Mheshimiwa Rais,

 

Nimechukua hatua hii ya kukuandikia waraka wa wazi nikiwa na kumbukumbu mbaya ya maafa yaliyotokea miaka 15 iliyopita. Januari 27, 2001 Chama cha Wananchi (CUF) kiliandaa maandamano ambayo Serikali ya wakati huo haikuyaridhia.

Sote ni mashahidi kwamba kilichotokea kiliitia dosari historia ya nchi yetu kwani nguvu ya dola ilitumika dhidi ya wananchi na matokeo yalikuwa mabaya kwa sababu kuna Watanzania waliopoteza maisha, damu ilimwagika, wengi walijeruhiwa na baadhi yao walipata vilema vya kudumu kama kukatwa miguu n.k.

Kwa mara ya kwanza Tanzania ilizalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni nchini Kenya. Tunaoitakia mema nchi yetu hatutaki historia mbaya ijirudie, ndio maana tunaona kuzuia ni bora kuliko kuponya.

Wenye kumbukumbu tungali tunakumbuka vyema kwamba maafa hayo yalitokea baada ya viongozi wa Serikali ya wakati huo na viongozi wa CUF wote kwa pamoja kukaidi na kupuuza ushauri wa Mama Maria Nyerere na Mzee Joseph Sinde Warioba (Waziri Mkuu mstaafu).

Mama Maria Nyerere na Mzee Warioba walitoa kauli zisizoelemea upande wowote wakisema kwani CUF wasipoandamana watapoteza nini? Ama Serikali ikiyaruhusu hayo maandamano itapoteza nini?

Sote tunajua CUF hawakukubali kuacha kuandamana na Serikali haikukubali kuruhusu maandamano hayo; matokeo ya mashindano ya pande mbili yaani mashindano yaliyojengeka katika msingi wa kiburi na jeuri ya viongozi (wa Serikali na CUF) waliokosa unyenyekevu yalizaa janga. Watanzania tunao wajibu wa kuzuia majanga yanayotengenezwa kwa makusudi na wanadamu.

Mheshimiwa Rais, ulipohutubia mkutano wa hadhara pale Manyoni, ulinukuliwa ukisema: “Hao wanaotaka kuandamana wataona, nawaomba watangulie wao wawe mstari wa mbele, wasitangulize watoto wa maskini na wao kujificha hotelini, mimi sijaribiwi.”

Kwa kauli hii ukiwa kama Amiri Jeshi Mkuu ni kama ulitangaza vita dhidi ya wananchi wasiokuwa na silaha, maana kuna swali lisiloepukika ‘hao’ watakaotangulia umedhamiria kuwaonesha nini?

Hivi ni kweli ukijaribiwa uko radhi kuwapatililiza hao watakaokujaribu? Hii ni kauli ya kukosa unyenyekevu maana ukiwa binadamu huna namna ya kuepuka majaribu. Asiyejaribiwa ni Mungu peke yake, ndio maana hata mwokozi wetu Yesu alijaribiwa na pia alitufundisha kwamba tunaposali tumwombe Mungu atuepushe na majaribu na hila zote zitokazo kwa yule mwovu, yaani ibilisi.

Mheshimiwa, ulipaswa kuwaambia wananchi tuombe Mungu atuepushe na hilo jaribu la wanaotaka kuandamana, maana tangu ulipoapishwa kuwa Rais umekuwa ukiwahamasisha Watanzania wamtangulize Mungu. Nionavyo katika suala hili la maandamano huoneshi kumtanguliza Mungu, bali umetanguliza jazba.

Baada ya hiyo kauli yako vyombo vya habari vimeendelea kuwanukuu wasemaji wa CHADEMA wanaosisitizia dhamira ya kuandamana pasipo kujali tamko la Serikali. Hizi ni ishara za mashindano yenye mwelekeo wa kufanya historia mbaya ijirudie.

Tunaoipenda nchi yetu hatuwezi kukaa kimya kama washabiki wa soka wanaosubiria pambano la Simba na Yanga kwa kuwa mapambano kati ya nguvu ya dola na wananchi watakaoandamana maana yake ni moja tu maafa, uharibifu na majonzi.  Neno la Mungu linasema “msimpe ibilisi nafasi”. Ni kwanini Watanzania chini ya uongozi wako tumpe nafasi ibilisi ya kutuvuruga na kuharibu mazuri?

Natambua kuna mazuri mengi ambayo umeyafanya ndani ya kipindi kifupi cha miezi minane na ndio maana wananchi wengi wamekukubali. Ushahidi wa kukubalika kwako ni mafuriko ya watu wanaokukusanyikia sasa, kwani wanazidi wale waliokuwa wakikusanyika kukusikiliza wakati wa kampeni.

Lakini naomba uelewe kwamba baya moja hasa la kumwaga damu za wananchi wako linaweza kufunika mema yote uliyowafanyia na pia litakupunguzia uhalali wa kuwatawala. Hakuna Mtanzania wa kurekebisha kauli zako isipokuwa wewe mwenyewe kwa mfano unapowataka “hao” watangulie mbele wasiwatangulize watoto wa maskini ili uwaoneshe, maana yake umedhamiria kutoa fundisho kwa Watanzania, kwamba wakiyaona madhara yatakayowakuta waandamanaji (uliokamia kupambana nao), wananchi wengine wasithubutu tena kuandamana!

Hili litakuwa funzo baya. Linaweza kuzaa matokeo hasi na usiyoyatarajia kwa sababu huna jeshi la kuua wananchi, jeshi letu la Polisi na JWTZ yapo kwa ajili ya kuwalinda raia na mipaka ya nchi, siyo kuwaumiza.

Somo utakalotoa limelenga kuwaumbia wananchi hofu na woga ule ule ambao serikali za kikomunisti ziliwaumbia raia wao, lakini ili wananchi watawalike kirahisi hawahitaji kutishwa wala kuogopeshwa. Wanatakiwa kukuheshimu wewe kama Rais wao na si kukuhofia.

Haki inayokuwezesha kuzunguka Manyoni, Singida, Nzega na Mwanza kwenye viwanja vya Furahisha, ukifanya mikutano ya hadhara kuwashukuru wananchi waliokuchagua, ni haki hiyo moja ndiyo waliyo nayo kina Edward Lowasa, Freeman Mbowe na wanasiasa wengine. Usiwaoneshe Watanzania kwamba ukiwa kama Mwenyekiti mpya wa CCM haki yako inaanzia pale zinapoishia haki za wanasiasa wa vyama vingine. Ukifanya hivyo utachochea maasi.

Kwa sababu Watanzania wanaokusanyika kwenye mikutano ya hadhara unayoifanya ndio hao hao watakaowakusanyikia wanasiasa wengine na ndio watakaoandamana; kwa kuwa CHADEMA haina Watanzania wake walio tofauti na hao wananchi wanaokukusanyikia wewe kwenye mikutano yako ya kisiasa unayoifanya hadharani. Usiwaaminishe Watanzania kwamba wakikutanishwa kwenye mkutano wa hadhara wa CCM wanakuwa na thamani kiasi cha kustahili kulindwa, lakini Watanzania hao hao wakikutanishwa kwenye mkutano wa CHADEMA au CUF wanakosa thamani kiasi cha kustahili kupigwa mabomu au kumwagiwa maji ya kuwasha. CHADEMA haina Watanzania wake.

Kuhusu kauli yako juu ya mikutano ya hadhara nakusihi ujikumbushe kauli ya Mwenyezi Mungu alimwambia Musa, hao watu unaowaongoza watanidharau hadi lini? Wasiniamini hadi lini licha ya kuwafanyia makubwa? Nitawaangamiza na kukufanya wewe uwe Taifa kubwa na lenye nguvu kuliko wao. Lakini Musa alimsihi Mungu akisema Wamisri watakaposikia umewaangamiza baada ya kuwatoa Misri kwa uwezo mkuu, watawaambia wenyeji wa nchi hizi kwamba tulijua hatawafikisha kwenye nchi aliyowaahidi ndio maana amewaua. Nakuomba uwakumbuke Ibrahimu na Isaka na Yakobo na viapo ulivyowaapia, kisha ughairi kwa hatua unayokusudia kuwachukulia watu hawa. Mungu akasema nimekusikia na nimeghairi kama ulivyosema, lakini nimeapa hawa watu hawataingia kwenye nchi niliyowaahidi, watatangatanga miaka 40 hadi kizazi cha waasi kitakapokwisha na kizazi kipya ndicho kitaingia nchi ile.

Kwa hiyo hata wewe Mheshimiwa Rais Magufuli unaweza kughairi ukaachana na dhamira ya kupambana na wanaotaka kundamana, badala yake ujikumbushe ahadi zako ulizowaahidi wananchi wakati ukiomba kura zao. Uliahidi Tanzania ya Magufuli itakuwa Tanzania ya viwanda. Hili ni jambo jema ambalo hakuna yeyote aliye chini yako anaweza kukuzuia usilifanye.

Bahati nzuri umeanza na gia nzuri ya kuisafisha nchi kwa kutumbua majipu na wananchi wamekukubali. Kwanini upotoke na kuanza tena kuwapiga wale waliokupigia kura uwe mkuu wao?

Tafadhali ghairi. Ukighairi haitamaanisha umeshindwa na wapinzani wanaotaka kukujaribu, bali itamaanisha umefikiri mara mbili kama Mungu alivyofikiri mara mbili dhidi ya wale waliomwonesha dharau ya wazi wazi. Kughairi si kushindwa.

 

Mwandishi wa barua hii, Mwinjilisti Kamara Kusupa, ni msomaji wa JAMHURI. Anapatikana kupitia namba 

0786 311 422

By Jamhuri