UNGUJA

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema hatua za serikali zinazochukuliwa dhidi ya wizi wa fedha za umma ni juhudi za makusudi katika kuhakikisha zinapokusanywa zinawafaidisha walio wengi badala ya kuwafaidisha wachache.

Dk. Mwinyi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipowahutubia wanachama wenzake pamoja na wananchi baada ya kulizindua Tawi la CCM la Sebleni lililojengwa upya pamoja na kuzindua kisima cha maji safi na salama kilichopo katika eneo hilo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Hatua tunayoifanya ni kwa nia njema. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha utendaji wa serikali unaimarika na unakuwa bora,” anasema Dk. Mwinyi. 

Katika hatua nyingine, ameupongeza uongozi wa Jimbo la Kwahani kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.

Anasema uongozi wa jimbo hilo umeweza kutekeleza mambo makubwa mawili, likiwamo la kuimarisha CCM na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wake.

Rais Dk. Mwinyi anasema tayari viongozi wa jimbo hilo wameshafanya kazi nyingi katika kutoa huduma za jamii ikiwamo hatua hiyo ya ujenzi wa kisima cha maji safi na salama, kazi ambazo zimefanywa kwa ushirikiano wa pamoja.

Aidha, Dk. Mwinyi aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi vitatu kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais anaeleza mipango ya serikali ya kuimarisha huduma za jamii ukiwamo mradi mkubwa wa maji safi na salama unaondelea katika Wilaya ya Magharibi ‘A’, Magharibi ‘B’ na Wilaya ya Kati kupitia Benki ya Exim ya India, huku akisisitiza kwamba hatua hiyo itaendelea na kwa wilaya nyingine zilizobaki.

Pia ametumia fursa hiyo kueleza mpango wa serikali anayoiongoza wa ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 220 katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba utakaofanyika ndani ya miezi 24.

Anasema kwa upande wa sekta ya afya tayari mipango madhubuti imeshapangwa katika kuhakikisha serikali inaiimarisha sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza huduma, hatua ambayo pia itachangiwa na fedha zipatazo dola milioni 100 za Marekani zilizotolewa kwa ajili ya mapambano dhidi ya corona (Covid-19).

Nao viongozi wa jimbo hilo wanasema wanaridhishwa na uongozi wa Rais Dk. Mwinyi kwa kuwa umeendeleza amani, umoja, utulivu na mshikamano mkubwa, hatua inayoimarisha maendeleo nchini.

Pia wamewataka wananchi na wana CCM wa jimbo hilo waweke matarajio makubwa kwa kuwa mambo mazuri zaidi yanakuja, huku wakisisitiza kwamba mafanikio hayo yanatokana na umoja na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya viongozi, hasa mbunge na mwakilishi, ambao wamekuwa kitu kimoja katika kuwatumikia wananchi na kuiimarisha CCM.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama, Tali Ali Talib, amempongeza Rais Dk. Mwinyi kutokana na juhudi zake za uongozi pamoja na kuwapongeza viongozi wa jimbo hilo kwa ushirikiano wao katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuwasogezea huduma za kijamii pamoja na kuwajengea Tawi la CCM kwa azima ya  kutekeleza Ilani  ya chama hicho.

By Jamhuri