Kesi inayowahusisha makamishna wawili wa polisi wanaogombea nyumba – Kamishna Suleiman Kova na Kamishna Msaidizi Mwandamizi Godfrey Nzowa inaendelea kesho mahakamani.

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Makumba  Kimweri, alipuuza maagizo ya Rais Dk. John Magufuli na kuzalisha mgogoro wa nyumba kati ya makamishna hao, ambao hadi sasa upo mahakamani.

JAMHURI imefuatilia sakata hilo kubaini kinachoendelea. Desemba, 2001 Jeshi la Polisi lilifanya uhamisho kwa maafisa wake ambao ni Suleiman Kova aliyekuwa RCO Arusha na kupelekwa Mkoa wa Kigoma na Godfrey Nzowa aliyekuwa RCO Kigoma akahamishiwa Mkoa wa Arusha.

Katika uhamisho huo, Henry Salewi aliyekuwa OCD Katesh alihamishiwa Arusha na Eliuko Elihaki naye alihamishiwa Arusha katika Kitengo cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU).

Baada ya uhamisho wa maafisa hao wa Polisi, Kamanda Nzowa alibadilishana makazi na Kamanda Kova ambaye alikuwa anaishi katika nyumba ya Serikali iliyotengwa kwa ajili ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), na Kova alikwenda kuishi nyumba aliyokuwa akiishi Nzowa mkoani Kigoma.

Baada ya uhamisho huo kukamilika na kila mmoja kuripoti katika kituo chake cha kazi, Mei 1, 2002 katika sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) zilizofanyika kitaifa Mkoa wa Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alitangaza Serikali kuuza nyumba zake kwa wafanyakazi.

“Wakati Rais Mkapa akihutubia, alieleza kuwa Serikali inatazamia kuuza nyumba zake na kipaumbele ni kwa wafanyakazi wa Serikali wanaoishi katika nyumba hizo, hivyo wafanyakazi walijaza fomu za kununua nyumba walizokuwa wakiishi,” zinaonesha kumbukumbu za kesi inayoendelea Mahakama ya Rufaa.

Mwezi huohuo, Kamanda Nzowa alienda Ujenzi kufuatilia utaratibu wa kupata nyumba hizo ambapo alielezwa kuwa bado hawajapata maelekezo kutoka juu, lakini SSP Salewi na Elihaki walipewa ofa ya kununua nyumba hizo wakati Nzowa akijibiwa hivyo.

Wakati Kamanda Nzowa akihangaika kupatiwa ofa ya kununua nyumba Na. 203 aliyokuwa akiishi iliyobadilishwa baadaye na kuwa Na. 140 iliyopo Barabara ya Sekei, alipata taarifa kuwa Kova tayari amejaza fomu kwa ajili ya kununua nyumba hiyo.

Kutokana na taarifa hizo, Nzowa aliwasiliana na Mkuu wake wa kazi wakati huo, IGP Omari Mahita, na kumweleza sakata hilo, jambo lililomlazimu Mahita kuwasiliana na Waziri wa Ujenzi wakati huo, Dk. Magufuli.

Mei 30, 2002, IGP Mahita alimwandikia Waziri wa Ujenzi kumfahamisha malalamiko yenye Kumb. Na. PHQ/PS/12316/A/43 ambayo ilimweleza kuwa Nzowa ndiye anayeishi katika nyumba hiyo, na ndiye anayepaswa kuinunua maana Kova tayari alishahama mkoa huo.

Juni 19, 2002 Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, John Kijazi, alimwandikia IGP Mahita barua yenye Kumbu Na. CCA.96/288/01/136 ambaye alisema: “Nimeelekezwa na Waziri wa Ujenzi kujibu barua yako kuwa Nzowa ndiye anayepaswa kununua nyumba hiyo na allocation ya nyumba hiyo kwa Kova imefutwa, kwa sababu mtumishi wa Serikali hawezi kununua nyumba mbili.”

Kijazi alieleza masikitiko yake ya ukiukwaji wa kanuni za utumishi serikalini na kueleza kuwa tayari wamefanya utaratibu wa Nzowa kununua nyumba hiyo.

Katika hali ya kustaajabisha, Kamanda Kova alijaza fomu ya kuomba kununua nyumba hiyo aliyodai ni makazi yake Mei 27, 2002 wakati aliyekuwa anaishi katika nyumba hiyo ni Nzowa.

Pamoja na kujaza fomu za kununua nyumba hiyo, Kova alitoa fedha za kuinunua wakati Nzowa akiishi humo.

JAMHURI ilipowasiliana na Kamanda Nzowa kupata ufafanuzi, alisema kesi ipo mahakamani na hilo anaweza kulizungumzia pale tu kesi itakapokuwa imehitimishwa na imepangwa kusikilizwa Februari 17, 2016 katika Mahakama ya Rufaa. 

By Jamhuri