1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliWiki iliyopita niliandika makala juu ya kijana aliyefuga kuku huko Singida. Nimebaini kuwa ufugaji ule umekuwa kivutio kikubwa kwa wengi waliosoma makala yangu. Hata hivyo, ingawa wengi walitaka kuwasiliana naye awafundishe, kijana huyo anasema yeye alifundishwa na mwalimu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro, hivyo anawasihi wengi kutafuta wataalam kutoka SUA.

Kijana huyu haonekani kuwa tayari kuwasiliana na watu: “Kuniona mimi haitawasaidia. Wambie niliyokuonyesha ukayaandika nami nimeyasoma umeyaandika vizuri sana, cha kufanya waanze kufuga kidogo kidogo na kadri wanavyoendelea kufuga watapata uzoefu. Wala huhitaji kuwa na shahada ya chuo kikuu ndipo ufuge na kufanikiwa. Wambie waanze tu.”

Idadi ya simu nilizopokea, nimeona fika kuwa Watanzania wana kiu ya uwekezaji, lakini kwa bahati mbaya hawajui waanzie wapi.  Hata hivyo, makala hii haitanoga, iwapo sitakukumbusha shairi murua tulilolisoma tukiwa darasa la nne, linalosema: KAMA MNATAKA MALI MTAYAPATA SHAMBANI.

 

Karudi Baba mmoja, toka safari ya mbali

Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili

Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali

Wakataka na kauli, iwafae maishani.

 Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli

Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali

Naona yachinjwa, kifo kimenikabili,

Kama mwataka kauli, semani niseme nini.

Yakawatoka kinywani,maneno yenye adili,

Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali,

Urith tunatamani, mali yetu ya halali,

Sema iko wapi mali, itufae maishani.

Baba aliye kufani, akajibu lile swali,

Nina kufa maskini, baba yenu sina mali,

Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

 Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,

Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,

Akili yetu nyembamba, haijajua methali,

Kama tunataka mali, tutapataje shambani.

Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,

Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,

Haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,

Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,

Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

 Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili,

Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,

Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

 Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,

Tangu zile za mibuni, hata zitupazo wali,

Na mvua ikaja chini, wakona na dalili,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Shamba wakapalilia, bila kupata ajali.

Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,

Wote wakashangilia, usemi wakakubali,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

 Wakawanunua na ngómbe, majike kwa mafahali,

Wakapata na vikombe, mavazi na baiskeli,

Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

 Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,

Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,

Walikiweka kibao, wakaandika kauli,

KAMA MNATAKA MALI, MTAYAPATA SHAMBANI.

 

 Sitanii, kwa miaka mingi nchi yetu imekuwa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ujamaa na Kujitegemea uliweka msingi kuwa Tanzania ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi. Ni kutokana na msingi huu, nchi ina mning’inio wa mawazo, kwani kufanya biashara inaonekana kama dhambi. Watanzania walio wengi tuliandaliwa kwa ajili ya uzalishaji wa kujikimu (hand to mouth production).

Ni kutokana na msingi huo, miaka yote tumekunjua mkono kuomba misaada. Tuliaminishwa kuwa hatuwezi kuendelea bila kupewa misaada. Hatukai tukajiuliza hawa walioendelea misaada wanayotupa wanaitoa wapi. Kuna bahati mbaya nyingine tuliyonayo, kuwa Watanzania tulio wengi hatuna mawazo ya ujasiriamali.

Katika kuwaza kwetu hatuwazi uwekezaji, tunawaza matumizi. Ndiyo maana watu wanakaa vikao kukusanya michango ya harusi vikao vinakaa hadi miezi 6 au mwaka wakikusanya michango. Kuna harusi zinafikia hadi Sh milioni 80, lakini watu wanaishia kunywa bia mbili au kula chakula kilichopoa. Hiyo Sh milioni 80 kwa China unapata mashine 10 za kukoboa kahawa!

Sitanii, ni kutokana na ufinyu wa mawazo unapoanzisha biashara baadhi ya watu wanawaza kwa nini isife. Wengine wanafikia hatua ya kuwaza kwa nini kama umejenga nyumba isiungue. Hawasiti kukuzulia kuwa unajidai kwa sababu una nyumba au gari zuri, lakini wanasahau kuwa ulifanya kazi kupata vitu hivyo. Hukupewa kama zawadi.

Ni bahati mbaya zaidi kuwa Watanzania tulio wengi hatujui hata kuomba. Hata tunapopata fursa ya kuomba tunaomba michango ya harusi na sasa nimeona sherehe za komunio na kipaimara watu wanapitisha michango. Sijaona Mtanzania aliyetengeneza kadi za michango akasema anaitisha vikao anunue mashine za kuranda mbao.

Sijaona Mtanzania yeyote anayeitisha kikao akasema anaomba mchango apate angalau Sh milioni 10 apate mashine ya kutengeneza tofali au nyavu za kisasa za kuvulia samaki. Sana sana anayejitahidi akafanya biashara kwa sasa limeibuka neno fisadi. Ukimiliki duka la kuuza sukari, unaambiwa wewe ni fisadi. Basi tu, ilimradi roho ya tukose wote ndiyo iliyotawala.

Katika shairi nililoliweka hapa juu, watoto walikuwa wakimuuliza baba yao mali iko wapi. Baba akawapa ushauri. Ushauri kuwa mali inapatikana shambani. Ikumbukwe hapa walikuwa wanatumia jembe la mkono na kutegemea kudura za Mwenyezi Mungu mvua inyeshe. Naamini ushauri wa baba kwa watoto hawa ni msingi muhimu kwa taifa letu.

Nakubaliana na Rais Magufuli asilimia 100 kuwa Tanzania si nchi maskini. Nakubaliana naye kuwa Tanzania inapaswa kuwa nchi ya viwanda. Hata hivyo, kuna mchakato wa kufikia hivyo viwanda. Kuna kitu kinaitwa uwezeshaji. Uwezeshaji huu unapaswa kuwa sawa na ushauri wa baba wa watoto katika shairi hili.

Serikali inapaswa kuwa na kitengo cha ushauri katika biashara. Najua ukienda utakuta kuna kaidara ka ushauri pale Wizara ya Viwanda na Biashara, hata hivyo ikiwa Rais Magufuli anataka kupata kodi za kutosha na ndoto yake ya nchi kuwa ya viwanda ikatimia, kitengo hiki kinapaswa kuwa katika kila wilaya na kikafanya kazi kwa lengo maalum.

Sitanii, Serikali inapaswa kuanzisha mchakato wa kuitisha zabuni ya mawazo ya wajasiriamali. Mawazo haya yakiletwa, wataalam wakae wayachekeche. Wawafundishe Watanzania kuwa huwezi kuanzisha biashara kubwa bila mkopo na huwezi kukopesheka bila kumiliki mali kihalali. Umiliki wa mali ni pamoja na kuzisajili.

Taratibu za usajili na gharama zake zinapaswa kuimbwa kama wimbo wa taifa. Tunapaswa kuondoa hofu mioyoni mwa Watanzania wanaoogopa kuweka rehani nyumba zao za kuishi au mali zao wakihofu kuwa zitachukuliwa na benki. Ni kweli zitachukuliwa na benki wakikopa bila mwongozo na kufahamu jinsi ya kufanya biashara.

Rais Magufuli kwa sasa anaweza kuwa ameongeza makusanyo ya kodi, lakini napata hofu. Napata hofu kuwa kwanza makusanyo kwa sasa yameongezwa na ukusanyaji wa madeni ya kodi za nyuma zilizokwepwa, lakini pili mizigo inayoagizwa kuingia nchini pale bandarini imeshuka kwa asilimia 50. Dhana kwa nini mizigo imeshuka, ni mtambuka.

Wakati nchi za wenzetu wanatoza kodi mizigo inayotoka nje sarafu ya nchi zao, sisi hatuiamini shilingi yetu. Tunatoza ushuru wa forodha wa dola ya Marekani. Hii inawafanya wafanyabiashara kutotabiri na kufahamu ni kiasi gani wanapaswa kulipa maana dola ikicheza, basi hata gharama za kutoa mzigo bandarini zinaongezeka.

Kubwa zaidi katika hili naasema wakati umefika sasa wa kuhamasisha viwanda vidogo vidogo na viwanda vya kati, vitakavyoiwezesha Serikali kuzalisha ajira na kuwa na vyanzo vipya vya kodi. Timu za ushauri wa biashara zipewe jukumu la kupendekeza angalau viwanda vitatu katika kila wilaya. Wataalam hawa hata kama viwanda ni vya mtu binafsi wapewe kazi ya kuvilea kuhakikisha vinakua hadi vinatengeneza faida.

Sitanii, ni lazima uwepo uratibu wa kitaifa. Hii itasaidia kuepusha wajasiriamali kuanzisha viwanda vinavyofanana. Unaweza kukuta kama mawazo haya hayataratibiwa, wilaya zote nchini zinaweza kuanzisha viwanda vya misumari kwa maana ni rahisi kuzalisha misumari na matokeo yake misumari itakosa soko.

Tutenge kanda katika nchi hii. Uwepo ukanda wa viwanda vya mazao yatokanayo na kilimo. Uwepo ukanda kwa mfano wa viwanda vya kusindika maziwa, viwanda vya kutengeneza viatu… hivi kweli nchi hii na ngozi zote zilizizopo tunashindwa kutengeneza hata viatu vya wazi (open shoes?). Njiti za meno zinatoka nje, nguo za ndani, sketi, gauni, mashati na suruali sisi ni wa kununua vitu hivi kutoka China?

Rais Magufuli nasema hapana. Tuchukue ushauri uliopo kwenye hili shairi. Unda kitengo cha kuratibu viwanda kwa kasi kubwa. Nimefurahi lugha yako ni kuwezesha wafanyabiashara. Bila kuwawezesha hawa hatutapata kodi. Nakusihi uzikatae harakati ninazoziona zimeanza kuwa nchi hii ni ya wakulima na wafanyakazi tu.

Wafanyabiashara ukiwageuza raia daraja la pili, kodi utazisikia kwenye bomba. Chonde chonde Mhe. Rais nakusihi kwa heshima kuu kuwa hakikisha kila wilaya inaibua mpango wa kujenga angalau kiwanda kimoja kama wakishindwa hivyo vitatu. Kwa kufanya hivyo, utazikimbia kodi. Tutakusanya fedha nyingi hadi tutoe misaada Marekani. Wala tusiogope, soko lipo kwa nchi zilizotuzunguka. Mungu ibariki Tanzania.

1912 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!