Rais Magufuli ameimarisha Bandari – Kakoko (2)

Wiki iliyopita makala hii iliishia katika eneo ambalo Mkurugenzi Mkuu, Injinia Deusdedith Kakoko, alisema kila mkurugenzi na meneja wa ngazi yoyote anayefanya kazi Bandari amepewa malengo ya kutimiza. Lengo kuu ni kukusanya Sh trilioni 1 katika mwaka huu wa fedha. Katika makala hii Injinia Kakoko anaelezea kuhusu hatima ya watendaji wazembe watakaoshindwa kufikia malengo. Endelea…

Wakati tukipunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa kila meneja, kila bandari, kila mkurugenzi ni lazima, kila meneja wa bandari atuletee na ukifanya vizuri, tunakupa motisha, ukifanya vibaya, uhakika wa mwaka wa fedha kwamba utaisha wewe ukivuka ni meneja wa bandari ni mdogo sana.

Kwa hiyo, ile fyeka fyeka fyekelea mbali, lazima itumike. Haiwezekani wewe unakuja na visingizio. Mimi nadaiwa na Bodi, Bodi inadaiwa na Msajili wa Hazina na Wizara kwa niaba ya Serikali, sasa lazima na mimi nikudai.

Kwa hiyo kabla ya mimi sijafyekelewa mbali, basi lazima tutaanza na wewe. Kwa hiyo Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, ambaye yupo ngazi ya mkurugenzi sasa, Meneja wa Bandari ya Tanga, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, zote kwa sababu ni mmoja, yeye na bandari zake zile zote ndogo ndogo, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Meneja wa Bandari zote za Ziwa Nyasa, kila mtu amepata share yake ya kuchangia, na kila mwezi tunakutana kukubaliana.

Hiyo ndiyo serikali ya ‘Hapa Kazi Tu’, serikali ambayo ina miaka mitatu madarakani. Kila mtu atapimwa, na wewe mwenyewe utaamua kama uendelee na hiyo nafasi au hata mimi kama Mkurugenzi Mkuu, niseme kazi imenishinda nitoke.

Kwa hiyo, ni vizuri tukafanya hivyo kuwa na upimaji. Kwa hiyo, haya ndiyo mafanikio tuliyoyapata, na hizi ndizo mbinu tulizozitumia kwenye maeneo yote. Na tumesema miradi hii tutaisimamia, najua yako maeneo ambayo yanakuwa mbali au yanakuwa na changaoto, baadhi ya magati yamejipanga, yako mbali, lakini tumejipanga kwamba miradi yetu yote haichelewi.

Tulikuwa na changamoto kubwa sana. Baadhi ya miradi unakuta makandarasi ndio wanapata kazi hapa, na wamezoea. Wengine ma-supplier wa spare parts wapo Kariakoo hapo na Kinondoni. Sasa tumeishawambia wakae mkao wa kufyekelewa mbali na wenyewe.

Wewe umeambiwa leta vipuri, sasa wewe kwa sababu ya kuzoeleka na umangimeza, badala ya kuleta vipuri muda tuliokubaliana mwezi mmoja, wiki nne, unafika wiki ya sita ndiyo unaomba kuongezewa muda.

Hao wote wajihesabu hawatafanya biashara na TPA. Popote wanapotusikia, huko Kariakoo, kama walizoea kuwa Bandari ndiko chakula chao kinapatikana cha kampuni, wengine hata kampuni hawana wamekuwa na briefcase, wote tutawaondoa. Hawatapata kazi, watusikie.

Kwa hiyo makandarasi nao walizoea. Wako makandarasi wengi sana ambao tumewaondoa. Na wengine wametuibia, tunafanya mazungumzo nao. Tena wengine walituibia wakakimbilia mahakamani. Tumewabana kule tumeimarisha kitengo chetu cha sheria, sasa hivi hakuna kesi tunashindwa.

Rekodi inaonyesha katika miezi sita hii iliyopita, hata wale waliokuwa wamekaribia kutushinda wamejiondoa na wanarudi tunazungumza nje. Sasa kama tulichelewa au tulipoteza sehemu yetu ya msimamo kisheria, tutazungumza tuelewane. Lakini ile pesa uliyokuwa unatudai hatutakupa. Tutakupa halali yako kama kweli tumekukosea.

Na tunataka tusiwe na kesi za aina yoyote na tukiwa na kesi zote tushinde mahakamani. Na tunadhani kama tuna imani na mahakama yetu na inatenda haki, manake kulikuwa na msemo zamani kuwa: “Serikali haishindani na mtu yeyote, Serikali itashindwa tu.” Na sisi tutakapojitetea tukaona jaji hatutendei haki, hatutaacha pia tukaishia hapo, tutakata rufaa.

Na kama tutakuta mpaka kwenye rufaa inakuwa kuna tatizo, basi tutapiga kelele sana, hatutakubali kuonewa. Hiyo ndiyo TPA ya sasa inayosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Tutafanya maamuzi sahihi, ili tusisababishe kesi, na wewe ukituonea, maana wapo watu walikuwa wanatuonea mpaka kwenye viwanja, basi tutapambana na wewe mpaka kwenye mahakama za rufaa na tutahakikisha kwamba tunapata haki zetu.

Kwa hiyo, ni eneo ambalo limetusaidia pia, kwenye miradi, ili miradi ikamilike haraka kwa sababu kama miradi isipokamilika haraka unaongeza gharama na nadhani ni vizuri wadau wetu, tunawapenda makandarasi na suppliers wanatusaidia, lakini waache mambo ya uzembe, au mambo ya kubahatisha, wafanye kazi kwa uhakika.

Kwa hiyo ndugu waandishi nadhani, hayo ndiyo maelezo ya jumla. Naweza kuangalia baadhi ya maeneo ambayo mlikuwa mnayataka, kama sijayaeleza vizuri nimalizie kwa kuyafafanua vizuri.

Kwa mfano, kuna maeneo mmehitaji kujua, kwamba kumekuwa na sehemu mnaiona, tunawashukuru sana kama kuna mabadiliko manayaona katika utendaji wetu.

Kwa kweli niwashukuru wafanyakazi wa TPA, niwashukuru sana, hasa hawa ambao wapo baada ya wale ambao wanaohusika kuwa wamepunguzwa hapa na pale, waliopo wana ari. Niseme tu ukweli, uzoefu wangu unaonyesha kuwa hata huko nyuma tatizo lilikuwa ni menejimenti, lakini watumishi hawa wa chini, wa kati, ni watumishi wazuri sana na wanafanya kazi kwa bidii, na wako na chama cha wafanyakazi wa bandarini.

[Chama hiki] kinafanya kazi vizuri kwa sababu tunapokuwa na changamoto tunakaa, tunaongea kwa ugomvi wa kawaida, lakini tunafikia mwafaka na hawatetei mfanyakazi mzembe. Kwa hiyo hili limejenga ari, kwa sababu tungetumia nguvu nyingi, lakini si nyingi kwa hivyo.

Kufanya kazi saa 24

Sasa wakati mwingine tumefika mahali pa kusema ni saa 24. Je, ni kweli na wote wanaweza na Tehama inaweza kuhimili? Kwa hiyo naweza kusema tumeweza, sitataja jina, kuna benki ilipewa nafasi humu bandarini tulipowambia kufanya kazi kwa saa 24 wakasema hawawezi labda walipwe.

Sisi tuliwambia ukweli. Wewe tumekupatia biashara, tumekuleta hapa bandari, wateja wetu wote maana yake unakuja kuwa na mtandao nao, tunakupa nafasi, benki nyingine hazijapata nafasi, wewe unaleta kiburi kwamba tukulipe wakati wewe unatakiwa kutulipa sisi? Kwa sababu tumekupa nafasi ya kufanya biashara, ilitakiwa utulipe wewe.

Ile benki iliyoleta kujuajua tuliiondoa na tuliwapa siku 7 walikuwa wanaringa. Tukawambia siku ya 7 hata hiyo cash box tutaisukumia baharini. Nashukuru kabla ya siku tatu kwisha walikuja na wakaapa, nashukuru hawa waliopo wote sasa masaa 24.

Kama mnataka kushuhudia njoo saa 8 usiku hata mta-draw hela kwenye kaunta, siyo kwenye ATM, kwenye kaunta. Na tunakwenda, tunaongea nao tunawaona, tunawapongeza, ambao wapo. Na kwenye jengo hili (jipya) benki zitaongezeka, kwa hiyo tutaongeza huduma.

Idara ya Tehama tumeiongeza mzigo, inaweza kufanya kazi saa 24? Ni kweli kadiri muda unavyokwenda karibu zimejaa na tunafanya kazi ya kuzipanua. Kama nilivyosema, hata wadau wengine wa sekta binafsi, lazima uwepo kwa saa 24. Hauwezi hata kama ni mkuu wa shirika ni wajibu wetu sisi TPA kutoa taarifa serikalini.

Tutatoa sisi taarifa serikalini, sasa serikali iliyokupa nafasi itaamua kama uendelee kuwapo au usiwepo. Wala hatutaacha. Hata kama wewe ni mkubwa kuliko sisi, tutakutolea taarifa. Hatujakuteua, lakini hatutaki utuharibie kazi.

La tano ni ushirikiano wetu na ICDs, zile bandari kavu. Kwa ujumla ICD siyo mbaya na siyo tatizo, kwanza zinatoa ajira kwa sekta binafsi. Tatizo ambalo lilikuwapo ICD kwa kweli, nyingine zilikwenda kinyume. Ziliongeza muda, unataka kutoa kontena lako uwe umeishalipa [au la], atakuongezeaongezea ili ulipe zaidi.

Sasa ile ndiyo ilituumiza kidogo kwa sababu wakati ule Bandari shehena ilikuwa inapungua, kasha zinachukuliwa zinapelekwa kule. Nikasema hapana, utaratibu ni kwamba Bandari ijae kwanza halafu tuanze kupeleka.

Kwa hiyo ndugu zangu sisi tunadhani kwanza, tufanye kazi kulingana na maelekezo ya wizara na serikali, maelekezo ya Bodi, tutashirikiana na ICD hata katika maeneo mapya ambayo tunakwenda.

Lakini nayo kulingana na sheria mpya ya TASAC, pia yeye atakuwa na wajibu wa kusimamia makasha. Kwa hiyo inawezekana kwenye ICD tukawa na muundo mpya, ambapo tutaona TASAC, ambaye yeye ndiye wakala mkubwa ingawa atawatoa wenzake, inawezekana tutampa na mengine asaidiane na ICD.

Lakini tunakupa mfumo wetu ule. Kwa hiyo wewe ni extension tu, hauna maanuzi ya peke yako. Kwa hiyo mfumo wetu unakuwa na sever moja. Umelitoa hili, ni automatic tunakuona, kwa hiyo tutakuwa tunaendesha kama canteen, lakini hauwezi kujisimamia, haiwezekani. Lazima serikali iangalie shehena zake.

Kwa hiyo lazima itaendelea kuwapo. Sasa, baada ya pale kwa kweli, tunaweza kuongeza mapato kwa sababu baadhi ya biashara tutaweza kufanya moja kwa moja, wakati huo ilikuwa likishuka kasha linakwenda moja kwa moja, sasa linabaki. Kwa hiyo, ile biashara tunakuwa tunaipata sisi ya kuhudumia kama Bandari.

Kwa hiyo hili nalo limechangia kuongeza mapato, siwezi kusema ni kiasi gani, lakini sehemu kubwa tumepata, na hasa kwenye magari. Kwenye magari tumepata mapato zaidi. Lakini niseme tu kwamba ICD tutakapopata shehena kubwa siku zinazokuja, bado tutaingia makubaliano maalumu, standard operating procedures, na service level agreement, na mikataba ya uendeshaji ambayo tutaisimamia.

Jingine ambalo tunalisimamia, ni, tumeweza kudhibitije mambo ya wizi. Tofauti na yale makontena yasipotee, ehee nimezungumzia hali ya ulinzi na usalama ambayo serikali yenyewe imetusaidia tuwepo.

Labda niseme tu, huku bandarini kama ilivyo mikoa au wilaya, na sisi huku tuna Kamati ya Ulinzi na Usalama. Tunakutana kila mwezi, na vyombo vyote vinakuwepo na tunazungumza jinsi ya kujilinda.

Kule wilayani mnamjua Mkuu wa Wilaya, ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Mkuu wa Mkoa mkoani, na Mheheshimiwa Rais ni Mkuu wa Baraza la Usalama la Taifa, na sisi tunayo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bandari, sasa hii inazuia.

Sasa tunazo njia sahihi, ukiweka hii mifumo hasa CCTV, mpaka kwenye ICD maanake kule kuna matatizo sana kwenye ICD ya usalama. Kuna nyingine tukizitamka hadharani hapa mtashangaa, nadhani mtazijua. Zinao watu waliokuwa wamekubuhu. Kwa kweli kwa kusimamia, tumesimamia kuzuia wizi.

Na hivi karibuni kuna nyingine tulikuwa tunataka kuzifuta, na nyingine zilikuwa na kesi nadhani mnazifahamu. Kesi ya upotevu wa madini, kulikuwa na kontena mbili zilikuwa na shehena, nadhani mnazifahamu.

Sasa njia nyingine ni kwamba tumeweza kuendeleza kuboresha mfumo wa utoaji habari. Kwa hiyo tuna watoa habari wetu. Na wengine ni wafanyakazi wa humo humo kwenye ICD. Kwa hiyo lazima waelewe kuwa hizo mbinu mpya tumefanya.

Kwa hiyo tumeweza kudhibiti, ukijaribu, habari itapatikana. Na hii ni mpaka ofisini kwenye shughuli za fedha za ofisini. Lakini CCTV zimetusaidia sana. Kwa sababu kila kona inaonekana. Yapo maeneo ambayo hayakuweza kuunganishwa na mradi wa kwanza, niwahakikishie speed tunayoendelea nayo, mwaka wa fedha ukiisha Juni, mwakani, tunataka Bandari yote ya Dar es Salaam ionekane.

Ndiyo tunaangalia, tupo kwenye manunuzi ya kuongeza kamera. Kila mahala hata kwenye Azam Cereal, kila mahali. Kwa hiyo wewe ilimradi upo ndani ya eneo la Bandari, utaonekana kwenye CCTV. Na tunaelimisha vijana wetu, wapate, tunaimarisha mafunzo, waweze kupata hiyo elimu, ya kuangalia zile taswira.

Wengine wanataka kujificha. Wapo watu wengi sana tumewafukuza kazi kwa kutaka kuficha sura zao. Kwa hiyo huku nako kwenye mapato yameongezeka. Kwa hiyo, tathmini itafanyika kuangalia imechangia kiasi gani, kwa sasa bado hatuna takwimu kamili, lakini tunafanya utafiti.

Eneo jingine mmetaka kuelewa, ni ufumbuzi gani tumeupata katika mifumo hii ya teknolojia na mawasiliano bandarini, yaliyokuwa yanaanza hayaishi? Najua, kwa mfano hii ERP niliyokuwa nawambia ni ya tatu.

Kwa karibu miaka 20 iliyopita, karibu miradi yote mitatu ikifika mahala inakufa, sasa hivi ukiiua unakufa wewe kabla haujafa wenyewe. Na nataka kuhakikisha hiyo ERP inawekwa. Na kama wewe ni mkurugenzi ambaye unasimamia mifumo huisimamii, huwezi kuendelea kuwa mkurugenzi, hata kama ni meneja, huwezi.

Tutawabadilisha mpaka tutakapopata wale wanaoweza kutusaidia. Na nimelihakikishia Bunge juzi PAC, kwamba kabla ya mwaka kesho kwisha nitakuwa niko full operational na ERP, na huduma ya call center. Mifumo yote itakuwa inafanya kazi mpaka ya ofisi.

Kwa hiyo tulilchokifanya ni kuwasimamia makandarasi, kuhakikisha tunaondoa vitendo vyote vya kuelewana elewana nao, vinavyoweza kuonyesha kuwapo kwa rushwa. Mikutano ya mara kwa mara kuwa na ratiba, programu ambazo tumezipitia zinatekelezwa, unahojiwa.

Kwa hiyo hawa washitiri, hawa makandarasi watoa huduma, wote hata kwenye CCTV, unapokuja ni ratiba na kusimamiwa na kutoa taarifa. Ukielekea kushindwa, na tukikufukuza ukashindwa mkandarasi au mtoa huduma tunakupeleka kule kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi.

Hautakaa uione tena TPA inavyofanya kazi, kwa sababu tutakupeleka kule na kukufutia kabisa na leseni. Hata kama ni injinia tumekupa kazi ya kusimamia mradi wa nje, tutakupeleka kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi, ikufutie leseni na uhandisi wako utaishia pale. Na mmeona tulikuwa na kikao nao juzi, ni katika kueleza haya. Lazima tufanye kazi, kwa haraka na kwa uadilifu.

Lipo swali la flow meter KOJ, kweli ni kwamba flow meter ile ya KOJ hata ilipotaka kujaribiwa kufanya kazi ilionekana kwa miaka iliyokuwa imesimama kwa sehemu kubwa iliharibika. Kwa hiyo matarajio yetu ni manunuzi, yanayoendelea, tulipata kutoa taarifa huko nyuma, manunuzi yote ya aina mbili, ya awamu mbili yote yalikwama.

Kwa sababu inaonekana kama kunakuwepo na collusion, kunakuwapo na njama, wanaorudisha wanakuwa wachache, wanaovinunua [vitabu vya zabuni] wanakuwa wengi. Sasa unapokuja mpaka kwenye kutathmini na kufika mwisho, tunaishia kwenye mgogoro.

Kwa hiyo, awamu ya pili pia tuliingia kwenye mgogoro. Awamu ya tatu tena tumeingia kwenye sheria na utaratibu mzuri wa tofauti. Tumeshirikiana na serikali nzima, kwa sababu hizi ni nyenzo za kimkakati za nchi, siyo za TPA. Tuna uhakika safari hii tufafanikiwa, kwa sababu tumekwenda nje, kuangalia watengenezaji wakubwa, tukisaidiana na serikali.

Kwa hiyo hapa siwezi kusema mengi, kwa sababu mchakato wa manunuzi huwa ni wa siri. Hauzungumzwi, lakini Watanzania na viongozi wengine na wadau waelewe kwamba gharama ni kubwa kabisa na huu mchakato wa tatu, kwa sababu umeenda kimkakati, na umeenda kuangalia wale wenye uwezo moja kwa moja, tutakayempata hatakwama.

Na wote wamekuja wameangalia kwa macho yao, kwa hiyo, hiyo KOJ, lakini Tanga, kwa sababu Tanga pale tulikuwa hatuna flow meter na Mtwara, kwa sababu Mtwara sasa meli za mafuta zinaenda, tutakuwa pia na flow meter pale.

Kwa hiyo mwaka huu wa fedha, haiwezekani, kwa namna yoyote ile, kwamba itakuwa awamu ya tatu imeshindikana, tutatumia njia zozote zile ambazo sheria inatupa mwanya kuhakikisha hata kama sasa ni kwenda dukani moja kwa moja kuchukua.

Nilitaka niseme tu kwamba, lakini kwenye hili wananchi waelewe. Flow meter hata mimi mwanzoni sikuwa najua ni nini. Flow Meter ni kiwanda. Siyo kama mita ya TANESCO ya kupima umeme au maji, ni kiwanda kikubwa sana ambazo kinachukua hata eneo la mita 20 kwa 50.

Na ni mashine. Kwa hiyo nadhani hili nalo lieleweke maana watu wanadhani si uende tu uchukue, kwa hiyo hili nalo nimelifafanua vizuri.

Je, unafahamu utendaji wa Bandari katika miaka mitatu iliyopita kwenye eneo la Bandari za Maziwa, wafanyakazi hewa, vibarua hewa na mengine? Usikose sehemu ya tatu ya makala hii inayoelezea mafanikio ya Bandari katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais John Pombe Mafutuli wiki ijayo.