ffUfisadi mpya na mwanya wa wizi wa mapato makubwa ya Serikali umebainika kufanywa kwenye uingizaji wa gesi, mafuta ya kula, mafuta ya magari na mafuta ya viwandani nchini kutokana na kupuuzwa kwa matumizi ya mita (flow meters).

Katika eneo la Kurasini Oil Jet (KOJ) Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ilifunga mita 16 mwaka 2004 kuhakiki kiwango cha shehena za mafuta ya aina mbalimbali yanayoingizwa nchini wahusika walipe kodi na ushuru stahiki.

Wakati mita hizo zilipoanza kutumika, mapato yalipanda kutoka Sh bilioni nne hadi Sh bilioni 60 kwa mwezi.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa pamoja na ukosefu wa mita, Shirika la Tanzania Italy Petroleum Refinery (TIPER) – ambalo ni la ubia kati ya Tanzania na Italy, linahusishwa na hujuma ya wizi wa mafuta.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa TIPER ambayo haiagizi mafuta kutoka ng’ambo, imekuwa ikitumia moja ya kampuni maarufu nchini kuuza mafuta ambayo upatikanaji wake unahusishwa na wizi huo unaoendelea bandarini.

Kampuni hiyo ambayo kwa sasa inaendeshwa na raia wa kigeni, imejenga uzio mkubwa ambao ndani imebainika kuunganisha mabomba kinyemela kutoka kwenye mabomba yanayoshusha mafuta kutoka kwenye meli.

Waagizaji mbalimbali wa mafuta nchini wamekuwa wakilalamikia wizi huo, lakini duru za uchunguzi zimebaini kuwa hujuma hiyo imekuwa ngumu kukomeshwa kutokana na kuwashirikisha watu maarufu-miongoni mwao wakiwa katika idara nyeti serikalini na wengine ambao kwa sasa ni wastaafu serikalini.

Malalamiko kuhusu wizi wa mafuta yalianza miaka mitano iliyopita, na hilo linathibitishwa na barua ya Novemba 7, 2012 na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER.

Barua hiyo iliitaka TIPER iondoe mara moja bomba lenye upana wa inchi 18 lililounganishwa kinyemela. Barua hiyo ilikuwa ni majibu kutokana na barua ya TIPER ya Oktoba 12, mwaka huo iliyokuwa ikipinga agizo la TPA la kuitaka ifungue bomba ililojiunganishia.

Hata hivyo, JAMHURI imebaini kuwa pamoja na ‘mrija’ huo, kuna ‘mirija’ mingine mitano yenye ukubwa mbalimbali ambayo TIPER imeiunganisha kwenye mabomba makuu yanayosafisha mafuta kutoka kwenye meli.

Vyanzo vya habari vimedokeza kuwa, TIPER kwa kuhakikisha haiguswi, imejenga uzio mkubwa ambao hakuna mtu yeyote asiye wa TIPER anayeruhusiwa kuingia ndani, wakiwamo wafanyakazi wa TPA.

“Ni ukuta mkubwa, hakuna anayeruhusiwa kuingia ndani kuona kinachoendelea. Mabomba yaliyounganishwa yamefichwa ndani ya ukuta huo. Wameweka ukuta kuzuia kujua kinachofanywa ndani.

“TIPER hawaagizi mafuta, wanatumia maeneo ya kuhifadhia mafuta ya kampuni nyingine na kuwatoza wenye mafuta. Tulitaka miundombinu hii irejeshwe serikalini, lakini tumegonga mwamba. Kuna wakubwa wengi wanalijua hili, lakini nani asiyejipenda anayeweza kupambana na haya mambo?” Kimehoji chanzo chetu.

Habari za uhakika zinaonyesha kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi walianzisha mchakato wa kununua hisa za TIPER kwa nia ya kuwaondoa nchini Wataliano hao ambao kwa sasa hawafanyia kazi ya msingi ya kusafisha mafuta iliyowaleta nchini, lakini waligonga mwamba.

“Mchakato ulikwenda vizuri, hadi mkataba wa makabidhiano ukaanza kuandaliwa, lakini ghafla tukasikia taarifa kuwa ofisi kuu imeagiza suala hilo liachwe liendelee kama lilivyo. Kwa kweli tulisikitika mno. Tunaamini Rais [John] Magufuli ataliingilia hili, hapa kuna mapato mengi yanapotea kwa TIPER kuendelea kushikilia matangi ya kuhifadhia mafuta peke yake wakati kampuni ina ubia na Serikali,” kilisema chanzo chetu kingine.

Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita timu ya uchunguzi ya JAMHURI ilizuru eneo hilo na kukuta ubomaji wa ukuta ukitekelezwa na kujengwa seng’enge.

Wizi wa mafuta katika eneo hilo unathibitishwa na aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu katika Wizara ya Nishati na Madini, Injinia Paul Masanja.

Barua yake ya Novemba 26, mwaka jana kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, inaeleza upotevu wa mafuta mengi kutoka kwenye eneo ambalo meli zinatia nanga (SPM) na pia katika eneo la Kurasini Oil Jetty (KOJ).

Hatua ya Masanja inatokana na kikao cha Desemba, 2014 kilichohusisha kampuni zinazouza mafuta (OMC) kupitia kwa Mratibu wa Uagizaji Mafuta (PICL).

Kikao hicho kilijadili upotevu wa mafuta na kufikia suluhisho la kuundwa kwa Kamati kupata ufumbuzi wa kero hiyo.

Masanja, katika barua yake aliandika mapendekezo kadhaa, likiwamo la kuitaka TPA ishirikiane na TIPER kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye ‘mirija’ ya TIPER; jambo ambalo TPA walilipinga wakisema kampuni hiyo haikupaswa kushirikishwa kwa kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa wakuu wa wizi wa mafuta.

 

Flow Meter zimehujumiwa?

Sakata la kusitishwa kwa matumizi ya flow meter lilianza mwaka 2011 wakati ambao Wakala wa Vipimo (WMA) alipozuia utumiaji wa mita hizo kwa madai kwamba hazifai kwa matumizi ya kupima mafuta yatokayo melini. Mita hizo ni mali ya TPA.

Kamishina ya WMA, Magdalena Chuwa, alichukua uamuzi wa kusitisha matumizi ya mita hizo kupitia barua yake ya Februari 02, 2011 kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA.

WMA walitoa sababu kadhaa za uamuzi huo, zikiwamo kwamba mita hizo zilikuwa zikifanya kazi katika kiwango cha nyuzijoto sentigredi 15 badala ya 20; na kwamba zilikuwa kwa ajili ya kujaza na si kupakua mafuta.

Dosari hiyo, kwa mujibu wa WMA, ilisababisha usumbufu mkubwa wa foleni kwa wateja na hivyo kuongeza gharama za bei ya mafuta kwa watumiaji na kuikosesha mapato TPA na Serikali.

Uamuzi huo wa WMA uliibua msuguano mkali kati yake na TPA ambao waliamini kuwa usitishwaji wake ulikuwa na athari kubwa mno kutokana na kuikosesha mapato yatokanayo na ushuru na pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukosa fedha.

Matumizi ya mita yaliafikiwa na Serikali kutokana na ushauri wa Bunge baada ya kubaini upotevu mkubwa wa mapato kwenye mafuta yanayoingizwa nchini kutokana na udanganyifu wa wafanyabiashara.

Hatua hiyo iliilazimu Serikali kuagiza matumizi ya vipimo vya uhakika zaidi badala ya ukadiriaji au kupokea taarifa kutoka kwa waagizaji pekee.

Pia hatua hiyo ililenga kuongeza mapato ya ushuru kwa TPA na kodi kwa Serikali. Hoja nyingine kubwa ilikuwa ni kwa Serikali kuwa na kumbukumbu sahihi za mafuta yanayoingizwa nchini.

Tangu wakati huo mita zilipositishwa, mafuta yamekuwa yakiingia nchini kwa kupimwa na kijiti (deep stick) na kuangalia ukubwa wa matangi yanakohifadhiwa.

Ufungaji wa mita hizo ulikamilika mwishoni mwa mwaka 2004 na kuanza kutumika mapema mwaka 2005.

TPA iliandaa mafunzo kwa wadau muhimu kwenye sekta ya biashara ya mafuta ambao ni TRA, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), WMA na TIPER.

Mei, 2010 TRA iliiandikia TPA barua ikidai kuwa mita hizo zilikuwa na matatizo, hasa kwenye mita za mafuta ya dizeli; wakati ambao TPA ilikuwa imebadilisha matumizi ya bomba la mafuta ghafi yaendayo TAZAMA ili kusafirishia mafuta ya dizeli.

Uchunguzi unaonyesha kuwa matumizi ya mita yalisaidia mno kuongeza ukusanyaji mapato kwa kiwango cha juu hadi ilipofika Februari 2011 ambako WMA walipoamua kusitisha matumizi ya mita hizo wakidai kwamba hazifai.

Ilielezwa kuwa WMA waliukataa mfumo wa upimaji mafuta unaoitwa Accuload III kwa madai kuwa haufai, badala yake TPA waweke mfumo mpya unaoitwa Sybertrol. Mifumo yote imetengenezwa na kampuni moja.

Kamati ya wataalamu iliyoundwa kuchunguza suala hilo hawakukubaliana na kubadilisha mfumo ambao TPA walikuwa wameona unafaa.

TPA ilichukua hatua za kujirisha kama kweli mfumo huo haufai; na ikaamua kuwasiliana na wataalamu kutaka ufafanuzi kuhusu ubora kati ya mifumo hiyo miwili.

Uchunguzi wa JAMHURI kupitia nyaraka za mawasiliano unaonyesha kuwa wataalamu walijibu kuwa mfumo wa Accuload III ni wa kisasa na unafaa zaidi kwa matumizi ya vipimo. Baada ya majibu hayo, TPA iliomba wataalamu wafike nchini kuikagua na kufanya marekebisho kama yangehitajika.

Wataalamu wa mifumo yote miwili walifika nchini Agosti, 2011 na kutoa ufafanuzi mbele ya wadau ambao ni wawakilishi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uchukuzi, WMA, TBS, EWURA na TPA.

“Wataalamu waliweza kutoa majibu juu ya masuala yote yanayowatatiza WMA kuhusu mifumo hiyo miwili na faida za Accuload III.

“Pamoja na juhudi zote hizo, WMA walisema kuwa kuleta wataalamu siyo sababu zitakazowafanya waruhusu mita kutumika,” kilisema chanzo chetu.

Mzunguko wote huo kwa wakati huo, yaani ukaguzi wa mita, ununuzi wa vipuri na matengenezo viligharimu dola 260,000 za Marekani. Kiwango cha dola moja ya Marekani kwa wakati huo kilikuwa Sh 1,600.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Rished Bade alishawahi kukiri kuwa ukusanyaji kodi ulikwamishwa na wahusika kukingiwa kifua na baadhi ya wakubwa serikalini.

 

Ukwepaji kodi

 Desemba 2013, iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma (PAC), ilifichua udanganyifu na mianya mikubwa ya ukwepaji kodi katika TRA.

 Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini-CHADEMA) (sasa Mbunge wa Kigoma Mjini-ACT), Kabwe Zitto, alisema kuwa pamoja na TRA kufikia malengo kwenye makusanyo ya kodi katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, bado kulikuwapo udanganyifu na mianya ya ukwepaji kodi katika maeneo kadhaa.

Eneo kubwa alilolitaja ni la kusitishwa kwa matumizi ya mita za kupima ujazo wa mafuta yanayoingia nchini kupitia kituo cha kupakulia mafuta cha Kurasini, Dar es Salaam.

 Kamati iliitaka Serikali kulieleza Bunge sababu za msingi za kusitisha matumizi ya mita hizo na TRA kuainisha athari katika ukusanyaji wa mapato baada ya kusitishwa kwa matumizi ya mita hizo.

Alisema TPA baada ya kusitisha matumizi ya mita hizo ilitumia vijiti vya kupimia ambavyo vipimo huchukuliwa wakati mafuta yako kwenye meli na baada ya kuwekwa kwenye matangi ya wafanyabiashara walioyaingiza mafuta hayo.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika taarifa yake ya 2010/2011 alihoji sababu za kusitisha matumizi ya mita hizo katika bandari za Tanga na Dar es Salaam.

Kamati iliwahoji maofisa masuuli wa TPA walioeleza kuwa mita hizo zilinunuliwa mwaka 2004 na TPA na kufungwa katika kituo cha kupakulia mafuta cha Kurasini (KOJ) na kuanza kutumika mwaka 2005 kwa lengo la kupima kiwango cha mafuta yanayoingizwa nchini kupitia Bandari za Tanga na Dar es Salaam.

Februari 2011, WMA iliyoridhia awali matumizi ya mita hizo, iliwaandikia barua TPA kusitisha matumizi ya mita hizo.

TPA kwa upande wao walisema mita hizo hazina matatizo yoyote na zinaweza kuendelea kutumika, lakini WMA wakasisitiza kuwa mita hizo hazitoi vipimo sahihi.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Shirika linalojihusisha na masuala ya uchumi la nchini Marekani la GFI mwaka jana ilionyesha kuwa Tanzania inapoteza Sh trilioni 3 kila mwaka kutokana na ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za uchimbaji madini na katika uingizaji bidhaa na kuuza nje.

Repoti hiyo ilibaini udanganyifu mkubwa katika uingizaji mafuta ya kuendeshea mitambo na magari kwa migodi mbalimbali nchini.

Kiwango hicho cha ukwepaji kodi kwenye eneo hilo ni sawa na asilimia 16 ya bajeti ya Serikali na ni mara tatu ya kile ambacho Serikali ilitangaza kukopa kupitia mashirika ya mikopo yenye masharti nafuu katika bajeti yake ya mwaka 2014/2015.

 

Kifo cha Ofisa EWURA utata

Meneja Biashara wa Petroli wa EWURA, Julius Gashaza, Mei mwaka juzi alikutwa amekufa hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kutoka Dodoma ambako alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti.

Meneja huyo, alikuwa mpangaji bei za mafuta za kila mwezi. Alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na EWURA kwenda kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Mfuko wa Barabara.

EWRA walionyesha takwimu za mafuta yaliyokuwa yanaingia nchini kuwa ni mengi kuliko zilizotolewa na TRA, hali inayodaiwa kuwa Gashaza alipewa vitisho vya ajabu baada ya ripoti hiyo. Alikutwa amejinyonga kwa kutumia tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo Vituka, Temeke.

Kamati ya Bunge ya Bajeti, iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ilikutana na maofisa wa EWURA, akiwamo Gashaza na wale wa TRA na kugundua kuwapo kwa tofauti katika takwimu za kiwango cha mafuta kilichostahili kutozwa kodi.

Takwimu za EWURA ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi ya zile zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe takwimu za TRA.

Baada ya kurejea Dar es Salaam Gashaza hakwenda nyumbani kwake na badala yake alikwenda kwenye hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako mkewe na ndugu yake mmoja walimfuata na akawambia kuwa anatishiwa maisha.

 

 Flow meter ya dizeli yafungwa

 Wakati hayo yakiendelea, TPA imetafuta fedha nyingine kiasi cha Sh bilioni 11, na kuamua kununua na kufunga mita nyingine ya kupima mafuta ya dizeli katika eneo la Mji Mwema, ambayo sasa iko tayari kupima mafuta ya dizeli.

Hata hivyo, wadau wanasema kwa mafuta ya petrol, taa, mafuta ya kula, ya mitambo na mengine kuendelea kuingia nchini kwa utaratibu wa kupimwa kwa kijiti, Serikali inapoteza mapato mengi ajabu.

Wanasema ikiwa mita 16 zilizopo KOJ zina matatizo, ni bora uanzishwe uchunguzi mpya utakaoruhusu marekebisho ya mita hizo na zile zilizoko Tanga ambazo ziligharimu mabilioni ya fedha lakini zote hazitumiki na nchi inaendelea kupoteza mamilioni ya fedha kwa mafuta kupimwa kwa kijiti ambayo ni teknolojia zaidi ya miaka 200 iliyopita.

3893 Total Views 2 Views Today
||||| 8 I Like It! |||||
Sambaza!