Rais Nyerere alipokosa maji ya kuoga Kibondo

 

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza Oktoba, mwaka jana. Tunaichapisha tena kutokana na umuhimu wa maudhui yaliyomo. Mhariri

Mwaka 1964, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Tanganyika, alitembelea shule yetu.  Nilikuwa nasoma Seminari ya Kaengesa Sumbawanga. Bendi ya shule yenye vyombo vyote vya brass band tulimpigia wimbo maarufu uitwao “The Washington Post”.

Clarinet ndicho chombo cha muziki nilichokuwa nakimudu barabara.  Kwaya nayo ilimwimbia wimbo, “Heri maziwa uliyonyonya, heri na tumbo lililokuzaa”.  Uongozi wa shule ulipanga Mwalimu apate fursa ya kujibu maswali mawili au matatu ya wanafunzi.  Nilikuwa mmoja wao.  Swali langu, “Mwalimu inakuwaje mtu akitaka kusafiri kutoka Tanganyika kwenda Zanzibar baada ya kuungana Tanganyika na Zanzibar kuwa nchi moja, atakiwe hati ya kusafiria kana kwamba anakwenda nchi nyingine?”  Wakati huo umri wangu ulikuwa miaka 18 hivi.

 

 

Kabla ya kujibu swali langu, Mwalimu alinimwagia sifa kwa kusema swali langu mtu asilione la kijinga au la kitoto. Machozi ya mchanganyiko wa furaha na unyenyekevu yalinilengalenga. Mwalimu alieleza kuwa Zanzibar wakati wa Mapinduzi walimwaga damu na kutokana na hali hiyo, walihitaji kujihakikishia kila aingiaye Zanzibar ana utambulisho wenye uhakika.

Kama nakumbuka sawa sawa, hivi ilikuwa mara yangu ya kwanza kumwona Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kumwuliza swali la kisiasa nikiwa kijana mdogo.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2000 niliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Mambo ya Muungano). Nilikumbuka swali langu kwa Mwalimu. Imekuwaje swali liulizwe na baada ya miaka 36 muuliza swali akabidhiwe dhamana ya jambo aliloliuliza?

Najua mwaka 2000 suala la kuingia Zanzibar kwa Watanganyika halikuhitaji hati za kusafiria kama hapo mwaka 1964. Kwa siku zijazo sijui. Nasema hivyo kwa sababu Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa mujibu wa marekebisho katika kifungu cha 4 cha sheria namba 9 ya mwaka 2010 ibara ya pili, inasomeka, “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

Kwa maoni yangu, ibara 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kutokuwapo nchi ya pili, yaani Tanganyika pamoja na mambo mengine, kunaondoa kuwapo kwa Muungano wenyewe. Itatubidi turudi kwenye hati za kusafiria kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Kabla ya marekebisho hayo, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la Oktoba mosi 1985 ibara ya kwanza inasomeka hivi, “1. Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Nayo ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaitambua na kuitamka Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Ninavyomjua Mwalimu angewauliza wale wanaoapa kuilinda, kuihifadhi na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kiapo cha kuudumisha Muungano, wako wapi na wanangoja nini kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza kiapo chao? Ukiukwaji na uvunjifu wa Katiba ni uhaini. Kiongozi anasaliti dhamana aliyoikubali kutoka kwa mamlaka na utashi wa umma.  Adhabu yake ni kifo au kifungo cha maisha.

Mwaka 1980 nilibahatika kuwa katika mazingira ya kumwona Mwalimu akiwa kazini. Safari hii ilikuwa wilayani Kibondo. Mwalimu alikuwa na ziara mkoani Kigoma. Wakati huo nilikuwa Kibondo likizoni au kikazi. Kazi za uchunguzi katika Kikosi cha Kuzuia Rushwa, hazikuwa na mipaka katika kufuata ukweli kabla ya kuwafungulia mashitaka watuhumiwa.

Nakumbuka Mwalimu alipangiwa kufungua ghala la mazao katika Kijiji cha Kabale kilichopo katika Wilaya mpya ya Kakonko.

Njia ya kutoka Kakonko kupitia vijiji vya Nyakayenzi, nyumbani kwa Askofu Mkuu wa Tabora, Mhashamu Paulo Ruzoka, haikuwa nzuri.  Sehemu ya mlima kabla ya kufika Kijiji cha Muhange, ilibidi mawe makubwa yalipuliwe kwa baruti, kutoka Muhange unateremka hadi Kabale. Mwalimu alifika kama ratiba ilivyoonesha. Ilikuwa wakati wa kiangazi na barabara za vijijini sote tunajua utajiri wa vumbi ulivyo.

Ulipowadia wakati wa kufungua ghala, mtunza funguo, Joseph Ntirukubitwa, hakuonekana. Kazi iliyompeleka Mwalimu Kabale haikufanyika. Viongozi walijizoazoa kwa aibu na kuanza msafara wa kurudi Kibondo. Sikumbuki Ntirukubitwa, jina lenye maana “kifo hakichapwi bakora”, walimchukulia hatua gani.

Siku hiyo ilikuwa mbaya kweli.  Mwalimu alipofika Kibondo, Ikulu ndogo, mabomba yalikuwa hayatoi maji. Ilikuwa mtafutano, lakini Mwalimu hakusema chochote. Alibaki chumbani alikopangiwa nadhani akisali au kusoma vitabu. Baadhi yetu tulitarajia karipio kwa uongozi wa wilaya kwa yale yaliyokuwa yakitokea katika sehemu ya ziara hii ya Mwalimu wilayani Kibondo, lakini haikuwa hivyo.

Ninapokumbuka matukio hayo ya siku ile, nakubaliana na sala ya marehemu Askofu Justin Samba wa Jimbo Katoliki la Musoma, katika sala ya kuomba neema kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu, Julius Kambarage Nyerere. Sehemu ya sala hiyo inasomeka hivi; “Huduma yake nyenyekevu kwa watu wa Mungu imebaki mfano wa kuigwa kwa watu wa vizazi vyote katika safari yao ya kuelekea kwako”.

Kama si unyenyekevu wa hali ya juu kabisa wa Mwalimu, hayo yaliyotokea Kibondo, wengine wangeng’aka kuonesha wao ni nani katika nchi hii. Naambiwa mmoja wa viongozi waliomfuata Mwalimu kuiongoza nchi yetu, alipoona maji ya bomba Kibondo yana rangi ya udongo wetu mwekundu, aliagiza yaletwe maji ya chupa apate kuoga. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuwa hivyo.

Binafsi nakiri na kumshukuru Mungu kwamba mwasisi wa Taifa letu alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Katika hili naamini si peke yangu.  Wapo wananchi wengi tu ambao wanawapima viongozi wetu, hasa marais, kwa misingi na maadili ya Mwalimu. Sijui kama wanalifahamu hilo au wanafanya makusudi kwa sababu wazijuazo wao kujitenga na misingi na maadili aliyotuachia Baba wa Taifa.

Mwishoni mwa mwaka 1980 nilijitokeza kugombea ubunge Jimbo la Kibondo. Baadaye 1995 Kibondo kama jimbo la uchaguzi ikagawanywa na kuwa majimbo ya Buyungu na Muhambwe. Wakati huo nilikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Kikosi cha Kuzuia Rushwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.   Nakumbuka nilitoka Arusha kwenda Kibondo nikiwa katika likizo yangu ya mwaka. Kwa upande wa fedha nilikuwa na akiba ya Sh 1,000 tu.

Kutokana na misingi na maadili ya Mwalimu Nyerere kwa chama chake na Taifa, kweli rushwa katika uchaguzi ilikuwa sifuri kabisa. Ingekuwa vinginevyo, elfu moja niliyotoka nayo Arusha kufika mwisho wa kampeni nisingekuwa na albaki ya Sh 300. Nakumbuka vema Sh 300 nilimpa kaka alipokuja kwenye mkutano makao makuu ya wilaya asishinde na njaa.  Sh 400 nyingine nilinunulia dawa ya meno, mfukoni nikabakiwa na Sh 300 tu hadi mwisho wa kampeni ya alama za jembe na nyumba. Hiyo ilikuwa CCM enzi za Mwalimu.

Leo hii mambo ni tofauti kabisa. Nakumbuka sana “tempora mutantur et nos cum illis mutamur sed peiora”– msemo wa Kilatini wenye kuelezea kuwa nyakati hubadilika, nasi twabadilika na nyakati, lakini kwa ubaya uliopitiliza. Ukweli wa kinachosemwa sote ni mashuhuda wake. Na kwa wale wanaobisha kinafiki, niwaombe wamsikilize Cyprian Musiba aliyekuwa mgombea wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Katika kichwa cha habari, “Ashauri CCM iombewe”. Mwandishi Christopher anaripoti kuwa Musiba anaeleza kusikitishwa na kukithiri kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa chama hicho na kuwaomba viongozi wa dini zote wakiombee chama hicho, vinginevyo kitakufa rasmi mwaka 2015.

 

“CCM ni chama changu ndiyo, lakini kinahitaji maombi ya nguvu ili kukinusuru mwaka 2015 kisije kikafa maana rushwa sasa ni nje nje kwenye chaguzi zake”.  Gazeti Mwananchi Ijumaa Oktoba 5, 2012 ukurasa wa 12.

Baba wa Taifa asingekubali hali ifikie hapo. Ushuhuda huu kautoa kwa niaba ya wana-CCM wasio wanafiki. Wale mabingwa wa vitendo vya rushwa na ufisadi watamcheka Musiba na kumkejeli kuwa ni kwa sababu alishindwa uchaguzi. Kibaya zaidi wanajifariji kwa kutiana shime ya kifisadi kuwa alizidiwa kiwango au dau la rushwa lililotolewa. Madhara ya ukweli wa rushwa kukithiri katika chama tawala ni kiama kwa Taifa.

 

Serikali inayoundwa kutokana na chama ambacho mungu wake ni rushwa, nayo itakithiri kwa rushwa. Maendeleo yatavia na shida za wananchi waliokubali kulaghaiwa na wazao wa rushwa wasitarajie viongozi kuwa watumishi wao. Viongozi watajigeuza kuwa watawala katili na hata wauaji wa wale waliowaweka madarakani.

Mwaka 1993, wakati wa hoja ya G55 nilibahatika kuwa miongoni mwa wale tuliokuwa tukikutana na Mwalimu.  Mshenga wetu alikuwa Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba.  Hatukutaka hoja ya Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano iwe siri kwa Mwalimu. Tulikutana naye si chini ya mara nne. Muda wa kukutana, Mwalimu alipendekeza iwe saa nne siku za Jumapili baada ya watu, baadhi yetu kutoka kanisani. Na tulikutana nyumbani kwake Msasani.

Baadhi ya majina ya wale tuliokuwa tukikutana na Mwalimu ni pamoja na Jenerali Twaha Ulimwengu, Njelu Edward Kasaka, marehemu William Mwagamalindo Mpiluka, Mateo Qaresi, Patrick Quorro, Phillip Sangka Marmo, mimi mwenyewe na Halimenshi Kahena Mayonga. Katika kubadilishana mawazo, siku moja Mwalimu aliuliza, “For how long can the army continue to obey and protect this corrupt government”. Nayakumbuka vizuri sana maneno hayo.  Sababu yake ni moja tu.

Mwaka 1971, Rais Milton Obote wa Uganda aliondolewa madarakani kwa nguvu. Jeshi ndilo lililofanya hivyo. Nilikuwa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Makerere. Moja ya sababu kubwa zilizotolewa na jeshi kumwangusha Obote ilikuwa madai ya corruption – rushwa. Nchini mwetu madai ya rushwa serikalini yalikuwa na yanaendelea kusikika sana siku hizi.  Katika mawazo yangu nilikuwa nahofu yasitukute yaliyomtokea Rais Obote.

Nilipomsikia Mwalimu akitamka maneno niliyonukuu hapo juu, nilifarijika. Faraja yangu ilitokana na kule kuona kuwa sikuwa pekee yangu kuwaza na kuhofu yaliyotokea Uganda wakati wa utawala wa Obote kwa sababu ya tatizo la rushwa. Mkutano mwingine ninaoukumbuka ni siku tulipomwambia Mwalimu kuwa hoja ya kuundwa Serikali ya

 

Tanganyika ndani ya Muungano, uwezekano wa kupitishwa na Bunge ni mdogo sana. Tulimweleza Mwalimu kuwa kwa muundo (composition) wabunge, waunga mkono hoja za serikali walikuwa ni wengi kuliko wale walioweza kupinga hoja za serikali.  Na hoja yetu kwa vile haikuwa ya serikali wangeipinga. Hata hivyo, tulitaka kuitumia hoja hiyo kuisema serikali. Mwalimu alisema, “Actually you have the wrong motion, the correct motion would be to impeach the President”. Lakini hata hoja ya kumshitaki Rais bungeni nayo ingeshindwa kwa kutoungwa mkono na waunga mkono hoja za serikali.

Baada ya kuachana na Mwalimu, mambo mawili yalitokea.  Mwalimu alimwita Rais, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na washauri wao waandamizi, la kwanza.  La pili, G55 tuliweka mkakati wa kuhakikisha hoja inaungwa mkono bungeni. Kuhusu la kwanza tulipata taarifa kuwa Mwalimu alimwambia Rais bila kumung’unya maneno kuwa ametutamkia kuwa hoja sahihi ingekuwa hoja ya ‘kukushitaki bungeni wewe Ndugu Rais’.

Aidha, Mwalimu aliwajulisha viongozi hao kuwa tulikuwa tumemwambia hoja haikuwa na nafasi ya kuungwa mkono bungeni na kushinda. Kuhusu mkakati wa hoja kushinda ndani ya Bunge ilikuwa kitu rahisi. Ilipangwa itakapofika wakati wa kuamua hoja tuhakikishe kuwa kura zinahesabiwa. Lugha ya kibunge maana yake mbunge aitwe jina aseme “ndiyo” au “hapana”. G55 tulifikiri mbunge aikane Tanganyika mwaka 1993 halafu akatafute kura Tanganyika mwaka 1995. Si wengi wangejijua kisiasa kuikataa Tanganyika.

Na kweli walipobaini mkakati huo wa G55 walikwenda mbio Butiama kumwarifu Mwalimu, kuwa wanakubaliana na hoja ya kuundwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.  Mwalimu aliwashangaa hadi akawatungia kitabu – Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania – akiwalaumu vikali sana.  Mkakati wa G55 ulishinda. Hoja ya kuundwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano ilipitishwa na Bunge.  Kilichofuata baada ya hapo ni jambo tofauti kabisa.

Katika suala la kuutetea, kuulinda na kuuhifadhi Muungano, hakuna kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Pamoja na kuwa muumini wa dhati wa kutekeleza Katiba, katika suala la Muungano, baada ya hoja ya G55 kupita bungeni, Mwalimu yaelekea alikubaliana na mtawala mmoja aliyesema siku si nyingi zilizopita, “liwalo na liwe”.

Yale yote yaliyofanyika baada ya hoja ya kuundwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano kupitishwa na Bunge, kubatilisha uamuzi wa Bunge nje ya Bunge, ilikuwa ukiukwaji wa ibara 100(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977. Katika suala zima la kutetea kuwapo kwa Muungano, Mwalimu alikuwa haambiliki.

Katika kitabu cha “Pan-Africanism or Prognatism?” cha Profesa Issa G. Shivji ukurasa 244 inasomeka, “Yet, left on his own it is quite likely that Nyerere might not have made the decision to go it alone with Zanzibar. But, the Western pressure overwhelmed him and he gave in. Once formed, Nyerere became almost paranoid to maintain the Union”.

Ni kweli Mwalimu alikuwa tayari kwa lolote kuhakikisha Muungano unadumu. Mfano hai ni kusimama kidete kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya Bunge kupitisha hoja ya kuundwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Huu ulikuwa mfano mbaya wa kuvunja Katiba, ibara ya 100. Ibara hiyo kwa muhtasari inakataza kabisa mamlaka yoyote kuhoji jambo lililoamuriwa na Bunge nje ya Bunge.

Hoja ya Mwalimu ilikuwa sera ya CCM – hadi leo, ni serikali mbili. Jambo la wazi ni kuwa sera ya CCM sawa kwa wana-CCM, lakini kwa wasio wana-CCM si lazima wakubaliane nayo. Na wasio wana-CCM ni wengi sana zaidi ya hao wana-CCM. Na hata hao wana-CCM, maoni yanayotolewa kwenye mikutano ya kupata Katiba mpya hawakubaliani na sera ya muundo wa Muungano wa serikali mbili, sera ya CCM.

Hata hivyo, Mwalimu pamoja na kuutetea Muungano kwa kila namna, wazo la uwezekano Muungano kuvunjika haiwezi kusemwa kuwa hakuwa nalo. Hebu tafakari maneno yafuatayo kwa lugha ya Kiingereza. “Nyerere consistently proclaimed that unity could not be imposed. It had to be with the consent of the people”.

Endelea kutafakari. “As President of Tanzania it is my duty to safeguard the integrity of the United Republic. But if the masses of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the Union was prejudicial for their existence, I could not advocate bombing them into submission.  To do so would not be to defend the Union. The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.”

Maneno hayo yanapatikana ukurasa wa 247 wa kitabu cha Profesa Issa G. Shivji kiitwacho “Pan-Africanism or Prognatism?” Binafsi naona ibara ya 2 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, inadhihirisha kuwa Muungano haupo kwa sababu “The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members (Zanzibar?)  was withdrawn”  na “consent” kutoka Tanganyika isiyokuwapo (does not exist) inaendelea kuwapo kwa vipi na kwa namna gani?

Nimalizie makala yangu kwa hitimisho hili. Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwasisi wa Taifa letu kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kila kiongozi wa Taifa letu ajue anapimwa kwa misingi na maadili aliyoyaweka na kutuachia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.  Wakati wa enzi za Mwalimu anachokilalamikia aliyewahi kuwa Waziri Mkuu Frederick Sumaye na Cyprian Musiba kisingekuwapo. Na rushwa katika uchaguzi wa CCM wenyewe wanataka tukubaliane nao kuwa “it’s the only game in town”.

Hili ni janga la Taifa kwa sababu chama cha waabudu rushwa huzaa serikali ya wala rushwa waliokubuhu – qualis peter talis filius – kama alivyo baba, ndivyo alivyo mwanaye.  Wanaosimama kwenye majukwaa na kujiapiza kuwa wanamuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere huku wakishindwa vibaya kuishi kwa vitendo, misingi na maadili aliyotuachia, hao ni wanafiki wakubwa wasiostahili hata chembe kuitwa viongozi. Dawa yao, nguvu na mamlaka ya umma, viko jikoni vinachemka taratibu kwa muda wa miaka takribani mitatu iliyobaki. Wakati ukifika lazima waiywe dawa hiyo.

Sijui kama makala imefanikiwa kuonesha kuwa pamoja na sifa chanya tele tele za Mwalimu, alibaki kuwa binadamu aliyeweza kufanya makosa. Kuna sentensi yake maarufu ya “tusifanye makosa, kwani sisi malaika? Wakati mwingine Mwalimu alituonya akisema yale mabaya acheni. “Tatizo lenu ni kuwa hata yale ya msingi mnayahoji”. Haya ni maneno ya kiongozi mkweli kwa nafsi yake, mnyenyekevu, kiongozi anayekubali kuwa yeye ni mtumishi wa watu.  Naamini ni kiongozi anayetambua kuwa kauli ya watu ni kauli ya Mungu, na hivyo kuomba msaada wa Mungu katika kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia waja wake Mwenyezi Mungu.

Viongozi, hususani watawala wa nchi yetu kwa sasa kwa yale mema ya Mwalimu, si dhambi kuanza upya na kumfuata Mwalimu kwa vitendo. Kwa viongozi wajao, wajue jambo hili. Mtahukumiwa kwa kuacha kuyaishi na kutekeleza kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu, uadilifu na misingi aliyotuachia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mungu ibariki Tanzania.

Mwandishi wa makala haya, Arcado Ntagazwa, amewahi kushika nyadhifa katika taasisi, Mbunge na Waziri katika Wizara mbalimbali. Kwa sasa ni mwanachama hai wa Chadema. Anapatikana kwa simu namba 0786 – 617777.