Katika miaka ya hamsini huko ambako wasomaji wengi wa waraka huu walikuwa ama wanazaliwa au watu wazima wa kupiga kura watakumbuka nafasi ya mwalimu katika jamii yetu. Mwalimu alikuwa ni nani na kwanini mtu alikuwa mwalimu, na mwalimu alifananaje?

Naamini kabisa kuna viashiria vya Julius kutaka kuwa mwalimu enzi hizo. Atakuwa alilazimisha maisha ya masomo yake yakaingie katika kozi ya ualimu. Ualimu ulikuwa ni kwa baadhi ya watu, tena ninaamini kabisa mwalimu wa wakati ule alikuwa akitengenezwa pindi anapoonyesha uwezo wa kuwa mwalimu.

Katika kitabu changu cha maisha yangu, nimeonyesha umuhimu wa mwalimu wangu wa darasa la kwanza ambaye ndiye aliyenifundisha kusoma na kuandika. Alinifundisha kusoma katika kibao changu cha shingo na alinifundisha kuandika katika ardhi kwa kuanza kutumia vijiti na baadaye penseli.

Ni mwalimu ndiye aliyenibadilisha tabia zangu za utotoni huko nyumbani. Mwalimu alichukua nafasi ya wazazi ambao nilikuwa naonana nao kwa nadra kutokana na majukumu yetu kuwa kikwazo cha kuonana. 

Wakati wazazi wangu wanajihimu shambani, nami nilikuwa ninatoka na mifugo kwenda machungani. Huko nilijifunza mengi, yakiwamo yale ya ujana maji ya moto na kuyapoteza machache ambayo yalikuwa maadili kutoka kwa wazazi. Ni walimu waliopokea kijiti cha mbio zangu za maisha.

Nakumbuka wakati huo wengi wetu tulikuwa tukiulizwa ungependa kuwa nani baadaye baada ya kumaliza masomo yako, basi jibu lilikuwa rahisi sana; baba nikiwa mkubwa ninapenda kuja kuwa Mwalimu. Halafu hatukuwa na mbadala wa kazi kama ukikosa ualimu utafanya nini. Hizo ndizo enzi zetu ambazo nafasi ya mwalimu katika jamii ilikuwa ni adimu na adhimu.

Julius alitaka kuitwa mwalimu, alikuwa mwalimu na siri mojawapo ya kuweza kujua kwamba alikuwa mwalimu ni pale ambapo alipoweza kulifundisha darasa la Watanzania katika mambo mengi sana kuhusu siasa, kazi, mshikamano, uzalendo, uwajibikaji, uhifadhi na mengi yasiyoweza kuandikwa hapa. Lakini pia katika darasa lake si kweli kwamba hawakuwepo watoro na wapiga kelele, la hasha! Kama mwalimu, alijua jinsi gani ya kuwafundisha wanafunzi ambao walikuwa kama sisi ambao muda mwingi tuliishi machungani ambako tulirithi tabia mbalimbali.

Kulikuwa kuna sababu kubwa ya watoto wengi kupenda kuwa walimu. Kwanza ilitokana na ukweli kwamba walimu wetu walionekana kujua mambo mengi kuliko sisi, kwa hiyo tuliamini kwamba ili uwe mwalimu lazima uwe umesoma sana na ufaulu. 

Pili, ni ile hali ya heshima ambayo walimu waliipata kutoka kwa watoto na wazazi wetu ambao walikuwa wakiwafurahia uwepo wao katika kijiji au nyumbani, nilitamani kuwa mwalimu hasa.

Wakati ule tukiulizwa swali hili kulikuwa na kazi nyingi kwa wakati huo ambazo tulikuwa tukiziona. Walikuwepo madaktari lakini hakuna aliyesema angependa kuwa daktari, kulikuwa na polisi na wanajeshi tuliwaona lakini hatukuvutiwa na kazi hizo, kulikuwa na mabibi na mabwana shamba wa kata lakini haikuwa njia ya kututoa kubadilisha uamuzi wetu wa kuwa walimu. Pia kulikuwa na watumishi wa Mungu kama mapadri, wachungaji, wainjilisti na mabruda – tuliona kama kazi za ziada baada ya ualimu.

Leo nimeamua kuandika hili kwa sababu ninajua jinsi gani mwalimu anapokewa katika jamii yetu. Walimu baadhi yao si wale ambao tulikuwa tukiwatamani zamani yetu. Zamani ambapo tuliamini mwalimu ni mtu pekee anayejua kazi yake na alithibitisha kwamba zaidi ya kazi, ualimu ni wito.

Leo ualimu ni kazi ambayo imevamiwa na wale ambao hawakufunzwa na walimu. Wapo ambao wamediriki kupeleka tabia za jela dhahiri katika mfumo wa elimu. Leo wazazi wengi hawawaamini tena walimu kama zamani ambapo mwalimu akiwatembelea nyumbani lazima mtoto uagizwe na mzazi kukamata kuku aliyenona ili aondoke naye.

Leo mwalimu anaangaliwa kwa jicho la husuda na baadhi yao wako tayari kutazamwa hivyo. Leo mwalimu si yule wa wito, leo mwalimu ni adui wa mzazi na mwanafunzi, leo mwalimu hafundishi tena, leo mwalimu hajitolei tena, leo mwalimu akionekana kwa mzazi anaweza akaadhibiwa badala ya kukabidhiwa zawadi.

Wapi tumekosea mpaka wanafunzi hawapendi kuwa walimu na badala yake wanataka kuwa wacheza mieleka au mabondia? Tutajadili pamoja.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

579 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!