa Muleba akisubiri.

Lakini tofauti na matarajio yao, Rais Magufuli msema kweli na mpenzi wa Mungu na mtoa haki hakufurahishwa na mpango wao huo mwovu. Aliwaonya watu wa Muleba kwamba wajitafakari ni wa aina gani? “Nyie watu wa Muleba nyie,” Rais alisema kabla ya kuondoka kuelekea Kyamyorwa ambayo ni jirani na nyumbani kwake Chato.

Yaliyojiri Kyamyorwa Taifa lote limeshuhudia. Rais Magufuli aliwashushua waliokuwa wamepanga kupora ardhi yangu na katika kufanya hivyo kunigeuza mimi mhanga ndiye mkosaji. Rais alieleza ukweli wa ardhi hiyo aliyowahi kuifanyia kazi alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Shamba limeendelezwa kwa kilimo cha mbegu bora, mifugo na uhifadhi wa mazingira na linalipiwa kodi ya ardhi kila mwaka. Shamba lina hati ya miaka 99.

Tukio hilo lilinipa faraja kubwa na ninalifananisha kwa namna fulani na tukio la mjane wa jana (Februari 2) au zaidi kwa sababu Mheshimiwa Rais alinitetea pamoja na kwamba sikuwepo.

 Kwa kuwa sikujua Rais angelisimama jimboni kwangu Muleba Mjini, mimi mara baada ya kukamilisha ziara yake Bukoba Mjini niliingia makubaliano na Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako kubaki Bukoba Mjini kumsindikiza Katibu Mkuu Elimu. Kwa pamoja tulimpeleka Balozi wa Uingereza, Sara Cooke, kutembelea Shule ya Wasichana Rugambwa ambayo nayo imeathiriwa sana na tetemeko ili ipewe msaada. Mimi nilisoma Rugambwa kwa hiyo ni mdau mkubwa. Nikiwa hapo niliweza kumweleza Balozi shule hiyo ilivyokuwa enzi zetu kama juhudi kuhamasisha msaada wake kwa ukarabati wa shule hiyo kama alivyotoa kwa sekondari kongwe ya Ihungo.

Kwa hiyo sikuwapo jimboni kwangu wakati ‘wategeshi’ wa siasa wananihujumu mbele ya Rais wa nchi.

Kwa hiyo kwa msaada mkubwa aliopewa mama yule mjane na kwangu mie na wengine ambao mambo yao labda hayapo hadharani nasema wanawake tujitambue bado tuna safari ndefu. Haijalishi wewe una elimu, cheo, au nafasi gani katika jamii. Mfumo dume unafanya kazi kukudidimiza.

Ikitokea Rais aliyeshika usukani si mtu mkweli na mcha Mungu na mtu wa haki, mwanamke utakuwa wa kwanza kulaumiwa, kuonewa na kutolewa kafara. Kwa mantiki hiyo wanawake ni wadau wa kwanza katika kuhitaji kiongozi bora. Tunategemea utetezi na ulinzi wake.

Niliwahi kusema na ninarudia. Katika Mheshimiwa Dk. John Magufuli, Tanzania tumejaliwa kupata kiongozi siyo tu Rais. Kiongozi anapopewa dhamana ya urais anaitumia kama tunavyoona sasa, kutengeneza upepo si kuufuata ili kufurahisha mifumo kandamizi kwa kuitolea kafara.

Nimalize makala hii na ombi. Mheshimiwa Rais Magufuli wanawake wengi tuko nyuma yako. Tatizo la kuwanyonga vikongwe kwa kudai ardhi na haki zao katika jamii huko vijijini bado lipo. Ninaomba ulitupie jicho jambo hili.

Kama ulivyomkabidhi mama mlalamikaji ulinzi wa polisi uwatake ma-DC na ma-OCD wote kuwalinda vikongwe katika maeneo yao dhidi ya dhuluma na vitendo vya ukatili.

Ninawasilisha, nikishukuru na kupongeza HAPA KAZI TU.

 

Mwandishi wa makala hii, Profesa Anna Tibaijuka, ni Mbunge wa Muleba Kusini, amepata kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Serikali ya Awamu ya Nne. Ni Mwanamke Mwafrika wa Kwanza Kuchaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Kuongoza mojawapo ya Mashirika yake. Amekuwa Katibu Mkuu Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT), ni

Mwanadiplomasia wa kimataifa, Mhamasishaji mwenye ushawishi, Mtetezi wa haki za wanawake na watoto na mlezi wa elimu bora kwa vijana. Anapatikana kupitia simu 0767 838722.

By Jamhuri