Hali ya mapori yote ya hifadhi nchini ni mwetu ni mbaya mno. Miaka michache ijayo, Tanzania itakuwa haijivunii hiki inachojivunia sasa, yaani wingi wa rasilimali za mapori, miti na viumbe wanaoishi humo.

Kilio hiki cha uhifadhi tumekuwa tukikiwasilisha kila mara kupitia safu hii ya Maoni ya Mhariri na katika makala na habari mbalimbali.

Tumekomalia uhifadhi kwa sababu tunatambua na kuheshimu faida zake. Takwimu zinaonesha utalii nchini mwetu unachangia asilimia 18 ya Pato ya Taifa. Kiasi hiki si haba, lakini kitaendelea kupungua kutokana na tasnia ya uhifadhi kuvurugwa.

Tumeandika habari nyingi na ndefu za kuvurugwa kwa Hifadhi za Taifa kama vile Serengeti, Tarangire, Manyara, Kilimanjaro na nyingine nyingi.

Mapori ya Akiba kama vile Maswa, Mapori Tengefu ya Loliondo, yale ya vijiji (WMA) kama Mwiba, yote yanakufa.

Wavamizi kutoka ndani na nje ya nchi wapo katika mapori yote ya hifadhi wakitamba na kuua wanyamapori, wakivua samaki na kukata miti bila hofu yoyote. Wana silaha kali.

Tunatambua kazi nzuri iliyofanywa wakati wa Operesheni Tokomeza, licha ya dosari za hapa na pale.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia, Dk. John Magufuli, kwa wadhifa wake ndiye mhifadhi namba moja hapa nchini. Tunamuomba asiwe na kigugumizi kuanzisha Operesheni Tokomeza II ili kuikoa uhifadhi nchini mwetu.

Loliondo, Serengeti, Ugalla, Muyowosi, Kigosi (iliyokwishakufa), Maswa, Katavi na maeneo mengine yote nchini yanahitaji kukombolewa.

Kazi hii ya ukombozi ifanywe na vyombo vya ulinzi na usalama chini ya uratibu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzaia (JWTZ). Rais asiogope lawama au kelele ambazo zinasambasawa sana na wanasiasa ambao wana maslahi ya kiuchumi kutokana na kujihusisha na ujangili na ufugaji ndani ya mapori.

Rais Magufuli, awe na roho ngumu kwa sababu bila hivyo wanyamapori kama tembo wachache alioachiwa na mtangulizi wake, watatoweka katika uongozi wake.

Kwa ufupi ni kuwa Rais atambue hali ya uhifadhi ni mbaya mno, na kwa kiwango kikubwa majangili na wavamizi wengi wana silaha na mbinu za kivita. Wanaowamudu majahili hawa ni JWTZ. Hatuoni kigugumizi kinatoka wapi wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni Kamanda wa JWTZ.

Chonde, chonde Ndugu Rais, okoa mapori na rasilimali zilizomo. Hali ni mbaya.

1322 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!