Nikiwa jijini Accra, Ghana katika toleo Na. 260 la Gazeti la JAMHURI, niliandika makala yenye kichwa hiki: “Poleni Bukoba, tuchunge wapigaji!” Hili ni toleo lililochapishwa Jumanne ya Septemba 20, 2016. Nilianza kupata wasiwasi kuwa huenda wakajitokeza watu wa kutumia janga la tetemeko la ardhi kujitengenezea utajiri hewa!

Kabla wino haujakauka yametokea. Serikali imesisitiza mara kadhaa kuwa inafungua akaunti ya maafa kwa jina la Kamati Maafa Kagera katika Benki ya CRDB. Akaunti hii ikatajwa kuwa ni 015 222 561 7300. Watu wakahamasishwa kutoa michango yao kusaidia wahanga. Niliporejea hapa nchini tu, ikabidi niende Bukoba, kwani nyumba ya mama yangu nayo imeanguka. Nashukuru familia imebaki hai tunaendelea na ujenzi/ukarabati.

Nilipopita maeneo ya Kashai, Kashabo, Nyanga, Katoma, Gera, Nshambya, Kahororo na vijiji vingine, nikapata wasiwasi. Kati ya mwaka 1994 na 1996, chini ya mpango wa kufundisha Kiingereza wa British Council nilipata fursa ya kufundisha mara kadhaa katika shule za Nyakato na Ihungo. Hivyo nazifahamu. Miaka hiyo nilikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari Mugeza. 

Nilichokishuhudia Nyakato na Ihungo, maelezo niliyopata kutoka kwa wananchi walioathiriwa na tetemeko kiliniacha hoi. Yupo mama mmoja anaitwa Paskazia Alphonce (0766 788 608) eneo la Kashabo, yeye alikuwa na nyumba ndogo ya nyuma na nyumba ya mbele, iliyokuwa na wapangaji zote zimevunjika kiasi analala kwenye mkungu.

“Tuliahidiwa msaada lakini jana (Ijumaa) ndipo nilipopewa turubai moja. Mimi na wapangaji tisa tunalala hapa kwenye mkungu, jua letu, mvua yetu,” anasema Paskazia ambaye ni mstaafu mwenye umri wa miaka 61 na kuongeza: “Tetemeko limemaliza maisha yangu. Nyumba hizi nilizijenga kwa tabu, sina ajira tena na hivyo nasubiri huruma ya Mungu. Sina pa kuomba msaada maana kila mtu anahitaji.”

Paskazia ambaye ni mkazi wa Kashabo Bukoba mjini, anawakilisha kilio cha wengi. Mwanzo familia hiyo yenye wapangaji tisa, waliitwa katika Shule ya Msingi Kashabo, wakapatiwa kilo mbili za mchele, nusu lita ya mafuta ya kula na nusu mche wa sabuni. Leo ukiwa karibu mwezi mmoja tangu tetemeko litokee, hakuna huduma ya maana waliyopewa wahanga Bukoba.

Sitanii, wengi wa watu walioko Dar es Salaam na nje ya nchi, wanaamini kuwa wahanga wanapewa huduma za daraja la kwanza. Hata ahadi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ya kuwapa wahanga mifuko mitano ya saruji, mabati 20, hela ya kujengea upya nyumba zao na kodi ya miezi sita kwa wapangaji, haitekelezeki hadi leo. Ni kilio kila kona.

Wakati nikiwaza hayo, kikabainika nilichokuwa nawaza. Ikagundulika kuwa imefunguliwa akaunti hewa. Katibu Tawala, Amantius Msole; Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Kelvin Makonda; Mhasibu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai;na Meneja wa CRDB Tawi la Bukoba, Carlo Sendwa; siwahukumu maana wapo mahakamani, wakadaiwa kufungua akaunti feki.

Akaunti hii imefunguliwa kwa jina lilelile la Kamati Maafa Kagera. Namba za akaunti baada ya 015 badala ya kusomeka kama akaunti halali inayofuatiwa na Na 222, wakapunguza Na 2 ya kwanza na kuweka Na 0, hivyo ikasomeka 022, lakini namba nyingine zikaendelea kusomeka vile vile. Akaunti halali ni 015 222 561 7300 na akaunti feki ni 015 022 561 7300 ila zote zinasomeka jina lilelile Kamati Maafa Kagera.

Sitanii, Serikali makini ya Rais Magufuli, imebaini hili. Imewachukulia hatua. Imewandoa kazini na wamefikishwa mahakamani. Wanaowafahamu watuhumiwa hawa, wanasema wanatokea mkoa mmoja, na huyo mwingine wamesoma naye tangu enzi za shule za msingi. Kimsingi, ni rahisi kuzungumza lugha moja. Ila mmoja wanasema ameingizwa mkenge, kwani yeye alikuwa anaambiwa tia saini tu.

Mpendwa msomaji, naomba univumilie. Safu hii ilipaswa kuwa nusu ukurasa. Hata hivyo, kutokana na uzito wa suala ninalolizungumza, nimeshindwa kuandika nusu ukurasa. Kwa ridhaa yako naomba uniruhusu niandike ukurasa mzima. Wakati nakushukuru kwa kunikubalia ombi langu, nieleze masikitiko yangu.

Watuhumiwa hawa wamefunguliwa mashtaka mawili. Shtaka la kwanza ni “matumizi mabaya ya ofisi” na la pili shtaka la “kula njama”. Nasikitika kusema na napata shaka kuwa huenda hata aliyefungua mashtaka ana uhusiano na akaunti iliyofunguliwa. Ama amewezeshwa au ni sehemu ya mtandao uliofungua hiyo akaunti, ikiwa itathibitika mbele ya sheria kuwa walifungua kweli akaunti hiyo.

Mhe. Rais John Pombe Magufuli nimeomba uingilie aina ya mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya watu hawa. Kwa makusudi, wametumia sheria inayotoa nafuu kubwa jinsi ya kutoa dhamana. Vifungu vilivyotumika ikiwa kweli wamefungua akaunti hiyo, wataishinda Serikali mapema kabla jua halijachomoza. Huu umekuwa mchezo au uzembe wa kitambo unaofanywa na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa nia ya kuwapa nafuu wasiyostahili watuhumiwa, na katika hili wanatenda tena.

Sitanii, kuamini kuwa ofisi ya DPP haifahamu kuwa walichofanya watuhumiwa hawa ikiwa kitathibitika kinaangukia katika uhujumu uchumi, inanipa shida. Kesi ya msingi imeegemezwa kwenye kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU). Kifungu hiki kinahusiana na matumizi mabaya ya ofisi. Mtu akikutwa na hatia, analipishwa faini isiyozidi Sh milioni 5 au kufungwa jela kwa muda usiozidi miaka 3.

Kosa la pili, walilowafunguliwa ni la kula njama chini ya  Kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (kama ilivyorekebishwa mwaka 2002). Kifungu hiki kinategemea kosa la kwanza chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambapo kifungu hiki kinasema iwapo kwa mfano watatiwa hatiani chini ya kifungu hicho cha 31, basi kosa la njama nalo litathibitika hivyo kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 7 bila faini.

Hii maana yake ni nini? Uhalisia kesi hii imeharibiwa tangu kwanzo (ab initio). Ndiyo maana siku ya Ijumaa iliyopita kutokana na wepesi wa makosa waliyoshtakiwa nayo wamepewa dhamana. Tena wakati wanatoka mahakamani, siwahukumu, ukiacha mmoja wao tu, wawili walioenekana kutojutia au kuona aibu kwa hilo wanalotuhumiwa kutenda. Tena mmoja alikuwa anacheka kabisa!

Sitanii, ni kwa msingi huo naomba Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli uingilie kati na kuitaka ofisi ya DPP ikiwa haina maslahi na kesi hii, watuhumiwa hawa iwafungulie kesi sahihi kwa kutumia Sheria ya Uhujumu Uchumi ya Mwaka 1984. Chini ya Kifungu cha 2 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, kosa la kula njama linahesabika kama uhujumu uchumi.

Kifungu cha 4(1)(d) cha Nyongeza ya Kwanza ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, kosa lililowekwa chini ya Kifungu cha 31 cha Sheria ya Takukuru, la matumizi mabaya ya ofisi na hivyo kuishia kutoa adhabu ndogo, sheria hii inaliweka kosa hili katika makosa makubwa ambayo hata dhamana yake inatolewa kwa masharti maalumu. Kifungu cha 57 (1) cha Sheria ya Uhujumu uchumi, kinaelekeza itumike nyongeza ya kwanza katika sheria hiyo kubaini makosa ya uhujumu uchumi.

Sheria hiyo iliyoanza kutumika Septemba 25, 1984 inaelekeza chini ya Kifungu cha 60 (3)(a), kwa kusema: “Kosa lililothibitika likiwa katika msingi wa kupanga uhalifu au jambo linalohatarisha uchumi wa Taifa au mali ya jamii, bila kuwapo mazingira yanayopunguza athari, anastahili adhabu ya juu.” Sheria ya Tafsiri ya Sheria ya Mwaka 2002 chini ya Kifungu cha 74(1) inatoa tafsiri ya maana ya “adhabu ya juu” kuwa ni ile adhabu iliyotamkwa ndani ya sheria.

Zimetamkwa adhabu mbalimbali ikiwamo kumfilisi aliyekula njama za kuhujumu uchumi au mali ya jamii, kulipa fidia, kutozwa faini na Mahakama imeachiwa uhuru wa kutoa adhabu yoyote itakayoona inafaa. Hii maana yake inaweza kuwa kufungwa maisha au kunyongwa hadi kufa (kulingana na ukubwa wa kosa), kwani kuhujumu uchumi ni moja ya makosa makubwa katika nchi hii.

Masharti ya dhamana kwa mtu anayetuhumiwa kuhujumu uchumi yanamtaka kulipa nusu ya kiasi cha fedha anazotuhumiwa kuchukua, lakini chini ya makosa waliyowashitakiwa nayo wamepewa dhamana kwa kupewa barua za utambulisho na maafisa watendaji. Hii maanake ni nini? Jinsi walivyopata urahisi wa kupata dhamana katika kosa kama hili ambalo watoto wanalala nje, watu wamekufa, Taifa linaomboleza, ikiwa mashtaka yataendelea kuwa haya wakubwa hawa watashinda kesi.

Sitanii, wameshindwa kupewa fursa ya kukiri au kukana tuhuma zao, na habari za chini zinasema watu hawa wanadaiwa kuchota hadi Sh milioni 300 katika akaunti hii feki. Serikali inakesha usiku kucha ikitafuta misaada kusaidia wahanga, halafu watu wanatumia uhuni kufungua akaunti feki. Ni ujasiri wa kishetani ikiwa itathibitika kuwa wametenda hivyo.

Mheshimiwa Rais, kwa kuwa kosa hili ni kubwa, na inaonekana kama ofisi ya DPP Bukoba inakufanyia utani kwa kuwafungulia mashitaka ambayo wana uhakika kuwa watayapangua kirahisi, nadhani utie mkono wako kuiepusha Serikali na kejeli hizi mbele ya macho ya jamii. 

Nahitimisha kwa kusema, ikiwa itathibitika kuwa hawakufungua hiyo akaunti, basi wataachiwa huru na maisha yatarudi kama kawaida, ila kama itathibitika kuwa waliifungua kihuni, wanastahili adhabu itakayokuwa fundisho kwa wanajamii wengine wenye mawazo hasi kama hayo.

Nafikiri kuwafungulia makosa haya ya kitoto ilhali tukijua kosa walilolitenda (ikithibitika) ni kubwa kiasi hicho, huo utakuwa utani dhidi ya Serikali yako Mheshimiwa Rais. Usikubali kujaribiwa. 

Poleni wana Kagera, na naiomba Serikali iongeze kasi ya misaada hali ni mbaya kwa watu. Kila mwenye kosa aadhibiwe kwa kiwango cha kosa alilotenda. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Kagera isiendelee kukumbwa na majanga.

1938 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!