MAGUFULIToleo Na. 198 la Gazeti la JAMHURI la Julai 14, mwaka huu kwenye ukurasa huu niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari: “Kwanini sitomsahau Dk. Magufuli”.

Maudhui ya makala hiyo yalikuwa kumpongeza yeye binafsi na wana CCM kwa uamuzi wao wa kumpitisha kukiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi wa rais.

Hatimaye Dk. Magufuli, amefanikiwa kushinda urais. Anakuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sidhani kama anahitaji maelezo ya nini anachopaswa kuwafanyia Watanzania, kwa sababu anajua shida zinazowakabili wananchi.

Tunasema “urais ni taasisi”. Ndiyo, urais ni taasisi, lakini mara zote ni vigumu sana kwa mabehewa kufanya kazi yake ya kusafirisha shehena kama injini inakuwa haitekelezi wajibu wake wa kuyavuta na hata kuyaongoza. Rais ni kama injini ya treni inayoongoza na kuyavuta mabehewa. Kama injini yenyewe ikiwa haitekelezi wajibu wake ni kosa kuyalalamikia mabehewa.

Rais akiwa legelege, hata hao wasaidizi wake watakuwa legelegele. Rais akiwa mkumbatia wezi na mafisadi, Serikali yake itafeli tu. Lolote linaloonekana kwenye utendaji kazi wa Serikali ni matokeo ya mazao ya mkuu wa serikali au dola husika.

Watanzania wana kiu ya kuona tofauti ya uongozi wa Dk. Magufuli na mtangulizi wake. Sijapata muda wa kutosha kufanya tathimini ya ushindi wa Dk. Magufuli, lakini lililo wazi ni kwamba amepewa ridhaa ya Watanzania yeye kama Magufuli, na si chama chake. Hili linathibitishwa na majimbo ambayo wapinzani wameshinda ubunge, lakini kura za urais kapewa yeye. Hiyo ni ishara kwamba wapigakura wamemwamini zaidi yeye kama yeye, na si chama.

Watanzania hawana shaka na uchapaji kazi wa Dk. Magufuli, ingawa sidhani kama wote wanajua nini kitakachofanywa na Rais huyu mpya katika kulitumikia Taifa letu. Watanzania wajiandae kuwa na Rais wa aina yake- Rais asiyekubali kuwabeba wazembe, wala rushwa, wahujumu uchumi na wanaofanya kazi kwa mazoea.

Chini ya Dk. Magufuli, hata wale mawaziri wezi na wenye kutumia vibaya madaraka yao wajue hawana nafasi. Juzi nimewaona baadhi yao wakijitajidi kwa kila namna kumsogelea ili pengine awakumbuke. Wanaomjua Dk. Magufuli, wanasema hao wanajidanganya. Amekuwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa miongo miwili. Anawajua watendaji wa kweli na watendaji wa hovyo. Anawajua wote walioshiriki na wanaoshiriki kuliangamiza Taifa. Anawajua nani waligeuza ofisi za umma kuwa ofisi zao binafsi. Anawatambua kwa matendo mawaziri ambao wamegeuza mali za umma kuwa za kuwanufaisha wao, ndugu, marafiki na warembo wao.

Anawajua vema kabisa wale waliofikia hatua ya kutoa zawadi ya wanyamapori 700; mali ya Watanzania; kwa rafiki zao Wamarekani bila kulipa japo shilingi moja! Fikiria, Waziri anatoa kibali cha zawadi ya wanyampori 700 kwa kutumia kibali cha Rais, halafu hata rais mwenyewe hashituki!

Kwa taarifa tu, tayari kuna waziri keshawapa kibali wawekezaji kuendelea kuwinda kwa miaka 30 wakati sheria inasema watapewa kila baada ya miaka mitano! Wahujumu wa aina hii si wa kuisogelea Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa miaka 20 Dk. Magufuli akiwa waziri amesafiri safari sita nje ya nchi! Hii ni rekodi ya aina yake. Muda mrefu ameutumia kufanya kazi za Watanzania.

Kwenye Baraza linalovunjwa wiki hii kuna mawaziri wanasafiri Marekani mara mbili kwa mwezi; na mara tatu Ulaya! Wengine wanasafiri wakiwa na warembo wakidai wanakwenda kutangaza utalii! Fedha za umma zinatafunwa kana kwamba hazina mwenyewe, halafu kabwela wa kule Kasesya, Rukwa anadaiwa mchango wa maabara!

Lakini kwa mawaziri wa aina hiyo hatuwezi kushangaa kwa sababu aliyewateua yeye mwenyewe hawezi kumaliza mwezi akiwa ndani ya nchi; na akisafiri ughaibuni anamaliza hadi wiki tatu! Rais wa nchi, huumwi; unakaa nje ya nchi kwa wiki tatu? Rais wa nchi, safari ambayo alistahili kwenda Katibu Tawala wa Wilaya, unakwenda wewe? Rais wa nchi, hakuna mwaliko unaoweza kusema “huu hapana, aende Katibu wa Wizara!”

Hao waliofaidi fedha za Watanzania kwa staili hiyo sasa wanapigana-kwa sala na pengine kwa nguvu za giza ili waweze kukumbukwa kwenye Awamu ya Tano. Rais Magufuli ambaye mara zote amemtanguliza Mungu, bila shaka atashinda yote hayo.

Kuna mawaziri walioziacha ofisi, wakahamishia kazi zao katika hoteli za kitalii kwa malipo ya mabilioni ya shilingi za walipakodi wa Tanzania. Hawa nao wanajitahidi kwa udi na uvumba kuona wanaendelea kuwamo kwenye Baraza la Mawaziri. Dk. Magufuli, akiwarejesha hao wapo watakaosema afadhali ya Kikwete, maana inawezekana yeye aliwateua akiwa hajui udhaifu wao, lakini Mheshimiwa Magufuli, amewaona na anajua udhaifu na dhambi zao!

Lakini wapo watendaji waliofukuzwa au kuachishwa kazi kwa majungu na udhaifu wa viongozi wakuu wa nchi. Mfano, hakuna asiyejua kwamba mtu kama Balozi Khamis Kagasheki, mchapakazi, aliondolewa kwenye nafasi yake kwa sababu ya udhaifu wa Waziri Mkuu na aliyemteua. Operesheni Tokomeza ilikuwa ni ya kijeshi. Waziri wa kawaida hana mamlaka ya kisheria ya kuzuia utekelezwaji wa operesheni inayoendeshwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Wala kiongozi wa operesheni hawezi kuripoti kwa waziri wa kawaida, isipokuwa kwa viongozi wakuu wa nchi.

Udhaifu wa Waziri Mkuu wa kushindwa kuwatetea mawaziri wake ni udhaifu mbaya, lakini udhaifu wa Rais kushindwa kumtetea waziri wake kwa jambo analojua huyo waziri hana mamlaka ya kulizuia, ulikuwa udhaifu mbaya kweli kweli. Matokeo ya udhaifu huu ni kuwapoteza wachapakazi wazuri.

Kilichofuata baada ya waziri huyo kujiuzulu ni “kuiuza” wizara kwa mtu ambaye hana sifa hata ya kuwa mtendaji wa kitongoji. Amevurunda wizara ambayo ndiyo injini inayoliingizia Taifa mapato mengi ya kigeni.

Kiongozi kama Dk. Emanuel Nchimbi, aliyekuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, alikosa kazi kwa staili hii hii ya udhaifu wa Waziri Mkuu na viongozi wengine wakuu wa Serikali. Huyu aliandika barua zaidi ya mara tatu akionya hatari iliyokuwa inaendelea kwenye Operesheni Tokomeza, lakini hakusikilizwa. Zawadi pekee aliyopewa kwa utoaji taarifa hiyo ni kuondolewa kwenye uongozi!

Kwenye kundi hilo wapo wachapakazi wengine waliofukuzwa kazi kwa sababu tu ya vita ya gesi. Kundi la matajiri kwa kutumia ukwasi na ushawishi wa vyombo vya habari wanaweza kuamua nani awe na nani asiwe kwenye Baraza la Mawaziri, na kweli Rais akanywea! Uchunguzi unafanywa, wanabainika hawahusiki na lolote kwenye ufisadi; lakini wanaachwa hivi hivi. Viongozi makini wanatupwa, wasiofaa wanabebwa.

Watanzania hawatarajii kuona matajiri wakitumia nguvu za fedha na vyombo vya habari kuwang’oa mawaziri na watendaji wengine wazuri. Hayo, bila shaka katika Serikali ya Rais Magufuli, yatabaki kuwa historia. Asikubali kuwapoteza viongozi wachapakazi kwa sababu tu ya chuki binafsi za kimaslahi.

Nchi yetu ina rasilimali kubwa mno ya watu waadilifu na wachapakazi. Ni suala la kuwaibua tu. Mfano mzuri ni kwa Dk. Magufili mwenyewe. Rais Benjamin Mkapa, alipomwibua mwaka 1995 aliwashangaza Watanzania wengi, maana jina lake halikuwa maarufu miongoni mwa wanasiasa. Kuibuliwa kwake kumekuwa na manufaa makubwa kwa Taifa, na sasa mtu aliyekuwa hajulikani, ni Rais wa Taifa letu. Rais Magufuli naye awaibue watu wa aina hiyo. Wapo Watanzania wengi kabisa wazuri kiutendaji.

Miongoni mwa matatizo kwenye Katiba ya sasa ni ya kumlazimisha Rais kuwapata mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge wa kuchaguliwa na wale wa kuteuliwa. Sioni ubaya endapo Katiba hii itapata kiraka kingine cha haraka haraka cha kumwezesha Rais kuteua mawaziri kutoka kokote-ndani na nje ya Bunge. Rais anahitaji wigo mpana wa kumwezesha kuwapata mawaziri wachapakazi. Bila kufanya hivyo, ataendelea na utaratibu wa kuli-circle humo humo. Ataendelea kuteua kwa misingi ya “huyu ana afadhali!”.

Dk. Magufuli anawajua wahujumu, na kwa hakika zawadi ya kwanza kwa wapigakura wa Watanzania ni kuhakikisha anawateua viongozi waadilifu. Sasa ni wakati wa rasilimali za Tanzania kuwanufaisha Watanzania wenyewe kwanza.

Sisi ambao tumewekwa kwenye Mhimili wa Nne wa Dola (usio rasmi), kazi yetu ni kumsaidia Rais Magufuli aweze kutekeleza ahadi zake. Tuna wajibu wa kumweleza wazi wazi nani anamkwamisha. Tuna dhima kubwa ya kumpa orodha ya wakwepa kodi na wahujumu uchumi. Tunayo mengi mno ya kumsaidia. Tulijitahidi kuyaweka wazi kwenye uongozi wa Awamu ya Nne, lakini hatukusikilizwa, matokeo yake ndiyo haya ya mambo kuparanganyika.

Vyombo vya habari vinawasilisha hisia za wananchi. Ukiacha machache, yaliyo mengi kwenye vyombo hivyo ni yale, ama yanayosemwa, au yanayotendwa ndani ya jamii. Wazanaki wanasema: Omubhehi ahabheha kinoaruzi (mwongo huongopa kile alichokiona).

 

Sehemu ya makala yangu ya Julai 14, mwaka huu ilisomeka hivi:

 “Dk. Magufuli amekuwa serikalini kwa miaka 20 sasa. Amekuwa chini ya marais wawili. Anazijua changamoto mbalimbali zilizowakabili.  

 Hatutarajii awe sehemu ya walalamikaji. Ajitahidi kuwa na jibu kwa kila swali. Atakapoona umaskini wa Watanzania unazidi kuongezeka, asiseme hajui kwanini unaongezeka. Sharti awe na jibu na suluhisho.

“Hakuomba kuwa rais wa kulalamika. Wana-CCM waliompa kura nyingi namna hiyo, na Watanzania ambao bila shaka watampitisha, hawatarajii kumsikia rais akiwa sehemu ya walalamikaji.

Watu wenye matarajio kutoka kwake endapo ataingia Ikulu ni wengi kweli kweli. Kuwaridhisha wote ni jambo lisilowezekana.

 Kazi yangu imenifanya niwe karibu na viongozi wengi waliojitokeza kuomba urais ndani na hata nje ya CCM. Mwandishi wa habari hana rafiki wala adui. Kwa maneno mengine, mwandishi wa habari kila mtu ni ‘abiria wake’.

 “Wapo wasiotaka kuutambua ukweli huo, na kwa maana hiyo haishangazi kuwasikia wakitoa tuhuma nzito dhidi ya waandishi wa habari, hata wakati mwingine wakisema wamenunuliwa au wamehongwa na mafisadi.

 Alhamisi ya Mei 28, 2015 ni siku maalum kwangu. Nitaendelea kuikumbuka. Nitaikumbuka kwa sababu ni siku ambayo Dk. John Magufuli, kwa kutumia simu yake, alinipigia na kunitaka tuonane katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma. Sikujua sababu ya mwito huo, na wala sikuwa na shaka kwa sababu Dk. Magufuli ni kiongozi tuliyefanya kazi nyingi njema kwa maslahi ya nchi yetu.

 Niliwasili kwenye Viwanja vya Bunge saa 5 asubuhi, na yeye akawa ametoka nje baada ya kipindi cha maswali na majibu. Ilikuwa siku moja tu baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.

 “Nje ya viwanja alitumia zaidi ya nusu saa akisalimiana na wabunge mbalimbali. Nikamsubiri jirani na mahali lilipoegeshwa gari lake. Punde, akajongea na tukaweza kuzungumza.

 “Nimekuita ndugu yangu kukueleza jambo moja. Naomba unisaidie. Chama kimetoa ratiba ya kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi. Mimi nitachukua fomu ya kuwania urais. Naomba unisaidie kulifikisha hilo kwenye vyombo vya habari.”

  “Aliniambia maneno haya tukiwa wawili tu. Yalinipa msisimko mkubwa. Gazeti la JAMHURI linatoka kila Jumanne. Siku ya kuipata habari hii ilikuwa ni Alhamisi; na kwa sababu habari hii ilipaswa isomwe mapema, nikaona sina sababu ya kuwa mchoyo.

  Nikawasiliana na wahariri wawili wa magazeti mawili – Mtanzania na Raia Tanzania. Nikawaeleza. Wakanikubalia. Nikawaandalia habari ndefu pamoja na wasifu wa Dk. Magufuli. Ilipofika jioni, nikawapelekea. Asubuhi iliyofuata, magazeti hayo mawili yakachapisha habari hiyo yakiwa yameipa umuhimu wa kwanza. Mjadala wa wagombea urais ukawa umekolea.

 Kusema kweli Dk. Magufuli alitangaza nia ya kuwania urais kwa mtu mmoja tu – mimi! Kwangu hii ilikuwa na itaendelea kuwa heshima kubwa sana.

 “Mwaka 2005 nilipata bahati kama hii. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, naye alitangaza nia ya kuwania urais kupitia kwangu katika mazungumzo yetu tukiwa wawili ofisini kwake, Dar es Salaam. Wakati huo nikiwa Mhariri wa Habari Mwanzilishi wa Gazeti la Tanzania Daima. Asubuhi, ni Tanzania Daima pekee iliyokuwa na habari hiyo.

 Kama hii ya Dk. Magufuli, ile ya Mheshimiwa Sumaye nayo ilikuwa na itaendelea kuwa heshima kubwa kwangu. Notebook nilizotumia kupata habari hizi sasa ni sehemu ya nyaraka muhimu katika makumbusho yangu.

 Mwaka 2005 Mheshimiwa Sumaye hakufanikiwa. Mwaka huu bila shaka Dk. Magufuli atapenya na hivyo kuzidi kuinogesha furaha yangu.

 Mwito wangu ni kwamba kama amekuwa rafiki wa vyombo vya habari siku zote, aendelee kuwa hivyo hivyo wakati huu wa kuelekea kwenye kampeni na hata kama atafanikiwa kushinda. 

 “Vyombo vya habari ni muhimu kwa kiongozi yeyote anayetaka kufanikiwa. Wengine walianza wakiwa marafiki, lakini mwisho wa siku wamewatupa wanahabari.

 “Nimeyasema haya si kwa sababu nyingine, isipokuwa kuonesha kuwa kama alinithamini na kunitambua, hata akaamua kutangaza nia yake ya urais kupitia kwangu, basi nami niitambue na kuienzi heshima hiyo.

  “Lakini ajue kazi yangu ni hii hii – kuandika. Sitoandika mambo ya kumfurahisha tu. Wakati mwingine nitaandika yatakayomchukiza lakini yenye ukweli kwani sipendi kumweleza mtu jambo lile tu analopenda kusikia. Nitamwandikia ya kumfanya achape kazi vema kwa maslahi ya Tanzania na Watanzania wote.

  “Hongera sana Dk. John Pombe Magufuli, mtangaza nia uliyetangaza nia kwa mtu mmoja.” Tamati.

 Nilichokiandika Julai 14 nikimtakia heri, kimetokea. Sasa Dk. Magufuli ndiye Rais wetu. Tumpe ushirikiano bila kuchoka. Waliomsaidia kufika hapo alipofika walitekeleza wajibu wao. Wasiwe na nongwa ya kutaka malipo ya vyeo. Malipo makubwa kwao ni kuona ahadi alizozitoa kwa Watanzania, anazitekeleza.

Litakuwa kosa kwa waliofanikisha ushindi kudhani kuwa kwa kuingia kwake Ikulu, basi mambo yamekwisha! Asiachwe. Tumsaidie kwa kufichua kila lililo ovu ili aweze kulishughulikia, na tuwe wepesi wa kusifu pale anapofanikisha jambo lenye manufaa kwa Taifa letu. Tumtie moyo. Anashika madaraka mifumo ya nchi ikiwa imekufa, isipokuwa mfumo pekee ulio hai ni wa “mambo kuharibika”.

Bila shaka yoyote ile Dk. Magufuli, atakuwa Rais wa kupigiwa mfano mzuri; na Tanzania mpya itaanza kuonekana punde tu. Mungu anaipenda Tanzania na Watanzania.

By Jamhuri