Raia maskini wakimbilie wapi?

Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, imethibitisha taarifa za polisi wake
kumuua mtuhumiwa aliyekuwa mikononi mwao.
Kijana ameuawa kwa kuchomwa kisu mgongoni. Hiyo pekee inajenga mazingira
ya kutuaminisha kuwa kijana yule hakuwa tishio kiasi cha kutumika nguvu kubwa
kumtoa uhai.
Kuchomwa kisu mgongoni kunaweza kutujengea mazingira ya kuamini kwamba
hakuwa kwenye mapambano na aliyemuua. Laiti kama kisu kile kingekuwa
kimemwingia kifuani au sehemu yoyote ya mbele, basi kungejengwa mazingira
hata kama ni ya uongo kutuaminisha kuwa kulikuwa na ‘mapambano’ kati yake na
muuaji.
Kuchomwa kisu mgongoni kunatoa picha ya kwamba yule kijana maskini wa watu
alifikwa na zahama hiyo wakati akiwa hana hili wala lile. Hata kama alikuwa
akiwakimbia polisi, unaweza kuuliza ni kwanini; jawabu likawa kumchoma kisu, na
si kumpiga ngwala.
Kuuawa kwa kijana huyu ni mwendelezo wa mauji yanayofanywa na baadhi ya
polisi nchini mwetu. Kumbukumbu za karibuni zinaonesha polisi walimuua
Akwilina Akwilini aliyekuwa ndani ya daladala jijini Dar es Salaam. Kuna mchuuzi
kijana mdogo kabisa alikamatwa na kesho yake akawa amefia mikononi mwa
polisi jijini Mbeya. Pia kuna mwingine aliyeuawa mkoani Simiyu.
Mauaji yale ya Simiyu yaliwafanya wananchi wajikusanye kwa wingi na kwenda
kukichoma kituo cha polisi. Kwa wanaowajua vema ndugu zetu wa ukanda huu,
hadi kuchukua uamuzi huo maana yake walichoka! Hili si jambo la kulitazama juu
juu na kuliacha. Lazima tulitafakari kwa lengo la kujua chanzo na tiba yake.
Kabla ya kuendelea na haya ya mwishoni mwa wiki, naomba niwashukuru
wasomaji wote walioniunga mkono kwenye makala iliyopita iliyohusu uamuzi wa
DPP kuwaachia polisi watuhumiwa wa mauaji ya Akwilina.
Nilipokea simu na ujumbe mfupi wa maandishi usio idadi. Wote waliopiga simu na
walioniletea ujumbe mfupi wa maandishi walionesha huzuni kubwa kwa familia ya
Akwilina.
Lakini wapo wasomaji waliosema DPP alikuwa sahihi kwa sababu hata kama
watuhumiwa wangeendelea kushikiliwa, bado wazazi wa Akwilina wasingefaidi
lolote. Wao wakapendekeza kuwa jambo la maana ni kwa Serikali kuwapa kifuta
machozi ‘cha maana’ wazazi wa huyo binti ili walau kwa hicho kitu waweze
kumaliza salama siku zao za kuishi hapa duniani.
Baadhi ya ujumbe ulioletwa kwangu na wasomaji waungwana
ulisema, “Manyerere, ahsante sana kwa makala yako ya DPP na suala la
Akwilina. Kwa hakika inauma sana. Ninasoma makala machozi yananilenga kana
kwamba Akwilina ni ndugu yangu.

“Ninavyojua mimi askari wanapochukua bunduki na risasi huwa wanasaini
wamechukua bunduki ya aina gani na risasi ngapi. Wanaporudisha wanasaini
wamerudisha bunduki walizochukua na idadi ya risasi walizorudisha. Hayo
mengine yoote wanayoyafanya akina Mganga [DPP] ni kuwaona wananchi
hawana akili.”
Msomaji mwingine akaandika, “Ndugu Manyerere hongera sana kwa makala yako
ya leo ndani ya JAMHURI. Wapenda haki tunakuunga mkono na kwa vitendo;
natamani hii makala ingewafikia wazazi wa Akwilina kama ninavyotamani
ungewaita waandishi wa habari uwaambie haya. Bwana awe nawe.”
Muungwana mwingine akaandika, “Habari Bwana Manyerere? Naitwa Kijazi-wa
Majohe. Makala yako ya leo imeniliza. Naamini umewapa faraja kubwa sana
wazazi wa marehemu Akwilina. Umeuvaa uhalisia wa wazazi husika. Mungu
akulinde na mabaya na akujaalie maisha marefu. Hongera sana kwa kujali hisia
za wengine.”
Mwingine akaandika haya, “Hujambo? Nimeilinganisha hotuba ya Mark Anthony
aliyoitoa baada ya kuuawa kwa Julius Caesar na article yako iliopo kwenye
JAMHURI ya kuanzia jana. It’s very touching man!”
Ndugu zangu, hii ni sehemu ndogo mno kati ya kubwa ya ujumbe mfupi wa
maandishi kutoka kwa wasomaji waungwana wa JAMHURI. Jambo moja kubwa
linaonekana kwenye ujumbe wao- hawaridhiki na namna kesi za maskini
zinavyomalizwa!
Hili likiwa bado halijapita, kumetokea mauaji mengine Sirari wilayani Tarime.
Nayajadili haya kulingana na taarifa ya awali ya Jeshi la Polisi, ya kukiri polisi
wake kumuua huyo kijana. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa kukiri kwa polisi
kwa mauaji yanayofanywa na polisi si jambo geni. Ni utaratibu unaorejewa mara
kwa mara, lakini mwishowe imeonekana dhahri kuwa Polisi imekuwa upande wa
polisi wauaji! Tunasubiri kumsikia DPP Mganga kwenye hili.
Nimepata msukumo wa kuyaandika haya kutokana na hamaki ya wananchi baada
ya mauaji hayo. Hapa ikumbukwe kuwa saa kadhaa baada ya mauaji ya kijana
huyo, kulitokea ajali mkoani Morogoro ambako basi lililobeba polisi kutoka
Dodoma liligongana na basi dogo lililopakia wanajeshi. Mwanajeshi mmoja na
mtoto wa mwanajeshi mwingine walifariki dunia.
Nini kilichotokea kwenye mitandao ya kijamii baada ya matukio hayo mawili – ya
Tarime na Morogoro? Mijadala iliyoendeshwa kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa
ya kusikitisha. Wachangiaji wengi waliandika bila kumung’unya maneno wakihoji
ni kwanini amekufa mwanajeshi na mtoto badala ya kufa polisi!
Ndugu zangu, michango hii ya wananchi kwenye mitandao ya kijamii si ya
kupuuzwa. Inatoa taswira ya namna baadhi ya wananchi wanavyoanza kukosa
imani na Jeshi la Polisi. Haya mambo tunapaswa tuyaseme ili wahusika wayajue.
Tusijifanye hayapo, hatuyaoni au hatuyasikii. Chuki ya wananchi kwa Jeshi la
Polisi ipo na inaongezeka.
Hii si mara ya kwanza kusoma maneno makali kwenye mitandao ya kijamii.
Itakumbukwa kuwa polisi walipouawa na wale majahili kule Mkuranga na Kibiti
wapo waliojitokeza waziwazi kupongeza mauaji yale! Haya ni mambo ya ajabu
kuonekana au kusikika kutoka kwenye jamii iliyozoea kuishi kwa upendo. Kwanini
watu wafurahi polisi wanapouawa au kuumizwa? Si bure, kuna jambo.
Kauli hizi za wananchi si za kupuuzwa. Zinapaswa kuwaamsha ‘wakubwa’ ili
wakae na kutafakari wapi kwenye kasoro. Kuna dhana ya kupuuza hisia za watu
kwa kusema “hao ni wapinzani” au “hao ni wahuni tu wa kwenye mitandao ya

kijamii”. Hii si kweli hata kidogo. Chuki ya wananchi kwa Jeshi la Polisi ipo na
inaongezeka.
Kwanini chuki inaongezeka? Kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na
mali zao. Dhima hiyo pekee ilitosha kuwafanya wananchi wakiwaona polisi,
wafurahi! Lakini ilivyo sasa ni tofauti. Polisi licha ya kuwa ni chombo cha maguvu,
maguvu hayo yanaelekezwa kwa wanyonge wasiokuwa na hatia. Polisi walivyo
sasa ni chombo kinachoogopwa na kukimbiwa na wananchi. Wanaogopwa kwa
sababu baadhi yao ni majambazi. Wamo wabambikiaji wa kesi. Polisi kadhaa
wanatuhumiwa kuwa wasimamizi wa dhuluma. Polisi wamekuwa walinzi wa dola
zaidi kuliko wananchi walipa kodi, na mbaya zaidi sasa baadhi ya polisi
wamekuwa wauaji wa raia wasio na hatia.
Tukirejea tukio la Tarime, kulikuwa na sababu gani kumuua yule kijana kwa
kutumia kisu, tena kisu chenyewe kiwe cha mgongoni? Kijana yule alikuwa na
nguvu gani zilizowashinda polisi wote waliokuwa kwenye doria?
Kama nilivyosema kwa Akwilina, bado narejea kusisitiza kuwa haki haina budi
kutendeka kwa maskini na wanyonge wa nchi hii. Majibu mepesi ya kwamba
Tarime au Mkoa wa Mara wakazi wake ni wakorofi hayawezi kuhalalisha mauaji
haya.
Mamlaka za kutoa haki zisimame upande wa wazazi au watoto wa kijana
aliyeuawa. Zitafakari namna ambavyo wangejisikia kama kijana wao ndiye
angekuwa kauawa kwa namna ile.
Natambua kuwa kilichofanywa na yule polisi wa Tarime hakiwezi kuwa ndiyo sura
halisi ya Jeshi la Polisi. Wala hatuna sababu ya kuamini kuwa kuuawa kwake
kumetokana na amri ya wakubwa. Lakini ukisikiliza maelekezo na vitisho vya
‘wakubwa’ unashindwa kabisa kuacha kuhusisha mauaji yale na baraka za
wakubwa. Mbaya zaidi ni pale ambako mnyonge anauawa, lakini hakuna sauti
yoyote ya wakubwa inayosikika kulaani kitendo hicho.
Tuione damu ya kila Mtanzania kuwa ni yenye thamani sawa na Mtanzania
mwingine, na kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa
mwingine nje ya sheria za nchi. Kumkamata kijana aliye baa baada ya muda wa
kuwapo hapo kwisha si kosa la kuhalalisha kuuawa kwake. Hata kama kutaletwa
ngonjera za kwamba aliwatukana polisi, bado matusi kwa walinzi hao wa amani
malipo yake hayawezi kuwa ni kifo. Hakuna.
Mwito wangu; mosi, Jeshi la Polisi liache mauaji ya raia wasiokuwa na hatia. Pili,
vijana wanaoajiriwa wafanyiwe uchunguzi wa kina (vetting) ili kujua historia zao
tangu wakiwa shule za msingi. Kigezo cha kwamba kijana aajiriwe kwa sababu
katoka JKT hakisaidii kupata vijana makini na wenye kujua au kuzingatia maadili
ya upolisi.
Tatu, matumizi ya nguvu yaliyopitiliza yaachwe. Nguvu zitumike kulingana na
ukinzani wa mshukiwa. Somo la haki za binadamu ikiwezekana lipewe uzito
unaostahili kwenye mtaala wa mafunzo ya Jeshi la Polisi. Miaka 57 ya Uhuru
hatuwezi kuruhusu kuendelea na mitaala ya kikoloni ambayo kwayo
kilichozingatiwa ni maguvu baadala ya weledi.
Nne, kama iliwezekana kulifumua jeshi la kikoloni la KAR na kuundwa kwa Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), basi tusione tabu kufanya hivyo kwa
Jeshi la Polisi ili tuwe na jeshi linalotambua na kuthamini maisha ya raia.
Tano, kama ilivyo kwa wahalifu wengine, polisi wanaoua raia wasio na hatia
washughulikiwe kwa mujibu wa sheria; na wananchi waone kweli haki
imetendeka.

Sita, muhimu zaidi ni kwa wadau wote kuja na suluhu ya kurejesha hali ya upendo
wa raia kwa Jeshi la Polisi. Hii habari ya wananchi kushangilia pindi polisi
wanapofikwa na mambo mabaya si nzuri hata kidogo. Naamini tukiyazingatia
haya na mengine yenye tija Jeshi la Polisi litakuwa kweli ni jeshi lenye kuyalinda
maslahi ya wananchi. Ilivyo sasa polisi ni maadui wananchi. Tusiruhusu hali hii
iendelee. Inajenga chuki, si kwa polisi tu, bali kwa Serikali. Tuwe na polisi
wanaokaribishwa, wanaoshangiliwa na wanaopendwa; badala ya sasa ambako
polisi wakionekana tu raia wanaona wamekutana na adui. Nauliza, walinzi wa
amani wanapokuwa wauaji, raia wanyonge wakimbilie wapi kwenye usalama?