Nianze kwa kulitakia afya njema Taifa letu kwa mara ya pili, afya ya amani na upendo, uzalendo uliotukuka na jinsi tunavyoweza kuwadhibiti wachache wenye tabia za ubinafsi na kuleta mtafaruku ya hapa na pale, namshukuru Mungu kwa kuwa ni muumini wa amani na mpenda amani siku zote.

Tanzania nchi niijuayo mimi tangu nikiwa mtoto, ni nchi ya amani, nchi ya upendo nchi isiyo na dini wala kabila, nchi ya kila mzalendo, nchi yenye neema ya mazao na mvua, nchi ya demokrasia ya kweli, nchi ya kubadilishana mawazo na kupingana kwa hoja.

 Nchi hii ya Tanzania ninayoijua mimi tumekuwa na utaratibu wa kuchagua viongozi kila baada ya muda tuliojiwekea tangu tumepata uhuru, pamoja na kwamba awali tulikuwa katika mfumo wa chama kimoja na upigaji wa kura wa picha na kivuli, nyumba na jembe na hatimaye mtu na mtu na chama na chama.  

Haya ni mabadiliko ya muda na namna ya siasa, lakini pia ni mabadiliko ya mfumo wa maendeleo ya ndani na nje, katika mfumo wa nje ni pale tulipobadilisha namna ya siasa yetu na kuwa ya vyama vingi, ya ndani ni jinsi ambavyo tumejikita katika demokrasia kubwa zaidi na kuleta maendeleo yanayoonekana kwa macho na yasiyoonekana.

Katika demokrasia hii tulionayo, uwanja mkubwa wa kukinzana kisiasa umeonekana, haujafungwa ili kutoa mwanya kwa kila mwenye uwezo wa kutoa mawazo yake mbadala aweze kufanya hivyo pasi na kupingwa bila sababu, wapo waliotoa mawazo yao na yakasikilizwa na wapo waliotoa mawazo yao hayakusilizwa lakini bado demokrasia iliwaruhusu kuchukua hatua iwapo wanaona hawajatendewa haki.

Miongoni mwa mifano hai katika uwanja huu mpevu wa siasa ya kidemokrasia ni pale serikali au chama kilipopelekwa mahakamani na raia na kesi ikasikilizwa na kutoa hukumu. Hii ni mifano ya demokrasia ambayo kwa dhati ya moyo wangu nakiri kusema ni msingi thabiti uliotokana na uhuru wa raia wa Tanzania kabla ya uhuru wa raia kutoka katika nchi za Magharibi ambayo leo tunaita demokrasia.

Mifano ipo mingi iliyokuwapo hata kabla ya uhuru huu wa Kimagharibi haujaja. Kuna wakati chama cha TANU kilishitakiwa, na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipotaka kukataa ilishindikana kwa hoja na chama kikashtakiwa na kikashindwa, huo ni wakati wa uhuru wa raia na siyo demokrasia yenu.

Tumetoka kumaliza uchaguzi na kesho rais wa awamu ya tano ataapishwa, huu ni uhuru wetu wa Tanzania ambao una misingi tangu tupate uhuru wetu, kwa mtindo huu tunampata yule wa wengi wape, wapo ambao watakataa kumtambua lakini ukweli uko palepale, hakuna aliyezuiwa kupinga na ndiyo maana taratibu zote zimezingatiwa, na uhuru wa raia tuliokuwa nao unaruhusu mtu kutoa maoni yake.

Tulikuwa na wagombea wengi sana na amepatikana kwa maana ya kushinda mmoja na huyo ndiyo rais wetu sote pamoja na hao aliogombea nao na wanachama  wao, hatakuwa rais wa upande mmoja na wala hatatambulika kwa kanda au kabila, hatatambulika kwa dini au rangi, atatambulika kwa umoja wetu na serikali.

Wiki jana niliandika barua nikitoa ushauri kwamba yale mataifa ambayo yalitaka yatumie udhaifu wa baadhi ya kasoro zitakazojitokeza katika uchaguzi huu kama kigezo cha kufeli kwa demokrasia ya kisasa Tanzania kwamba waache fikra hizo za kipumbavu, baadhi yao nawaheshimu sana na pia najua mchango wetu katika kuleta amani katika mataifa yao.

Sina hakika kama viongozi hao walikuwa na mapandikizi katika nchi yetu ili kuleta mvurugano, lakini hata kama walikuwa nayo naona yamegonga mwamba, Watanzania ni kitu kimoja na tuendelee kuwa kitu kimoja bila kujali demokrasia ya Kimagharibi ambayo inataka kuua uhuru wetu wa raia tuliokuwa nao.

Katika uchaguzi huu wapo mbuzi waliotolewa kafara, inaweza ikawa ya ushabiki, inaweza ikawa ya kura, inaweza ikawa ya unafiki, lakini wapo waliofanyiwa sherehe kwa kura, ushabiki, hata unafiki pia na bado wote ni mbuzi tu kwa mujibu wa matumizi.

Kwa kuwa tuna demokrasia yetu, na tusingependa tuige ya wale wanaopenda ugomvi katika demokrasia yao, vita baina yao, chuki, ukabila, udikteta, uvunjifu wa amani, udini, ukanda, ufupi, urefu, usomi na kadhalika. Basi ni vema tukajitenga nao na tukasema wote mbuzi hata kama matumizi yalikuwa tofauti.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1356 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!