Wingu zito limegubika hatima ya kesi inayowahusu wafanyabiashara matajiri wanaotuhumiwa kumuua John Massawe, katika Kijiji cha Kindi, Kibosho mkoani Kilimanjaro.

Watuhumiwa watatu kati ya watano walikamatwa hivi karibuni mkoani Mwanza na kurejeshwa Moshi, kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani.

Masawe aliuawa kikatili Juni 9, 2009 kijijini hapo, lakini baadaye watuhumiwa wa mauaji hayo wakaachwa. Waliokamatwa na kuwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi ni John Kisoka (Magazeti) na mkewe ambaye jina lake halikuweza kufahamika. 

Mwingine ni mdogo wake John aitwaye Deo Kisoka. Wanaoendelea kusakwa ni Lucas Joseph Kisoka na Musa Joseph Kisoka; ambao wanadaiwa kukimbia baada ya kupata taarifa za kutafutwa.

Katika hatua iliyoanza kuwatia shaka ndugu wa marehemu John Massawe, jalada la kesi hiyo limekwamia katika Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) jijini Dar es Salaam tangu lilipopelekwa huko Januari 20, mwaka huu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI). 

Kukwama kwa faili hilo kumeibua minong’ono mingi ya kuwapo mipango mahsusi ya kuvurugwa kwa kesi hiyo kama ilivyotokea awali.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Ofisi ya DPP imerejesha jalada hilo kwa DCI mara tatu akihoji mashahidi wengi kuwa ni wapya. 

Hata hivyo, ukweli wa jambo hilo ni kwamba uchunguzi huo wenye mashahidi wapya ni mpya baada ya jalada la awali lililokuwa na maelezo ya mashahidi kuibwa katika Ofisi ya RCO Kilimanjaro. 

Pili, watuhumiwa waliokamatwa sasa ndiyo wanaodaiwa kuwa wahusika wakuu kwenye kesi hiyo ya mauaji. Walitoroka nchini mwaka 2009 na kurejea mwaka 2012 baada ya PI ya kwanza kukosa nguvu na kufutwa kutokana na watuhumiwa kuwa hawajakamatwa.

Tatu, mauaji haya yanadaiwa kufanyika hadharani kijijini, hivyo wanakijiji wengi waliyashuhudia na walijaribu kuwaokoa vijana wanne waliokuwa wakiteswa pamoja na John.

Nne, polisi ndiyo wahusika wakuu katika upelelezi na walikuwa na maslahi binafsi katika suala hilo na ndiyo maana waliondoa baadhi ya maelezo ya mashahidi na pia kughushi ripoti ya kifo cha John. 

Tano, chanzo cha habari kinasema DPP anatakiwa ajue ushahidi huo madhubuti unatokana na uchunguzi mpya uliofanywa na makachero wa Ofisi ya DCI bila kuwahusisha polisi wa Kilimanjaro, ikiwa ni baada ya ndugu kumwandikia barua Rais John Magufuli na kuonesha kutokuwa na imani kabisa na polisi mkoani humo.

Pia chunguzi wa aina hiyo unaelezwa kuwa si wa kwanza kufanywa na Ofisi ya DCI na ushahidi mpya kupatikana, kwani mwaka 2000 kuna kesi inayofanana na hii ya sasa ambako polisi walivuruga upelelezi ili kuwabeba watuhumiwa wawili waliokuwa marafiki wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wa wakati huo, Omar Mahita, na Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kilimanjaro, Dk. Mohamed Chicco.

DCI alifanya upelelezi upya na ushahidi mpya na madhubuti (kama wa kesi hii ya sasa) ulipatikana ukihusisha pia mashahidi wapya na DPP akapekeka kesi mahakamani lakini washitakiwa walikuwa wameshatoroka nchi. Hati ya kuwakamata watuhumiwa bado ipo.

“Inavyoelekea kwenye hili suala DPP hana taarifa na mchezo unaoendelea, sisi tunapata wasiwasi kwa sababu huku (Moshi) kuna tambo mitaani kwamba vita inapiganwa nje ya rumande, na kwamba kuna fungu limetengwa kufanikisha ushindi. Hatutaki kuamini mambo haya, lakini lisemwalo lipo maana watuhumiwa ni matajiri na wana ndugu na marafiki wenye uwezo mkubwa sana kifedha,” kimesema chanzo chetu.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa DCI na timu yake wamefanya kazi ya ‘kutukuka’ na kwa kupata mashahidi 17 wakiwamo walioshuhudia mauaji yale. 

Uchunguzi huo mpya ulitokana na jalada la mwanzo lenye maelezo ya mashuhuda kuibwa kutoka ofisi ya RCO Kilimanjaro.

“Minong’ono ni mingi, mara zimetengwa Sh milioni 100 suala liishie hapo hapo ofisi ya DPP ndiyo maana kuna kigugumizi. Taarifa ni kuwa DPP amelirudisha jalada hilo kwa DCI mara tatu akihoji mashahidi wengi mbona ni wapya,” kimesema chanzo cha habari.

Msemaji wa familia ya John, Beda Massawe, alipoulizwa na JAMHURI kuhusu suala hilo, amesema hawajui ni kwanini suala hilo bado linasuasua.

“Bado tuna imani kubwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano na bila shaka kesi hii itafikishwa mahakamani ili haki iweze kutendeka kwa ndugu yetu aliyeuawa kinyama wakati wananchi ambao sasa ni mashahidi wakishuhudia,” amesema Massawe.

Juhudi za kumpata DPP, Biswalo Mganga, ili kuzungumzia kesi hii zinaendelea.

2257 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!