Majaribu ni mtihani. Kumbuka kuwa bahari shwari haitoi wanamaji stadi. Watu wema wamefinyangwa na mitihani ya maisha yenye sura mbaya. Nakubaliana na Matshona aliyesema: “Roho zenye urembo zinafinyangwa na mapito yenye sura mbaya.”

Wakati mwingine tunawajua watu wenye majina makubwa lakini hatujui majaribu makubwa waliyoyapitia. Tunajua umaarufu wao, hatujui hadithi zilizojaa huzuni za maisha magumu waliyoyapitia.

Kila jambo zuri ambalo unastahili kuwa nalo linakuja limezungukwa na majaribu. Ingawa majaribu ni mtihani kila jaribu limeficha dhahabu. Kila ulemavu umeficha kipaji, kila balaa limeficha bahati. Kila gumu limeficha tabasamu, kila aina ya kelele imeficha vigelegele. 

Majaribu ni mtihani. Kuna mtu ambaye alikuwa amechelewa kuhudhuria mkutano. Aliona mahali kuna kibao kimeandikwa maneno: “Hakuna maegesho hapa.” Aliegesha gari lake pale na kuandika maneno kwenye karatasi: Utusamehe makosa yetu. Karatasi yake aliichomeka kwenye gari karibu na kioo cha mbele.

Askari aliyekuwa analinda sehemu hiyo aliandika kwenye karatasi na kuiweka karibu na karatasi nyingine: Usitutie majaribuni. Majaribu yanapokuwa mtihani usiwatie wengine majaribuni. Majaribu yanaweza kukuleta karibu na watu au kukuweka mbali na watu. Majaribu ni mtihani.

Majaribu yanaweza kukuinua au kukuweka kwenye mtaro. “Majaribu kila mara yanabadili uhusiano wetu na Mungu. Yanaweza kwa upande mmoja kutuweka karibu naye au kwa upande mwingine kutuweka mbali naye. Kiasi cha hofu ya Mungu na ufahamu wetu wa upendo wake vinatusaidia kuamua upande upi wa kwenda,” alisema Jerry Bridges.

Hofu ya Mungu inatusaidia kufanya uamuzi. Kujua kuwa Mungu anatupenda ni jambo linalotusaidia.

Kupitia majaribu Mungu anakuandaa kwa mambo makubwa. Mt. Yohane wa Msalaba alisema: “Kuvumilia giza ni maandalizi ya mwanga mkubwa.” Baada ya dhiki faraja.

Nakubaliana na Franklin Graham aliyesema: “Haijalishi aina ya dhoruba unayoikabili, unahitaji kujua Mungu anakupenda. Hajakuacha.” Wakati kuna wingu zito jua halionekani lakini lipo.

“Majaribu ni dawa ambazo daktari wetu mwenye hekima anapendekeza kwa sababu tunazihitaji,” alisema Yohane Newton. Daktari huyo ni Mungu. Mungu anatuletea majaribu kutuimarisha. Kuna methali ya Wahaya isemayo: “Anayekuongoza usiku unamshukuru wakati wa mapambazuko.”

Ukitazama nyuma na kutafakari mitihani uliyoishinda unamshukuru Mungu. Kuna mambo ya kufanya unapopitia majaribu.

Kwanza, linda mawazo yako. “Adui yako mkubwa sana hawezi kukuumiza kama mawazo yako ambayo hujayalinda yanavyoweza kukuumiza,” alisema Buddha. Ubongo ni uwanja wa mapambano. Mambo mengi ni matokeo ya mawazo. Waza mambo chanya.

Pili, kumbuka ushindi wa nyuma. “Unapopitia kwenye majaribu kumbuka ushindi wako wa nyuma na uhesabu baraka,” alisema Ezra Taft Benson (1899 – 1994), kiongozi wa kidini wa Marekani na ofisa wa serikali. Jiambie: “Zamani lilikuja jaribu kubwa nikapita, nalo likapita na hili nalo litapita.” Yatafakari maneno ya Matshona Dhliwayo: “Usikubali dhoruba la jana likuzuie kufurahia jua la leo.”

Tatu, ona fursa na uwezekano katika majaribu. Radi yenye mwanga mkali inatoka kwenye wingu jeusi. “Tukiona matatizo tu, tutashindwa; lakini tukiona uwezekano katika matatizo, tunaweza kuwa na ushindi,” alisema Warren Wiersbe.

Nne, majaribu yape maana nzuri. Majaribu ni dawa. Majaribu ni mwalimu. “Maisha ni chuo kikuu cha mwenye hekima; mateso ni profesa wake,” alisema Matshona Dhliwayo. Tunaweza kusema maprofesa wa Chuo Kikuu cha Maisha ni matatizo, kushindwa, dhiki na karaha.

Tano, jikumbushe kuwa Mungu yuko karibu. “Inapoonekana Mungu yuko mbali, jikumbushe kuwa yupo karibu. Ukaribu si suala la jiografia. Mungu yupo kila mahali,” alisema Warren Wierbe. 

Please follow and like us:
Pin Share