Rais Samia choma kichaka nyoka wakimbie

Na Deodatus Balile

Wiki mbili zilizopita niliandika makala nikipongeza hatua anazozichukua Rais Samia Suluhu Hassan. 

Nimeeleza kukubaliana naye katika dhana ya kuchimba madini au mafuta hata kama yapo kwa maana kwamba hizi rasilimali zipo kwa ajili ya kusaidia kulikomboa taifa letu kutoka katika umaskini uliotopea. 

Narudia, mimi naamini kizazi chetu cha sasa kinazo akili za kutosha kuchimba madini hata kwenye mbuga au mafuta na gesi bila tatizo.

Suala kubwa la msingi ni kuwa tuwe na sheria murua kabisa zitakazotuongoza kutumia vema fedha zitakazopatikana. 

Nimeona yaliyotokea Wizara ya Fedha, ambapo wafanyakazi wametumbua bilioni 1.6 kati ya Machi 31, hadi Mei 3, 2021. Nimeyasikia malalamiko ya baadhi ya makandarasi kuambiwa wameishalipwa madai yao wakati bado wanadai.

Nafahamu tatizo la wazabuni wengi kuidai serikali madeni lukuki, ambayo mengine nyaraka wanaambiwa zimepotea, vikiwamo vyombo vya habari vinavyodai mamilioni. 

Naomba nitumie mfano wa Wakala wa Usajili wa Biashara (BRELA). Miaka ya nyuma ilikuwa vigumu kupata jalada la kampuni ukafahamu nani anamiliki nini. Baada ya siku za karibuni kuboresha mfumo wanapotumia ORS, kwa sasa ukiwa na namba ya kampuni kupata taarifa za kampuni ni sekunde 10 tu.

Sitanii, kupitia makala hii wala sitaki kutumia mifano ya nchi za nje kama Norway, Finland, Marekani au Uingereza. Nataka tuufikiri huo mfano wa BRELA na mingine tuone jinsi gani tunavyoweza kumaliza kero nyingi hapa nchini kwa msaada wa teknolojia ya habari. 

Sekta ya benki nayo ni mfano bora siku hizi. Kwa kutumia utaratibu wa Internet Banking, benki zimepunguza migogoro na wateja.

Kwa sasa ukiweka fedha benki, simu yako ya mkononi iliyounganishwa na akaunti yako inakupatia taarifa. Ukichukua fedha au benki wakikata riba au tozo yoyote kwenye akaunti yako, unajulishwa. 

Hata inapotokea ukawa na shaka na muamala uliofanyika, unaweza kuingia kwenye akaunti yako hata saa nane usiku, ukajiridhisha iwapo taarifa ya benki (Bank Statement) ya akaunti yako inaeleza uhalisia au kuna mtu amekuchukulia kitu.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nayo imeingia katika mifumo ya kielektroniki. Leo mimi nina siku nyingi bila kuandika hundi ya kwenda benki kuilipa TRA kodi kama PAYE, SDL na nyingine. Tukiwa hapa ofisini tunatengeneza namba ya malipo (control number), kisha ukiingiza namba hiyo kwenye akaunti yako, inakueleza kiasi unachopaswa kulipa na ukiweka nywila (password) yako, malipo yanahama hata iwe sikukuu, Jumapili au usiku wa manane.

Leo mimi ninalipa ankara (bill) za maji anayotumia mama yangu Bukoba kwa Mamlaka ya Maji Bukoba (BUWASA) nikiwa Dar es Salaam. Ukipata ankara ya malipo, unaulizia nyumbani iwapo ‘uniti’ za maji unazotaka kulipishwa wamezitumia kweli, wakisema ni kweli, unaingiza hata kwenye simu ya mkononi unalipa mara moja bila kupanga msitari. 

Hapo sijazungumzia TANESCO na ununuzi wa umeme kwa njia ya Luku. Tulipinga sana ujio wa Luku tukitaka mita zetu za zamani, lakini leo tunafurahia Luku bila karaha yoyote.

Sitanii, nimeyasema yote haya kujenga hoja. Kujenga hoja kuwa nchi yetu inaweza kupiga hatua kubwa na kwa haraka katika kudhibiti wizi, ubadhirifu, uvujaji wa mapato, matumizi mabaya ya madaraka, kutowajibika, uvunjaji wa sheria na mengine mengi, iwapo Rais Samia utafanya marekebisho ya sheria zikaruhusu haki ya kupata habari ikatamalaki, kwani kwa sasa inatolewa na sheria kwa mkono mmoja, ikachukuliwa kwa mkono mwingine.

Mfano Kifungu cha 5 cha Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa (ATI) ya Mwaka 2016, ukikisoma unaiona Tanzania kuwa iko peponi. Hata hivyo, ukisoma Kifungu cha 6, kinazuia kila kilichoruhusiwa chini ya Kifungu cha 5. 

Hali kama hiyo ipo kwenye Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016), kinatoa uhuru wa kutafuta, kuchakata na kuchapisha taarifa. Kifungu cha 7(3) karibu kinachukua kila chembe ya uhuru uliotolewa.

Nalenga kusema nini? Ninachosema, ikiwa sheria zitarekebishwa, haki ya kupata habari ikawa wazi na habari zikawekwa wazi mtandaoni, zikionyesha haki na wajibu wa kila mtu. 

Kama mtu anadai deni lake, iwe kwenye halmashauri, wizarani au taasisi yoyote likawekwa wazi mtandaoni (bila nafasi ya kulihariri), hali hii itaipunguzia serikali mzigo mkubwa.

Itapunguza wizi wa mali za umma, lakini pia itaongeza kiwango cha serikali kuaminika mbele ya wananchi, kwa kuonyesha kuwa haina cha kuficha. Narudia niliyoyasema wiki iliyopita, kuwa ukiwapo uwazi wa kiasi hiki, hakuna atakayepata nafasi ya kudai Sh bilioni 40, wakati deni halisi ni Sh bilioni 1! 

Rais Samia badili sheria uruhusu uwazi kisheria na haki ya kupata habari, mambo yakunyookee. Watenda maovu wanajificha kwenye mfumo wa sasa wa sheria zenye upenyo wa maficho. Choma kichaka, nyoka wakimbie. Mungu ibariki Tanzania.