Rais John Pombe Magufuli amelipongeza gazeti la JAMHURI na kulitaja kama gazeti mfano wa kuigwa nchini kutokana na habari zake za uchunguzi uliobobea.

Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Rais Magufuli amelipa gazeti la JAMHURI  heshima ambayo haijapata kutolewa kwa gazeti lolote tangu nchi hii ipate uhuru mwaka 1961.

Rais Magufuli alianza kwa kusema: “Nipende pia kuchukua nafasi hii kuvipongeza vyombo vya habari. Vyombo vya habari mmetusaidia sana. Mmeisaidia sana Serikali hii, naomba msichoke. Naomba msichoke. Mnatoa elimu ya kutosha, mnatoa maelekezo ya kutosha, na sisi ndani ya Serikali huwa tunafuatilia.

“Juzi juzi kuna gazeti moja liliandika. Ni Gazeti gani la? La JAMHURI . Likawa linatoa michoro ya huko, tukawa tunaulizana na Waziri Mkuu, hawa wamejuaje sisi tunapanga mikakati na wao wameshajua? Tunawapongeza. Vyombo vya namna hiyo ndivyo vinatakiwa kufanya. Siyo vyombo ambavyo vinakaa pale kwa ajili ya kuitafu… kuitukana Serikali na Tanzania.

“Sisi Watanzania hatuna mahali pengine pa kwenda kukaa. Yako kwa kweli magazeti mengine yanavyoandika mpaka unashangaa. Unajiuliza huyu ni Mtanzania au siyo Mtanzania? Yeye kila kitu ni kuichafua tu Tanzania. Kana kwamba yeye pakitokea machafuko hapa ana mahali pengine pa kwenda kukaa.

“Lakini kwa ujumla vyombo vingi vya habari, vimekuwa very supportive kwenye government hii. Nawapongeza sana keep it up. Na ndiyo maana nimeweza kutoa mfano, nimetoa mfano wa gazeti la JAMHURI  lilivyotoa uozo kule kwenye flow meter. Tunataka magazeti mfanye hivyo. 

“Pakitokea kuna uozo mahali, uandike. Sisi tunasoma. Sisi wote ni Watanzania, sisi wote tuna wajibu wa kuipeleka Tanzania mbele. Na tuiweke Tanzania yetu kwanza. Hakuna mtu anayeisemea uzuri wa Tanzania. Ni vema sisi Watanzania, tuisemee Tanzania mazuri ili hata wa nje watatusemea mazuri. Nawashukuru sana waandishi wa habari.”

Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI , Deodatus Balile, alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi alisema: “Rais Magufuli ametupa heshima ya aina yake. Tangu nchi hii ipate uhuru, haijapata kutokea Rais aliyepo madarakani akatambua kazi ya gazeti lolote kwa kulitaja jina. Rais Magufuli ameweka historia mpya, nasi tunafarijika na tunamshukuru mno kwa kutambua kazi yetu.

“Wakati tunaanzisha gazeti hili miaka mitano kasoro kidogo iliyopita, tulisema tunataka kuanzisha chombo kitakachofanya uchunguzi, kikawa na mawazo huru, na tukachagua kaulimbiu kuwa ‘Tunaanzia Wanapoishia Wengine’. Tumejipanga kwa dhati kufanya kazi ya habari za uchunguzi wenye matokeo chanya kwa jamii, na nasisitiza kuwa tunafarijika Rais anapotambua mchango wetu.

“Tunawashukuru wanahabari wenzetu, ambao mara kadhaa hutupa mawazo tuchunguze nini, wasomaji wetu waliotuwezesha kuendelea kuwapo sokoni kwa kulinunua gazeti letu linaloongoza kwa habari za uchunguzi na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa kutuwezesha katika mafunzo ya habari za uchunguzi, na tunawaahidi Watanzania kuwa hatutakata tamaa, hatutachoka, tutaendelea kuijenga nchi yetu kupitia habari za uchunguzi. Nasema asante sana Rais Magufuli kwa heshima uliyotupa.”

Kwa mchakato jinsi JAMHURI  ilivyofuatilia kwa kina habari za Bandari, soma ukurasa wa 14 na 15 wa toleo la leo.

1405 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!