“Wamo kwenye ulimwengu, waovu na wazandiki,

Nikisafu moyo wangu, sina kinyongo na chuki,

Masifu si sifa yangu, na kugombana sitaki.

Stahamili na upowe, zidisha uvumilivu,

Stahamili uridhiwe, Mungu ndiye mwenye nguvu.”

Maneno haya ni sehemu ya wimbo STAHAMILI ukiwa ni utunzi na mwimbaji wake Othuman Sudi, alipokuwa wa watribu wenzake Tanzania One Theatre – TOT – miaka ya 1980 – 1990.

Nimenukuu maneno haya na mengine yatakayofuatia kutokana na sababu zifuatazo; mosi, nakubaliana na mtunzi kwa ushairi na maneno anenayo. Pili, ni ujumbe wenye hoja kwa binadamu mwenye akili na uwelewa wa mambo. Hasa ukizingatia wimbo ni kielelezo cha utashi na utamaduni.

Ni muda sasa unapita katika mitandao ya habari na mawasiliano nje na ndani ya Tanzania, utakutana na watu wanatoa kauli zinazotia hofu na kichefuchefu au furaha na vicheko nyoyoni mwa watu, zikizungumzia yanayotendwa na serikali yetu katika anga ya siasa.

Katika ujumla wake si kauli nzuri, ni mbaya. Zina dalili ya chokochoko na kutia taharuki na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini mwetu. Ole wetu. Wasiopenda na wapenda amani pamoja na waasisi, wafuasi, washauri na wakemefu wote tutakuwa shakani. Janga kama hili halichagui.

Ulimwengu unao waovu na wazandiki. Ewe Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwingi wa kurehemu, tuepushe na zahama inayoandaliwa na ndugu zetu na marafiki wetu ambao ni malipyoto. Wasieneze tabia mbaya hiyo kwa nchi ni kosa.

Wimbo unatutahadharisha tuwe macho kwa wazandiki na unatukumbusha tuwadhibiti waovu. Tafakuri zetu kwa watu kama hawa ziwe pevu na sahihi. Tuwe wastamilivu, tupowe na tuzidishe uvumilivu. Mungu yupo pamoja na wenye subira, na shetani yupo pamoja na wenye haraka na wivu wapate kufanya zahama.

Tuelewe na wengine tukumbuke Mungu ni mwenye hukumu ya haki na nguvu. Si vema kuombeana mabaya. Lakini ni nini sababu ya watu wa sampuli kama hii kubembea ulimwenguni, hasa kwa wale waliopata kututawala, kutunyanyasa na kutudhulumu, na hatimaye tuliweza kuwatoa nchini kwetu na wakarejea kwao.

Leo tunapokwenda kwao kupiga magoti, kusujudu na kusema: “Hewala bwana” maana yake ni nini? Ziko maana nyingi chafu zenye kutoa uvundo mkali na unaofumbwa na kuumbiwa sura ya haki na demokrasia. Tukasahau kila taifa au nchi ina demokrasia yake. Na Mungu ndiye mwenye haki.

Chuki na hiana zimeota mizizi katika nafsi zao. Ubinafsi na miyongo inanyevua nyevua akilini mwao na kuwaaminisha wao ndio peke yao wenye akili, maarifa na uwezo wa kuleta mabadiliko ya uchumi na ustawi wa jamii kupitia mlango wa demokrasia. Ndiyo maana wanakwenda ughaibuni kulialia na kulalama, wapate huruma na misaada.

Kurudisha heshima na nidhamu makazini ni kosa? Kuboresha na kutoa huduma bora ya elimu, afya na maji, bila kupuuza kujenga miundombinu ya uchumi na jamii na kwa mfumo wa kidijitali ni dhambi? Usafiri na usafirishaji wa barabara, majini na angani alhamdulilah. Vipi tuchukie?

Je, ni kosa serikali kukataa kuibiwa na kuhujumiwa katika madini, nishati, wanyama na mazao yetu? Uongozi ni kuwa na mkakati na mipango himilivu. Kupanga ni kuchagua. Kucheleweshwa mifuko kunona iwe mwao kuzoza? Uhuru wa kupata na kutoa habari una mipaka. Mbona Ulaya kuna mipaka na kanuni? 

Rais, Magufuli, wananchi na hasa wazalendo tusitaharuki. Waovu wana hila na mbinu mbaya. Hawa ni askari wa kukodiwa  ambao wana tabia ya uhayawani. Rais Magufuli endelea na msimamo wako. Tuokoe na tuvushe katika bahari hii ya dhuluma. Weka hali za wananchi sawa.

Wabaya tuwafurahie na marafiki wema tuwazidishie upendo. Tuwe macho nao, na hakimu wa haki yupo. Atatufungua pingu na atatubariki. Tangu zama viongozi na wananchi wao hawakuwa ni watu wa kutaka misukosuko na kutiana kashikashi kama simba na mbogo.

Wazalendo hushindana kwa hoja na kupata maafikiano yao kwa maelewano na makubaliano. Mambo mazuri hayapatikani kwa vitisho na viburi. Vitisho na viburi si tabia ya waungwana. Na mwaka huu wa uchaguzi tuwe makini na watu hawa waovu. Tunahitaji maendeleo si mapigano.

Dua tuwaombee wale waliotamalaki. Wazidi kuendelea katika uongozi, kuweka mipango mkakati na utekelezaji bora wa mipango ya taifa. Iko siku watajua ukweli haufichiki.

86 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!