Rais Magufuli na maslahi mapana ya Taifa (1)

1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliKwa rehema na mapenzi yake Mwenyezi Mungu, Tanzania ilikamilisha Uchaguzi Mkuu tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani.

Kwa upande mwingine, uchaguzi huo haukwenda vizuri kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Inabidi tuwaombee wanaohusika na uamuzi wawe na hekima na kufanya uamuzi utakaodumisha amani kwa Zanzibar na Tanzania Bara. 

Napenda nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia kuukamilisha uchaguzi huo na kufanikiwa kumpata Rais John Magufuli.Sasa ni miezi mitatu tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.

Pili, nimshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye mfalme wa amani na muweza wa yote, kwa kutujaalia amani na utulivu ndani ya Taifa letu. 

Tangu Rais Magufuli aapishwe Novemba, mwaka jana, ameonesha dhamira ya kweli ya kutaka kuwatumikia Watanzania kwa kuzingatia hali halisi aliyoikuta – kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Kusema kweli, hali ambayo Rais Magufuli ameikuta haikuwa nzuri maana iligubikwa na changamoto nyingi mno. Hata wakati wa kampeni zake alijua fika kuwa Watanzania, hasa mijini, walikuwa hawaipendi CCM irejee madarakani. Kwanini? Ziko sababu nyingi ikiwamo kukithiri kwa vitendo viovu kama ufisadi, rushwa karibu katika sekta zote; uzembe serikalini katika kutoa huduma za afya, elimu, maji, miundombinu; kukithiri kwa biashara ya mihadarati na mengine mengi. 

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alifahamu fika kuwa angelegea katika kampeni asingesonga mbele. Ndiyo maana alikuja na kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu, Chagua Magufuli”. Katika kampeni akaonesha kuwa akichaguliwa nguvu ya kufanya kazi anayo kwa kuingiza vibwakizo vya “push-ups”.  Baada ya kuingia Ikulu akawaonesha Watanzania kuwa kazi aliyoiomba na akabahatika kuipata kweli anaiweza. Kwanza, kwa kupiga hodi Hazina (Wizara ya Fedha); Hospitali ya Taifa Muhimbili na hatimaye Serikali yake ikatinga bandarini Dar es Salaam. Yote hayo yamefanyika bila ya kuwa na Baraza la Mawaziri na matokeo ya kutia moyo tumeyaona.

Siku 100 za Rais Magufuli kazini

Ndani ya miezi mitatu, Rais amefanya mengi ikiwamo kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na ushuru wa Serikali. Tunaona angalau huduma pale Muhimbili zimeimarika; mfano, mashine muhimu za vipimo zinafanya kazi na duka la kuuza dawa kupitia wakala wa Serikali wa Dawa (MSD) limeanzishwa na wagonjwa wanapata dawa kwa bei nafuu. 

Hata kama dawa au huduma Muhimbili hazijatosheleza mahitaji, lakini tunaona mwelekeo ulivyo. Hospitali nyingine, vituo vya afya na zahanati sehemu nyingine nchini zinaiga mfano huo kwa kujitahidi kuboresha huduma kwa wagonjwa. 

Tumeshuhudia elimu bure hadi kidato cha nne inatekelezwa hata kama ni kwa kusuasua, lakini watoto wengi wameanza masomo. Mikakati ya kuimarisha miundombinu hasa barabara inaendelea kwa kuwalipa makandarasi. 

Tusisahau kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mvua kubwa inayonyesha inasababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu na ni gharama kubwa kufanya matengenezo. Isitoshe, maeneo mengine yamekumbwa na ukame, hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa chakula.

Vilevile, waliokumbwa na mafuriko na kupoteza mashamba hakuna jinsi, bali wanahitaji mkono wa Taifa uwafikie ili wasaidiwe waweze kuishi. Mtu wa kwanza wa kukabiliana na haya yote ni mkuu wa nchi na Serikali yake.

Kusema kweli juhudi anazozifanya Rais wetu zimepokewa kwa hisia na mtazamo tofauti. Mimi naamini pengine wengi wetu tutapenda ‘akaze buti’ ingawa nasikia baadhi wanasema: “Hakuna jipya, ni yale yale tuliyoyazoea”. Yapi tuliyoyazoea? Wakati Rais anaingia madarakani hali ya huduma za kijamii zilikuwa haziridhishi na ndiyo maana tulitaka mabadiliko kupitia Uchaguzi Mkuu.  

Kwa hali ilivyokuwa, Watanzania wengi walichoshwa na Serikali ya CCM isiyowaletea maendeleo wakati kila aina ya rasilimali zipo. Huduma nyingi za kijamii zilizorota kwa kisingizio kwamba Serikali haina fedha za kutosheleza mahitaji ya nchi.  Kawaida watu hatupendi kulipa kodi. Unapopata mwanya wa kukwepa kodi unafanya hivyo bila ya kusita. Uzalendo unakosekana na maadili yakaporomoka kwa kasi mno kiasi kwamba kila mwenye uwezo wa kuchukua chake mapema alifanya hivyo. 

Ndani ya Taifa moja tukazalisha ‘walionacho’ na ‘wasionacho’; na wenye kuwa nacho wakawa nacho kweli kweli. Kwa hali hiyo tukasahau tulikotoka, yaani kwenye Taifa lililolenga kujenga usawa kwa kuhakikisha hatuzalishi ‘mabilionea’ kama siyo ‘matrilionea, wa kutisha. 

Waliopata nafasi za uongozi wakasahau kuwa wamepewa dhamana ya kutuongoza kwa kutuonesha njia iliyo sahihi na badala yake kikawa kinyume chake. Ikafika mahali wale wenye nafasi kiuongozi na wafanya uamuzi wakaundoa ule mwiko wa kuwataka viongozi wenye nafasi za kufanya uamuzi na kutunga sera za kuendesha nchi wasijihusishe na biashara (wasifanye biashara wenye na familia zao). 

Kwa kufanya hivyo ikawa chanzo cha maadili ndani ya nchi yetu kubomoka; mianya ya rushwa ikashamiri; ufisadi ukaotesha mizizi na kadhalika.

Sasa Serikali ya Awamu ya Tano hata kama ni ya CCM imeingia madarakani kwa kufahamu fika kuwa Watanzania hawataki mchezo, wamechoshwa na ubadhirifu wa mali za umma hivyo wanataka mabadiliko kifikra na kimatendo. 

Inakuwaje ‘milango ya nyumba yetu iko wazi (yaani haijafungwa), lakini baadhi ya watu wakiwamo wageni waingie ndani kwa kupitia madirishani tena kwa kusukumana na kelele ziwe nyingi ndani ya nyumba?’ Kwa hali kama hiyo, kuna tatizo la msingi ambalo Rais anajitahidi kupambana nao ili arejeshe hali ya kawaida na tuweze kuingia ndani ya nyumba kwa kutumia milango iliyowekwa, na si vinginevyo.

Pamoja na jitihada zote anazozifanya tena kwa muda mfupi tu, wapo wanaosema hakuna la maana analolifanya, bali anavunja sheria, taratibu na kanuni. 

Kwa mfano, Gazeti Mwananchi – Ijumaa, Februari 5, 2016 toleo namba 5670 Uk. 3; pamoja na mambo mengine lilitoa habari “… Serikali ya Rais Magufuli haifuati Sheria na kanuni za utawala bora – tumeona unyanyasaji mkubwa kwa wafanyabiashara, bomoaboma ambayo haifuati misingi ya haki za binadamu”. 

Mahali pengine nimesikia wakisema: “Sheria zinavurugwa” na wengine kudai Rais ni “dikteta analazimisha mambo”, na kadhalika. 

Yote hayo nayakubali maana tangu ukoloni na baada ya Uhuru; sheria, kanuni na taratibu vimekuwapo; udikteta tunaufahamu upo na uvurugaji wa sheria hufanyika. Cha kujiuliza hapa sheria zinapovurugwa au udikteta ukawapo vinafanyika kwa faida ya nani?

 

>>ITAENDELEA