Hotuba ya Rais John Magufuli kwa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyotoa katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam mnamo Februari 13, 2016.

 

Sitajisikia vizuri kama sitasema, shikamoni,

Waheshimiwa viongozi wote mliohudhuria hapa na itifaki imezingatiwa

Mheshimiwa Mzee Mkali na Mwenyekiti wa Wazee wa hapa Dar es Salaam na waheshimiwa Wazee wa Dar es Salaam, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyetujaalia sisi wote kwa pamoja tuweze kuhudhuria hapa, lakini nikushukuru sana mwenyekiti na wazee wa Dar es Salaam kwa kutukaribisha sisi, tuje hapa tupate mawaidha ya wazee ambayo nina uhakika yatakuwa ni mwongozo mzuri katika kipindi cha kumaliza siku 100 ili tuwe na direction nzuri ya kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote. Tunawashukuru sana.

Lakini kwa niaba ya wazee wa Dar es Salaam niwashukuru Watanzania wote, wa vyama vyote, wa dini zote, wa makabila yote waliotuwezesha sisi kuweza kutuchagua ili tuwe viongozi wenu katika Awamu ya Tano, hakika napenda niwathibitishie wazee na Watanzania wote kwa ujumla, hatutawaangusha.

Tuliahidi kufanya kazi ili kuwa na Tanzania mpya. Tanzania ambapo kero nyingi tuweze kuzitatua. Nataka kuwathibitishia kwa niaba ya viongozi wenzangu, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri, makatibu wakuu, tutafanya kazi kwa juhudi kubwa, tutamtanguliza Mungu katika kuhakikisha kwamba yale tuliyowaahidi kwa ajili ya kuwafanyia kazi Watanzania tunayatimiza kwa nguvu zote. Ninachowaomba wazee na Watanzania kwa ujumla, mtuamini…mtuamini kwa sababu tuna lengo kubwa la kuibadilisha Tanzania. 

Katika shughuli zozote za kufanya mabadiliko huwa kuna changamoto zake, na changamoto zake zingine zinaweza zikawa zinawagusa baadhi ya watu, lakini nataka kuwakikishia Watanzania na wazee wa Dar es Salaam, watakaoguswa ni wachache sana kwa faida ya Watanzania walio wengi hasa masikini.

Tanzania hii, na mimi nataka niseme kwa dhati kwa wazee na viongozi wa dini haitakiwi kuwa maskini, Tanzania hii ina kila kitu, Tanzania hii ina utajiri wa kila aina, Tanzania hii haitakiwi kuwa na wanafunzi wanakaa chini, Tanzania hii haitakiwi watu wawe wanakosa maji, Tanzania hii haitakiwi unapoenda Muhimbili au kwenye hospitali zetu unakuta watu wamelala kwenye kitanda watu watano wengine chini. Tanzania hii ni yenye neema.

Lakini ni lazima tujue, wapo watu wachache waliotufikisha hapa. Wapo watu wachache waliotufikisha hapa. Mlituchagua kwa mioyo yenu yote, mlimtanguliza Mungu mkasema tunataka ninyi muwe viongozi, ndio maana nasema kwa dhati ndugu zangu wana – Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla, tunaomba mtuamini ili haya tunayoyatekeleza tuyatekeleze kwa kweli kwa sababu tunaamini tukiyatekeleza haya, nchi hii itabadilika na kuwa nchi ya mfano Afrika kama si duniani.

Ndugu zangu wana-Dar es Salaam, ninyi wenyewe mmekuwa ni mashahidi, mabilioni ya fedha za Watanzania zinavyotumika ovyo. Sitaki kutoa mifano mingi, lakini pamekuwa na mabaya… ya ovyo yanayofanyika katika nchi hii. Na ni kila sehemu, sio Dar es Salaam tu, nenda wilayani, nenda mikoani, nenda kwenye vijiji, kila mahali. Kwa hiyo ifike mahali sisi Watanzania tujiulize, tulimkosea nini Mungu. Kwanini Mungu asitusamehe kwa makosa yetu tuliyofanya? Ndiyo maana ninawaambia Wazee wangu hawa wa Dar es Salaam, mimi na serikali yangu tumejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania. Tunaomba muendelee kutupa nguvu, muendelee kutuombea kwa mwenyezi Mungu ili haya matamanio yetu  tunayotaka kuyafanya kwa ajili ya nchi ya Tanzania tuyatimize  kwa haraka sana na kwa speed kubwa sana.

Na sisi ndani ya Serikali tumejipanga, yule yeyote atakayejaribu kutukwamisha, tutambomoa. Tutambomoa kwa faida ya Watanzania hasa wanyonge.

Haiwezekani Watanzania kila mahali unapokwenda unawakuta wanalia. Wakati Tanzania ina rasilimali za kila aina. Ninyi wote wazee, Mzee Mkali na wazee wengine, mkiongozwa na Baba wa Taifa, mliihangaikia hii nchi tukapata Uhuru miaka zaidi ya 50 iliyopita. Uhuru tumeishaupata, sasa hivi kinachotakiwa ni maendeleo ya huo uhuru mliokuwa mkiutafuta.

Na jukumu letu, sisi kama vijana wenu ambao mmetutuma tufanye kazi, tutaitimiza kwa nguvu zote. Katika siku 100 ambazo sisi ndani ya Serikali tumefanya kazi, tumejifunza mengi; tumekumbana na changamoto nyingi. Wapo watu katika nchi hii, kwao fedha siyo tatizo na angalau basi zingekuwa hizo fedha wangekuwa wamezipata kwa uhalali, fedha hizo wamezipata kutoka kwa masikini ambao wanahangaika sana.

Kila tulipokuwa tukigusa, kuna maajabu. Nilimtuma siku moja Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenda bandarini, aliyoyakuta kule ni uozo, tumeanza kuchukua hatua, kila mahali ukigusa, ni shida.

Nilimtuma Katibu Mkuu wa Tamisemi kwenda Bariadi kule alikuta barabara moja, kilometa moja imejengwa kwa bilioni mbili, na ni barabara ya halmashauri ya wilaya, mimi nimekaa serikalini miaka 20, huwa kuna barabara kuu, barabara za mkoa na kuna barabara za wilaya. 

Upana wa barabara kuu ni tofauti na upana wa barabara ya mkoa na ni tofauti na barabara ya mkoa na ni tofauti na barabara ya halmashauri ya wilaya. Katika barabara kuu tangu nikae serikalini sijawahi kutengeneza barabara kuu, kilometa moja kwa bilioni mbili, lakini barabara ya halmashauri ya Bariadi kilometa 4.5 imetengenezwa kwa bilioni 9.2. Viongozi hao wapo, Mkuu wa Mkoa yupo, mkuu wa wilaya yupo, mkurugenzi yupo, injinia yupo kwa hiyo ninapozungumza kutumbua majipu ndugu zangu Watanzania mtuunge mkono tuyatumbue kweli kweli.

Barabara hizo, nimetoa mfano wa Bariadi zilikuwa zinatosha kutengeneza kilomita 22 hadi 23 za barabara za lami, leo zinatengeneza kilometa 4.5.

Juzi Mheshimiwa Waziri mkuu ameenda kuangalia tu yale mafuta yanayoingia nchini, Kampuni ya Puma na Oryx zote zile serikali ina share ya asilimia 50 iliyobaki ndiyo share ya makampuni hayo ya mafuta. Kwa hiyo 50 kwa 50. Ameenda kule kitu kinachoitwa flow meter ambacho ndicho kinaruhusu kupima mafuta yanayoingia nchini tujue mafuta yanayoingia nchini ni kiasi gani, miaka mitano hakifanyi kazi. Kwa hiyo, mafuta yamekuwa yakiingia katika nchi, yanagawiwa kwa watu na ndio maana mnaona ukitoka Dar es Salaam kwenda Kibaha kila mahali kuna sheli. Zile fedha zingeweza kununua madawa ya wananchi, zile fedha zingeweza kusomesha watoto bure, hizo fedha zingeweza kutengeneza barabara hata flyover za kila aina. Hiyo ndiyo Tanzania tuliyoikuta sisi Awamu ya Tano. Najaribu kutoa mifano hii, ni michache sana. Ningeweza kutoa mifano hii ni mingi ya kila aina.

Nimeenda Hospitali Muhimbili juzi, nilikuta akina mama wakanisimamisha wakaniambia Mheshimiwa Rais, nenda ukaangalie kwenye wodi ya wakinamama, mara kwanza nilienda upande mwingine, sikujua huko wodi ya akinamama ikoje.

Wasaidizi wangu wakaniambia usiende, nikawaambia ninaenda huko huko. Nilipoenda niliyoyakuta ni maajabu. Wodi Na 36, maji yaliyokuwayanavuja kutoka chooni yalikuwa yamesambaa hadi kwenye sakafu. Wakinamama wale wamelala kwenye magodoro unakuta godoro moja kuna watu watano. Hiyo ndiyo Tanzania. Lakini wakati unaenda kule Muhimbili, jirani kuna jengo ambalo linahudumiwa, linatumika kama ofisi ya wazazi na watoto, lina wafanyakazi 70, ni jengo la ghorofa tatu hadi nne. Lakini ukisogea mbele zaidi kuna jengo ambalo lilianza kujengwa tangu Awamu ya Pili, enzi za Mwinyi, jengo la ghorofa nne, halijaisha. Mwinyi hakulimaliza, akaja Mzee Mkapa hakulimaliza akaja Kikwete hakulimaliza na sasa niko mimi bado halijaisha.

Contractor anaitwa Masasi Construction Engeneering, lakini viongozi wote Muhimbili wapo. Walishindwa kumfukuza, mimi nilipokuwa Wizaya ya Ujenzi, nikiwa waziri tu nilifukuza makandarasi 3,000. Sijawahi kuona jengo la ghorofa tatu au nne likajengwa zaidi ya miaka 20. Nafikiri limechukua rekodi duniani, lile jengo linaweza kubeba watu 342, leo lina watu 100 wamewekwa kwenye ground floor, maji hayajawekwa, umeme hakuna. Ni aibu.

Lakini palepale Muhimbili, kuna jengo la MOI jipya ambalo linajengwa na kampuni moja ya China, ni la ghorofa sita nalo limejengwa kwa zaidi ya miaka minne, halijaisha mpaka leo pana mabishano ya namna ya kumlipa huyo kandarasi.

Kandarasi anadai bilioni tisa wao wanataka kumlipa sijui kiasi gani. Wamechukua tu wagonjwa wachache, floor ya kwanza, ya pili na ya tatu. Floor ya juu kule hakuna watu kwa sababu jengo halijakamilika. Jengo lile lina standby generator, bado haijafungwa. Hiyo ndiyo Tanzania.

Kwa hiyo ndugu zangu wazee wa Dar es Salaam, tunapochukua hatua, sisi viongozi mliotuchagua sisi si wakatili sana, tunawawakisha nyinyi uchungu wenu ili Tanzania iwe njema. Ninafahamu mawaziri wangu wanafanya kazi nzuri sana. Wanajifunza lakini wanaendelea kufanya kazi. Ninawapa muda na nyinyi muwape muda lakini na mimi mnipe muda tuweze kushughulia hizo changamoto ambazo ni kwa ajili ya Taifa hili.

Kwa Muhimbili kwa sababu nimefika mimi mwenyewe, niliahidi kulitatua hilo tatizo na kwa bahati nzuri waziri yupo hapa nilishatoa maagizo, lile jengo linalotumika kama ofisi ya uzazi wa mpango sijui na watoto kwa watu kama 70 hivi wahame ndani ya siku mbili. Sasa waziri na katibu mkuu watajua watawatafutia wapi kwa sababu ni ofisi kama ilivyo ofisi ya waziri, wanaweza kwenda Ofisi ya Waziri na Katibu Mkuu kukaa nao ofisini kwake pale Wizara ya Afya.

Lakini ndani ya siku mbili hizo hizo pawe pameshajaa vitanda, wale wakinamama waliokuwa wanalala chini wahamie kwenye jengo jipya la pili.

Lakini nina uhakika lile jengo jipya linalojengwa na Masasi Construction pamoja na lile jingine, kama kuna matatizo ya pesa pesa ipo, lakini kama tatizo ni mkandarasi afukuzwe kwa sheria za makandarasi Na. 17 ya mwaka 1997.

Tukianza kuvumulia na kulea huu uzembe hatutafika. Tusipoanza sisi kuchukuliana hatua hatutafika. Tanzania  itakuwa ombaomba wakati tulitakiwa sisi tuombwe.

Ninawaomba wazee wangu katika kipindi hiki, na sisi tunakiita kama kipindi cha mpito, mtuvumilie, kama ni majipu tutayambua kweli kweli. Likiota hapa, tutalitumbua, likihamia huku tutalitumbua likienda kichwani tutalitumbua, likienda mgongoni tutalitumbua, likienda kifuani tutalitumbua ili majipu yote yaweze kuisha na Tanzania iende mbele.

Nchi ya Tanzania haiwezi ikaendelea bila kuwa na mapato yake, lakini ni kweli wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikwepa kulipa kodi. Tumeanza, mara ya kwanza tulipoanza kuchukua hatua fedha zilioongezeka tukapata trilioni moja point something, mwezi uliofuata tukakusanya trilioni 1.592 na mwezi tulisanya trilioni 1.1063.

Tutaka hizi fedha tunazozikusanya ziende kuhudumia wananchi wa maisha ya chini. Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka katika Awamu ya Tano. Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka.

Kwa hiyo Mzee Mkali, kwa maana ile ile na jina lako kuwa mkali, sisi hatutafikia sifa za ukali wako, tutakuwa wakali wa kadiri ili kuhakikisha nchi inaenda.

Zipo kejeli nyingi wanasema nguvu ya soda, hata kama ni soda ukiweka gongo utalewa, kwa hiyo hii ni soda special ambayo tumedhamiria kwa ajili ya kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania. Haiwezekani nchi tajiri kama hii ya Tanzania, tunakuwa ombaomba, haiwezekani. Na ndiyo maana katika makusanyo tu ya muda tumeanza kuyaelekeza kwenye maeneo ya maendeleo.

Palikuwa na mradi wa Kinyelezi II ambao umekwama tangu mwaka 2012. Wafadhili Wajapani walitoa dola za Marekani  milioni 292 tulitakiwa tuchangie asilimia 15 ili katika gridi ya taifa ziongezeke megawati zaidi ya 240. Fedha hizo tumezitoa. Wajapani kampuni ya Somitomo imeshaanza kufanya kazi, na mwezi unaokuja tunakwenda kuweka jiwe la msingi.

Fly overs ya Dar es Salaam, kandarasi amesdhaanza kazikufanya mobilization. Na fedha za advance payment ameshalipwa na mwezi unaokuja tunakwenda kuweka jiwe la msingi.

Barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze, ile ya njia sita umembuzi yakinifu umeshakamilika, design imeshamalizika transaction advisor wa ule mradi ameshamaliza kazi yake kuna makandarasi 12 wameomba kujenga na ile barabara itakuwa barabara ya njia sita na itakuwa na fly over saba. Tunamalizia taratibu ili process zimalizike nina uhakika ile nayo kipindi hiki hiki cha Awamu ya Tano, barabara ile iweze kujengwa na kukamilika na pale tutakuwa tumepunguza msongamano. 

Barabara hizi za Dar es Salaam kwa sababu nipo Dar es Salaam ni lazima nizungumze ya Dar es Salaam, tumeshapata fedha zaidi ya bilioni 260 za kuanza kujenga daraja lingine kutoka Coco Beach hadi kwenye hospitali ya Aga Khan zaidi ya kilometa 7.4 na daraja lile litapita baharini, barabara ya Rangi Tatu kuja mjini pale nayo nilikuwa nazungumza na ubalozi wa Japan wanafanya process na ikiwezekana mwezi huu watangaze tender kwa ajili ya kujenga.

Ile interchange ya Ubungo, Benki ya Dunia walitoa fedha kwa ajili ya kufanya feasibility study na detailed design na wamekubali kutoa fedha karibu bilioni 7 kwa ajili ya kujenga interchange paleUbungo ya ghorofa tatu. Nina uhakika watani zangu Wazaramo watakwenda pale kufungia ndoa. Dar es Salaam ndiyo kioo cha Tanzania. Bila Dar es Salaam hakuna Tanzania.

Tuna mpango pia wa kufufua shirika letu la ndege ndio maana tumekuwa tunachukua hatua mbalimbali. Zingine ni ngumu. Zingine zinaumiza baadhi ya watu. 

Yuko mmoja pale alikuwa anashikwa alikuwa anataka kubadilisha fedha aweke kwenye akaunti yake bilioni 1,7  tukamkamata, zingine hatutaki kusema mengi kwa sababu yapo kwenye utaratibu wa Mahakama.

Tunasubiri ndege moja wafanyakazi zaidi ya 200 na kitu, ni lazima tubadilike, lakini ukitaka kununua ndege moja aina ya air bus yenye watu zaidi ya 120 kwenye soko la dunia leo, ukiwa na bilioni 140 unanunua. Sasa kama makusanyo yetu ni matrilioni kwanini tusitenge kila mwezi. Kupanga ni kuchagua.

Na sisi kwa niaba yenu, tumeamua kupanga na katika mipango yetu lengo letu kubwa ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa na maisha bora. Tuliahidi kutekeleza haya ni lazima tuyatekeleze kwa nguvu zetu zote.

Na ndiyo maana siku zote tumekuwa tukisisitiza, ndugu zangu Watanzania tujifunze kulipa kodi, ukienda hotelini omba risiti, ukienda dukani omba risiti, chochote unachokwenda kununua omba risiti ili kusudi wafanyabiashara katika risiti ile kuna percentage ambayo inabaki ya Serikali. Inayobaki ile ndiyo tunayoipekeleka kwenye huduma za wananchi.

Tumezungumza wanafunzi wasome bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Changamoto Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amezieleza hapa, lakini kwa Tanzania nzima wanafunzi waliingia darasa la kwanza ni milioni 1,300,o37. Darasa la kwanza.

Na hii kujitokeza watanzania wengi wamekuwa na maisha magumu. Wamekuwa ni maskini, wanakuwa wanashindwa hata kupeleka watoto wao kwenda kuanza shule. Kwa bahati mbaya wakipelekwa shuleni michango inakuwa ni ya ajabu. Unaombwa mchango huu, mchango huu mwishowe unaamua mtoto wako nenda kauze vitumbue.Wwao watoto wao wanasoma, watoto wetu hawasomi. Ndiyo maana tumesema elimu ni bure, changamoto zimetokea. Kila kitu kilicho kizuri kina changamoto zake. Nataka kuwahakikishia Wazee wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla, changamoto hizi tutazimaliza.

Tulitenga bilioni 137 katika bajeti inayokuja tutawaomba Waziri wa Fedha na Bunge nina uhakika wataturuhusu, Mheshimiwa Zungu yupo hapa tuongeze mara mbili zaidi. Lakini kwa changamoto ya Dar es Salaam hii ambayo nimeona ninyi viongozi wa Dar es Salaam mmeanza kuchukua hatua. Na niwapongeze sana wazalendo wa Kitanzania ambao Mungu amewabariki akawapa kitu na wao wameana kutoas sadaka kwa ajili ya kuwasaidia watoto wao wasome.

Nimemuona Mheshimiwa Makonda akihamasisha hili sana. Mheshimiwa Makonda nakueleza hili limekujengea heshima kubwa kwa hiyo ukipanda hata cheo, watu wasikuonee kwa sababu you deserve it.

Kwa sababu na sisi tunakaa Dar es Salaam, nilikuwa nazungumza na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Kuna mawaziri hapa, naibu mawaziri na makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu, nilipopiga hesabu mpaka na Spika na kuona wote tunakaa humu Dar es Salaam tukaona kama watu 82 hivi.

Nikasema kwa sababu siku nilipokuwa nawateua hawakuniomba, na wakakubali uteuzi wangu, nikitoa amri leo watoe milioni moja moja kwenye mshara wao ni vibaya? Kwa hiyo, wakitoa milioni moja moja zinafika milioni 82. Inabaki milioni 18, lakini kuna Makamu wa Rais, kuna Waziri Mkuu, kuna mimi. Tuigawane ile milioni 18 kila mmoja achangie milini sita sita itimie milioni 100.

Kwa hiyo tunaileta kwenye uongozi wa Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kwa sababu tumebanabana matumizi pahali pengine pengine kwa mamlaka mliyonipa, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa nataka nikuhakikishie nitakuongezea bilioni mbili zingine. Bilioni mbili maana yake ni milioni 2,000. Ole wako sasa ukazitumie vibaya hizo.

Msema kweli ni mpenzi wa Mungu na kwa sababu sasa tuna wilaya, tuna wilaya ya Temeke, kuna wilaya ya Ilala, kuna Kinondoni, kuna wilaya ya Ubungo, kuna wilaya ya Kigamboni. Muzigawe hizo fedha katika wilaya tano, ziende zikachague maeneo ambayo yatajenga shule ili watoto wetu hawa ambao ni taifa la kesho liweze kupata mahali pa kusoma.

Ukiziongezea hizi milioni 100 zetu hizi ambao ni wakazi wa Dar es Salaam ninafikiri zinaweza kutoa wito. Kwa hiyo nitoe wito, kwakuwa michango ni hiari, pasitokee watu kupitia hii hotuba wakaanza kulazimisha watu, atayeguswa kuchangia kwa ajili ya shule, atoe. Usiende ukamtafuta mzee mmoja ana shida unamlazimisha lazima uchangie, saa nyingine unatoa hata ndoo yake au sufuria yake ya kupikia. Wale watakaoguswa kuchagia, wachangie lakini mchango si lazima.

Kwa hiyo, niwaombe viongozi wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi na nirudie wito wangu, ni aibu sana kwa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi unakaa kwenye ofisi nzuri unakuwa kwenye gari zuri, unalala kwenye nyumba nzuri halafu jirani kuna shule wanafunzi wanakaa chini. Kama unajua kujipima vizuri, kiongozi huyo ujitambue kwamba hutoshi kuwa kiongozi.

Ninajua sijateua wakuu wa mikoa, maDC na wakurugenzi, nimefanya kwa makusudi ili niendelee kuwachambua vizuri, ni wa nani wanaotosha na ni wa nani hawatoshi, kwa hiyo kutosha kwao ni lazima wajipange namna gani watatua kero za wananchi.

Ni lazima tufike mahali sisi viongozi tujue jukumu letu, unapopewa uongozi wowote ujue wewe ni mwakilishi wa watu hasa walio wanyonge hasa katika kutatua shida zao.

Niwaombe viongozi wenzangu tulio katika Awamu ya Tano, kila mmoja ajipange na ajitume namna gani atakuwa mbele katika kutatua shida za wananchi. Na hiyo ndiyo thawabu ya pekee kwa Mwenyezi Mungu kwa kazi yake tutapokuwa tunaifanya hapa duniani.

Tuliuomba uongozi na hayo ndiyo masharti ya uongozi. Lakini niwaombe viongozi pia na Watanzania wote, ninajua mmetupima sisi katika siku 100, inawezekana mnatuonea pia kwamba siku 100 za Magufuli, siku 100 za waziri mkuu, makamu wa rais na mawaziri, mmesahau ninyi kujipima siku 100 mmefanya nini kwa ajili ya Watanzania. Kila mmoja wetu, kila mahali alipo ana wajibu na yeye wa kujipima kwamba katika siku hizi 100 za Awamu ya Tano ameifanyia nini Tanzania.

Kama ni mkulima umeifanyia nini Tanzania, kama ni mvuvi umeifanyia nini katika siku 100, kama ni mfanyabiashara umefanya nini katika siku 100 kama ni muuza vitumbua umefanya nini katika siku 100, ili kwa umoja wetu kwa pamoja tutaijenga Tanzania yetu yenye neema.

Haiingii akilini, haiingii akilini kwa sasa hivi kila mahali kuna mvuna zinanyesha, kila mahali madaraja yanakatika, lakini unamkuta kiongozi mmoja anasema hakuna chakula maana yake ameshindwa kuutumia vizuri muda wake wa kuhamasisha wananchi hata kulima mchicha tu.

Nguvukazi kubwa za Watanzania, hasa vijana utawakuta wanacheza pool, wakati wa asubuhi. DC upo, katibu tarafa upo, mtendaji wa kata upo ukifika wakati wa mavuno, huku sisi hatuna chakula.

Natoa wito kwa viongozi wenzangu, katika mkoa au wilaya au tarafa itakayokuwa haina chakula kwa mwaka huu ambapo mvua zinanyesha sana, naye ajitambue kwamba hafai kuongoza katika nchi hii.

Ni lazima sisi viongozi tuseme ukweli, na msema ukweli ni mpenzi wa Mungu na ndiyo maana kauli yetu tunazungumza asiyefanya kazi na asile, na hapa tunasema “Hapa ni Kazi Tu”.

Tumeshindwa kutoa huduma nyingi kwa watu wnaostahili kupewa huduma. Katika kampeni nilizungumza kwamba wazee watakaofikia umri fulani ni lazima tuwape hata fedha za kuwasaidia kuishi kwa sababu wamefanya kazi kubwa katika nchi hii. Lakini hili haliwezi likawezekana kama kuna vijana ambao hawafanyi kazi, ni lazima kila mmoja wetu afanye kazi. Na hili lazima nisema ukweli kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu.

Kwa hiyo Mheshimiwa RC wa Dar es Salaam, ninajua watakuuliza sana wakuu wa mikoa wenzako kwamba nitateua lini, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, kwanza tarehe ya kuteua hutaijua na wao hawataijua.

Lakini ninaendelea kuwachambua, lakini angalau Mheshimiwa nani huyu…nani huyu… Makonda umeshajihakikishia utakuwamo, lakini na wewe sasa usiende kulala, kaendelee kufanya hizo juhudi, lakini mimi nawapongeza Dar es Salaam hata kuniandalia mkutano kama huu wa kuja kutupa maelekezo yenu, tunajisikia vizuri sana, mimi na wenzangu ndani ya Serikali. Mungu awajalie sana.

Waheshimiwa Wazee wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla, sisi ni watumishi wenu, napenda kuahidi kwenu waheshiminiwa wazee Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla yale yote tuliyoyaahidi wakati wa kampeni, kila mkoa, kila wilaya, tutayabeba.

Tunafahamu mwanzo ni mgumu, una changamoto zake. Nina uhakika Mungu atatujalia kuzikabili pamoja na ninyi. Ni maeneo mengi yana changamoto, kwenye kilimo kule kuna machangamoto mengi, kwenye mashamba na ndiyo maana mmeona mawaziri wangu wanavamia usiku kwenye hata machinjio usiku wa manane ni kwa sababu wanataka kutimiza yale ambayo waliahidi kwa Watanzania.

Kwa wakulima tumefahamu kumekuwa na mashamba mengi mashamba pori, tumeanza kuyafuta hati zake ili Watanzania wengi wapate mahali pa kufanyia kazi. Kwa Dar es Salaam, nataka niwaahidi Dar es Salaam itabadilika. Nafahamu kuna changamoto ya kivuko cha Kigamboni. Daraja lile sasa la Kigamboni limekamilika. Kwa hiyo mambo yatakuwa murua, tunafanya haya yote kwa sababu tutimize wajibu wetu kama tulivyoahidi kwenu.

Napenda kuvipongeza sana vyombo vya ulinzi na usalama katika siku hizi 100 zilizopita na zitaendelea hivyo katika kulinda ulinzi na amani ya Tanzania. Na ninaposema amani ya Tanazania ni mpaka Zanzibar na Pemba. Vyombo vyetu viko imara na mambo yataenda shwari.

 Napenda pia kuwashukuru viongozi wa dini mbalimbali kwa jinsi ambavyo mmekuwa mkiendelea kuliweka Taifa hili katika mikono ya Mungu, kwa ajili yenu Tanzania itapona. Endeleeni kuliombea Taifa hili ili liwe Taifa lenye amani katika maisha yake yote.

Kuhusu mipango ya maendeleo ya miaka mitano, yako mengi ambayo tumeyapanga ikiwa ni pamoja na kujenga uchumi wenye viwanda. Tumeanza kuandaa mazingira ya kufanya hivyo.

Nipende pia kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana waandishi wa habari. Vyombo vya habari mmetusaidia sana. Mumeisaidia sana Serikali hii, naomba msichoke. Naomba msichoke. Mnatoa elimu ya kutosha, mnatoa maelekezo ya kutosha, na sisi ndani ya Serikali huwa tunafatilia.

Juzi juzi kuna gazeti moja liliandika. Ni gazeti gani… la JAMHURI, likawa linatoa michoro ya huko, tukawa tunaulizana Waziri Mkuu, hawa wamejuaje sisi tunapanga mipango katikati na wao wameshajua. Tunawapongeza. Vyombo vya namna hiyo ndivyo vinatakiwa kufanya, siyo vyombo ambavyo vinakaa pale kwa ajili ya kuitafu…kuitukana Serikali na Tanzania.

Sisi Watanzania hatuna mahali pengine pa kwenda kukaa. Yapo magazeti mengine kwakweli yanaandika mpaka mtu unashangaa. Unajiuliza huyu ni Mtanzania au sio Mtanzania? Yeye kila kitu ni kuichafua tu Tanzania kana kwamba yeye pakitokea machafuko hapa ana mahali pengine pa kwenda kukaa.

Lakini kwa ujumla vyombo vingi vya habari vimekuwa very supportive kwenye Government hii. Nawapongeza sana keep it up. Na ndiyo maana nimeweza kutoa mfano, nimetoa mfano wa gazeti la JAMHURI lilivyotoa uozo kule kwenye flow meter. Tunataka magazeti mfanye hivyo. 

Pakitokea kuna uozo mahali uandike. Sisi tunasoma. Sisi wote ni Watanzania, sisi wote tuna wajibu wa kuipeleka Tanzania mbele. Na tuiweke Tanzania yetu kwanza. Hakuna mtu atakayeisemea uzuri wa Tanzania. Ni vema sisi Watanzania, tuisemee Tanzania mazuri ili hata wa nje watatusemea mazuri.

Kuhusu suala la uchaguzi Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, nafikiri ni  kifungu namba 112 au 115 lakini kama ilivyo kawaida kwa Tume za Uchaguzi zilizo huru duniani, haiwezi ikaingiliwa na rais yeyote. Ni kama ilivyo NEC ya Tanzania na ZEC ya Zanzibar na ndiyo maana tume zote za uchaguzi duniani huwa ni huru. Huwezi upande mmoja pakawa huru upande mwingine pakawa siyo huru. Ninapenda kuheshimu sheria.

Kwa hiyo ZEC ina uhuru wa kuamua mambo yake, na haiwezi kuingiliwa na mtu yeyote. Lakini kama kuna tafsiri yoyote ambayo ni mbaya, ambaye anayetaka kuitafuta hiyo tafsiri aende mahakamani, Mahakama iko hapo hutaki kwenda halafu unamwambia Magufuli ingilia…si nenda mahakamani wakatoe tafsiri iliyo ya haki. Kwa hiyo siingilii, nitaendelea kukaa kimya.

Jukumu langu kama Amiri Jeshi Mkuu ni kuhakikisha usalama wa Zanzibar na Pemba unaimarika, yeyote atakayeleta fyoko fyoko mahali popote, iwe Ukerewe, iwe Nachingwea, iwe Dodoma, iwe Dar es Salaam, iwe Pemba, iwe Zanzibar wajue vyombo vya usalama vipo kwa ajili ya kuwashughulikia hawa.

Ndugu zangu, wanaDar es Salaam, na Mheshimiwa Mzee Mkali na wazee wangu na Watanzania kwa ujumla, napenda niwashukuru sana Watanzania wote. Na ninaposema Watanzania wote nina maana wa vyama vyote, Watanzania wa dini zote, wa makabila yote. Tudumishe amani yetu, tudumishe mshikamano wetu tudumishe mshikamano wetu kama Watanzania. Itatusaidia sisi viongozi wetu kuyafanya yale tuliyowaaahidi.

Huwezi ukajenga kiwanda, huwezi ukatengeneza barabara, huwezi ukatoa elimu bure wakati mahali hapo  hakuna amani. Tushikamane kwa umoja wetu katika kuhakikisha Tanzania yetu inasonge mbele.

Napenda kuahidi kwenu wanaDar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kwa niaba ya Serikali ninayoiongoza, sisi tuko makini, tumeamua kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa. Kila mmoja katika nafasi yake, anajitahidi kufanya. Nataka niwahakikishie tutaweza, nataka niwahakikishie Tanzania tutaivusha, nataka niwahakikishie Tanzania itakwenda mbele kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania wote. Nataka niwakikishia tutajali watu wanyonge ili kuhakikisha shida zao tunazimaliza. 

Naomba wazee wangu na Watanzania kwa ujumla mtuamini, lakini mwendelee kutuombea. Kila palipo na wazuri na wabaya yapo. Kila palipo malaika hata shetani anakaa pembeni. Kwa nguvu zetu, na kwa sala zetu na kwa dua zenu. Tutaivusha Tanzania kwa sababu hilo ndilo lengo letu. Na kwa wale wanaolalamika wachache muwapuuze kwa sababu ni miongoni ya waliofaidi matunda ya wanyonge kwa miaka ya nyuma. Hatuwezi tukakubaliana nao.

Lakini nataka niwahakikishie wafanyabiashara wote wa Tanzania tuko pamoja na wao, wafanye biashara halali, kwa manufaa yao na kwa manufaa ya Watanzania. Kwa wale wanaotaka kuanzisha viwanda wajenge viwanda hata mamilioni, kwa wale wanaotaka kuwekeza katika nchi hii nawawekeze, na kwa wazalendo wa Tanzania nataka niwaambie wafanyabiashara wa Kitanzania ni huu ni wakati wenu. Nchi hii haiwezi ikajengwa na watu kutoka nje. Rasilimali hii ya Tanzania tumepewa na Mungu, lazima tuiendeleze sisi.

Kwa hiyo niwaombe wafanyabiashara wa Kitanzania, watumie nafasi hii ya Awamu ya Tano katika kufanya kila kitu wanachokiweza kwa ajili ya kufanya biashara. Ukianzisha kiwanda cha matunda, fanya. Hata pangekuwa na kiwanda cha vitumbua, wewe tengeneza kusudi uwe usafirisha upeleke nje. Tunataka Tanzania iende mbele kwa faida ya Watanzania wote. Sapoti ya Serikali yangu na wizara zangu zitawapa sapoti kubwa. 

Mheshimiwa Mzee wetu Mwenyekiti wa Wazee wa Dar es Salaam, Waheshimiwa viongozi wa dini, Wazee wa Dar es Salaam wote na Watanzania kwa ujumla, niliona nizungumze haya, na saa nyingine unapozungumza na wazee lazima uwe mwangalifu kwa sababu unaweza ukakosea na ukatandikwa viboko hapohapo, lakini kama yapo wazee wangu niliyowakwanza mnisaheme. Lakini nimezungumza haya yote kwa sababu ya uchungu wa Tanzania yangu.

Nimezaliwa Tanzania, nimekulia Tanzania, mimi ni Mtanzania, nitafanya kazi Tanzania, nitafia Tanzania, nitazikwa Tanzania. Kila mmoja wetu katika mahali pake, afanye kazi kwa ajili ya Tanzania hii. Mungu atatusaidia, atatujali kwa yote. Mungu ibaraki Tanzania, Mungu wabariki wazee wa Dar es Salaam, Mungu wabariki Watanzania wote, Mungu wabariki Watanzania wote kwa faida ya Watanzania wote. Ndugu zangu ninawashashuru sana, wazee wangu ninawashukuru sana. Asanteni.

1916 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!